Nikvisions

Karibuni sana Micshariki Africa jukwaa la Hip Hop, linalowaletea taarifa, habari, mahojiano yanayoendana na utamaduni wetu wa Hip Hop. Leo tumepiga gumzo na mchoraji mkali sana anayetokea Dar Es Salaam anaejulikana kwa jina Nikvisions. Kwa hivyo karibu ili muweze kucheki gumzo letu na huyu jamaa ambaye pia sisi kama Micshariki Africa tumefanikiwa kufanya nae kazi huhusan inapokuja kwenye artwork za kipindi chetu tunachoshirikiana na emcee Adam Shule Kongwe, Shule Na Shule.

NB: Kama ungependa kuskia podcast ya gumzo hili nenda moja kwa moja mpaka mwishoni mwa makala haya.

Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu unaitwa nani, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Asante sana kaka. Kwa majina naitwa Deogratius Martin Gwassa aka Nikvisions lakini wengine huwa wananiita Nik Duncan. Natokea jijini Mbeya, ni mwana sanaa, najihusisha na kazi mbali mbali za sanaa za ubunifu au kwa wenzetu wanaiita creative artist.

Tueleze kidogo kuhusu historia yako ya nyumba ya sanaa, ulizaliwa wapi, unapatikana wapi na umesomea wapi kimasomo?

Mimi napatikana jijini Mbeya, ninaishi Mbeya, ila pia ni mkazi wa Dar Es Salaam kutoka na nature ya kazi yangu huwa inani force au inanilazimu kuishi katika sehemu hizi mbili tofauti kwa wakati tofauti kulingana na mazingira ya kazi kwa muda husika.

Naweza kusema nimezaliwa mkoani Mbeya na nimeweza kusoma katika shule tofauti tofauti zilizopo mkoani Mbeya za primary lakini secondary pia. Moja ya shule za primary nilizosoma ni Nonde Primary School, nimesoma pale miaka kadhaa lakini pia nimesoma Nzongwe Primary School, Jitegemee Primary School. Nimesoma pia shule nyingine iko Iyole, umeona nimebahatika kusoma shule tofauti tofauti katika shule ya msingi.

Pia secondary nimeweza kusoma elimu yangu ya secondary katika wilaya ya Rungwe, Mkoani Mbeya. Shule inaitwa Mwakaleli Secondary High School, niliweza kupata elimu yangu ya secondary pale ilhali chuo nimesoma katika Chuo Kikuu Cha Sayansi Na Teknologia kilichopo hapa hapa jijini Mbeya ambapo nilikuwa nachukua masomo ya Usimamizi Wa Biashara yaani Business Adminstration.

Hii ndio historia yangu fupi kuhusu mimi na kuhusu masomo yangu

Jina lako la kazi Nikvisions lilikujaje na linamaanisha nini? Nikvisions anajishughulisha na nini kiujumla?

Kuhusu jina la Nikvisions ni jina ambalo lilitokana wakati nikiwa chuo ambapo nilikuwa na girlfriend wangu hivi yeye alikuwa anasoma tuition secondary maeneo karibu na chuo chetu, so yeye akitoka akimaliza mda wake wa tuition alikuwa anakuja chuoni, lazima anisubirie mimi. Kwa sababu mimi nilikuwa sikai maeneo ya chuo wala sikai in campus nilikuwa nakaa mbali kwa hiyo ina maana hata kama nina kipindi jioni ilibidi nisubirie hadi mda wa jioni kwa hiyo nilikuwa siondoki maeneo ya chuo. Kwa hiyo unakuta sometimes labda kuna kipindi asubuhi, kipindi kingine mchana kingine jioni kwa hivyo kivyovyote vile mimi nilitakiwa niwe chuo kwa sababu nilikuwa nakaa mbali na chuo.

