P Mawenge

Msanii: P Mawenge
Wimbo: Mitaa Nayotoka
Album: Single

Karibu kwa safu hii ya Nyuma ya Pazia (NyP) upate mawili matatu kuhusiana na kazi ya P Mawenge - ‘Mitaa Nayotoka’

Twenzetu bro…Mambo niaje P? Hebu niambie mzazi, kwa nini ‘Mitaa Nayotoka’?

Fresh kabisa aisee…Mitaa Nayotoka kwa sababu ndio namna pekee niliyoichagua kuelezea mazingira (maisha) yangu ya mtaani na ya watu walionizunguka.

Hebu niambie bob, ulipataje pataje wazo hilo la kuandika kuhusu mitaa yako na uandishi wake ulikuwaje

Wazo la wimbo lilikuja mwaka 2016 na hii ni baada ya kupokea midundo tofauti toka kwa watayarishaji tofauti lakini kwa mrindimo wa mdundo niliopewa na Abby MP nikasema "humu sasa ndo pahala mahususi kwa lile wazo”.

Uandishi haukuchukua zaidi ya siku 3 lakini pia haukuwa uandishi wa mwanzo mwisho, kama uandishi wa nyimbo zangu zote ulivyo. Kwa wimbo huu ilikuwa kikija kitu cha wazo husika basi nakihifadhi mahala huku nikifikiria kingine, hata nikakamilisha wimbo.

Kwa nini Abby MP? Ushirikiano wake ulikuwaje na mlitumia muda gani kukamilisha kurekodi?

Halikuwa wazo langu kuwa ntafanya na mtayarishaji gani, bali nilikuwa nikiangalia upande utakaonipatia mdundo mahususi wa wazo langu na bahati hiyo ikaangukia kwa Abby MP. Ikumbukwe kuwa Abby MP amefanya miziki yangu kadhaa hivyo ushirikiano wetu ni bora kabisa ikizingatiwa mimi ni moja kati ya marapa wakali walio kwenye list ya Abby MP.

Nilitumia takriban mara tatu kurekodi huu wimbo na sababu ya hayo ilitokana na mic ya studio (Chatta Noga) kutatiza (changamoto) hivyo tukawa tunafanya kwa kulazimisha na kila Abby MP aliposikiliza kwa umakini aligundua mic inatia uchafu kwenye wimbo hivyo akawa ananipigia simu kunishauri turudie kurekodi na mara ya 3 ndipo tukapata tukitakacho.

Wimbo ulichukua takriban mwaka hadi kutoka na hii ilitokana na mimi kudai usitoke mpaka niuandalie mazingira ya video kabisa. Abby hakunipinga kwa kuwa pia aliamini ingeongeza utamu wa wimbo zaidi na ndivyo ilivyokuja kuwa.

Nini hasa ujumbe uliolenga kuufikisha kwa jamii?

Ujumbe wa Mitaa Nayotoka ni, kwanza kwa jamii kuona uhalisia wa mazingira anayoishi P The MC wanayemuona kwenye matamasha na kwenye Tv na mitandaoni na kumsikia redioni tu mara kwa mara bila kujua ni mtu anayeishi mazingira gani kiuhalisia na jamii anayoishi nayo ni ya namna gani.

Pia kuzionesha sekta zihusuzo mipango ya kimaendeleo nchini kuwa hata kwetu (Kiwalani) kuna haja ya kuboreshwa miundo mbinu lakini pia kuingizwa kwenye mipango ya kimaendeleo (kina mama wapewe mikopo ya biashara zao, watoto wasizurure na kuwa waporaji bali wapelekwe shule na wakubwa watafutiwe mazingira ya kujipatia vipato).

Na pia nimetumia mitaa ninayotoka kama kielelezo cha hali halisi ya sehemu nyingi nchini, kwa hiyo nimewakilisha na kilichobaki ni kazi ya wenye dhamana kuangalia vipi wata deal na sehemu husika kwa changamoto na fursa kufanyiwa kazi.

Uliyaonaje mapokeo ya wimbo huo kwa jamii?

Mapokeo yalikuwa makubwa saaana kwa sababu kwa takwimu nilizopokea ni kuwa ndio wimbo pekee unaofanya vizuri mitaani hususani kwenye mitaa ifananayo na hiyo iliyozungumziwa kwenye huo wimbo (yaani mitaa yangu). Kwa kuwa ndani ya nchi inayoendelea kama Tanzania mazingira hayo yapo maeneo meeengi sana.

Je una chochote cha kukumbuka kuhusiana na wimbo huu?

Cha kukumbuka kuhusu wimbo huu, kwanza ndio wimbo wangu pekee uliochezwa kwenye vituo vingi vya redio na televisheni bila wao kuupata toka kwangu (yaani waliutafuta wenyewe baada tu ya kuusikia kwa sababu wazo langu halikuwa uwe wimbo wa kwenda *media*) na ulinipa mahojiano mengi kutokana na wengi kuwa na shauku ya kutaka kujua kama ni kweli au utunzi tu. Pili ndo video pekee yangu inayoonesha sura za watu niliokua nao baadhi tangu utotoni na mitaa niliyokulia kuoneshwa (kumbukumbu ya kudumu).

Una lolote la kumalizia kuhusu Mitaa Nayotoka?

Ni wimbo ambao unaweza kuwa unafanana kimaudhui na nyimbo nyingi tu lakini utofauti mkubwa unaotakiwa kutambulika na kuheshimika ni kuwa umeandikwa kwa namna ya tofauti sana na hizo zingine hasa kwa kuhusisha vina mkupuo kwenye kila mstari mmoja (multi-syllable rhymes) na hii ni kwa wimbo mzima tena bila kupoteza maana.

Shukrani sana kwa ushirikiano wako bro

Shukrani kwako pia kwa kunipa nafasi hii.

Mcheki P Mawenge kupitia;

Facebook: P Mawenge
Instagram: pmawenge
Twitter: pmawenge

Pia mcheki Iddy Mwanaharamu mwandishi wa makala haya kupitia;

Facebook: Iddy Mwanaharamu