Nikki Mbishi, Unju Bin Unuq au ukipenda Baba Malkom ni mmoja wa emcee hatari wa kizazi chake kuwai kutokea ndani ya sio tu Tanzania bali Africa Masharariiki. Emcee huyu ambae ana miradi zaidi ya sita chini ya ukanda wake pia ni muigizaji na mtaalam wa teknologia kando na kua mchanaji. Tumepata fursa ya kupiga nae gumzo kuhusu maisha yake ya muziki pamoja na album yake mpya Katiba Mpya.
NB: Kama ungependa kuskia podcast ya gumzo hili nenda moja kwa moja mpaka mwishoni mwa makala haya utapata link.
Karibuni sana Micshariki Africa jukwaa la Hip Hop na leo tumefika Dar ili kuweza kuonana na kupiga gumzo na mmoja wa wachanaji bora wa kizazi chake kuwai kutokea hapa sio tu Tanzania bali hata Africa Mashariki. Simzungumzii mwingine bali ni kaka yetu emcee Nikki Mbishi, Baba Malcom, Unju…
Karibu sana Micshariki Africa kaka Nikki Mbishi. Kwanza kabisa tuanze kukufahamu majina yako rasmi, unapatikana wapi na unajihusisha na nini?
Majina yangu halisi naitwa Nicas John Marwa Machuche au sio alias Nikki Mbishi kama wengi wanavyopenda kuniita au Unju Bin Unuq. Mimi ni rapper/emcee/beatmaker/actor na chochote kinachohusika na sanaa au sio, na hicho ndio kitu ambacho najihusisha au najishughulisha nacho.
Kaka Nikki ningependa utupeleke wayback; ulizaliwa wapi, ulisomea wapi, shule za msingi na upili na pamoja na masomo yako ya baadae.
Aah mimi, shule ya msingi nimesoma shule nyingi kidogo kabla sijamaliza darasa la saba ila sekondari nilisoma Juhudi Sekondari iko gongo la mboto Dar Es Salaam hapa hapa. Baadae nikachaguliwa kwenda kusoma Chuo Cha Mbeya (hapo zamani kilikua kinaitwa MTC na baadae ikaja kuitwa MIST na sikuhizi kinaitwa MUST, yaani Mbeya University Of Science & Technology), nikasoma pale Diploma ya Computer Engineering.
Nikaandelea, ila sikuajiriwa, nikaendelea tu na muziki na vitu kama hivyo.
Je utoto wako ulikuaje na uligunduaje kua una kipaji cha muziki?
Kuhusu kugundua kama nina uwezo wa ku rap au nina kipaji cha kuwa ni mchanaji ilikua ni utotoni tu, unaanza kuskia miziki ya watu wengine una kua inspired, una iga wanavyofanya au sio, na kadri siku zinavyo zidi kusonga na wewe pia unakomaa, ile misingi inakujenga na kama kitu unakipenda unajikuta na wewe ni part ya hiyo kitu.
Mbona jina Nikki Mbishi? Jina lilikujaje na lina maanisha nini?
Kuhusu jina, jina kwanza credit zinaenda kwa mwanangu mmoja anaitwa Alex, sahizi nafkiri ni afisa wa Ustawi Wa Jamii huko Kisarawe. Yeye ndio alinipatia jina la Nikki Mbishi enzi hizo bado ni yanki sana, una rap na nini na ulikua unaweza ku rap na watu wengine wakubwa kuliko wewe ki umri, watu walikua wana rap wengine wakubwa kuliko mimi lakini Alex alikua anasema, “Ah ah, wote mmemaliza haya muacheni sasa huyo dogo. Huyo dogo mbishi sana. Wee dogo unaitwa nani?” Mimi nikamwambia naitwa Nikki, “Ah huyu Nikki, mbishi sana.”
Kwa hiyo ikawa Nikki Mbishi, Nikki Mbishi maskani, kuanzia hapo mpaka ikawa ndio jina langu la kazi.