So kuna huu huyu jamaa Fred Vekaeli mara nyinyi tulikuwa tunakutana nae nikiwa na huyo girlfriend wangu ananiona “Oya vipi?”, “Shwari shwari!” Kwa hiyo tukikutana tukiwa sisi wawili tukiwa darasani ananiita “Oya Nikki, oya Nikki vipi?” Sasa mimi nilikuwa sielewi kwa nini ananiita Nikki kwa hiyo ikabidi siku moja nimuulize, “Oya vipi? Kwa nini unaniita Nikki? Mbona sikuelewi mwanangu mimi naitwa Deogratius”. Jamaa mwenyewe alikuwa ni funny guy flani hivi, yaani mtu anayependa utani, kwa hiyo huku anacheka akaniambia, “Mwanangu mimi jina lako naona gumu kukuita Deogratius, naona ni jina gumu naogopa kujing’ata. Mimi nakuita Nikki kwa sababu ya yule dem wako ambaye huwa nakuona naye mara nyingi alivyo umbile lake yaani anavyoonekana yuko kama Nicki Minaj”. So jina la Nikki ndio lilianzia hapo na kwa sababu ndio tulikuwa tunaanza chuo watu wengi hawanijua vizuri na yule jamaa alikuwa ni mtu funny, mwenye ucheshi na urafiki na kila mtu. Kwa hiyo jina likaja kuwa powerful, nikawa naitwa Nik, Nik na watu wengine wakajua mimi naitwa Nik hadi pale waliposkia jina langu la darasani kuwa naitwa flani, unaona?

Kwa hiyo ikawa imeenda hivyo na kama wanavyosema jina ukilikataa ndio mda mwingine ndio huwa linakua zaidi. Kwa hiyo baadaye ikabidi nilikubali. Sasa baadaye watu wakawa wananiuliza, “So wewe unaitwa Nik nani, labda Niksone au?’ Nikawaambia mimi siitwi Nicksone wala Nik nani. Nilikua nina jersery ya jamaa mmoja wa basketball (mimi ni mpenzi sana wa basketball) ya jamaa mmoja anaitwa Tim Duncan so nilikua naivaaga sana ile Jersey so watu wengine wakawa wananiuliza “Oya unaitwa nani?” Nikiwa nawaambia naitwa Nik Duncan kwani huyu mwamba nilikuwa namkubali. Lakini baadaye miaka ilivyoenda hadi tulipomaliza chuo nikawa nafkiria how to turn my art ili iwe kazi au kuwa biashara. Katika ku brainstorm namna ya kuweka model nzuri ya biashara yangu na jina nikafikiria it’s ok kutumia jina la Nik kwa sababu watu wengi wananijua Nik kuliko Deogratius. Kwa kuwa sanaa yangu inahusiana na kuona zaidi ndipo hapo nikafikiria kuongeza Visions ikawa NikVisions, umeona eeh? Hapo ndipo jina la NikVisions lilipopatikana mpaka leo. Kwa hiyo hiyo ndio historia fupi ya NikVisions.

Lakini hili jina halikuishia hivyo kuitwa NikVisions ikabidi niliwekee maana kibiashara kwa hivyo kwa ile NIK – N - Native I - Infinity K – Knowledge ambayo inakupa Nartive Infinity Knowledge ambayo Native inamaanisha kitu halisia au kitu kile chenyewe, Infinity ni kitu ambacho hakina mwisho wala mwanzo na Knowledge ni maarifa ambayo mimi au mtu mwingine anaweza kuyapata kwa kujifunza kwa watu wengine, kujisomea na kadhalika. Kwa hiyo NIK ni Nartive Infinitive Knowledge yaani maarifa halisia yasiokuwa na mwisho.

Kwa hiyo NikVisions sanaa yangu ni ya kuona, ninafanya graphics inaonekana, nachora inaonekana, kitu kama hicho. Kwa hiyo, hiyo ndio maana ya NikVisions.

Kuhusu kujihusisha na nini kiujumla huwa tunajihusisha na sanaa ya ubunifu kwa ujumla kama vile kufanya kazi za uchoraji na ubunifu, aah pia tunafanya kazi za utengenezaji wa kazi za mikono (handcraft), vile vile tunafanya kazi za uchapishaji wa vitu na bidhaa tofauti tofauti kama vile nguo na vitu vingine ambayo ni vya kiofisi au vya ki stationary.

Pia tunafanya consultation ya art and creativity yaaani ushauri wa kibunifu na kisanaa lakini pia tunatoa mafunzo kwa watu wanaopenda au wengependa kujifunza moja ya kazi za kibunifu. Kwa mfano hivi majuzi tumekuwa tukifunza watu ku design graphics kwa hiyo tuna madarasa ambayo tunakutana na wanafunzi kwa appointment ya ku design ila pia kuna wale wanaopenda kujifunza kuchora. Kwa hiyo mbali na kutoa hizo huduma pia tunafundisha watu wengine ili waweze kuwa na kile kitu ambacho tunacho waweze kuwa nacho ili waweze kukiendeleza.

