Malle Hanzi, "Kawaambie Madogo"
Msanii: Malle Hanzi
Wimbo: ‘Kawaambie Madogo’
Album: Kitabu
Utangulizi
Ukonga Mombasa.
Taratibu Malle anatembea kuelekea studio kwa Ray Teknohama, safari hii haikuwa ya lengo la kurekodi bali kuwafanyia mahojiano P the Mc na Zaiid ambao walimuarifu kuwepo pande hizo za Bantu Record, hiki kilikuwa ni kipindi Malle akikamilisha uandishi wa kitabu cha “Chuo Kikuu Cha Hip Hop” hivyo alikuwa akifanya mahojiano ya hapa na pale na safari hii alikuwa na miadi na mapacha wasiofanana, P The Mc na Zaiid.
Ukaribu wake na Producer Ray ulikuwepo kitambo vile alishakutana nae mara kadhaa kwa Nash Mc lakini safari hii ukaribu huo ulizidi zaidi, na cha zaidi ni kwamba sasa wakawa wanatembeleana.
Baada ya kufika kwa Ray na wakipiga stori za hapa na pale huku Ray akipigapiga midundo, kuna mdundo mmoja Ray alivyoupiga tu Malle akahisi kuna kitu anahitaji kufanya katika mdundo huo, japo hakuwa amefanya ngoma kwa muda kidogo lakini mdundo huo ukamchangamsha damu, Yap Yap, akamwambia Ray….'bro, Stooop!! nahitaji huo mdundo niufanyie kitu!!' ndio huo mdundo wa Kawaambie madogo’ na hivyo ndivyo ulivyopatikana.
Malle akaanza kuuchorea mistari mdundo huo na baada kukamilisha akaenda kwa Ray kurekodi wimbo huo na ikawa pouwa mgoma huo ukakamilika.Malle akajikataa na wimbo wake ukiwa full wimbo huo uliitwa “Jina La Kitabu” ndio ni Jina LA kitabu.
Chuo cha Ustawi wa Jamii
Mwaka 2012 Malle akiwa chuoni hapo, ndio kipindi hicho anarekodi wimbo wa ‘Jina la kitabu’
Siku kadhaa mbele akiwa na Producer wake wakaona kama bado haijakaa sawia so wanakubaliana kama vipi waifanye tena hiyo ngoma ya ‘jina la kitabu’. Mambo yakawa yanaingiliana na ratiba za chuo na vile Malle alikuwa kwenye mitihani’ Semester ya 1’ kwa hiyo pilika pilika za chuo kama unavyojua kipindi cha mitihani ikapelekea Malle kushindwa kurudi tena studio kwa muda waliokubaliana.
Wazo La Wimbo
Siku moja akiwa ametoka kwenye mtihani, akitazama zile mishemishe za hapa na pale, purukushani za wanafunzi baada ya paper wengine hai wengine hoi akajikuta anashika peni na kuandika “Kawaambie Madogo’ kifupi idea ya kawaambie madogo ilichipukia katika mazingira hayo ya chuo na zaidi ilikuwa kipindi cha mitihani, ilichukua muda mchache tu katika siku hiyo Malle kumaliza kuandika mashairi ya wimbo huo na kwa kutumia mdundo uleule aliokuwa nao(aliofanyia Jina la kitabu) basi akaanza mazoezi ya hapa na pale, Siku alipoenda kwa Ray haikuwa kuifanya tena ‘Jina la kitabu’ bali ilikuwa ni kitu kipya kabisa ndio ‘Kawaambie Madogo’,
Changamoto
Changamoto kubwa kwenye kurekodi ilikuwa ni kukatika kwa umeme. Malle alikuwa akitoka Sinza kwenda Ukonga, ile akishuka kituoni tu umeme unakatika, anakaa hadi jioni lakini wapi, akiondoka tu umeme unarudi. Kukatika kwa umeme kwa kipindi hicho cha mwaka 2012 kilifanya Malle kutumia muda mrefu akila timing ya kurekodi hata akaja kufanikiwa ilikuwa si mchezo, na hiyo ni moja wapo ya sababu ngoma kuchukua muda mrefu maana plan ilianza mwezi wa 2 na ngoma ikaja kukamilika kwenye mwezi wa 4 hivi, na ndio mwezi huohuo Malle aliuachia wimbo huo kama "Zawadi ya Pasaka" kwa wapenzi wa Hip Hop.
