Obby Mjuzi ni kijana anaevaa kofia nyingi; ni mzazi, ni mwalimu wa uchumu na hisabati, ni mtaalam aliebobea kwenye mambo ya TEHAMA(Technologia ya Habari na Mawasiliano) au kwa kimombo IT.

Kando na haya Obby ni mwana Hip Hop ambae amehusika kwa kuunda jalada za albam za ma emcee wengi waliopo handaki ya Tanzania wakiwemo Watunza Misingi, Teddy Boombap, Wasadikaya, Mfalanyombo, Adam Shule Kongwe, Lugombo na Momumo MaKaNTa nk. Kando na hili Obby ni emcee mwenye uwezo wakuchana nakukuacha kinywa wazi.

Leo tumepata fursa yakufanya mahojiaon nae ili tumfahamu vizuri kaka Obby Mjuzi.

Historia yako ni ipi? Unajishughulisha na nini kimaisha?

Kwa majina naitwa Theophil Obeid Kassian, ni mtoto wa pili kati ya watoto wanne, yaani nipo mimi na dada zangu watatu. Ninajishughulisha na kazi za teknolojia (ni mmiliki wa kampuni iitwayo WATU MAKINI TECHNOLOGIES, pia ni mwalimu wa sekondari kwa masomo ya hisabati na uchumi.

Nembo ya Watu Makini Technologies

Niambie kidogo kuhusu Obby Mjuzi, umetokea wapi ulikulia wapi, utoto wako ulikuwaje,umesomea wapi umefikia wapi mpaka sasa?

Kama nilivyosema hapo awali jina langu halisi ni Theophil Obeid Kassian nimezaliwa jijini Dar Es Salaam na nimekulia huko na kusomea huko pia. Maisha yangu ya utoto yalitawaliwa na michezo tu, mimi nilikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu, kwa watu wa mbagala na police barracks watakuwa wananifahamu vizuri. Kwa upande wa elimu mimi nina Diploma ya IT, Degree ya Uchumi, na Post Graduate ya Education,  zote kutoka St Augustine University of Tanzania.

Eimu ya msingi niliipata katika shule tatu tofauti kutokana na baba yangu kuwa mtu wa kuhamahama kikazi, nimesoma shule ya msingi Kizuiani, Mgulani na Kizwite,  elimu ya sekondari nimesoma shule mbili yaani shule ya Sekondari Jamhuri(iliyopo Dar kidato cha kwanza na cha pili) na shule ya Sekondari Kizwite (iliyopo mkoa wa Rukwa kidato cha tatu na cha nne)

Jina la OBBY MJUZI nilipewa nikiwa kidato cha tano katika shule ya sekondari Kibiti Boys (iliyopo mkoa wa Pwani) huko nilikuwa vizuri sana  kwenye Mathematics hapo nikabatizwa majina mengi wengine waliniita Calculator wengine wakaniita Mjuzi, hapo jina la Obby Mjuzi likakua zaidi na likaendelea kukua hadi chuo. Jina lilizidi kuwa kubwa zaidi mara baada ya kumaliza chuo, nilipoamua kuanza kufundisha Teknolojia online kupitia YouTube, blog na private website.

Nilifungua darasa la online nikawa nafundisha na nikawa nalipwa pesa. Nikaenda mbali zaidi nikatengeneza APP yangu ambayo niliiweka playstore na watu waliipakua ili kuendelea kujielimisha kupitia mimi.

Kwanini uliamua kuwa Graphics designer?

Ninaweza kusema mimi nilizaliwa na nililetwa duniani kuwa mtu wa IT (Information Technology) na designer, maana pamoja na vyote nilivyosomea mimi ninapenda kazi za IT na designing kuliko chochote.

Kwenye shughuli hii ya designing mimi napenda kubuni kila kitu lakini napenda zaidi kubuni logo (nembo au chata/machata) maana huwa zinanipa tafakari zaidi na hunipa muda wa kuongeza uwezo wangu wa kufikiri.

