Nuru Bahati

Akiwa ni mtu aliyeanza  sanaa tangu utotoni, Nuru Bahati amefanikiwa kwenda na wakati kwa kuzidi kuwa mbunifu na sanaa yake. Enzi hizo akiwa shule ya upili aliweza kuchora akitumia kalamu ya wino (biro au bic). Michoro yake ilimuwezesha kushinda tuzo kadhaa na kutambulika kama mtaalam anayechora kwa kalamu za wino.

Nuru ameweza kukuza kipaji chake hadi amekuwa mtaalam wa michoro ya kidijitali. Mbali na uchoraji, Nuru ni mshairi, mwanaharakati na pia ni mfadhili anayependa kusaidia, kuinua na kuipa sauti jamii inayo mzunguka akitumia vipaji vyake. Hichi ndicho humpa furaha zaidi ya yote maishani mwake.

Tulipata fursa ya kupiga naye story ili kuweza kumfahamu vizuri mwanasanaa huyu…

Nuru Bahati ni nani?

Nuru Bahati ni mwanasanaa.

Historia yako ni ipi na unafanya nini maishani mwako?

Historia yangu ni kuwa mimi napenda sana sanaa na napenda kuinua maisha ya watu sana.

Tueleze kidogo kuhusu Nuru, ulikulia wapi na utoto wako pamoja na historia yako Ki masomo

Nilizaliwa na kukulia Mombasa na toka utotoni nilipenda kuchora baada ya kuona vibonzo kwenye magazeti.

Pia nilisomea somo la sanaa (Art & Craft) pale shule ya msingi ya Sacred Heart Mombasa na pia kusomea somo hilo hilo nilipoenda shule ya upili ya Sacred Heart ambayo pia ipo pale Mombasa

Kisha nilisomea Stashahada ya miaka mitatu ya Fine Arts and Painting pale Buru Buru Institute of Fine Arts mjini Nairobi.

Kwanini uliamua kuzamia kwenye shughuli za ubunifu (designing)?

Niliamua kuwa mbunifu kwani ni shughuli inayonipa furaha na mimi hufurahia ninapobuni au kuunda kitu kipya.

Unajihusisha na sanaa/ubunifu  gani?

Nafanya shughuli za kuunda nembo(logo), picha za watu za kidigitali, pamoja na mabango ya kielektroniki (electronic/E-posters)

Baadhi ya kazi za nembo za Nuru

Je umefanya miradi yoyote na wasanii wa Hip Hop?

Ndio, nimefanya kazi na msanii wa Hip Hop Fikrah Teule mpango unaitwa YETU uliokuwa na maana hiyo hiyo iliyonuiwa.

YETU lilikua jukwaa lilioandaliwa ili kutoa nafasi salama ya kujadili na kuhamasisha uelewa  wa jamii kando na Kutoa fursa kwa wana spoken word pamoja na kinasa huru pamoja na kufanya shughuli za Hip Hop.

Kando na wasanii wa Hip Hop je umeshafanya miradi na wasanii wa tasnia zingine za mziki?

Ndio nimewahi kuunda mabango kwa ajili ya matamasha ya mashairi pamoja na nembo zinazo watambulisha.

Kwenye  shughuli nzima ya biashara ya ubunifu ni kipi hukugusa sana wakati upo katika zoezi la kubuni?

Ni muhimu kuelewa  maono na dhamira ya mteja na kisha kuyaweka vizuri pamoja na huduma yake au bidhaa yake kwenye soko analolilenga.

Ni ujumbe gani unadhamiria kufikisha wakati unafanya kazi yako?

Kitu ambacho ni rahisi kueleweka ni rahisi kuuza.

Je kazi yako hulenga kusema chochote kuhusu jamii inayokuzunguka pamoja na hali ya kisiasa?

Inategemea  kama nimeshamaliza kazi za watu nilizokabidhiwa kisha naweza pata muda kubuni sanaa zinazoongelea jamii yangu.

Ni kipi kilichokuvutia sana hadi ukaweza kujikita kwenye shughuli za designing?

Ukweli ni kwamba urahisi katika muundo husaidia sana katika kufikisha ujumbe kwa suala la urembo na utendaji.

Ni kipi hukusukuma na kukupa morali ya kuendelea na kazi hii ya kubuni?

Kinachonisukuma ni kuwa kila faida ninayopata huenda kuinua jamii inayonizunguka na pia mteja anaporidhika  baada ya kuona maoni yake yametimia kwenye kazi aliyonipa.

