Oscar William Masanja aka Odilla Beatz

Kwa mashabiki wa Hip Hop mwezi wa Februari huwa special sana. Wakati watu wengine  wanausubiria mwezi huu kwa sababu ya Valentine’s Day wana Hip Hop husherehekea mwezi mzima kama Dilla Month.

J Dilla Month ndio mwezi ambapo wana Hip Hop humuenzi producer James Dewitt Yancey ambaye anajulikana kwa jina la usanii kama J Dilla au Jay Dee. Producer huyu ambaye alijulikana sana kutokana na mtindo wake mpya wa kuandaa midundo alizaliwa Februari 7 1974 na kufariki Februari 10 2006 kule Marekani.

Japokuwa J Dilla ametuacha, kazi zake kibao alizotuachia zimewahamasisha watayarishaji kibao duniani kama vile Odilla Beatz ambaye ni mzaliwa wa Mwanza, Tanzania. Odilla Beatz nilianza kuskia midundo yake kwenye miradi ya ma emcee kadhaa na nikaona ni vyema tumkaribishe mtayarishaji huyu ili tuweze kujua je, Odilla Beatz na J Dilla ni mtu na ndugu yake?

Karibuni.

NB: Kama ungependa kuskia podcast ya gumzo hili nenda mwishoni mwa makala haya utaikuta.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Odilla. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu jina lako rasmi ni nani?

Shukrani sana bro, kwa majina naitwa Oscar William Masanja. Hilo ndo jina langu official kabisa ndo jina nalotumia sehemu nyingi kama jina langu la siku zote.

Unatokea wapi au unawakilisha Hip hop kutokea wapi?

Asili yangu mimi ni mtu wa Mwanza, Msukuma. Mzee wangu ni Msukuma ilhali mama ni Mnyakyusa, ila kwa sasa ninaishi  Dar Es Salaam, hivyo basi Hip Hop yangu naiwakilisha kutokea Dar Es Salaam.

Odilla unajishughulisha na nini?

Kwa sasa mimi nimeajiriwa kwenye mradi wa Stieglers Gorge kama lab technician kwa hiyo shughuli zangu za kikazi nazifanyia huko.

Jina la Odilla lilikuaje? Pia ningependa kujua wewe una signature tune au jingle inayoweza kumjulisha mtu kuwa mdundo anaopiga ni wa kwako?

Jina la Odilla limetokea hapa

O- hii inawakilisha jila langu ambalo ni Oscar.

D- Nikikupa historia yangu ya nyuma miaka ya nyuma kabla sijaanza kazi ya muziki nilikuwa napenda ku downlod instrumentals kwa hivyo mara nyingi nilikuwa nikikutana na washikaji zangu na mashabiki zangu walikuwa ni watu wanaopenda kuchana sana na saizi yangu ambayo mara nyingi nilikuwa na wanangu kama akina Fivara na baadhi ya wasanii wengine ambao wana hit kwa sasa kama Rasta(Michael) kuna msanii mwingine anaitwa Mad Scientist pamoja na Swahili The Son.

Sasa muda mwingi nilikuwa na instrumental za J Dilla, 9th Wonder pamoja na Pete Rock. Hao ni baadhi ya ma producer ambao nilikuwa napenda kuwasikiliza sana tena sana, ila midundo mingi ambayo nilikuwa nayo na producer niliyekuwa namkubali mpaka kesho Rest In Peace ni Dilla (J).

Kwa hiyo mda mwingi sana nilikua namsikiliza J Dilla na pia nilipata mda mrefu sana kuuumiza kichwa  na nilitumia mda mwingi sana kuhusu J Dilla na pia nilitaka kujua producer huyo alikuwa anatumia technic gani na hilo likafanya mpaka watu wakaanza kuniita Odilla, hususan marafiki zangu wa karibu.

Kuhusu swala la signature tune au jingle ninayo ili watu waweze ku recognize hizi projects nimefanya mimi. Jingle yenyewe ina represent jina langu la kazi ambalo ni Odilla Beats. Kipindi cha nyuma baadhi ya projects zangu zilikua na signature.

Tueleze kidogo kuhusu historia ya nyuma ya shughuli zako za mziki au production?