Pia una majina kibao kama vile Baba Malcom, Unju (Bin Unuq) na kadhalika. Tueleze kuhusu hizi aka zako, maana zake na umuhimu wake kwenye sanaa yako.
Kuhusu hizo aka nyingine zilikuja baada yakupata mtoto wangu wa kwanza Malcom, Unju ilitokana na ile fiction story ya Unju Bin Unuq (The Great Myths Of Unju Bin Unuq), kama wanavyosema kuhusu Luanda Magere au kama wanavyo sema Mwana Marundi, hivyo vitu kama hivyo.
Ila nilichagua Unju kuji depict mimi mwenyewe, au sio. Kwa hiyo kitu chochote Unju anagusa it becomes big, even bigger, Unju is the greatness.
Wewe ni mmoja wa ma emcee waliotokea kwenye kundi la Tamaduni Muziki. Tueleze historia kidogo kuhusu wakati ule. Wewe binafsi ulijipataje kwenye harakati zile?
Tamaduni Muzik ilikua ni independent platform ilikua sio kundi as such, watu wengi wanapata confusion hapo kua Tamaduni Muzik ilikua kundi. Tamaduni Muziki halikua kundi, Tamaduni Muzik ilikua ni independent label ambapo ndani yake ndio kulikua na makundi tofauti tofauti. Kwa hiyo na ma founder wa Tamaduni Muzik, akina Duke (Tachez), Lindu au sio na ukizingatia Duke nilifanya nae kazi pale MLab kwa hiyo hata hizo idea walipoanza ku initiate hiyo independent label ambayo ni Tamaduni Muzik. Mostly emcees ambao tulikua tunafanya MLab chini ya Duke pale tulikua around pale; mimi, Stereo, One (The Incredible), au sio, mara nyingi ndio tulikua hapo.
Tulikua lazima tutoe influence kwa kuwaambia watu kwanini, ndio maana watu wanapotuona sisi kinacho wajia kwanza ni Tamaduni Muzik, wengine wanakumbuka Lunduno and stuff.
Je impact ya Tamaduni Muzik kwako wewe na kazi zako ni ipi?
Tulileta hamasa kubwa sana. Ilileta ushawishi wa kurudisha vilinge vilivyo potea kwa miaka mingi sana. Tulifanya vilinge vikafunguliwa Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Mbeya, yaani sehemu kibao kukawa kuna vilinge. Kwa hiyo impact ilikua nzuri kwa namna moja au nyingine na kwa watu wa Utamaduni wa Hip Hop wali appreciate hiyo, tulifanya movement.
Wakati ukikuza kipaji ni akina nani walikua wanaku inspire sana, na kukuvutia kwenye utamaduni huu?
Mimi enzi zile naanza kupenda rap ya Kiswahili, kwasababu zamani rap ya Kiswahili ilikua ni ngumu sana kuipata kwa maana ya kwamba ukienda kwenye cassettes zile ambazo ziko pale sebuleni unakuta zile tapes ambazo amenunua mshua. Sasa mshua ana kanda zake za kwaya, jumapili ataskiza, ana kanda zake za misimu ya siku kuu, Christmas, Mwaka Mpya, Pasaka, utakuta kuna tape za kina Jim Reeves, zile “Jingle bell, jingle bell…” Ukipindua sasa unakuta miziki ya kilingala ambayo ni ya ki Congo ambayo unakuta akina Lokasa Ya Mbongo, Arlus Mabele, Defao, Pepe Kale akina Madilu (System), Franco, Luombo Makiadi huko na watu kama hao.
Kwa hiyo kwa umri ule, ni kazi sana wewe ku access muziki wa rap, sana sana, tutakua tunapata tu tapes za nje, kwasababu ngoma ya kibongo, rapper wa kibongo ilikua kuitoa, umeskia mtu ame rap kwa Kiswahili ilikua kitu flani cha kushangaza kwasababu walianza kwa kuigaiga wasanii wa nje na hata beats walikua wakitumia za wasanii wa nje.
