Ngwesa

Ngwesa ni mtayarishaji anaepatikana kule Dar Es Salaam Tanzania. Mtayarishaji huyu ambae amejikita kwenye midundo ya Hip Hop tu pia mtaalam wa TEHAMA, baharia na alishaiwai kuchezea timu za mpira wa miguu Ligi Kuu, Tanzania bara.

Mwaka huu mtayarishaji huyu baada ya kimya cha mda mrefu alirudi booth na akishirikiana na wachenguaji tofauti tofauti aliamua kutuonesha Uwezo wake.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Ngwesa. Jitambulishe kwanza kwa wasomaji wetu, majina rasmi, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Kwa majina naitwa Hemedi Wales Ngwesa natokea, Dar es Salaam, Tanzania. Najihusisha na sanaa ya upigaji midundo ya muziki wa Hip Hop.

Tuanze kutoka mwanzo; shule ulisomea wapi, ya msingi na upili na baada ya hapo ulifikia hadi wapi? Pia tungependa kujua historia yako ki muziki wakati ukiwa mdogo ulitambuaji kipaji chako na umewezaje kukikuza hadi sasa kinakulipa?

Shule ya msingi nilisomea Mapambano Primary School ambayo ipo Dar es Salaam na secondary nilisoma pale Green Acres. Baada ya hapo nilienda chuo nikasomea mambo ya IT na baada ya kumaliza nikasoma tena mambo ya ubaharia na huku nilikuwa nikicheza mpira wa miguu nilichezea team kama Pan Afrika wakati ipo ligi kuu Tanzania na nikacheza team ya JKT Ruvu pia team ya jeshi ila kipindi nasoma ndio nilikuwa nikijifunza mambo ya music production mwenyewe na muda nwingine nilikuwa nikienda Mosad Studio ambayo ilikuwa ya rafiki zangu ambao nilisoma nao elimu ya msingi ambao walikuwa ni Duke Tachez na Eric Abisai na muda mwingine alikuwa akija Profesa Ludigo.

Mwanzo mziki nilikuwa napenda sana kuskiliza muziki lakini nilikuwa nikijiuliza, “Hivi hizi beat wanafanyaje mpaka zinatokea?”, nikajikuta na maswali na kutaka kujua ndio hapo siku nikakutana na rafiki yangu Duke na kumbe alikuwa na program ambayo inaitwa Fluity Loops 2 na Hip Hop DJ zote zilikuwa za production basi ndio nikaanza kujifunza mpaka leo nimekuwa mpigaji midundo.

Nipeleke nyuma hadi ngoma yako ya kwanza uliowai kuiunda, ni ipi na ya masanii gani na mapokezi yalikuaje ilipotoka?

Ngoma ya kwanza kabisa kuiachia nakumbuka ilikuwa ya Dizasta Vina ilikuwa inaitwa Miss Tamaduni ila nyimbo iliyonitambulisha zaidi ni Natoka Tanzania ya Nikki Mbishi ambayo iliwashtua watu kwa ujumbe na beat yenyewe. Pia watu walipokuwa wakisikia Ngwesa alafu hawakuwa wakimjua kwa hiyo ilileta shauku miongoni mwa watu wengi kutaka kufanya kazi na huyo Ngwesa.

Wewe pia ulikua mmoja wa watayarishaji wakati wa ile TamadunMuzik era. Tueleze kuhusu wakati huu, ulifakiwa kufanya kazi na akina nani na kwenye miradi ipi?

Ni kweli nilikuwa miongoni mwa ma producer wa Tamaduni Muzik na bado nipo licha ya kuwa nilikuwa na studio yangu ya 84Studio

Nilifanikiwa kufanya mixtape ya Boshoo Ninja ambayo inaitwa Ujamaa Shari na ilikuwa na nyimbo kama kumi na ushee flani.

Nikafanya mixtape yangu ya Uwezo ya kwanza ambayo ilikuwa na nyimbo 16 na nikaja kufanya tape ya Logic/Mantik wa uwakika ambayo iliitwa Miaka 9 Ya Ukubwa ilikuwa na nyimbo 20

Ni watu gani walikupatia motisha ya kuwa mtayarishaji? Nani mtayarishaji wako pendwa kwa sasa iwe ni wa nyumbani au mamtoni?

Kwa hapa bongo hauwezi kuacha kumtaja Duke Tachez ila Mujwahuki na Rey Tech, hao walikuwa wakinikosha sana na aina ya upigaji wao.