Baada ya kumaliza tu Diploma yangu ya Civil Engineering 2016 hapo kati kati kuanzia 2016 hadi 2017 sikuwa na ishu ya kufanya, na nilijaribu sana kutafuta kazi lakini sikufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali za maisha. Muda mwingi sana nikaanza kujifunza kufanya production ya msingi kwa sababu ilikuwa kwenye damu na nilikuwa napenda sana, lakini sikuwa na nafasi ya kufanya ishu ya production kutokana na mambo yaliyokuwepo ikiwemo na shule nikaanza kuwaza baada haya kumaliza Diploma nikawaza nianze kazi ya production.

Kufanya hivyo nilikuwa na vitendea kazi kama Computer, kwa hiyo nikaanza mdogo mdogo kuanzia 2017 ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa ku download FL Studio na kuanza kufanya ishu ya production ya muziki. Mimi kama mimi kwa kupitia media mbali mbali kama YouTube nilichukua muda mwingi kujifunza jinsi ya kutengeneza biti na nini, unaanzaje. Pia nikasoma nakala mbalimbali, jinsi ya kutengeneza biti, jinsi ya ku finalize biti mpaka likamilike na mpaka linakamilika, hivyo basi nikasemaje, kama ma producer wengine wanaweza na walianza kama mimi je ni kipi kinashindikana?

Huwezi amini bro, mimi usiku wangu ulikuwa kama asubuhi na mchana nilikuwa silali, nilikuwa nalala kesho yake pakikucha, kwa hiyo nilikuwa nachukua mda wangu mwingi mwingi sana nikijaribu kujifunza vitu vingi sana kuhusu swala la production mpaka nikakamilisha mwaka mzima ambao ulikuwa 2018. Namshukuru Mungu mafanikio yangu yalikuwa ni mazuri kwa hiyo baada ya washkaji kunipa big up sana kwa kitu ambacho nilikua nakifanya na mimi nikapata energy ya kufanya vizuri zaidi Career yangu (ya mziki) ikaanzia hapo.

Mtu akitaka kuwa producer anatakiwa afanye nini au awe na nini ili afanikishe maono yake?

Kwa mtu ambaye anaanza kabisa na anataka kuwa producer kitu cha kwanza kabisa mimi ningemshauri awe na PC au anunue PC na pia atafute quality headphone kwa ajili ya audio production ambazo zitamsaidia kwenye swala la mixing. Namshauri atumie mda mwingi sana in a private way kwa sababu music production mda mwingi sana unahitaji space kwa sababu mda mwingi unakua unatumia kiungo cha skio kuskiliza kazi yako ambayo unaifanya.

Kitu ambacho anatakiwa afanye siku hizi tumerahisishiwa sana kwani kuna YouTube wana fundisha vitu vingi sana kuhusu audio production halafu pia kuna nakala nyingi sana Google na wameelezea vizuri sana kuhusu audio production.

Na pia akipende kitu anachokifanya wala asikate tamaa even though ni long process ila inabidi apambane mwanzo mpaka mwisho ili aweze kutimiza ndoto zake.

Unadhani ma producer wa Hip Hop huwa wanapata heshima wanayostahili? Je kwa upande wa kipato  kuwa producer kumekupa manufaa yoyote?

Ma producer wengi ambao wanafanya mziki wa hip hop wapo ambao wanaopata heshima inayostahili kutokana na kazi wanazozifanya na hata mifano tunaiona. Tuliona kipindi cha nyuma hapa Duke Tachez akiwa na akina Nikki Mbishi, Stereo, n.k baada ya wasanii hawa kuachia mixtapes au tape zao, Duke Tachez alipata jina kubwa na mafanikio na tunaona hata pia kwa Majani ambaye pia ni producer mwenye jina na ni icon na ni legend kwenye game ya Hip Hop. Tumeona kuwa amepata mafanikio makubwa tu na tuzo mbalimbali. Kwa hiyo it doesn’t matter kwa kitu ambacho unakifanya kama producer wa Hip Hop as long as unafanya kitu kizuri lazima utapata heshima yako ambayo unastahili.

Kwa upande wa kipato hiyo imekuwa ni changamoto kutokana na asilimia kubwa ya wasanii wa Hip Hop, sijui ni kwa nini ila asilimia kubwa ya wasanii wa Hip Hop wengi wana kipato cha chini sana, sana. Sasa mwisho wa siku ukija ukifanya kazi na mtu kama huyo obviously utapata kipato cha chini sana.

Sometimes naona ma producer wengine unakuta anafanya na msanii wa Hip Hop just for free lakini as long as mtu ana kipaji atafanyaje na anapenda Hip Hop. Kwa hivyo hiyo ni moja ya changamoto ambayo inawakuta ma producer wengi wa Hip Hop na hata pia mimi nishakumbana nayo sana tu. Kwa hiyo kipato kwa kweli ni cha chini sana.