Kwa hiyo nilipenda kuskia rap za Kiswahili baada ya kuskia akina Mr. II (Sugu), niliskia Kwanza Unit vile walivyotoa Msafiri, nilimskia Prof. Jay (Nigga Jay). Sasa Jay ndio alinivutia zaidi, ndio nikasema now this is it! Nikapenda akina Inspector Harun (Gangwe Mob), OGWM, Wamenikuta, Kipi Kitu, long time, ’94, 95, huko.
Ngoma yako ya kwanza ilikua inaitwaje na uliifanyia wapi? Je mapokezi kutoka kwa mashabiki zako ilikuaje?
Ah, official release ya kwangu mimi ya kwanza ni debut track kutoka kwa album ya Sauti Ya Jogoo ilikua ni Punchlines ambayo niliifanya na Grace Matata. Kwa hiyo that time nilikua nimeanza chuo, kwa hiyo ufuatiliaji ulikua chini ya label yangu. Hiyo ki msingi nilikua naona tu ngoma zinaenda, si unajua tu mtu unaenda kwa ku grow, ikaja ikatoka ngoma nyingine watu wakaendelea kupokea na nikaendelea kua Nikki Mbishi na album ilifanya vizuri sana.
Kaka Nikki Mbishi una catalogue kubwa ya muziki, naomba kufahamu zile main projects ulizoachia iwe ni mixtape, EP au album, zinaitwaje, zilitoka lini na mashabiki watazipataje kazi hizi?
Aah mimi mpaka sasa hivi officially kabisa nina official projects ambazo ni album tano na mixtape moja ambayo album yangu ya kwanza ni iyo Sauti Ya Jogoo ilitoka Novemba 26, kama sijakosea mwaka 2011, ndio ilitoka. Album yangu ya pili ilikua ni Malcom XI, sasa hapo ni baada mkataba wangu na MLAB kuisha kwa hiyo nilipoanza kua solo artist, independent artist sina label yoyote, album yangu ambayo niliitoa mimi mwenyewe ilikua ni Malcom XI ambayo ilitoka 2013 mwezi kama wa kumi, tarehe 12. Ilipishana miaka miwili na ile (ya kwanza). Album yangu ya tatu ilikua Ufunuo Wa Unju Bin Unuq. Hii nayo ilikaa miaka miwili ikatoka, ilikua 2015, ilitoka kama (tarehe) Nane Nane, tarehe 8 mwezi wa 8. Kisha ikaja kufuatia album yangu ya nne inaitwa Sam Magoli, hii ilitoka kama tarehe 18 mwezi wa 11 au 12 na ilikua ni 2018. Kisha 2022 nilikuja kutoa album yangu ya 5 ambayo ni Welcome To Gamboshi au sio na mwaka huo huo kabla haujaisha ndio nikatoa mixtape (K.I.G.U – Kisirani Ghubu Cha Unju) wakati ninawapa watu gap yaku kumpuzika tunaanda vitu vingine.
So far ninafanyia kazi project yangu ambayo ni ya saba ambayo hii ni album ya 6, official studio album ya 6 ambayo inaitwa Katiba Mpya.







Kaka Nikki pia nimeona baadhi ya kazi zako kwenye streaming platforms pia nafahamu kua kunazingine zinapatikana kwako mwenyewe tu. Hili linakuaje, na je hizi streaming platforms umeshaona matunda yake tangu uanze kuzitumia?
