Ommy Pah/ Ommy Daddy

Ommy Pah ni mmoja wa watayarishaji wazuri wanaopatikana handakini mwa Tanzania. Ommy Pah ni mtayarishaji aliyebobea kwa kuunda midundo ya Boombap japokua pia anaunda midundo ya mahadhi mengine tofauti na Hip Hop. Ommy Paha aliweza kuingia kwenye kinyang’anyiro cha mtayarishaji bora wa Hip Hop nchini Tanzania mwaka 2023.

Skia Playlist ya Ommy Pah/Ommy Daddy hapa

Karibu sana kaka Ommy Pah hapa Micshariki Africa…Hivi kabla sijaenda mbali je Ommy Pah na Ommy Daddy ni mtu mmoja au watu wawili tofauti? Hili jina lako la kazi lilikujaje na linamaanisha nini? Hebu tueleze kuhusu historia yako kidogo, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi na ulifikia wapi ki masomo, kwenye familia mpo wa ngapi na utoto wako ulikua vipi?

My brother mambo vipi? Sasa wana Micshariki Africa, nikianza kujibu haya maswali yako kama Ommy Pah na Ommy Daddy kama ni mtu mmoja, ndio huyu ni mtu mmoja, yaani Ommy Daddy ndio anaitwa Ommy Pah na Ommy Pah ndio huyo huyo Ommy Daddy. Hawa sio watu wawili tofauti.

Hili jina la Ommy Pah alinipa Chidi Benz, my brother Chidi Benz ambaye nilikua nafanya nae sana kazi, kwa hiyo alikuja kugundua kuwa napenda kupiga sana ma beat flani ya Hip Hop, wenyewe wanapenda kusema mabiti ya kuchapa, kwamba oyah tunachapa ile”Paah” ndio wakaniita Ommy Paaaaah! Ndio hapa likapatikana jina la Ommy Pah!

Ommy Daddy nilijipa mimi mwenyewe kwenye hustle zangu za mziki. Kwa nini nilijipa hili jina? Ni kwa sababu, kwenye familia sisi tulizaliwa watatu, watoto wa baba na mama mmoja na wote tulikua watoto wa kiume. Mmoja wetu aliyekua wa katikati alifariki alikuwa anaitwa Micky Daddy, kwa huyu katika swala zima la kutaka kuendelea kumuenzi nikachukua ile Daddy yake mimi nikabaki na Ommy jina likawa Ommy Daddy kwa hiyo hii Daddy inamuwakilisha yule ambaye amefariki. Kwa hiyo mpaka leo bado anaendelea kuishi kwa sababu ni my brother ambaye mimi hata kumuona sijawahi kumuona kwani niliskia kuwa nilikuwa na braza anaitwa Micky Daddy, Micky Daddy tu.

Tuendelee kwa kukufahamu majina yako rasmi kaka, unatokea wapi na unajihusisha na nini?

Kwa majina rasmi naitwa Omary Silaha lakini kwa majina ya kutafutia ugali au majina ya sanaa naitwa Ommy Dady au Ommy Pah. Wengi wananifahamu kwa hayo majina.

Mimi ni mzaliwa wa mkoa wa Tanga, wilaya ya Tanga mjini sehemu moja panaitwa Kivuleni, Pande. Kiomoni, Pande kwa wale wanaokaa Tanga wanapajua kwani mie nimetokea pande hizo za Tanga.

Najishughulisha na maswala ya utayarishaji na ninapatikana kwenye studio za MV09 Records. Studio hizi zamani zilikuwa zinapatikana Tangi Mbovu, Mbezi Beach ila kwa sasa hivi zinapatikana maeneo ya Kijito nyama.

Mimi ni producer ambaye niliingia kwenye tuzo za muziki nchini Tanzania, producer wa Hip Hop wa mwaka 2023. Mimi ningependa kuwapongeza serikali, BaSaTa pamoja na wizara kwa kuniona kwa bila kufanya kazi nisingeonekana. Kwa hiyo mimi ni producer ambaye nilikuwa nominated kwenye tuzo za muziki nchini Tanzania kama producer wa Hip Hop na hawakukosea japokua hatukushinda.