Pia tunajihusisha kutengeneza content za kibunifu za watu wengine, yaani tunafanya kazi za project za watu wengine, yaani ni miradi ambayo sio ya Nikvisions ila inahitaji ubunifu. Yaani hua tunashirikiana na watu mbalimbali kufanikisha miradi tofauti tofauti ambayo ni ya kibunifu; hapa tunaweza kutoa ushauri, tunaweza kutoa huduma ya ku design au ya kuchora au whatever ambayo sisi tunaweza tuka input.

Tueleze kuhusu mchango wa utamaduni wa Hip Hop kwa sanaa yako na mchango wako wa sanaa yako kwenda kwa utamaduni huu wa Hip Hop. Je umehusika kwenye miradi gani ya wana Hip Hop na kwa njia ipi?

Mchango wa Hip Hop katika sanaa yangu; kwa kifupi naweza kusema kuwa Hip Hop ina mchango sana mpaka hapa katika sanaa yangu kwa sababu Hip Hop inaweza kunikutanisha na watu tofauti ambao leo hii ninafanya nao kazi ambao leo hii nime connect nao kwa sababu ya Hip Hop. Kwa hiyo Hip Hop ina mchango mkubwa sana kwenye sanaa yangu kutokana na kujihusisha katika namna moja au nyingine mimi na utamaduni huu nimeweza kukutana na watu tofauti ambapo leo hii wengine wamekuwa ni wateja wa biashara yangu, wengine wamekuwa ni washiriki ama patners ambao ninafanya nao kazi pamoja kibiashara lakini watu wengine inakua watu ambao ninafanya nao kazi na nimeweza kuwapata katika kujihusha na huu utamaduni wa Hip Hop.

Kwa hiyo Hip Hop ina mchango sana kwangu kwa sababu kwanza imeniletea watu na siku zote wanakwambia mtaji mkubwa ni watu, vitu vingine vinafuata.  Hip Hop imeniletea watu kiasi kwamba leo hii hata nikienda Morogoro huwa siwazi kwa sababu najua nitakutana na watu ambao ninafahamiana nao kwenye utamaduni, sawia na kama nikienda Mwanza. Kwa hiyo Hip Hop imenifanya nijiskie kama nchi nzima ni nyumbani na imenipa confidence ya kufanya zaidi na zaidi. Vile vile pia nimejifunza kupitia Hip Hop, kwani kuna watu wengine ambao ninashirikiana nao kazi ambao ni wana utamaduni au wana muziki wa Hip Hop wamekuwa na msaada mkubwa kwangu kwani wamekuwa wakiniongezea ubunifu kutoka labda na kumfanyia project yake anaweza kunipa ushauri kuhusu vitu ambavyo mwanzoni sijawahi kufkiria kuwa kinawezekana au sijawahi kufikiria kama mimi naweza kufanya. Kwa hiyo wamenipa new insights, kwa hiyo Hip Hop bana ina mchango mkubwa kwenye sanaa yangu na mchango wake hauwezi ukaelezeka kiharisi lakini ni mchango ambao ni mkubwa sana na unaendelea kuwepo.

Nikisema kuhusu mchango wa sanaa yangu kwenye Hip Hop, yes ofcourse. Kama Nikvisions, sanaa yangu nina mchango sana kwenye utamaduni wa Hip Hop kwa upande mwingine kwa sababu nimeweza kuhusika katika miradi tofauti ki utamaduni ya ki Hip Hop.

Ki haraka haraka moja ya miradi yangu niliowahi kuifanya ni KiNaSa Wazi (Kitaa Na Sanaa), Mbeya. Wakati wanaanza msimu wa tatu nikaona kuna mapungufu ya kuwa na ile nembo/logo. Kuna jamaa yangu alinicheki anaitwa Emmanuel Mushi pamoja na Paul Matrix wanakiambia wanahitaji nembo ya KiNaSa Wazi. Haikuwa rahisi kutengeneza nembo ile kwani ilinichukua 3 days ndio nikaipata, kisha nikawatumia wakaipitisha. Kwa hiyo kwa kuona nembo ile ambayo nilishindwa kuiwekea bei na mimi nilikuwa shabiki wa KiNaSa Wazi sikuwalipisha chochote, nilifanya for love. Napenda na nashkuru kuwa hadi sasa nembo ipo na inatumika hadi sasa na watu wanai appreciate.