Na kuhusu kazi zangu mara nyingi tuna wa direct hawa watu kutufuatilia sisi kwasababu ya ku keep in touch na yule artist unae mfeel, ndio unaifanya iwe poa zaidi. Unajua unaweza uka suggest uende kwenye streaming lakini if you contact me directly and I can respond personally, hiyo mimi na feel ni bora zaidi kuliko vile pesa zetu zinapopitia kwenye mifumo mingine alafu then zinatoka kwenye namna ambayo watu wata lalamika. Utasubiri pesa mda mrefu, alafu pesa unayoenda kukutana nayo ina disappoint vitu kama hivyo.
Kwa hiyo kama mimi hua wananiuliza kwanini kazi zangu zingine zinapatikana kwangu mimi mwenyewe, I think ndio hawa watu wa hizo platform wakae, waangalie potential ilipo, waangalie exclusivity na specialty ya yoyote ambayo impact ipo kwasababu sasa hivi platform zimekua kama the shit platforms, yaani anybody can put anything he wants. Kwa hiyo sio kitu ambacho kinatufavor sana sisi watu ambao hatuna vitu vya ovyo ovyo vya kutoa toa, sisi ambao tunajua misingi ya vitu tunavyo simamia.
Kwa hiyo we need something official, we need respect, mutual respect, between the mediator, the media and the platforms and the artist. Ushanielewa hapo? Nilishatumia baadhi ya platforms lakini ilikua na utata utata kwenye maswala ya malipo ya hapa na pale na mingine nikaamua tu kujitoa. Lakini if in the future I will see the use of me being in these digital platforms, nitakua hapo.
Tuongelee kuhusu chata lako la UNJU, hii concept ilikujaje na chata linakuwakilisha vipi wewe na brand yako ya Nikki Mbishi? Je mashabiki wamepokeaje chata lako na kwa wale wenye uhitaji wapi watalipata na kwa bei gani?
Chata la Unju Bin Unuq, nishaelezea wapi lilitokea na mimi nikawaza ni kitu poa sana kwenye bidhaa kwasababu sasa hivi tunatoa kofia, tunatoa t-shirt, tunatoa ma pullover lakini pia inabidi tupanue bidhaa zetu zifike kua tunatoa mpaka lighter za kuwashia mafegi, kuwashia ma kaya lakini yote yatakua Unju Bin Unuq. Kwa hiyo bado tunajaribu kuunda brand iwe kubwa zaidi na yeah, fans wame respond poa. Wamependa chata la Unju na ukhiitaji ni simple tu, wasiliana nami kwani mimi sijafa bado au nikifa ua nikitoa taarifa kua vitu vyangu vitakua vinapatikana pale, na pale na pale, hapo ndio utakua utaratibu lakini so far namba zipo kwenye social media zote ambazo mimi nipo na utaratibu wakunipata wote uko pale.
Na kwa bei za machata kuna bei zake elekezi, atakae piga simu ndio atakae jua gharama kwani wengine wapo mbali na watabeba gharama za usafari, delivery na kila kitu. Ma t-shirt ni alfu 25 Tshs au mpaka 30,000Tshs, ma pull over ni 40, 000Tshs, ikitegemea quality na namna mzigo ulivyo agizwa na wapi ulipo.
Pia ningependa kukushukuru kwa supoti yako kwenye mradi wetu wa Mashariki Ya Fikra. Wewe ni mmoja wa ma emcee waalikwa kwenye mradi huu uliowaleta pamoja ma emcee chipukizi kutoka Kenya (Msito) na Tanzania (Fedoo). Kwanza kabisa unajiskiaje kushiriki kwenye mradi huu unaoleta na kuhimiza umoja na mshikamano kwa ma emcee na wana Hip Hop wa East Africa?
Kwanza nafurahi kwa kua sehemu ya ushirika wa hii project ya Mashariki Ya Fikra. Huyu Msito is from Kenya, sio familiar kwangu ila I recognize Fedoo, Fedoo namfahamu, yeah freshi tu. Kwanza nimeshiriki kwenye project ya watu ambao ninao waamini na waonesha nia ya kufanya hicho kitu.