Ulianzaje hizi mbanga za muziki? Tupe historia yako husu hili…

Rasmi nilianza muziki kama mwaka 2011, hapa naongelea utayarishaji ila kabla ya hapo 2008 nilikua nafanya hizi harakati za muziki. Nakumbuka kipindi niko Tanga nilikuwa naenda studio mbali mbali, studio moja iko sehemu moja inaitwa Mwako, kuna braza mmoja aliyeni inspire mimi kuendelea kufanya muziki, mpaka leo kwa hiyo nilianzia huko Tanga.

MVO9 Records ni studio nimeanza kuiskia kutoka kwenye miradi iliyoachiwa hivi majuzi. Lini mlianzisha studio hii, inapatikana wapi na inajihusisha na nini? MVO9 pia inamaanisha nini?

Kwanza naweza kusema kwamba studio yetu ipo mda mrefu, naweza kusema kwa sasa nina kama miaka mi sita au saba. Tulianzisha studio 2018 na tukawa tunapatikana maeneo ya Mbezi Beach. Tulianza mda mrefu na miradi mingi ilikuwa inafanyika.

Ni mda mrefu tupo na kazi zilikuwa zinafanyika, kwa hiyo tunafanya kazi nyingi na tunafanya kazi nzuri, watu mtaani wanaona kuwa tunafanya kazi nzuri, wanasema “Jamaa Hip Hop sana”, ila tunafanya kila aina ya muziki ila sanasana tume base kwa Hip Hop kwa sababu mimi binafsi naipenda pamoja na jamii ya watu ninao deal nao kwa asilimia kubwa ni Hip Hop. Nashkuru Mungu kwa hilo.

MVO9 Records

Je MV09 Records mnahusika na utayarishaji wa muziki wa Hip Hop tu au zozote zile?

MV09 inajihusisha na uzalishaji wa kila aina ya muziki, sema tu ile hali kwamba mimi mwenyewe muziki wa Hip Hop ni muziki ambao naupenda kusema kweli kuliko hii miziki mingine. Ni studio ambayo tunazalisha kila aina ya muziki. Hapo tunazungumzia sijui Bongo Flava, Hip Hop na kadhalika ila mimi kama Ommy Pah kwa sababu napenda Hip Hop na kwa kuwa jamii yangu ni watu wa Hip Hop basi watu wanajua pale MV09 ni Hip Hop tu, ila sio kweli, sisi tunazalisha kila aina ya muziki.

Hapa MV09 Records je mmewasaini wasanii au nyie mnahusika kwenye maswala ya utayarishaji tu? Tuzungumzie Kiota…mnajihusisha na nini hapa? Wazo la Kiota lilikujaje na malengo yenu ni yapi na je mmeweza kuyafanikisha?

Kiukweli MV09 hatuna msanii tuliemsajili. Sisi tunahusika kwenye maswala ya uzalishaji tu lakini pia tuko katika swala zima la kuwasaidia watu wenye vipaji. MV09 ndio imezaa Kiota ambayo ni platform ambayo tumeanzisha kwa ajili ya watu kuja na kuweza kukuza vipaji vyao na baadae unaondoka unaenda kuendeleza kipaji chako. Kwa mfano naweza muongelea mtu kama Fresh Boy, mtu kama T Boy. T Boy nae alikua MV09, walipitia Kiota akiwemo pia Mickpeace Yaani hii ile platform inayozalisha vipaji, wanakua, wanaenda.

Wazo la Kiota nikiongezea sio kundi la watu flani bali ni platform ambayo mtu yoyote anaweza kuja akakua kama vile ndege wanavyokua kwenye Kiota kisha wakikua wanaota mabawa wanapaa wanaenda zao.

Mipango ipi endelevu mnayo kwa ajili ya Kiota na tutarajie nini kutoka kwenu huko mbeleni?

Mipango endelevu ipo kwa ajili ya Kiota na moja kati yao ni kuandaa album tukiwa na wale watoto ambao tumepita nao baadhi ya sehemu wakaonekana, yaani hii ndio itakua shukran yangu kwao, ili kutaka kuwaonesha zile sehemu ambazo nimepita na wao wajione na baadae waweze kurudi hata wenyewe. Hilo ndio lilikua lengo langu mimi la Kiota. Na ndio lengo ambalo tutaishi nalo mpaka kesho.