Tukija upande wa miradi ambayo nimehusika kwa upande wa Hip Hop, nakumbuka nishawahi kuhusika kwa miradi ya wasanii mbali mbali kama Fivara ambae nilihusika kuunda jalada la mradi wake wa kwanza ambao unaitwa Fikra Ni Vazi La Rap ambayo ilitoka mwaka 2018 nikishirikiana na jamaa mmoja yuko Kitunda hapa, mshkaji wangu anaitwa Tuki Arts, lakini vile vile miradi mingine ambayo nimeweza kufanya kuna Nala Mzalendo ambaye nimehusika kwenye miradi yake tofauti lakini kuna lile chata la Nala Mzalendo Uhalisia ile pia ni kazi ya NikVisions, pia kuna miradi kama Nani Kama Mungu wa Rasta Michael ulitoka 2018/2019.

Kuna miradi ya Trickson Knowledge, Miracle Noma, Adam Shule Kongwe ambaye mpaka sasa naendelea kufanya nae kazi, kuna Micshariki Africa, kuna watu kama Boombap Clinic (B.B.C), hawa jamaa tumefanya nao project nyingi tofauti. Kuna project yao ishatokaga miaka ya nyuma inaitwa the Drum Ape, pia merchandise ya BBC kuanzia ile logo yao mpya na merchandise zao za sasa hivi tunafanya Nikvisions, halafu pia kuna jamaa zangu wako Mbeya wanaitwa Underground Gangsterz Crew (UGC), kuna watu kama akina Trickson Knowledge, Genry Ukokola, Daz P Mwafrika, hawa wote nishafanya nao kazi.

Kuna jamaa anaitwa Dizzle White Mkatili pia nishawahi kufanya nae miradi, kuna jamaa anaitwa Zero Budget Emcee anatokea UGC pia, kwa kifupi miradi ipo mingi na kwa kuitaja kwa haraka haraka mingine naweza nisiikumbuke.

Kwa hiyo huo ndio mchango wa Nikvisions kwa namna moja au nyingine kwenda utamaduni wa Hip Hop.

Tueleze kuhusu haya machata yenu Hatua na Nartive African, nini story ya machata haya, yanapatikana wapi na kwa bei gani?

Kwanza kabisa ningependa nieleze Nartive African halafu nitakuja Hatua. Nartive African ki historia ni nembo ambayo nilii design wakati nikiwa chuo, mwaka wa pili kwenye kipindi darasani, sijui kilikuwa ni cha hesabu. Nilikuwa napenda kukaa sana back bencher na wakati somo lilikuwa linaniboa ilinikuta nime sketch ramani ya Africa ambayo ilikuwa ina mizizi, kitu ambacho sikukifikiria ki ukweli kisha nikaachana nayo.

Miaka ikawa imeenda nikawa nimemaliza chuo na chata nikawa bado ninalo ila kuna siku wakati napitie zile sketch zangu nikaikuta nikafikiria sana kuwa naweza nikaifanyia nini. Siku zilipoenda ndio nikapata hilo wazo, Nartive African, ikawa ime fit kabisa na ule mchoro kabisa, yaani Nartive na ile Africa ikawa imekaa kama ina mizizi ambapo Nartive African inamaanisha Mzawa Wa Africa. Nartive African nili design 2015.

So kuna wakati nimesafiri nimetoka Mbeya nimeenda Dar na Fivara. Wajua Fivara ni mmoja ya watu ambao wana mchango sana kwenye sanaa yangu, ni mtu ambaye nimefanya nae kazi kwa ukaribu kwa mda mrefu so kipindi hicho nikamuonesha design mbili tofauti. Akaniuliza nina mpango gani na haya machata na kisha akaniambia kuwa hii ni biashara na inabidi tuyaingize sokoni. Namwamini sana Fivara huwa ananishauri vitu ambavyo mara nyingi akinishauri vitu huwa vinaleta impact so nikafanyia kazi na rasmi tukaziingiza sokoni Nartive African by 2018 na hadi leo ipo.

