Uchambuzi Wa EP: Overdose [EP]
Msanii: Nyenza Emcee
Tarehe iliyotoka: 06.01.2020
Nyimbo: 4
Muunda Midundo/Mtayarishaji: Mtata
Mixing Na Mastering: Mtata
Studio: Soweto Records
Nyenza Emcee
Japokua mradi huu umetoka mwaka 2020 niliona ni vyema ni uchambue kwani ulinigusa sana. Baada ya kuanza kupata kazi toka kwa jamaa flani wanaojiita Vichwa Vya Habari, nilianza kuwafuatilia na ndipo nikapata neema ya kununua EP hii ya emcee Nyenza iitwayo Overdose kwa buku tano (Tshs 5,000.00 au Kes 250) tu hela ya kitanzania.
Mradi huu ambao Nyenza alifanya chini ya VcW ulisimamiwa na producer Jerry Mtata anaefanyia shughuli zake Soweto Records, Kahama kwa sasa. Mradi huu ni moto, mashairi, ubunifu mwanzo mwisho.
Dose ya kwanza ya mradi huu ni wimbo Sub Concious ambapo kwenye mdundo mzuka Nyenza anaanza kuonesha kujiamini kwa anachofanya akisema,
“Wengi wanafanya ili kujithibitisha/
Mi hua ninafanya ili kujiimarisha/”
Wimbo huu una mashairi yanayo kufanya na wewe pia ujiamini kando na kukupa fikra chanya kuhusu maisha yako,
“Ukikubali madini ninayokupa/
Utaanza kutafakari ni kwa nini unajuta/
Hakuna zali mjini ni kutafuta/
Ukikwepa makali ndio mpini utavuta/
Mikono yenye ganzi haikamati maisha/
Sub conscious hadati anadatisha/
Ukipenda uwazi haki atakufikisha/
Jino la mzazi haling’ati linatisha/”
Baada ya kumaliza na mstari huu, “Mbu hua mfalme kwenye neti japo mdogo” anakuambia kuwa wewe pia ni wa maana sana kwani,
“Sauti ya kwako/
Sauti ya kwangu/
Wote kwa pamoja ndio sauti ya mtaa/”
Dose ya pili toka kwa mradi huu ni Jana Mchana ambao ni wimbo wenye kusikitisha, ucheshi, elimu na hadithi mzuka sana kuhusu ukeketaji, Jana Mchana. Mtata anatubariki na mdundo mzuka sana wakati Nyenza akituonesha uwezo wake wa kutuhabarisha akitumia hadithi. Kwenye beti ya kwanza unao vile emcee huyu anaweza kukuchorea picha kamili ya tukio akitumia mashairi yake akisema
“Mnatangaza mambo ya uchekeshaji/
Leo ninaangaza jando na ukeketaji/
Mke pambo isiwe usengenyaji/
Make sure hili ua linalo chanzo cha maji/
Pale chini binti alivyoinama/
Kama niimbwe mimi na hizo nyimbo za laana/
Akili za mjini ndipo zikaulizana/
Hawakuamini kua nilivyo watawanya/
Hip Hop ni leader kukemea utapeli/
Hua tuna haiba ya kutetea ukweli/
Nikawa jibwa njoo nikung’ate kweli/
Ndipo yule ngariba kisu chake kikafeli/
Shujaa nakuja tusumbuane/
Nyoyo zenye usaha nakuja tutumbuane/
Kisa hujamzaa si lazima mtengane/
Heshima ikifaa si lazima mpendane/”
Dose ya tatu ni wimbo mzuka sana unao kutia moyo na kukuinua kwa kukuambia kuwa kila kitu kipo sawa sawa kwenye Sawa Sawa 2. Aisee hapa Mtata alibariki mashairi ya Nyenza kwa sauti za wanakwaya pengine toka Kahama. Kama kawa mashairi ni mwanzo mwisho ila yaliyonigusa sana ni,
“Je ni kweli utayapita majuto/
Je una sindano ya kuyatisha maputo/
Bora uwe moto wawe na picha ya fusho/
Au kuishi kwa kwa picha ile kuisha kupo/
Hukumu huja na nyaraka/
Jukumu lako kubwa ni kupunguza mashaka/
Jua tunu haitakuja kwa haraka/
Kigumu na kikubwa hukaa kwenye pakacha/
Kifo kweli ndio puto la buriani/
Ni pozo la kweli kwa fukuto la duniani/
Penzi la tapeli ni majuto ya njiani/
Kwa sababu tu upendo wa kweli upo nyumbani/”
Na kwenye ubeti wa pili,
“Kufanya yote bila ya kufikiria/
Utataka yote bila ya kuzingatia/
Mwisho wa yote uje kupotea njia/
Usipate lolote huko ulipokimbilia/
Kwenye mia mbili tumia hamsini/
Labda nikupe siri kuhusu mia ya mkini/
Ukishapata dili je kiufatie nini?/
Lengo niwe tajiri nisaidie maskini/
Nataka nawe uwe mtu wa kati/
Kwenye kupanga mawe kuujenga mkakati/
Fursa zigawe zitengeneze bahati/
Ndipo sandakalawe itakuja kwa wakati…/"
Au
“Tumebarikiwa medulla ya onyo/
Kuna kukubaliwa na kuna sura ya No-No/
Usije kuvimbiwa chakula cha ngono/
Lengo likizaliwa jua chakula ni nyonyo/…”
Sawa Sawa 2…
Dose ya nne na ya mwisho ni wimbo mzuka sana uitwao Mgumba ambapo emcee Nyenza anaweka wazi penzi lake kwa mke wake ambae hajabarikiwa kuzaa. Mstari mmoja tu nitanukuu hapa unaonesha thamani anayompa mke wake mgumba akisema,
“Mgumba siku zake zote ni salama…/”
Mradi huu ni msingi mzuri unaonesha hili; watu wanapoungana kwa kuunda kitu na kila mmoja akasimama kwa zamu yake matokeo huwa chanya sana. Kongole kwa Nyenza Emcee, Jerry Mtata(Soweto Records) na Vichwa Vya Habari kwa mradi huu ambao japokua ni mfupi (nyimbo 4) ni mrefu kwa urithi mliotuachia mashabiki wa Hip Hop.
Kupata nakala yako ya EP hii wasialana na Jeremy kuptia:
WhatsApp: +255743884065
Instagram: jeremy_vcw