Odilla umeshawahi kufanya kazi na emcee ganii au umeshawahi kuhusika kwenye miradi ipi?

Mpaka sasa oficial nimeshafanya kazi na wasanii takriban wa watano. Wa kwanza kabisa nimefanya kazi na Rasta Michael. Huyu nimefanya naye project kama tano au sita  ambayo moja tayari imeshatoka inaitwa Huu Sio Muda ambayo ipo kwenye albamu yake iliyotoka mwaka jana inaitwa  Nje Ya Dunia, pia kuna albam nyingine imetoka inaitwa Yedidia nimefanya naye ngoma kama tano hivi.

Msanii mwingine ambaye nimefanya naye ni Fivara kwenye hii EP yake ambayo ameachia hivi karibuni 259. Nimefanya ngoma moja ambayo inaitwa Katikati. Pia kuna wasanii wawili, mmoja anaitwa Gwiji huyu ni rapper/emcee. yupo kwenye single niliyoachia hivi karibuni inaitwa Cycle. Pia kuna msanii mwingine ambaye ni mdogo wangu anaitwa Hans D kwenye single niliyoachia ya Cycle. Mle kuna Gwiji na Hans D ambao nimewashirikisha mimi kama Producer.

Je wewe mwenyewe ulishawahi kutoa mradi wako mwenyewe kama vile beat tape, Ep mixtapes au hata albam?

Mwaka 2013/2014 niliachia ngoma zangu mbili kipindi hicho nilikuwa rapper. Kuna ngoma moja inaitwa Next Level ukiingia SoundCloud ipo utaipata pale Oscar D. Kipindi hicho nilikuwa nafahamika kama Oscar D and Hans De Tulifanya mimi na mdogo wangu inaitwa Next Level na pia kuna ngoma nyingine nishawahi kufanya inaitwa I Still Got It nilifanya mimi pamoja na wenzangu, Hans D pamoja na mwanangu mmoja anaitwa Tisha T au Tisha Terrible.

Kwenye ishu ya mimi kuachia beat tape au EP, Mixtape au albam bado ila niko kwenye mchakato huo mwaka huu, Mungu akinijalia uhai, maisha na afya kwa sababu nipo kwenye maandalizi ya kumaliza album yangu ya kwanza na nitakua nimewashirikisha wasanii mbali mbali. Nawakaribisha mashabiki wangu wote ambao wananifuatilia na kuniskiliza tayari kuskia album yangu ya kwanza kabisa ambayo nimefanya production ya audio nikishirikiana na ma producer wengine ambao wame base kwenye sound engineering na vocal mixing pamoja na wasanii ambao nimefanya nao kazi

Kwa hiyo itakua bonge moja la album na wata enjoy sana. Album inaitwa Try This Joint. Soon Mungu akisaidia nitaiachia.

Kando na mziki Odilla unajishughulisha na nini kingine ili kuweza kujikimu kimaisha?

Kwa sasa ni mwajiriwa kama nilivosema hapo nyuma na sina shughuli nyingine yeyote ambayo inaniingizia kipato zaidi ya mimi kuajiriwa kazini. Kwa hiyo ajira ndo maisha yangu ambayo yananiweka mjini kwa sasa na kuniingizia kipato.

Mbali na hip hop una produce aina gani nyingine ya mziki? je unapounda mdundo mchakato mzima unakuwaje?

Basically mi ni producer ambaye nime base sana sasa kwenye muziki wa Hip Hop. Utamfahamu vipi Odilla kwa kupitia mdundo wake? Cha kwanza kabisa ni drums. Mimi niko so selective sana when it comes kwenye ishu ya drums.

Nachaguaga instruments au circle za drums ambazo ziko realistic, ambazo hata unaweza ukazipiga live kwa hiyo mda mwingi huwa nachukua mda mrefu sana kuzichagua hizo drums na base sana kwenye ma producer wa zamani ambapo boombap ilianzia na walikuwa wanatumia drums gani. Kwa hiyo unakuta labda naweza nikachagua labda drums za J Dilla au nikachagua drums za Pete Rock au nikachagua drums za 9th Wonder.