Tukija kuelezea maudhui ya Nartive African, maudhui yamejikita kwa mtu kuwa proud of being African. Vijana wengi huona kwamba mwafrika ni mtu ambaye amelaaniwa, au ni mtu ambaye ni wa chini sana, au kuwa mwafrica ni kitu cha kukataa, au kuwa mwafrica ni kitu cha bahati mbaya, lakini ukweli being an African is a blessing. Kwa hiyo Nartive African inamkumbusha mwafrica hasa kijana wa Africa kujivunia kuwa mwafrika, kwamba ukijivunia utaipenda Africa na hivyo basi utaendeleza na kutengeneza future nzuri kwa ajili ya Africa kama ambavyo walivyofanya baba zetu na babu zetu kama vile Marcus Garvey, Nyerere, Nelson Mandela, Kwame Nkurumah. Hawa wote walikuwa ni Nartive Africans . Hili chata nilimhusu yoyote yule ambaye ni mu Africa na ana sense of responsibility for his country and continent ya kubadili bara lake.

Ikija chata la Hatua naomba nielezee kwanza historia ya Hatua halafu nielezee maudhui yake; kwenye historia kwanza hili neno Hatua ni neno ambalo lipo kwenye lugha ya Kiswahili na linatumika kila siku kwenye mazingira tofauti. Mimi nilipata wazo au nilitamani kuwe na wimbo ambao unaitwa Hatua ila kwa bahati mbaya mimi sio mwanamuziki. Hilo wazo nikamshirikisha Fivara nikamuomba kama anaweza kufanya wimbo unaitwa Hatua, akaafiki. Fivara akaunda ule wimbo kisha ukaja ukatoka 2018 na ilikua track nzuri ambayo bado inaishi na itaendelea kuishi. Wimbo huu upo kwa platform za muziki.

Baada ya hapo muda ukawa umeenda kisha Fivara akaja na wazo la kuwa Na brand nyingine tofauti na Nartive Africa ambayo tutaiita Hatua na hapo ndipo chata likazaliwa baada ya mimi kufanya design na mzigo kuingia sokoni rasmi 2020.  Brand ilipokelewa vizuri na mashabiki na watu kibao walikua interested na sisi lengo letu target yetu ilikua ni vijana ila tukaja kugundua sio tu vijana wanapenda kuvaa tu hatua bali hata wazee na akina mama na watoto.

Maudhui makubwa ya Hatua ni kwamba kila kitu ni Hatua as long as kila kitu unachokifanya kina hatua zake; huwezi kufikia mbili pasipo kuanzia moja na kila mtu ana Hatua zake. Kila mtu ana define hatua ama mafanikio kulinga na mtazamo wake na mahali aliposimamia lakini hakuna mtu ambaye hapigi Hatua as long as anaishi.

Tukija kwa upande wa upatikanaji wa hizi bidhaa zetu ni kuwa hizi bidhaa zinapatikana kwangu mimi binafsi na pia kwa kupitia Fivara pia. Kwa upande wa bei zipo tofauti ila kwa T-shirt huwa tunaanzia shilingi 25000 na pia tuna hoodies 40,000Tshs, ma sweater/jumper 35000Tshs, long sleeves T-shirts 30,000Tshs, short sleeves 25,000Tshs. Mtu anaweza pia akaweka order mtandaoni na bidhaa zetu tunazituma sehemu yoyote pale Tanzania na hata nje ya nchi. Karibu tuwahudumie kwani bidhaa zetu ni za hali ya juu ambazo zinaendana na thamani ya pesa.

Unaweza kutu follow kwenye mitandao yetu ya kijamii na kupata bidhaa zote hizi kama vile Nikvisions na Hatua (Hatua_tz) na pia kwenye page ya Nartive African (nartive_african).

Swala la ajira limekuwa changamoto kote duniani, je vijana unawashauri nini kuhusu kukuza vipaji vyao ili kuweza kujiajiri?

Ajiri imekuwa ni changamoto duniani kote, sio Tanzania au Africa tu. Mimi ushauri wangu kwa vijana ni kwamba inabidi wao watambue kwanza kuwa wanataka nini kwani huo ndio mwanzo wa kupata kile unachokitaka. Vijana wajifunze, wakuze vipaji vyao, wajifunze kwa watu waliotangulia, wasiishie tu kubweteka, waende huku na kule, waangalie ni namna gani wanaweza kutoka walipo ili kuendeleza sanaa yao au vipaji vyao ambavyo wamezaliwa navyo kwa sababu kila mtu ana kipaji chake. Kwa hiyo mwisho wa siku kama mtu mmoja akiweza kujisimamia vizuri katika kipaji chake atakuwa amemaliza swala la ajira kwake na ataweza kuwasaidia watu wengine akawaajiri. Rai yangu ni kwamba vijana tusidharau kitu tulicho nacho ni kitu kikubwa kama una kipaji chochote aidha ni mwanamuziki, unachora na kadhalika shikilia ulichonacho.