Kama mtayarishaji umewezaje kujenga jina lako toka studio ulipofanikiwa kuanza mpaka sasa?

Mimi kiukweli kujenga jina langu na watu wakaniamini kusema kweli ni ule ufanyaji wangu wa kazi. Unajua huwezi kujenga jina kama hufanyi kazi zilizo bora. Ni ile hali ya kuhakikisha kua ninafanya kazi zilizo na ubora, kazi za quality kutoka kwangu kama Ommy Daddy na Ommy Pah!

Changamoto ya kazi zako ni zipi na unakabiliana nazo kwa njia ipi?

Kama unavyojua jamii ya watu wetu wa Hip Hop ni watu wa hali ya chini sana. Kwa hiyo unajaribu kuishi nao hivyo hivyo kwa sababu huwezi ukasema hutofanya nao kazi, kwa hiyo unajitahidi ili ufanye mishe zako zingine huku mambo mingine yanaendelea huku watu wanapiga kazi kama kawaida.

Je inapokuja kwa miradi mikubwa ya wasanii, hapa nazungumzia EP, Mixtape, Album au hata beat tapes, nyie mlisha husika kusimamia miradi ipi na ya wasanii gani?

TK Nendeze, “A Letter To My Son” lakini pia kuna miradi kwa mfano kama album ya Dizasta Vina, “The Verteller”, ilirekodiwa pale, pia kuna album ya Chidi Benz ambayo bado haijatoka, ilitoka tu baadhi ya kazi, lakini pia kuna kazi kama ya One The Incredible, “Vitendo Dhidi Ya Maneno”. Pia kuna miradi kama wa Moh Rhymes, na mradi kama wa Mabeste, (ngoma ya “Kinafiki”, Mabeste ft. Country Boy, “Backoff” pamoja na “Qualified” za Mabeste pia).

Pia nishawahi kutoa mradi wa beats (beat tape), lakini pia kuna miradi ya Kiota, kuna ma album bado yapo chimbo mpaka saa hizi hayajatoka. Pia kuna “Beberu Declaration” ya Wakazi. Pia kuna my sister ambaye pia anaitwa Rozy M, wote hawa nimefanya nao kazi….yaani wengi wengi nimefanya nao kazi.

Kaka pia niliona kuwa mna MV09 Online TV, hila nalo vipi? Mnajihusisha na nini pale?

Hili ni wazo ambalo lipo kichwani kwangu mda mrefu sana, niile tu tufanya kazi tofauti sio kama zile za udaku. Hii ni ile kama kuna msanii ninaefanya naye kazi basi nitafanya naye interview, ili hali ile ya kuwa wanaomba ma interview kwenye maradio na inashindikana basi hii online TV inawapa fursa na wasaa wa kuongea mambo yao.

Unakuta pia ukienda kwenye hizi radio station mda unaoupata kwa ajili ya kueleza kazi zako ni mchache mno so hapa msanii anaweza kujieleza freshi tu.

Emcee Wakazi alirekodi kazi yake mpya Beberu Declaration pale MV09. Kwanza hii ilikujaje na unaliangaliaje inapokuja kwa hatua ambazo mmezipiga tangu kuanzisha studio ya MV09?

Kwanza kitu ninachoweza kusema kuhusu kaka yangu Beberu ni kuwa ameniheshimisha sana pamoja na studio yetu ya MV09 kwa sababu msanii kama Wakazi anafahamu studio nyingi lakini kuwaacha wale wote na kuja kuunda album yake kwetu ni heshima kubwa sana jamaa katuonesha. Kwa hiyo sisi tunashukuru. Ningependa kumuomba aendelee kujenga imani na sisi.

Changamoto za kazi kama mtayarishaji wa Hip Hop na unavyokabiliana nazo?

Changamoto zipo kama vile kwa sehemu nyingine kama vile zipo kwenye kazi nyingine. Mtu anaweza kuja kurekodi kwako, mmemaliza kazi ila inajitokeza usumbufu kwenye maswala ya kulipana msanii anapoanza kuuza kazi.

Hip Hop watu kadhaa wanasema haiuzi, je kwako wewe kama mtayarishaji?