Muda
Mzunguko mzima wa wimbo ulichukua zaidi ya Miezi 2 hadi kukamilika na hii ni kwa sababu kwanza., Japo Malle aliuandika wimbo huu kwa siku moja tu lakini kukatika katika kwa umeme ilikuwa changamoto kubwa, hii ilifanya Malle awe analia timing umeme hadi kuja kufanikiwa ilichukua muda kiasi.
Upande wa Ray naye pia alikuwa ana mgogoro na mmiliki wa studio hiyo ndio maana mwishowe ilimbidi kumkabidhi wimbo Malle bila kuweka bass katika mdundo wa wimbo huo.
Upande wa Nash Mc hiki kilikuwa ni kipindi akishiriki kipindi cha TV cha DalaDala hivyo alikuwa na ubize flani hivi ndio sababu ikamchukua kama wiki 2 hivi, pale alipopata wasaa akaenda kukamilisha mpango mzima.
Ushirikiano na Nash MC
Hapo kabla Malle hakupanga kumshirikisha msanii yoyote lakini baada ya kumaliza kuingiza verse zake na ngoma ikiwa studio siku moja Nash Mc alikuja hapo, alipoisikia akasema ebwanaee itabidi nifanye kitu hapa....kweli akafanya na ngoma ikatoka mchicha.
Malle alikuwa amepanga kwenye chorus kuwe na maneno tu."Nenda kawaambie Madogo, nenda kwaambie madogo" lakini Maalim Nash MC akaongezea "Waache kiburi Wapige Msuli hii ni HIP HOP"
Nafasi/Mchango wa Nash MC
Malle anasema ushiriki wa Nash uligeuza maana kwani Nash ni kama alihimiza zaidi katika kusoma na tena ukiongeza na ule mstari wa Malle 'wasidharau Veta wakitepeta Form 4" ndio kabisa wimbo ukaja kuwa kama "maalumu kwa wanafunzi" ndio maana wasomi wengi kwa sasa wamekuwa wakitumia wimbo huu kukumbushiana kuzingatia masomo kabla na pia huutumia kutiana moyo baada ya matokeo ya masomo yao.Hii imepelekea Malle awe anapokea jumbe na simu kila mara toka kwa wanafunzi hasa kipindi cha mitihani wakisema namna wimbo ulivyowa inspire katika kuzingatia elimu yao.
Kwa wengi wimbo umekuwa mwongozo katika maisha yao hasa upande wa elimu. Japo Nash amefanya kajisehemu kadogo tu katika wimbo mzima lakini impact yake katika wimbo huo ni kubwa.
Ujumbe Wa Wimbo
Ujumbe wa wimbo huu ni kuondoa 'Fikra hasi' kwa jamii na hasa rika letu la ujana ambalo katika makuzi yake linapita katika changamoto nyingi na kubwa za kukatisha tamaa, lakini tamaa haitakiwi kukatwa bali iunganishwe ili kufikia malengo ingawaje kuna wakati mwingine 'kutokata tamaa kwenyewe kunaweza kukatisha tamaa'
Katika kipindi ambacho nchi inashuhudia vijana wakiwa katika mkwamo wa matumizi ya madawa ya kulevya,wizi,uvivu na kuporomoka kwa maadili kwa kiwango cha kutisha 'Kawaambie Madogo' inakuja kama daraja la kuvusha na kuokoa kizazi potevu na potofu toka walipo na kuwaweka sehemu salama kifikra.Wimbo huu ni faraja kwa waliokata tamaa kwani unamulika tumaini lililopotea.
