Uchambuzi Wa Album: Welcome To Gamboshi
Emcee: Nikki Mbishi
Tarehe iliyotoka: 04.03.2022
Nyimbo: 21 + Outro
Watayarishaji: Black Ninja, SlimSal, Black Beats, Kita The Pro, Kise P, 10th Wonder, Ringle Beats, Unju(Nikki Mbishi), Hunter, Chizzan Brain, Paul Loops, Goncher Beats,
Mixing & Mastering: Watayarishaji Tofauti
Studio: Boom Bap Clinic, Tongwe Records

Nyimbo Nilizozipenda: Wazee Wabishi, Sinza, Nataka Kutoka, Nitumie Link, Uswazi Kishua, Straight Outta Gamboshi, Vita Ya Bengazi, Da Vinci Codes, Haijaeleweka, Adimu II, Jojo (Diss Track), Nyegere, Wanyonge, Nenda,

Nikki Mbishi

Baada ya kutuachia ngoma moja moja mwaka jana hadi mapema mwaka huu Nikki Mbishi aliamua kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kuachia album yake mpya na ya tano Welcome To Gamboshi. Kazi za Unju za awali zilikuwa ni Sauti Ya Jogoo, Sam Magoli, Malcom XI pamoja na Ufunuo Wa Unju Bin Unuq.

Maandalizi ya mradi huu yanaonekana yalianza miaka miwili iliyopita kwani kabla ya mradi huu kudondoka rasmi Bin Unuki alikuwa ameshaanza kuachia ngoma kadhaa zilizokuwa zinatuandaa kwa ujio wa kazi hii. Kwa mfano singo ya kwanza ambayo ndio imebeba jina la album hii Welcome To Gamboshi iliachiwa mwishoni mwa mwaka 2019.

Kwa wale wasiofahamu, Gamboshi ni Kata (Ward) ambayo inapatikana wilaya ya Bariadi, mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania. Gamboshi imesifika sana kutokana na hadithi nyingi zinazo enea kuwa eneo hili lipo vizuri inapokuja kwenye masuala ya ushirikina. Ngoma ya Mzimu Wa Gamboshi inawakilisha vizuri hii agenda ambapo wazee wanamfuata na kumuambia kaka Unju akomae na kuzidi kufanya anachofanya kwani wao wanamkubali kama alivyo na wanaamini, “Ipo siku utauheshimisha ukoo wa mzee Machuche”. Kise P ndio alikuwa ameshika usukani hapa kama mtayarishaji.

Nchini Kenya mtu mwenye uwezo wa “kumuvuzisha” umati anasemekana kuwa anajua kuroga na basi pengine Nikki Mbishi naye pia kaamua kuwaroga na kinasa sauti kama kuhani mkuu wa Gamboshi. Kama inavyoitwa ngoma moja ujue kuwa Unju ni Straight Outta Gamboshi.

Kazi hii inatupatia vitu vingi ambavyo tumeshazoea kuvipata toka kwa Nikki kama vile mashairi ya kijanja, uwasilishaji mzuri wa mada zake, uchaguzi wa midundo murua, uthubutu pamoja na kufanya kazi na wasanii ambao nao pia wanaleta vitu tofauti kwa mradi.

Mradi huu ambao umeunganisha vizazi unaanza kwa kuwakutanisha Nikki Mbishi na Ally Choki kwenye Wazee Wabishi, Baba Malcom na Baba Malcom. Goma la ki utu uzima kabla ya Nikki kutuachia mafumbo flani kwenye ngoma Da Vinci Codes.

Baada ya hapa emcee huyu anapiga kazi na emcee na wakati huo huo mtayarishaji SlimSal kwenye wimbo mzuka sana Sinza. Wawili hawa wamefanikiwa kufanya kazi kwenye ngoma mbili kwenye mradi huu, wa pili ukiwa ni Nataka Kutoka wakati huu wakiwa na Chuga. Sinza inapiga vizuri sana ikiwa na mpangilio mzuri wa mdundo na tarumbeta flani ilhali kiitikio kinakupeleka Sinza, mzuka sana. Nataka Kutoka nayo ni wimbo ambao unakejeli ma emcee ambao wanataka kutoka, goma la kejeli na ucheshi akiuliza SlimSal, “Wataka kutoka kwani we mwali?” Swali la balaga.