Kwa hiyo pia imeleta ukaribu, ushirikiano, kule ku collaborate, kuna mwingine anaona mtu flani huwezi kumfikia, wanakua kama “mungu” yaani mtu flani kufanya nae kazi haiwezekani. Yeye labda anaweza kuenda kuomba kazi na wasanii wengine wa nje hata kama in terms of payment, watu wanalipana ua nini, ila chamsingi once you go over the borders or you are popular overseas you need to hold the hands of the people you left behind from your country. Yaani sio tu wewe ukienda ndio wewe tu ndio umeenda, naah it is never like that. Mimi nimejiskia poa kushirikiana na Micshariki kama hivyo, yeah we keep pushing.
Mashabiki watarajie nini kutoka kwako kwenye huu mradi wa Mashariki Ya Fikra. Pia ningependa uwape ushauri hawa vijana wako walioshiriki na kwa yoyote yule ambae anajaribu kupenya kwenye hii rap game.
Ushauri ninaoweza kuwapa vijana walioshiriki kwenye huu mradi ni consistency. Wanasema kuna vitu vitatu, wanasema the Triple P. Cha kwanza unatakiwa uwe na Persistence ambayo persistence hiyo ndio ina determine consistency yako. Persistence ndio ile hali ya kua mbishi, king’ang’anizi, sio mtu wa ku give up. Uwe unaanguka, you stand up again, you keep moving, hivo. Hiyo ndio consistency na ndio persistence.
Alafu kitu kingine kinachotakiwa ni Passion, uwe uko Passionate. Unatakiwa uwe na passion ya kile kitu unacho kifanya, unachokipenda, you do it from the core of your heart. Baada ya hapo unatakiwa uwe na Patience, hii ni subra, uvumilivu, endurance. Unaweza kukaa, sio tu uingie kwenye muziki au kwenye utamaduni kupata umaarufu na pesa (money and fame). Hata Snoop Dogg anakwambia ukienda kazini ukiwa unafikiria utalipwaje, kazi lazima utaiona mbaya. Kwa hiyo unapokwenda kazini fikiria kufanya kazi bora then the returns of what you did ndio iwe ina determine efficiency yako na wewe ulichostahili kukipata au hata ukifanya kazi bora matokeo yakiwa mazuri it makes you feel much better.
Kwahiyo watu wajifunze utamaduni, wasikurupuke, wauelewe ausio, wasije kua wakitaka kua akina Jay-Z.
Changamoto za hizi kazi zako ni zipi na unakabiliana nazo kwa njia ipi? Kando na kua mchanaji nimeona bro wewe pia ni mtayarishaji wa muziki. Hii ishu ya utayarishaji ulianza lini na nini kilikuvutia ukajikuta hadi unaanda midundo?
Changamato kubwa ya kazi ninazo zifanya nafkiri ni ongezeko la wimbi la wajinga au ujinga. Unajua, ujinga sasa hivi ndio umeenea kwa sana na upo kwa kiasi kikubwa sana, kwahiyo watu wanaofanya vitu vya maana hawawezi kupata nafasi kuonekana ua kuskika kwasababu everybody wants to listen to stupid things, foolish things.
Ukiwa na kitu cha maana nobody cares. The rest, mimi sizioni kama changamoto kwasababu I can go to the studio I can make a record, I can shoot a video, I can do what I want to do and I’m still living. Lakini ukisema mifumo ya usambazaji, uuzaji, everything is open right now, it is a matter of choice, wewe mwenyewe ndio utachagua ufanye nini, ila changamoto ambayo mimi naipata kwenye kazi zangu ni kukutana na wimbi kubwa la wajinga ambalo linazidi kuongezeka ambayo hata ukimwambia mjinga kwamba hii ni asali kula, hataki yee anaweza akachukua kinyesi aka king’ang’ania. Kwa hiyo, hiyo ndio changamoto ambayo naipata lakini najitahidi kukabiliana nayo. Waswahili wanasema asiejua maana, haambiwi maana lakini kama usiejua maana na huambiwi maana utabaki kua mjinga, kwa hio inabidi uambiwe maana ili ujinga ukutoke.