Nafasi ya wimbo kwa Malle
Kwa Malle'Kawaambie Madogo' ilifungua njia, sio tu Tanzania bali ilifanya afahamike hata nchi za jirani, sina shaka hata wewe unayesoma hapa sasa hivi inawezekana ulimfahamu kupitia wimbo huu,na kwa vile hii ngoma ilitoka kabla ya kitabu 'Chuo kikuu Cha Hop Hop' basi usikivu wake ulikuwa ni kama Promo kwa kitabu.
Mahusiano yake na watu mbalimbali yalichipua na kuimarika zaidi na zaidi na zaidi ni kwamba Mchumbake Malle yule mwenye rasta rasta alikuwa ni mmoja wa shabiki wakubwa wa wimbo huu japo sina hakika kama wimbo huu pia ndio uliofungua njia ya Mahusiano yao. Itoshe kusema tu 'Kawaambie Madogo' imechukua nafasi kubwa sana katika maisha ya Malle kisanaa
Kama ndio leo...angeufanyaje wimbo huo?
Malle anasema kama ndio leo angekuwa anafanya wimbo huu wa 'Kawaambie madogo' bado angeufanya vile vile kama alivyoufanya hapo awali, kwake wimbo umekamilika kila idara hivyo haoni cha kupunguza wala kuongeza. Na hilo linathibitishwa kwa jinsi jamii ilivyoupokea vizuri wimbo huo.
Malengo
Malle anasema "Malengo ya kuandikwa kwa wimbo huo yamefikiwa kwa kiasi kikubwa, ni zaidi ya asilimia 90 kwani ujumbe umefika na umeeleweka vyema...
zipo sehemu chache ambazo zilileta sintofahamu kwa shabiki kwa mfano pale ninaposema "Dogo janja, Usigome kama TUTKA//hauto manage kwa GANJA, ukiweza kamsome GUPTA//
Hapa wengi walidhani nimemlenga Dogo Janja wa TIP TOP ambaye kwa kipindi kile wimbo unatoka nadhani alikuwa anakimbia kimbia shule, na kuleta usela katika elimu lakini 'Dogo janja' ni jina tu ambalo nilitumia kwani ni jina maarufu na hutumika sana kimtaa mtaa na vile mimi nilikua naimulika mitaa hasa madogo basi nilitumia jina hilo nikilenga madogo janja wa kitaa ambao ni sehemu ya hadhira"
Msimu wa dhahabu
Ni zaidi ya Miaka 10 sasa tangu Malle atoe wimbo huu, Malle anasema kwa hisia kali sana kwamba kila anapousikia huu wimbo anakumbuka mbali sana. Anakumbuka siku ameenda kushuhudia mashindano ya freestyle pande za Sansiro Sinza ambapo Duke na Nash MC ndio walikuwa majaji, baadae Duke anamwambia Malle, "Kuanzia sasa wewe ni Tamadunist".
Hapo kabla walikuwa wana ushirika tu lakini sio rasmi, hii ni kabla ya Kilinge, ndio baadae sasa kinaanzishwa Kilinge. Malle anakumbuka zama za Tamaduni Muzik, enzi hizo Tamaduni ipo katika ubora wake, ulikuwa ni wakati mzuri sana kuliko nyakati zote zilizopata kutokea kwao, wasanii wote walikuwa wapo katika ubora mzuri, sio Nikki, sio Stereo yani ilikuwa ni full VIBE.. wasanii wakali producers hatari....ilikuwa ni full VIBE..
Mfuate Malle Hanze kwenye mitandao ya kijamii;
Facebook: Malle Hanzi (Hanzi at work)
Instagram:mallehanzi
Twitter: MalleHanzi
Pia unaweza kumfuate mwandishi wa makala haya Iddy Mwanaharamu;
Facebook: Iddy Mwanaharamu