Oksyde

Oksyde ni mmoja wa waimbaji walio na uwezo zaidi waliowahi kushika kinasa nchini Kenya. Baada ya kupata hamasa akiwa na umri mdogo kutoka kwa kaka yake mkubwa, Oksyde aliamua kujinoa zaidi kwa kuandika mashairi yake na kuanza kujifunza jinsi ya kuchana.

Miaka mingi baadaye fani hii imekuwa ujuzi wake muhimu sana ambao umemwezesha kupata mkate na siagi yake ya kila siku. Akiwa na ujuzi wa zaidi ya miaka 10 Oksido kama anavyojulikana pia ni rapper mmoja mbunifu, mwenye utubuthu na anayefahamika kwamba haogopi kamwe kuvuka na kuvunja mipaka yake.

Mabibi na mabwana tunamleta kwenu, Oksyde.

Karibu Micshariki Africa kaka. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu, Oksyde ni nani ; majina yako rasmi, na unafanya kazi gani, historia yako ya elimu ni ipi?

Oksyde ni jamaa mnyenyekevu...mtafutaji ambaye huwa napiga kazi hadi ikamilike, hakuna kuremba. Majina rasmi Freimah Aseka Mukanga, mimi ni msanii. Ninafanya muziki na biashara nyingine kwa ajili ya kujikimu na pia ni mmiliki mwenza wa lebo ya Feel Hood Establishment.

Oxide ni mbunifu anayepatikana Kenya, ni mmoja kati ya rapper/msanii bora kutoka nchini, nawakilisha watafutaji, watu ambao hawataki kusimama na hawawezi kusimama, nawakilisha watu ambao hawafurahii  pahala walipo ila wana nia ya kwenda zaidi ya walipo.

Tuambie kidogo kuhusu historia yako, uliingiaje kwenye muziki? Jina lako la kisanii Oksyde lilikujaje na linamaanisha nini?

Nilianza kupendezwa na muziki kutokana na kumtazama kaka yangu mkubwa wakati akiwa kijana na akichana kwa mitindo huru (freestyle) kila mara …Yeye ndiye aliyenitambulisha kwa utamaduni taratibu.

Jina la jukwaa lilikuja mnamo 2008 nilipokuwa najiandikisha kwenye shindano la "Florida 2000 jam session battles" ambalo nilishinda…Hakuna maelezo mengi au maana ya kina nyuma ya jina hilo, linasikika tu kuwa la kustaajabisha na la kipekee na lililojaa vaibu na ndiyo maana nililichagua.

Kwa nini wanakuita Chief Rocker?

Ni jina nililopata kutokana na uwezo wangu waku changamsha mashabiki zangu ninapo kua majukwaani kila ninapo tumbuiza.

Umekuwa katika rap kwa muda mrefu, tafadhali tueleze kwa ufupi mambo muhimu ya safari yako ya muziki.

Nimekuwa hapa kwa zaidi ya muongo mmoja sasa. Kumekuwa na misukosuko lakini tunamshukuru Mungu kwa kufanya kazi pamoja nami kila mara. Mojawapo ya mambo yaliyoangaziwa zaidi ni kufungua tamasha la mhandisi wa sauti na DJ wa Jay Z alipokuwa Kenya na pia kupata kazi na Back Road Gee kutoka Uingereza.

Inadaiwa kuwa katika anga ya Hip Hop ya Kenya wewe ndiye rapper mwenye miradi kibao zaidi ya yoyote. Tafadhali tueleze majina ya miradi yako yote (EP, Mixtapes na albamu) na lini uliiachia.

Nina katalogi kubwa iliyo na miradi 10 chini ya ukanda wangu.

2010 - Thee Emcee Mixtape
2011 - Mixtape ya pamoja na Khaligraph Jones inayoitwa - Undisputed- Headz
2012 - King Kong Ep
2015 - Oksyde Music Collection Mixtape
2016 - Niko True Ep
2018 - Before The Album Mixtape
2019- Drip Morio Ep
2020 - Albamu ya Kalesa Na Earpods
2021 - Deliver The Package No Excuses Ep
2022 - Strictly for my hoodlums Album

Kitu kingine ambacho ninavutiwa na maadili ya kazi yako ni idadi ya video za muziki ambazo umeweka pale YouTube kwa ajili ya mashabiki wako. Ni nini kinakuchochea kutengeneza video hizi na ni waongozaji gani wa video ambao umefanya nao kazi kwenye miradi yako?

Jambo la mashabiki wa kizazi hiki kipya ni kwamba wanapenda kutazama (video) zaidi ya kusikia tu...Hapo ndipo video za muziki huingia. Asilimia 50 hadi 60 ya video zangu za muziki kwa kawaida husanifiwa na mimi kwa msaada wa wakurugenzi ninaofanya nao kazi. Nimepata fursa ya kufanya kazi na watu kibao kwa mfano Rango, Robert Wesley, Mike Lolly P, Johnson Kyalo, Atura Images n.k.