Pia mpangilio wa drums unakuwa upo tofauti kidogo. Naweza nikaskia loops zao ila nitajaribu kutengeneza za kwangu mimi mwenyewe kwa hiyo huwa si base sana kwa mpangilio wa loops zao ambazo zilikuwa zinatumika ambazo ukigonga zinaweza zika sound the same. Kwa hiyo mara nyingi huwa natengeneza loops zangu mwenyewe na soon mambo yakiwa mazuri kabisa nitaanza kufanya loop making za drums pamoja na melody.

Kwa hiyo ikija kwa upande wa melody nachagua melody ambayo sio computerized. Nachagua melody ambazo unaweza ukazipiga live kama kinanda, trumpet, flute ambazo hata ukizigonga kwenye beat za boombap ina sound so natural kabisa.

Je una uwezo wa kupiga chombo chochote cha mziki

Kifaa ambacho naweza kupiga vizuri kwenye audio production ni piano ingawa  kwa sasa bado najifunza aina ya instrument nyingine kama gita na drums ila kwa sasa kifaa ambacho naweza kukipiga ni piano na naendelea kujifunza baadhi ya chords hadi chords zingine ili niweze kufika ile level ambayo nitaona hapa kweli naweza kufanya muziki wa aina yoyote.

Changamoto za shughuli zako ni zipi?

Changamoto inayotukuta sisi ma producer au producer kama mimi  ambao ndo tunaanza game ya mziki kwanza kabisa huwa ni vifaa. Hii inatokana na kuwa na uwezo binafsi wa kifedha ili kuweza kukamilisha studio yako mwenyewe

Je unamiliki studio yako mwenyewe au umeajiriwa kwenye studio yoyote ile?

Hapana, similiki studio wala sija ajiriwa kwenye studio yoyote kama nilivo nilivyoeleza hapo awali ninafanya kazi na rafiki yangu (Rasta Michael) kwa kupitia studio yake ambayo ipo maeneo ya Buza. Kwa hiyo kazi zangu nyingi nikitaka kufanya na wasanii nafanyia hapo kwenye studio ya Rasta na tayari nishaingia mkataba naye kwa hiyo wasanii wote  wakitaka kupata ladha za O Dilla wanakaribishwa Buza hapo, utanicheki kwa contact zangu ambazo zipo kwenye page ya Instagram ukitaka kufanya kazi na mimi tutafanya kitu kizuri sana ila kwa sasa sina studio.

Tutarajie nini toka kwako hivi karibuni?

Tutarajie vitu vingi sasa kwa sababu mwaka huu nimeweka target zangu ambazo nina uhakika asilimia mia kuna tape ambayo nimepanga kuichia hivi karibuni na ndani ya hiyo tape zilikua zimebaki kama track mbili ndio nikamilishe album. Na hizi track mbili wasanii wapo tayari na ndani ya mwezi huu wanamalizia recording kwa hiyo target zangu ni kati ya mwezi wa tatu au mwezi wa nne ila sana sana mwezi wa tatu nina uhakika nimeshakua nimemaliza

Na si album tu bali pia nitaachia pre instrumental tape ambayo itakua na ladha zote za beats za Odilla hiyo nitakua naifanya kila baada ya miezi 6 ambayo itakuwa na Vol. 1 na 2. Kingine, nitakuwa na session ya kila baada ya mwezi naachia instrumental moja baada ya nyingine na pia nitaachia tape za instrumental ambazo zitakuwa ni official just for business ambazo zitapatikana kwenye platform mbali mbali kwa ajili ya Hip Hop na zitakuwa ni kali kweli kweli.

Je ni kipi ambacho sijakuuliza ambacho ungependa kutuambia?

Brother natumaini umeniuliza maswali mengi ambayo watu wameweza kumfahamu Odilla kwa kina.

Shukran sana kaka Odilla kwa kukubali wito wetu na kufika kwenye jukwaa letu la Hip Hop la Africa Mashariki, Micshariki Africa ili tuweze kukufahamu wewe na shughuli zako zote za utayarishaji. Binafsi nimejifunza toka kwako na najua waskilizaji na wasomaji wa makala zetu pale kwenye tovuti yetu wataweza kupata madini flani kutoka kwako.

 Nashukru sana kaka asante sana  kwa interview yako Mungu akujalie kwa kitu unachokifanya naimani tutafika mbali siku moja na kuweka historia kwenye muziki huu wa hip hop. Shukran sana.

Wasiliana na Odilla Beatz kupitia

Instagram: Odilla_Beatz
Twitter: BeatzOdilla