Kwa upande wa utayarishaji, wanasema kukaa karibu na mahakama sio kujua sharia lakini mimi pia nimeishi ishi kwenye kota za kijeshi, kwa hivyo nikajikuta kuna vitu flani vya ki askari mimi navijua. Kuna sehemu nilikua nafika na nikawapiga mkwara wakajua mimi ni mzee, ni askari. Kwasababu nimekaa kwenye mazingira yale, I see what they do, kila siku.
Nimekaa na Duke, nimekaa na ma producers wengi kwahiyo I like to learn by watching. Me I was always watching what Duke was doing, Duke alikua hapendi mambo ya maswali maswali, sijui hapo umefanyaje, umefanyaje, anaweza akakufukuza, “Toka niwache nifanye kazi yangu”. Lakini ukitaka kukaa nae, wee kaa kimya, akibonyeza wee mwangalie hivi. Kwa hiyo practice makes perfect, so after sometimes unajikuta wee umejua vitu naturally. Umejifunza funza, vimekukaa na wee umeweza kujaribu jaribu, ehe, you have a system, ukizingatia mimi mwenyewe ni mtu wa ma computer computer hayo, ma PC hayo ninayo from wayback ni swala la ku install apps, ukifanya vile na vipi ausio, kuingiza ma plugins, unachezea chezea, unajikuta unatoa kitu kwasababu wanasema, “Nzi akiacha ujinga anaweza akatoa asali”ndio hivyo mjinga.
Kwahiyo hiyo inspiration ilikuja baada ya kuishi mda mrefu kwenye mazingira ya studio na nimeshafanya kazi baadhi zipo kubwa tu, na wasanii wakubwa tu ambazo zimetengenezwa na mimi mwenyewe.
Ningependa kujua kuhusu mchakato wako wakuandaa muziki, hivi hua unaanzaje kutoka pale unapo pata wazo hadi kuingia studio na kukamilisha wazo?
Mimi mchakato wangu wakuandaa muziki kwanza na fluctuate na seasons of time, mfano unaangalia msimu tupo, what is really current right now, what is being spoken by the people, nini sasa hivi ndio mada, majanga gani, shida gani zinazowakuta watu kwa sasa, what is really going on in the world, hivyo ndio vitu vina ni inspire.
Kwa mfano ukiangalia project kama ya Katiba Mpya you see kwa sasa tupo katika mchakato wakutafuta constitutional amendment (change), mabadiliko ya katiba, kwa hiyo the right timing. Kwa mfano kipindi cha miaka ya nyuma, Ukimwi ndio ulikua ndio dili hivyo wasanii wengi walienda na hii mada. Mwana FA – Alikufa Kwa Ngoma, Ferooz- Starehe, Professor Jay – Usinitenge, those were the seasons. Hata kipindi cha Corona watu waliongea kuhusu Corona lakini mimi napenda kuongea kuhusu vitu ambavyo vita sustain na vitaishi na hata vizazi vinavyo kuja vitaendelea kuvitumia kwasababu ukiimba kuhusu Corona, Corona ikiisha ule wimbo wako wenyewe ndio umeisha, lakini katiba haiishagi, wee utaondoka, atakuja bibi yako nae ataandama, ibadilishwe ila Corona ishaisha.
Kwa hiyo naanda concept kwa maana ya theme ya album itakavyo kua, na sio kwasababu ni katiba mpya ndio itakaa kisiasa, no, mimi katiba yangu imeegemea kwa wananchi kwasababu wananchi ndio wanao hitaji katiba mpya sio viongizi wanao ihiitaji katiba hio, kwani wao wako pale na ile katiba ya zamani ina wanufaisha wao zaidi kwa kusimamia haki zao.