Je, ni watayarishaji gani wakubwa wa Hip Hop ambao umefanya nao kazi?

Nimefanya kazi na karibu kila producer wa Kenya toka miaka ya 2010...Sniper G Ganji (RIP), Alex Vice, Misee Billions , Vince On The Beat, Ares 66, GKV Samora , Ndovu Kuu nk.

Katika umri wako mdogo umepata fursa ya kufanya kazi na baadhi ya wasanii bora wa Hip Hop waliowai kushika kinasa; Abbas Kubaff, Kama K Shaka, Khaligraph Jones, Smallz Lethal, Chiwawa n.k. Je, unajiskiaje kufanya kazi na wasanii hawa?

Inastaajabisha kufanya kazi na wasanii hawa wote. Wanamtia motisha na kumtia moyo kaka kwa njia nyingi sana zisizofikirika.

Mmoja wa wasanii walioshirikishwa kwenye albamu hiyo ni Kamah wa Kalamashaka, tuambie kwa ufupi ilianza vipi kabla ya nyie kuingia pamoja studio, ukizingatia, Kamah ni mmoja wa wakongwe wa Hip Hop toka kundi la Kalamashaka na pia mwanzilishi inapokuja kwa Hip Hop ya Kenya?

Mda wetu na Kamah K- shaka ulikuwa mzuri. Alikuja ku support harakati zetu, alisafiri kutoka Naivasha kwani alikuwa nje ya mji wa Nairobi wakati huo. Yeye ni mkongwe mnyenyekevu, kupatana naye haikuwa rahisi kusema kweli. Nilimpata kupitia kwa Roba K - Shaka na Labalaa . Kamah ni mzuri sana, alipokuja nilifurahi sana, heshima ni kuheshimiana. Namshkuru kwa yeye kutokea kwenye albamu yangu.

Oksyde, Kamaa (Kalamashaka)

Feel Hood Est. ? Hii ishu inajihusisha na nini? Je, wewe ni msanii wa kujitegemea au umesainiwa na mojawapo ya lebo hizi kuu nchini Kenya?

Feel Hood Est ni lebo yangu…Iliyoundwa na mimi na kaka yangu mkubwa.

Sisi tunajihusisha na vipaji, haijalishi ni kurap au kuimba au kuelekeza au kutengeneza...Vipaji vyote vinakaribishwa hapa.

Binafsi niko chini ya Feel Hood na kwa sasa ndiye msanii pekee aliye chini ya lebo hiyo kwa sasa.

Ninaona kuwa unauza miradi yako mipya kwa njia kwa mteja mmoja mmoja? Ni nini motisha ya kuuza kwa njia hii? Nini maoni yako kuhusu DSPs kwani nimegundua kuwa mradi kamili tu ulionao hapo ni EP ya DTP(No Excuses). Nini sababu?

Ninapendelea zaidi mtindo huu wa uuzaji wa zamani kwa sababu mimi huwasiliana na mashabiki wangu moja kwa moja tofauti na DSPs ambapo mashabiki hutiririsha(stream) tu lakini hawawezi kuwasiliana na msanii wanayempenda. Maoni yangu tu.

Je, una maoni gani kuhusu hali ya sasa ya Hip Hop ya Kenya na Afrika Mashariki? Je, ungependa kufanya kazi na nani Tanzania?

Hip Hop ya Kenya na Afrika Mashariki kwa sasa inafanya vizuri. Hip Hop inazidi kuwa kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa maoni yangu nadhani Afrika Mashariki inatengeneza muziki bora zaidi wa Hip Hop/Rap barani. Nadhani tu tunahitaji kufanya kazi pamoja zaidi.

Ukiangalia gumzo la hivi punde la muziki, angalau tuna nyimbo 6 za Hip Hop kati ya kumi kutoka ukanda huu wa Africa Mashariki. Hili linaonesha jinsi Hip Hop ya Kenya inavyokua. Watu wanaupa mda muziki wetu wa Hip Hop. Tuko kwenye njia sahihi.

Mmoja wa wasanii ambao ningependa kufanya naye kazi kutoka TZ ni Young Lunya . Napenda muziki wake sana.

"Hip Hop iliokoa maisha yangu" alisema Lupe Fiasco lakini je, Hip Hop inalipa bili zako mara tu unapotoa mzigo mpya kwa ajili ya mashabiki wako Bw. Oksido ?

Rap inalipa kaka...lazima ujue jinsi unavyokamua ng'ombe wako.