Japokua nimeligusia kule juu kitu naweza kuongeza ni kuwa watu kadhaa wanasema kuwa Hip Hop hailipi ila kwa upande wangu nasema Hip Hop inalipa kabisa. Kama unavyoona nilianzisha studio kutoka mwaka 2018 mpaka leo studio bado ipo na ninaendelea kufanya kazi.

Nilikuwa Mbezi Beach kitambo sa hizi nipo Kijitonyama.   na nalipa kodi kama kawaida, na studio ipo kwenye standard na quality ya juu. Muziki huu unalipa, ni vile wewe unavyojiweka, yaani kama kitu kinakuingizia hata shillingi hamsini basi hicho kinakulipa.

Nani watayarishaji walio ku inspire?

Mtu ambaye aliniinspire mimi kuingia kwenye swala zima la production ni ile hali nilikuwa najikuta naenda kwa ma studio ya watu na unasumbuliwa na ma producer halafu inakupa msukumo kuwa mbona mimi hili swala naweza. Basi hili swala la usumbufu ndio lilinisukuma ili kuweza kuingia studio na kuweza kujifundisha mwenyewe.

Pia mtu kama Duke Tachez alini inspire mimi kufanya aina hii ya muziki wa Hip Hop. Kuna watu kama akina Lindu, John Mahundi, akina Nice P hawa wote ma producer wameni inspire sana mpaka leo napenda hichi ninachokifanya.

Lakini pia changamoto ndio zilinifanya mimi kujifunza utayarishaji. Kabla ya kuwa producer nilikua rapper, rapper mzuri tu kwa wale wanaonijua, ni rapper ambaye nachana vizuri tu.

Tukimalizia wape wasanii na vijana ushauri kuhusu muziki na biashara ya muziki…

Muziki ni mgumu sana na kwa ushauri kwa vijana na wahimiza tuendelee kukaza. Hakuna mtu atakushika mkono hapo ulipo. Kama utakuja kwa Ommy Pah na umepata nafasi na nimekushika mkono na nimekupa nafasi kwa hizi cyphers, nawapeleka radio, nawafanyia hivi na nawafanyia vile basi mnatakiwa na nyie muoneshe ile ari ya kwamba jamaa amefanya kwa nafasi yake basi mambo mengine na wewe mwenyewe jiongeze ili kufikia lengo lako.

Wapi unapatikana ki anwani na pia kwenye mitandao ya kijamii na pia kupitia njia ya simu?

Kwa sasa tunapatikana kule Kijitonyama, Mbezi Beach kule tulitoka. Kule Mbezi Beach tunapatikana mtaa wa Bukoba, ukiingia tu ukiulizia studio MV09 au Kiotani basi watakuleta studio. Hapo ndipo tunapatikana na hapo utakutana na watayarishaji wengi wengi tu kama vile akina Ringle Beatz pamoja na wadogo zangu akina Black, RN Beats, yaani ni wengi ambao tunafanya nao kazi.

Pia najaribu kuwapa nafasi producers wenzangu hususan upcoming ambao wana ndoto za kuwa kama mimi kwa sababu mimi naamini kile nilichonacho ni Mungu pia na juhudi zangu. Pia natoa hii nafasi kwa mtu mwingine anayetamani pia kujifunza kuwa producer anicheki tu, afike tu MV09, tutaelekezana, kwa sababu wanasema hicho unachokijua wewe mpe na mwenzako pia utajiskia faraja.

Kwa mitandao ya kijamii sisi tunapatikana MV09 Records pale Instagram, Facebook, sehemu yoyote Pia utanipata kama Ommy Daddy au Ommy Pah pia napatikana Instagram na Facebook. Namba zangu za simu ni +255714921185. Karibuni tufanye kazi wenye miradi yao ya Hip Hop au tasnia yoyote ile, tunawakaribisha. Bei zetu ni rafiki sana. Pia tutatoa fursa kwa watu kufanya interview kwenye online TV yetu ili waweze kujinadi vizuri.

Shukran sana kaka kwa mda wako….

Kwa haya machache natoa shukran za dhati, tuendelee kukaza, tuendelee kufanya kwa sababu bila wewe kufanya hakuna mtu atakuja kukushika mkono. Pia usisahau kumuomba Mungu, kwa sababu Mungu naye ndio kila kitu.