Baada ya hapa emcee huyu anagusa mada ya mapenzi kwenye Nenda ambapo hapa emcee huyu anajivika kofia ya utayarishaji na kutuundia mdundo mzuka sana akiwa na Ringle Beats na wanamshirikisha muimbaji  Otuck William. Unju anamwambia mrembo wake asepe kama vipi mbwai mbwai….Ila pia kuna ngoma nyingine hapa za mapenzi ambazo emcee huyu analainika na kuchana maneno yenye uwezo wa “kumuingiza mtoto kwenye box” kama vile kwenye Kama Namuona akiwa na Fama pamoja na Gamboshi Love akiwa na TK Nendeze.

Nikki anaonesha ubaya wake kwenye Haijaelewaka akimshirikisha muimbaji mzuri sana Becka Title ambaye washapiga nae sana akituuliza “Uko na pesa yetu hapo au story ndefu?” Black Beats kaua sana kwenye mdundo ilhali Becka kazika kabisa kwenye kiitikio.

Pen game Nikki Mbishi inaenda level tofauti pale anapoendelea kutuonesha u wana harakati wake kwenye Wanyonge akiwa na Makamua kwenye ngoma iliyoundwa freshi na Kise P. Tarumbeta linapiga kama ule msemo wa mbiu ya mgambo ikilia kuna jambo na hapa unaona emcee ana hoja nzito inayomkera na ameona aiwakilishe kwenye kinasa akisema kwenye beti ya pili,

“Akitembeza karanga mzururaji/
Akiuza sigara mlanguzi/
Sasa ataishi vipi huyu mshkaji? /
Baadhi ya viongizo mwanzo hamkuwa na mitaji/
Zaidi ya porojo zenu na kujifanya wajuaji/
Tumewapa ajira leo mnatuita wanyonge/
Wanyama samaki na sijashtua kidaka tonge/
Mashavu yote ya Simba Bin Kiba na bwana Konde/
Tutapata Suluhu tukiacha Pombe tusonge/
Mnyang’anyeni ardhi huyo hawezi kuwekeza/
Na mikataba yenu ongezeni kiingereza/
Maskini tabula rasa asielewe akielekezwa/
Hana umuhimu zaidi ya miradi mnayotekeleza/
Msijali njaa zetu komaeni na miundombinu/
Nyie mnajua kila kitu sie wengine hatuna elimu/
Basi nitaitwa mchochezi na wenye akili finyu/
Mchi ni ule ule hata mkibadili kinu/
Nasema ninayoyaona mitaani nakupitia/
Wajuu njaa bibi hana kuni za kupikia/
Majiko ya gesi na umeme hajawahi kuyaskia/
Na hata ukimpatia hatomudu kuigharamia/
Uchumi wake duni umetekwa na maharamia/
Kama wazee flani wa bandari mabaharia/
Tuna njaa ya vitendo wanatulisha nadharia/
Wanaharakati bandia mkitishwa mnakimbia/”

Harakati hizi pia zinaendelea kwenye Uswazi Kishua ambapo Becka Title anashirikishwa tena kwenye kiitikio kwenye ngoma hii iliyotayarishwa na Hunter pamoja na mtayarishaji/ emcee gwiji Chizan Brain.

Kwenye Nitumie Link emcee huyu anaongelea majaribu na changamoto za mtandao na mitandao ya kijamii akiongelea kizazi ambacho kina uelewa tofauti kuhusu neno connection kuliko vizazi vya awali.

Pia kama emcee mwingine yule anayejiamini majigambo hayakosekani kwenye mradi huu. Kwenye Jojo akiwa na mtayatishaji 10th Wonder na Black Ninja anarusha dongo kwa ma emcee akijifananisha na Hamza na kabla ya kuungana na wakongwe JCB na Diz Africana kwenye Nyegere ambapo magwiji hawa wanasema wao ni watu ambao hawashindwi na hawaogopi chochote kama alivyo mnyama Nyegere/Honey Barger.

Watu wamekuwa wakisema kuwa Unju wa siku hizi sio yule wa Sauti Ya Jogoo ila nadhani kupitia mradi huu Unju amewaonesha kuwa yeye bado  yupo na uwezo bado upo  na ukitaka kuliona hili basi Welcome To Gamboshi.

Kupata nakala yako ya Album hii Welcome To Gamboshi kwa Tshs 10,000.00 (Kes 500.00) pekee wasiliana na Nikki Mbishi kupitia;

WhatsApp: +255747828275
Facebook: Nikki Mbishi Baba Malcom
Instagram: Nikkimbishi999
Twitter: NikkiZohan