Je umeajiriwa au umejiajiri na una studio yako binafsi ya kufanyia kazi?

Nimejiajiri,  na ni msanii wa kujitegemea anayefanya kazi kutoka nyumbani kwani kazi zangu zote zinafanyika mtandaoni.

Nini kinachomtofautisha Nuru na wabunifu wengine?

Huwa namaliza miradi yangu yote ndani ya muda na pia ni muaminifu kwenye nyanja zote za biashara! Pia kazi zangu ni rahisi kueleweka na ni safi.

Uliwezaje kukuza kipaji hiki hadi sasa ambapo kinakupa mkate wako wa kila siku?

Kwa kuthubutu kila siku na kubaki kuwa mwanafunzi wa sanaa kila iitwapo leo.

Unapataje fursa za kazi?

Kwa kuongea na watu na pia kwa kuwasaidia kwenye miradi yao.

Kazi zako hupatikana kwa bei gani?

Kazi inategemea na mradi, idadi ya michoro inayohitajika kwenye mradi na pia kaisi cha muda kitakacho tumika kwa mradi huo na bajeti.

Je kwa ujio wa sanaa ya kidigitali unadhani kuwa sanaa ya mkono ndio itaanza kupotea?

Sanaa ni soko, chochote ambacho mtu anauza kutatokea mnunuzi aliye tayari kununua. Pia kuna soko linalo tutosha sisi sote.

Ni nini unatakiwa kuwa nacho ili uweze kuzama kwenye shughuli hii na kuifanya vizuri?

Nidhamu na dhamira.

Je umewahi kufanya miradi nje ya Kenya? Ni mafunzo gani muhimu uliyoyapata ambayo unaweza kushiriki na msomaji?

Ndio, bado ninafanya kazi kwenye soko la ulimwengu katika sanaa ya picha za dijitali. Somo ni kwamba sanaa yako ni ya thamani zaidi huko nje na kuna watu ambao watakulipa kamili kabla mradi haujaanza.

Je umeshawahi kuonesha kazi yako kwenye exhibitions za sanaa?

Ndio nilishaonesha kazi zangu kule Dust Depo Nairobi.

Unapopata kazi unaanzaje kufanya kazi kwenye mradi mpya? Je! Unawazaje wazo kutoka mwanzo hadi mwisho wa mradi?

Ninakwenda na muhtasari wa mteja na kumuuliza mteja juu ya kazi ya hapo awali ambayo amependa na ambayo inaweza kujumuishwa katika mradi wake.

Yote ni juu ya mawasiliano mazuri ya kila wakati.

Inakuchukua muda gani kumaliza kazi za mteja?

Vile mteja anavyonipa taarifa zaidi kuhusu kazi anayotaka nifanye pamoja na kulipa mapema basi inakuwa rahisi kufanya kazi haraka”

We huanzaje siku yako?

Huwa naanza siku yangu na maombi.

Je unapenda nini juu ya kubuni na uliwahi kufikiria kuwa msanii?

Ninapenda utafiti na maana nyuma ya miradi yote ambayo imefanikiwa na ina athari nzuri kwa tamaduni.

Sanaa ni upendo na upendo ni maisha.

Je kuna kazi ya sanaa au mradi ambao umefanya ambao unajivunia zaidi ya miradi yote?

Kama nimeweka tabasamu kwenye uso wa mtu kazi yangu imekamilika!

Mbali na kazi za sanaa na ubunifu je una vipaji gani vingine?

Sanaa ndio chanzo cha furaha yangu. Pia napenda kupanga hafla na kuandaa mipango tofauti inayoshirikisha jamii.

Ungetoa ushauri gani kwa yeyote yule anayetaka kufuata nyayo zako na kuwa designer?

Anza na uwe mwanafunzi kila siku.

Ungependa kusema nini cha mwisho ambacho sijakuuliza?

Natumai wasanii wataweza kulipwa kwa kila mahojiano wanayofanya kwani msanii aliyekufa hahitaji pesa.

Tuzidi kusaidia na kuinua biashara ya mtu mweusi.

Wasiliana na Nuru Bahati kupitia;

Facebook: Nuru Bahati
Facebook: Biro Art
Twitter: nurubahati
Instagram: nurubahati
WhatsApp: Nuru bahati +254721267239
Email: Nurubahati@gmail.com