Justine Kakoko

Justine Kakoko enzi hizo akitambulika kama GSP(Great Sense and Power) ni mmoja kati ya Emceez wakali sana kuwahi kutokea, kwa aliyepata kusikiliza albamu yao ya DIRA kutoka After Pain Records atakubaliana nami kuwa, kwa nyimbo kama Kengele, Sauti, Maswali, Nasema Na Wewe, Nimechoka Kusikia na Silence kwa hakika wametendea haki maana ya neno Emcee.

Albamu hiyo ya DIRA imejaa miongozo ya kila aina kwa Mwafrika na uafrika wake

Ni muda sasa tumeshuhudia Justine Kakoko akijihusisha zaidi na ushairi na kuipa kisogo Rap…

Kunani nyuma ya Pazia

Justine Kakoko anasema Rap na Hip Hop ndivyo vimemkuza na kumpa ufahamu zaidi hata ya walimu shuleni/darasani, kifupi hajawahi kuiacha na hawezi kuiacha ila kwa sasa ameamua tu kujikita kwenye ushairi lakini zipo Project nyingi za Rap ambazo ameshirikishwa zinakuja.

Kakoko anasema zipo sababu nyingi zilizomfanya kwa sasa aegemee kwenye ushairi zaidi ya Rap.

Kwanza, kabla ya yote yeye ni mshairi tangia zamani, kwa sasa alichoamua ni kukitumia tu kipaji chake na ukizingatia nchini kwetu washairi wa kisasa ni wachache kwa hiyo pia ameamua kuongeza nguvu upande huo.

Kakoko anaendelea kusema “Ushairi unaniruhusu kuyaelezea mawazo yangu au mambo mbalimbali ninayoyajua kwa kina zaidi, Ushairi unanipa uwanja mkubwa katika uwasilishaji na sibanwi sana na vitu kama midondoko, urefu wa wimbo wala bunifu mbalimbali zinazotakiwa kwenye Rap.

Na zaidi ni kwamba, niliamua kuua(kuondoa) uburudani kwenye sanaa yangu ili nibakize elimu pekee, hapa lengo kuu ni kuiondoa ile hadhira inayopenda burudani ya kutikisa kichwa kuendana na midundo ya Rap pasi na kuzingatia chochote kile kinachohusiana na maudhui ya ndani ya Sanaa”

Shairi la kwanza kuandikwa toka kwa kakoko lilikuwa ni “HATUFUNDISHWI SHULENI” Shairi lililoelezea madhaifu ya mfumo wetu wa elimu na kushauri nini kifanyike kuboresha, shairi hili aliandika mwishoni mwa mwaka 2013.

Kiujumla mapokeo ya kazi yake ya ushairi yalibashiri mwanzo mzuri, kwani alipokea ujumbe na simu nyingi kutoka sehemu mbalimbali toka kwa ndugu, jamaa, marafiki au kwa mashabiki wakieleza kuguswa kwao na kazi zake, huku wakiuliza masuala na hoja mbalimbali kutoka katika mada alizoziibua katika ushairi wake.

Kakoko anasema kwa sasa hatua aliyopiga kiuelimishaji ni kubwa sana kulinganisha na ilivyokuwa enzi ya Rap, kwani ushairi wake umekuwa ukisikilizwa na watu wote bila kuchagua rika na anafikiri hali haikuwa hivi katika Rap kutokana na picha iliyotengenezwa na wahusika wa ushairi na Rap na jamii nzima kiujumla kwamba, muziki wa Rap ni kwa ajili ya vijana na watu wa mtaani peke yake.

Kakoko anasisitiza kuwa asingeweza kuwafikia watu wengi kwa kiasi hiki cha sasa kama angekuwa kwenye Rap.

Kakoko anasema kuwa ushairi umemjenga sana kiuandishi na kifikra, kwani ili uandike juu ya mada fulani katika ushairi inakupasa uzame ndani haswa na kuchimbua kisha kuchambua kwa kina na kiyakinifu huku ukifanya tafiti mbalimbali na tafakuri za kina kabla ya kuandika.

Kakoko amepata nafasi ya kughani mashairi yake kwenye majukwaa mbalimbali ya kitaaluma kama vile shuleni na vyuoni haswa na wakati mwingine huwakilishwa na kusomewa mashairi yake. Na pia ameweza kuhudhuria majukwaa mbalimbali ya kitaifa kama vile jukwaa la Siku Ya Mazingira, na tena ameweza kuwafikia watu mbalimbali wanaojifunza na kuelimika kwa kazi yake na hii imepelekea kuongeza hadhira ya watu wengi sana ambao wanampenda na kumuheshimu kupitia kazi yake ya ushairi. Haya ni mafanikio makubwa.

Akiwataja kwa uchache tu baadhi ya washairi ambao amekuwa akisikiliza sana kazi zao ni pamoja na Mrisho Mpoto, George Kyomushula, Zuhura The African Lioness, Mama C na Vital Maembe.

Kakoko anapatikana kwenye mitandao ya kijamii

Facebook: Justine Kakoko