Na hapo hapo kwenye miradi uliowai kuifanyia kazi pengine hadi sasa umeshahusika kwenye miradi gani iwe ni EP, Mixtape au album na iwe ni yako au ya wasanii wengine?

Katika miradi ya watu nishahusika kazi nyingi kama za Izzo B, kuna kazi nilifanya na Azma pia na za Nikki Mbishi, Ghetto Ambassador, kuna kazi nilifanya na Kaa La Moto Kiumbe aliomshirikisha One The Incredible.

Nimeona pia una studio yako 84 Studios, hapa mnajihusisha na nini? Na je wewe ni producer wa midundo ya Hip Hop tu au wa muziki wowote?

Katika studio yangu mimi najihusisha na Hip Hop tu nyingine sijawai kujihusisha nazo.

Bio profile yako inasema wewe pia ni Seaman na Computer Technician. Unapo vaa hizi kofia tofauti na mtayarishaji hua ni kwasababu muziki haulipi au nikuzidi kucheza na talanta tofauti ulizo barikiwa nazo?

Ni kweli muziki wetu haulipi inabidi muda mwingine niangalie na fani nyingine kama mwaka juzi sikuwepo kabisa nchini nilikuwa kwenye fani yangu nyingine kwa hiyo muziki nikauweka pembeni kabisa.

Mwezi huu tu umeachia album yako mpya Uwezo. Tueleze kuhusu kazi hii, mbona Uwezo, ina ngoma ngapi na wachanaji gani wamehusika humu? Maudhui ya mradi huu ni yepi?

Tape yangu niliamua kuipa jina la Uwezo, sababu ya kutaka watu wajue uwezo wangu wa upigaji midundo na wachanaji kuonesha uwezo wao kwa hiyo kila kinachosikika ndio uwezo wenyewe na ndio maana kuu ya jina la album Uwezo.

Nini kilikusukuma kuandaa album yako na jee wewe pia unachana mle?

Mtu alienisukuma sana kufanya hiyo tape ni Catalyst na Black Ninja. Hao walikuwa mara kwa mara nikiwa nao lazima waniambie swala la kufanya tape sababu nilikuwa kimya muda mrefu. Mimi si mchanaji licha ya kuwa na uwezo wa kuchana kwa kiasi changu.

Mashabiki watarajie nini kutoka kwa kazi yako mpya na je wataipata wapi wakiihitaji?

Mashabiki watarajie kazi nzuri na midundo mizuri kutoka kwa wachanaji wazuri kwa hiyo wachukue tape wapate burudani. Wanicheki kwa no (+255) 0713795673/0785267171

Changamoto unazokabiliana nazo kwenye hizi mbanga za utayarishaji ni zipi na unazimudu vipi?

Changamoto ni nyingi mfano watu wengi wanataka kazi bure na wengine unakuta mtu anahitaji kuelekezwa kwanza, unakuta bado kufikia kuanza kurekodi ila sababu unakuta kashatoa pesa yake hapo aelewi kabisa swala la yeye kufanya mazoezi yeye anataka kurecord tu.

Mchakato wako wa uundaji anapokuja msanii ili muunde kazi ni upi, kutoka akupe wazo hadi ukamilishe kazi na kumpatia?

Mara nyingi hua napenda mtu kwanza anipe mada husika ya hiyo nyimbo, hapo sasa mimi nakua na picha kabisa ya aina ya mdundo kichwani sasa hapo kazi ndio itaanza.

Tukimalizia ningependa kujua kama una chochote cha kutuambia ambacho pengine sikukuuliza?

Kitu kikubwa naweza sema ushirikiano tuongeze baina ya watunzi wa midundo pia tunakaa nyuma sana

Shukran zako ziende kwa akina nani ambao wamekua nawe kwenye hii safari yako ya utayarishaji?

Shukran zangu ziende kwa watu kama Duke, Mujwahuki, Texas, The MC, Black Ninja, hawa watu kwa muda tofauti tofauti washanisaidia sana kwa mawazo na kwa ujuzi.

Mawasiliano na anwani za mitandao ya kijamii?

Email: Ngwesajr@gmail.com
Facebook: Hemedi Ngwesa
Instargram: Hemedi ngwesa

Shukran sana kaka kwa mda wako. Mimi mwenyewe nishajinyakulia nakala yangu wacha sasa nikavunje speaker, mcheki mwana upate nakala yako.