Je, ni nini kingine unachofanya mbali na kuimba ili kuhakikisha unaweka chakula kwenye meza yako?

Mbali na muziki nafanya mambo kadhaa pembeni. Ninakusanya sneakers (viatu vya sports) na kuuza tena pamoja na mambo mengine mengi.

Je, ni msukumo gani nyuma ya mradi uliotolewa hivi majuzi, Strictly for my hoodlums ?

Strictly For My Hoodlums ni mradi wangu shirikishi, ambapo Feel Hood ni lebo yangu, mimi ndiye Mkurugenzi Mtendaji. Kwa hivyo msukumo nyuma ya mradi huu, niliona kuna pengo kati ya wasanii kutofanya kazi pamoja, kama kuna makundi au matabaka na hii sio nzuri kwa tamaduni (wa Hip Hop). Kwa hivyo ninajaribu kuziba mapengo yaliyopo kati ya madarasa ya Hip Hop ambayo yamekuwepo na hayajafanya kazi pamoja. Tunakumbatia aina zote ndogo za Hip Hop, kama vile watu wanaofanya Drill kuweza kufanya kazi na wasanii wa Boombap .

Katika mradi huu nina wachanaji wanaopenda midundo ya Drill, Boombap emcees, wasanii wachache wa zamani wa kitambo na wapya. Mradi wote una nia ya kuziba pengo lililopo ili kupata sauti mpya ya Hip Hop.

Je, mchakato mzima ulikuwaje, katika kutengeneza mradi huu wa pamoja?

Kuunda mradi huu kulichukua muda mwingi, kuleta watu tofauti pamoja haikuwa rahisi, kutoka kupata wimbo hadi kiitikio, mmoja baada ya mwingine. Nilifurahia sana kipindi hicho. Hasa na Katapilla na Kamah Kalamashaka . Mixing & mastering pia ilikuwa ya hali ya juu, kufanya kazi na mtayarishaji Ares 66 ilikuwa moja ya hisia poa, tulichukua muda kuhakikisha hii inakuwa kazi bora.

Albamu yako mpya inapaswa kuja na upya flani bila ya kuwa na vizuizi vya EP yako ya awali (No Excuses DTP), umejifunza nini kutoka mradi wako wa awali DTP?

DTP ilikuwa EP tu, haikuwa mbaya sana. Nilikuwa nikifanya kwa ajili ya kujifurahisha, ilipokelewa vyema kinyume na matarajio yangu. Niliiharakisha kwa sababu ya soko na kuwaweka mashabiki wangu sawa.

Strictly For My hoodlums ni kubwa na bora zaidi. Nilileta watayarishaji na wasanii mbalimbali. Studio ipo nyumbani kwangu, kwa hivyo kila wazo lilipokuja nilikuwa huko kulirekodi. Mchakato wa ubunifu ulikuwa wa hali ya juu!

Mashabiki wako watarajie nini kutoka kwa Strictly For My Hoodlums, je itakuwa albamu yenye dhamira flani au itakua mradi wa kujaribu mitindo yako mipya ya muziki au pengine ni mlolongo wa simulizi za hadithi zenye mada zinazounganika katika kila ngoma mle ndani au albamu ya majaribio ili kujaribu kuongeza hadhira yako?

Stricly for hoodlums yangu ni mradi wenye mada flani kwani  kwa kawaida mashabiki huniita ' Jamaa wa miradi yenye mada' , itakapotoka mwishowe, utaisikiliza, kutoka kwa wimbo wa kwanza ikiwa unapenda utamaduni wa mtaani au mijini, mradi utasikika kama sinema vile, mada ziliundwa kuwa kama filamu, kwa hivyo kazi ikitoka utaliona hili.

Baada ya Strictly for my hoodlums, nini kinafuata toka kwa Oksyde ?

Miradi zaidi, miradi ya ushirikiano zaidi imepangwa kuachiwa, albamu nyingine pia, mambo mengi yamepangwa, ikiwa ni pamoja na mtindo wa mavazi / mavazi. Taarifa kamili kuhusu hili zitatoka baadaye.

Je, tunaweza kuwa na tarehe ya kutolewa?

Albamu hiyo ilitolewa tarehe 21 Oktoba 2022 .

Neno lako la mwisho?

Pongezi kubwa kwa kila mtu ambaye aliniamini tangu siku ya kwanza, mmekuwa mkinipa motisha, namshuru kaka yangu mkubwa Fello, Robert Wesley na kila mtu aliyejiunga na msafara njiani. Mkae hapo mlipo kwani albamu inakuja, kitu ambacho hakijawahi kutokea nchini Kenya tangu 'Dandora Burning'.

Mcheki Okysde kupitia mitandao ya kijamii;

Facebook: Oksyde Musik
Instagram: oksyde
Twitter: oksydemusik