Na vile vile pia tuweze kutumia vizuri hizi teknolojia ambazo tunazo ili kuweza kuuza bidhaa zako popote pale duniani. Kwa hiyo ukiamua kubweteka unakaa mtaani tu na kusema kuwa wewe umesoma chuo na kuwa hauna ajira na umekaa tu unalalamika huyo kaamua mwenyewe kwani leo hii kila kitu kipo na unaweza amua ukafanya muziki, kuna mitandao ya kijamii na unaweza kufanya kazi zako na mtu bila hata kuonana nae ana kwa ana na akakulipa na mambo yakaenda freshi tu. Tujifunze mtandaoni, sio lazima uende ukakae darasani kwani kama unavyoona hakuna mfumo rasmi inapokuja maswala ya muziki, sanaa, kuchora na kadhalika, ila haimaanishi kuwa hizi elimu rasmi hazipo la! Mtu anaenda YouTube na akajifunza freshi tu. Tutumie kile tulichonacho.Tukitumie vizuri, tukikuze, tukiendeleze kilete impact na kilete matunda.

Kazi yako ina changamoto zipi na unakubaliana nazo vipi?

Changamoto ya kwanza ni kutopatikana malighafi au ukipenda raw materials za kufanyia kazi kwa mfano rangi, canvas. Wakati mwingine inakulazimu ununue mtandaoni au uagize nje ya nchi. Mda mwingine ukizipata hapa kwetu ukizipata kwa quality nzuri ila unakuta gharama ipo juu na ukija ukitengezea labda bidhaa na ikakamilika huoni sasa utauza shilingi ngapi hivyo unakuta ni hasara kwako.

Changamoto nyingine pia ni kwamba watu wanakuwa sio waelewa, wateja wengi, jamii. Unakuta mtu anasema umbunie nembo na kabla ya kazi unampa ile quotation anaona kama unamuibia kuwa umemtajia bei kubwa. Wanarahisisha sana uundaji wa nembo na hawaheshimu au hawa appreciate au hawajui thamani ya kazi ambayo mtu amekuwa anafanya ya kibunifu.

Halafu changamoto nyingine ni ile tu kutolipwa kwa wakati. Unakuta umemfanyia mtu kazi vizuri ameridhika, ume deliver ndani ya muda ila inapokuja swala la malipo mtu anakulipa kidogo kidogo akisahau kwamba wewe ume invest muda, pesa zako pamoja na ujuzi mpaka ile kazi inakamilika. Kwa hiyo wateja wengine wanakuwa ni wakorofi wanakulipa kidogo kidogo na sio eti kwamba hawezi kulipa, basi tu inakuwa ni changamoto ya kazi tunachukulia hivyo.

Vitu vingine inapokuja kwa changamoto ni kutopata kazi katika mashirika makubwa pamoja na serikali. Kwa mfano nimeenda kuomba kazi kama Nikvisions na sina mtaji wa kutosha ila nina uwezo wa kufanya kazi nzuri ila fursa inaniponyoka na kwenda kwa kampuni kubwa yenye uwezo zaidi.

Serikali pia nilikuwa naomba kwa upande mwingine iweze kuliangalia hili ili sisi watu wa chini tuweze kunufaika na hizi tender za serikali. Kwa mfano kupata tender ya serikali labda ya ku print au kuchora ni vigumu sana kwasababu wao wanaamini mimi ni mdogo ki mtaji ila sio ki uwezo. Ndio maana unakuta watu wengi wenye vipaji wanaachana na sanaa kwani wanaona haiwalipi kutokana na hali kama hizi. Hizi ndio baadhi ya changamoto kwenye hizi kazi zetu ndugu yangu ingawa changamoto ni nyingi.

Ili kuweza kufanikisha zoezi la uchoraji huwa unatumia vitendea kazi vipi?