Kazi zangu zote huelezea hisia halisi iliyotarajiwa na mteja na kuna muda huwa nafanya zaidi ya kile mteja alikuwa anawaza, nadhani hii imenisaidia sana kunitofautisha na ma designer wengine.

Kwenye jamii kazi zangu zimekuwa zikitumiwa kufikisha ujumbe mbalimbali kwa hadhira kusudiwa, mfano katika kipindi cha Covid 19 nimekuwa nikishiriki kufanya kazi za taasisi mbalimbali kuwaelimisha watu juu ya kujikinga na Covid 19.

Je ni nani aliyekuvutia pakubwa  kwa mambo ya designing na kukupa hamasa ya kuwa graphics designer? Pia, ni nini hukupa hamasa na motisha ya kudesign?

Kiukweli mimi kwenye hili sina mtu aliyenivutia kwenye graphics design, mimi nilianza mwenyewe baada ya kusoma vitabu vingi vya teknolojia na kugundua kwamba dunia ndipo inapoelekea, na kwa kuwa mimi napenda maisha haya ya teknolojia basi ilikuwa rahisi kuingia huku na kuishi. Kitu kinachonipa motisha ya kudesign ni meditation (hali ya kutafakari), mi huwa nakaa na meditate na kutengeneza picha ya kile nnachotaka kubuni kichwani halafu ndio nakiwasilisha kwenye computer.

Tuelezee kidgo kuhusu kazi yako, ni nini unahitaji kuwa nacho ili uweze kufanya kazi vizuri?

Kwa upande wa designing hitaji kubwa ni laptop au desktop yenye uwezo wa ku support softwares, kwa upande wangu nikipata yoyote kuanzia Core I5 inatosha kabisa. Ila kwenye upande wa printing (kutoa chapa) ni muhimu kuwa na printer zenye uwezo.

Umekuzaje kipaji hiki mpaka kuwa  kuweza kukupa ajira?

Mimi huwa nasoma kila siku, ndio maana tuna kaulimbiu yetu inasema,”Jifunze kila kitu jifunze kila siku”. Kwahiyo siri kubwa ni kusoma na kujifunza bila kuchoka.

Je unapataje fursa?

Mi huwa natumia door to door system, yani naenda kila ofisi najitambulisha, najieleza na nawaonesha sampuli za kazi zangu , hapo huwa sikosi watu wanaovutiwa na kazi zangu na kunipa tenda.

Kazi hizo hupatikana kwa bei gani?

Bei huwa zinatofautiana kulingana na aina ya kazi, maana huwa tuna kazi za designing na printing.

Kwa upande wa logo designing ni Tzs 80,000/= ila za Hip hop ni Tzs 50,000/=, brochure Tzs 30,000/= flyers, product labels, posters Tzs 20,000/= ilhali album covers TZS 20,000/=.

Ilikuwaje hadi kufikia kufanya kazi na ma Emcee wa Hip Hop toka Tanzania? Umewahi wafanyia kazi akina nani?

Kufanya kazi na ma emcee wa Hip Hop ilikuwa rahisi kwa sababu mimi pia ni muumini wa huu utamaduni, kwa hiyo kupitia groups za WhatsApp niliwaonesha watu nnachofanya na wengi wananifahamu kuipitia lile darasa langu la online maana wengi ni wafuasi wangu. Kiukweli ni ngumu kuwataja wote niliofanya nao kazi maana ni wengi sana kwa uchache tu nimefanya logo ya Watunza Misingi, Wasadikaya, MaKaNTa na Wanaboma.

Pia nimefanya album cover na cover za nyimbo za ma emcee wengi wa handaki, kwa uchache nimefanya  kazi na Lugombo, Momumo, Adamoe, Adam Shule Kongwe, Miracle Noma, Testa Tungo Tata, K Wa mapacha, Mfalanyombo, Nash Mc, Vioxee Dede(toka Kenya), Gsp, Ghost The Living, Albeez, Colins MaKaNTa, Jedi Kuoga Mtawala (RIP), Hostzee, Teddy Boombap, Salu Tee,  na wengine wengi. Ninaweza kusema nimefanya kazi na 80% ya watu wa Hip Hop.