Kwa hiyo wananchi ambao wako makini wameamka wanasema wanataka Katiba Mpya, kwasababu ingekua wale ndio wanataka katiba mpya ingekua ni swala wakiamka tu asubuhi wanapeana tu vi notisi/memo kisha wanatangaza katiba mpya, they can do it in one night.
Lakini kwanini inakua ni mchakato mrefu kwasababu ile ni katiba ya watawala sio katiba ya wananchi. Wananchi ndio wanataka ibadilike. Kwa hiyo mimi sijakua wa chama hiki wala wa chama kile, I’m tying to be in the middle of my fellow citizens, watanzania wa kawaida na watu wote ambao wanaona kuna uhitaji wakupata katiba mpya, Tanzania.
Tuongelee Katiba Mpya, kazi yako unayo tarajia kuachia hivi karibuni. Mbona Katibu Mpya, maudhui ya mradi ni gani na nani wahusika iwe ni watayarishaji au wasanii waalikwa? Mashabiki watarajie nini kutoka kwako kwenye mradi huu na pia kazi hii itapatinaka wapi?
Kuhusu Katiba Mpya I will say it again kwamba ni project imekuja ambayo hata kama haitosababisha katiba ibadilishwe, lakini ita spark the minds of the people who want changes. Kwa hiyo italeta cheche, itaamsha kidogo wanaohitaji mabadiliko, hapa na pale kwa ajili ya vizazi vijavyo, prosperity of future generations. That’s what I mean.
Kuhusu nani wahusika mimi napenda kufanya rewiew ya mradi wakati ushatoka, siwezi kukwambia vitu vinavyoendelea. What I can say is, work in silence, let the outcomes make noise, hiyo ndio kitu mimi naamini. Kwa hiyo let me work first alafu nitakuja kuweka kila kitu hadharani na wataambiwa tarehe na walioshiriki, producer gani.
Katiba Mpya


Tungependa kumalizia kwa kujua kama una chochote cha kutuambia ambacho hatujakuuliza. Shukran sana kwa mda wako na tunapofunga kipindi tupe mawasiliano yako na anwani zako za mitandao ya kijamii.
Mashabiki watarajie the best of Nikki Mbishi, like always na upatikanaji wa album yangu kila kitu kitatangazwa kitakapokua tayari. Kwa hiyo they just chill out kila kitu kitakua poa…
So far umeuliza maswali mengi na hivyo kuhusu kuna swali hujaniuliza…yanatosha, ni ya msingi, uliouliza ni ya msingi. Unajua bora maswali macheche ya msingi kuliko maswali mengi alafu hamna kitu. Alafu maswali mengine tushayajibu kwa zaidi ya miaka 15 huko iliyopita, tunafanyaje, tunayajibu hivyo hivyo kwa hiyo ukiyajibu tena, ukiuliza hayo hayo unaonekana wee kidogo uko nyuma ya muda.
Nashkuru kwanza kupata fursa hii kuongea chochote au kuchangia chochote kuongelea jambo lolote juu ya huo mradi wa Mashariki Ya Fikra, also to the fans and followers of Nikki Mbishi mimi napatikana kwenye mitandao yote ya kijamii,
YouTube: Nikki Mbishi [Unju]
Instagram: @NikkiMbishi999
Facebook: Nikki Mbishi Unju
Twitter: @NikkiZohan
Mitandao karibia yote tutakutana huko.
Ukihitaji personal contacts au business contacts, unaweza ukanifuata mimi on my most active page, Instagram, kule tutakutana na utaona maelekezo na namna ya kunipata na kila kitu. Kwa hiyo ndio hivyo it is peace yo, get ready for Katiba Mpya, Nikki Mbishi hapa, Unju.
Shukran sana waskilizaji/wasomaji wetu, huyo alikua ni Nikki Mbishi ambae alikua amefika Micshariki Africa kwa mara ya kwanza, asante na nawatakia siku njema.