Ili kuweza kufanikisha swala la uchoraji vitendea kazi vinategemeana na kazi ninayoenda kufanya. Kama naenda kuchora ukutani labda nitatumia rangi ya maji au mafuta (acrylic) na brush. Pia kuna michoro mingine ya ukutani watu pia wanatumia spray, vile vile kuna michoro mtu anachora kwenye canvas, kwenye board, kwenye karatasi na unaweza kutumia karatasi, brashi rangi.

Vile vile kuna michoro ambayo ni soft copy kama vile nembo ambayo vifaa ni PC na software na wakati mwingine unatumia graphic tablets ni device unachora kwenye tablet unaona kwenye screen.

Kando na shughuli hii ya sanaa unafanya kazi gani nyingine ili kuweza kujikimu kimaisha?

Mbali na kazi na sanaa hakuna kazi nyingine ninazozifanya ili kuweza kujiongezea kipato, mimi kazi yangu ni sanaa yangu. Kipato changu huwa nakipata kutoka kwenye sanaa yangu sema ninaweza kui extend zaidi ili nipate kipato zaidi. Nisipo design leo graphics kesho nitachora, nisipochora kesho nitamfundisha mtu kuchora, nisipomfundisha mtu kuchora nitamfundisha mtu ku design. Nisipo mfundisha mtu ku design kuna hizi merchandise zetu, leo nitauza Nartive Africa kesho Hatua. Pia kuna machata mengine ambayo nafanya na watu wengine ambao wanafanya kazi na mimi kwa hiyo nisipo print nguo nitaunda bracelet, nisipofanya kazi za mikono naweza kumpa mtu ushauri kuhusu brand yake, pia ni content creator naandika content tofauti tofauti. Sanaa yangu nimeweza kui extend kidogo nimewekeza kwenye vitu tofauti tofauti.

Je unaona kama sanaa yako inapewa thamani na heshima inayostahili?

Naweza kusema ndio na hapana kwa wakati mmoja. Ndio kwa sababu kwanza kile kitendo mtu kunitafuta mimi Nikvisions kuwa anataka kununua machata yangu ni heshima tosha, na pia mtu kunitafuta kuwa anataka tufanye nae kazi flani ni heshima tosha, kwani kitu changu kina thamani flani na ndio maana amenitafuta kwa kiasi chake kwa upande mmoja.

Lakini pia kwa upande wa pili nikisema hapana ni kwa vile watu wanavyoichukulia sanaa na kutoipa heshima yake na kutothamini unachokifanya. Kwa mfano mtu umemfanyia kazi ila hakulipi unachostahili na akalalamika na kutokuonesha appreciation. Au ukamfanyia kazi mtu na asitake kukulipa kabisa na akapotea mazima na hapo mahusiano yakaisha kabisa.

Lakini vile vile niongelee upande wa hapana kuwa sanaa haipewi heshima inayostahili hususan sanaa ninayofanya mimi (ya uchoraji) ni upande wa serikali na jamii ki ujumla. Serikali imekua ikiwaaminisha watu na watu wengi wamekuwa wakiamini kwamba msanii Tanzania ni yule anayefanya maigizo na mwanamuziki tu. Wasanii wengine kama mimi hatutambuliki.

Ndio tumejisajili BaSaTa kule na tunalipa ada ya kila mwaka ila serikali haijaweka kipaumbele kwenye sanaa ya wachoraji na wabunifu wengine. Imewekeza sana nguvu kwenye sanaa ya wanamuziki na filamu, kitu ambacho sio sahihi kwa sababu kama msanii akihitaji kutoa wimbo au video atamuhitaji mtu wa graphics  kwa namna moja au nyingine sawia na msanii wa bongo movie na hawatambuliki na serikali ilhali wao ndio wana shoot zile video. Kwa hiyo kwa upande mwingine serikali haitendei haki sanaa ya Tanzania kwa sababu imeigawa na kuidogosha sana sanaa na imesahau kwamba sanaa ni pana kama bahari.

Serikali haiwezi ikafanya kila kitu ila ikaweka mazingira sawa kwa kila msanii lakini inatakiwa iwape kipaumbele wana sanaa kama mimi au ikawapa mazingira mazuri kwa mfano inapokuja kwa upatikanaji wa malighafi, masoko mazuri.

Ni nini kinachomfanya mwana sanaa awe mbunifu mzuri na je wewe unafanya nini ili kuweza kuwa tofauti na wabunifu wengine wanaobuni kama wewe?