Je wewe mwenyewe ni emcee?

Ndio mimi ni emcee na nina kazi nyingi nilizotoa mwenyewe na nyingine kushirikiana na ma emcee wengine. Nimefanya nyimbo kadhaa zikiwemo Mwambie, It’s all about time, Sisikii, Hiyo siku ikifika pt 1 na pt 2 ambazo ni special project nk.

Design ya jalada la album unapopata kazi huwa unaanzaje kuliunda? Unapataje wazo kutoka mwanzo hadi mwisho? Na huwa inakuchukua muda gani hadi tamati?

"Wazo la kazi ya albamu huwa linatoka kwenye lengo kuu la kazi na ujumbe kusudiwa, hapo mimi huweza kutumia jina la album au wimbo uliobeba jina la album, lakini pia huwa namtafuta muhusika kwa simu ili aniambie wazo lake yani aliwaza nini kuipa album yake jina hilo.

Baada ya kupata hayo basi huwa najipa muda wa ku meditate na kutengenza wazo kwenye lugha ya picha, hii huweza kunichukua siku moja hadi tatu kulingana na ugumu wa idea husika."

Wewe huwa unapenda kusikia mziki napofanya kazi? Kama jibu ni ndio huwa unasikiliza mziki gani?

Ukija ofisini kwetu kuanzia mwanzo tunafungua ofisi mpaka jioni tunafunga ofisi ni Hip Hop tu na spoken word!.

Siku yako huanzaje?

Siku yangu huanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu halafu baada ya hapo naendelea na ratiba iliyobaki jana. Kama hakuna basi huwa natengeneza ratba ya siku husika.

Je kuna kazi uliwahi kufanya huwa unajivunia mpaka leo?

Kiukweli kazi zangu zote huwa nikizona navutiwa nazo sana kwahiyo hakuna kazi ambayo naona ni bora saana kuliko nyingine.

Tofauti na kazi hii ya designing una kazi gani nyingine?

Kama nilivosema hapo awali mimi ni mchumi, IT, na mwalimu, kwahiyo mbali na kazi za designing mimi ni mwalimu wa sekondari kwa somo la Mathematics na Economics, pia huwa natoa ushauri wa biashara yaani business consultancy, pia natengeneza websites na blogs pamoja na Apps na kazi nyingine za IT.

Tueleze kidogo kuhusu kitabu

Ni kweli kwamba nipo katika hatua za mwisho za kuachia kitabu changu kinachoitwa Psychology Of Color Made Easy. Kama nilivyosema nimekuwa mwalimu wa graphics design kwa muda mrefu sana kwahiyo ninayajua matatizo mengi ya madesigner na watu wanaotamani kuwa madesigner.

Kwenye kitabu hiki nimezielezea rangi kiundani sana, yaani uhusiano uliopo kati ya rangi na rangi, matumizi ya rangi, maana za rangi kibiashara na kisaikolojia na mambo mengine mengi.

Una ushauri gani kwa designer anayeanza?

Ushauri wangu ni kwanza ajue kwa nini anataka kufanya designing, pili ajipe muda wa kuisoma graphics design kwa undani na kuijua vizuri asisome juu juu, tatu ajue kwamba designing ni chaguo sahihi sana kwake kwani akiifanya vizuri inaweza kumlisha yeye na familia yake pia kumpeleka kwenye maisha ya ndoto zake.

Kipi kingine ungependa kusema ambacho sijakuuliza?

Ninapenda tu wateja wetu wote wajue kwamba graphics design ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, hivyo wateja watuheshimu na watulipe iliostahili yetu maana watu tunalipa kodi za ofisi na makazi pia na tunalipia watoto ada, na kulea familia zetu na wazazi wetu kupitia hii hii graphics design. Asante.

Mfuate Obby Mjuzi kwenye mitandao ya kijamii:
Facebook: Obby Mjuzi Mtu Makini (obby mjuzi)
Instagram: obbymjuzi