Kinachomfanya mwana sanaa awe mbunifu ni kuwa mbunifu, hakuna njia nyingine mwana sanaa awe mbunifu. Ukiona mwana sanaa ni mbunifu jua yeye ni mbunifu, hakuna namna nyingine. Na kitu ambacho kina mtofautisha mwana sanaa mmoja na mwana sanaa mwingine ni vitu vingi lakini pia nia namna ya mtu anavyochukulia kazi yake.

Kwa mfano kama mimi kinachonifanya niwe mbunifu ni kuwa kwanza naichukulia kazi yangu kuwa ni kazi ambayo ni endelevu yaani ni kitu ambacho kinaendelea kukua. Nikisema kitu ni endelevu ni kitu ambacho kinaendelea kukua yaani kwamba nimetoka sehemu flani nikafika nilipofika ila naendelea kukua. Kwa hiyo sanaa ni kitu ambacho kipo kwenye movement. Kwa hiyo kama mwana sanaa kila siku unatakiwa u move. Una move vipi? Una move kwa kujifunza kwa watu wengine, watu waliokutangulia.

Pia kinachomfanya mwana sanaa awe mbunifu ni kushirikiana na watu wengine, wana sanaa kama yeye lakini pia hata pia watu wengine wanaomzunguka, wanaofanya nae kazi. Kwa mfano ukimskiliza mteja hakikisha na unamskiliza anataka nini na ana maanisha nini vita ku boost creativy/ubunifu wako kwani anaweza kukupa wazo nawe ukaliwasilisha vyema kwenye aidha mchoro au wimbo wako. Pia ni muhimu kuwasikiliza watu unaofanya nao kazi. Pia msiache kujifunza na pia usiache kuwa original, yaani sio lazima tuige. Tujiamini kwa kile tunachofanya. Ukitaka uwe tofauti basi lazima ufanye kitu tofauti na lazima ujiamini na usiogope kukosea.

Kitu kingine kinacho limit creativy ni kuwa watu wengi wanaogopa sana kukosea lakini the good news and bad news ni kwamba kwenye creativity hakuna kukosea wala kupatia as long as mtu yuko open kujifunza.

Kipi cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza?

Ni kwamba pia kupitia chata letu au brand yetu ya Hatua tuna platform yetu ya kusoma na kujisomea vitabu ambayo inaitwa Hatua Book Club. Kwa sasa inapatikana kwenye platform ya WhatsApp na ni community ambayo ina watu zaidi ya 250 ambayo mle ndani tuna share na ku recommend vitabu mbali mbali, kusoma, na pia tunajadili mada ambazo zinaendelea kwa wakati husika. Lakini pia Hatua Book Club ambapo watu tunakutana watu tofauti na ningependa kuwaalika kama mngependa kujiunga nasi tuwasiliana katika mawasiliano ambayo ni +255 659 896 374. Ukinicheki nitaku add au kukutumia link itakayokupeleka kwa group au tuta ku add kule. Pia mtu anaweza kuwasiliana na Fivara ambaye namba zake ni +255 769 477 219. Vile vile hizo namba za simu zinaweza kutumika kupata bidhaa zetu za Hatua na Nartive African na huduma zozote zile kutoka NikVisions. Sina kingine cha kuongeza, nishkuru kwa mda wako.

Asante sana na ningependa kushkuru Micshariki Africa kwa ujumla kwa kazi hii ngumu na kuweza kutufikia sisi wabunifu wa Africa Mashariki na kutu elimisha na pia vile vile kutuburudisha. Mnafanya kazi kubwa sana. Hongera kwako kaka Kefa (MkoKeNya) pamoja na team nzima ya Micshariki Africa kwa niaba ya kama mimi NikVisions na team yangu nzima, nasema asante, asanteni sana kwa mda wenu.

Shukran sana NikVisions kwa mda wako, najua wasomaji wetu pamoja na waskilizaji wetu watakuwa wamejifunza mengi kutoka kwako na tunashkuru sana kwa kuweza kuitikia wito wetu na kuweza kupiga gumzo nasi.

Asante.

Mcheki Nikvisions kupitia mitandao ya kijamii;

Instagram: nik.visions
Instagram: hatua_tz
Twitter: Hatua_tz
Facebook: Hatua