Ukaguzi wa Albamu: Africa The Album
Msanii: Producer Pallah Midundo akiwashirikisha wasanii tofauti
Tarehe iliyotoka: 15.12.2020
Nyimbo: 32 na bonasi 2
Producer/Mpiga midundo: Pallah Midundo
Mchanganyaji sauti na midundo: Pallah Midundo
Studio: Kinasa Records

Kwa producer ambaye awali alikuwa emcee, Pallah Midundo ameweza kujitengenezea jina kama producer ambaye ma emcee wa Hip Hop nchini Tanzania wanamtafuta kwa wingi ili waweze kufanya naye kazi. Inawezekana umeshawahi kuskia nyimbo zilizo tumia midundo yake ila kwa kuwa hana sign tunes inayomtambulisha ukasema hujawahi kumsikia.

Pallah aliyezaliwa mwishoni ya miaka ya sabini nchini Tanzania alianza kughani akiwa kijana kabla ya kuanza kugusa mitambo mpaka kujua kuunda midundo na kuwa stadi kwa hili. Baada ya kuangusha kandamseto yake ya kwanza Utajiri Usiothaminiwa takriban miaka nane iliyopita, Pallah aliibuka tena na albamu yake ya kwanza aliyokuwa anaifanyia kazi chini ya maji kwa muda mrefu iitwayo Africa The Album.

Africa The Album ni album inayohusu Afrika na Waafrika, uzuri wake na watu wake pamoja na changamoto zilizopo kwenye bara hili. Kwa kuwa taswira ya Afrika imechorwa tofauti na watu tofauti Pallah aliamua kuchukua vinanda kuichora upya Afrika akishirikiana na washairi waliobobea nchini Tanzania.

Albamu hii inafunguliwa na ma emcee wawili toka Dar, P Mawenge na Wakazi wakiweka msingi wa album hii kwenye wimbo uliobeba jina la albamu, Afrika. Humu, Pallah anaunda mdundo murua unaochukua sampuli kwa wimbo toka kwa gwiji wa Senegal, Ismael Lo uitwao Africa pia.
Sauti ya Lo pamoja na gita lake la nyuzi moja aina ya Kora linaskika vizuri baada ya kuongezwa spidi kidogo. Pia sampuli ya hotuba ya mwimbaji Akon ambaye pia mtu wa Senegal aliyezaliwa America, imetumika vizuri sana kwenye wimbo huu.

P Mawenge anatufungulia mradi kwa kutuachia madini akisema,

“Nyumbani kwa ma Mwinyi ma Chifu na ma Farao /
Na ngozi nyeusi ndo utakatifu wa bara lao/
Bara la mashujaa wenye nguvu za kijadi/
Japo wengi walipotezwa na wazungu wajuaji/
Vita za wenyewe kwa wenyewe tusahau/
Wageni wakituona hivi wanazidi kutudharau/
Nchi kibao tunabaguliwa/
Halafu tunapigana wenyewe ka tumechanganyikiwa/
Ni muda wa kusimama na kusema sasa basi/
Ubaguzi katika bara letu hatutaki/
Tupeni mbali visu mabunduki na risasi/
Ili upendo na furaha ndo vije karibu nasi/
Kwetu midundiko aghalabu/
Hasa tukiwa tunayaenzi matambiko ya mababu/
Tumefunga rubega madada wanavibwaya/
Wakicheza kwa kukata mauno kwa kujimwaya/
Hivyo ndio vitu tunavihitaji/
Dunia itambue kwamba kwetu sio sehemu ya mauaji/
Na hapa ndio Musa alichapa maji/
Mtayajua mengi nilichowapa ndio kwanza dibaji/”

P Mawenge kwenye mradi huu ameshikishwa kwenye ngoma tatu zingine kando na Africa zikiwemo Nitawanyuka akimshirikisha Hayati John Pombe Magufuli na Malaria ambao ni wimbo wenye mdundo mzuka sana ambapo kinanda kinapigwa vizuri sana unaoelezea Malaria kwa kupitia mashairi yenye mafunzo kwa umma. Pia anapatikana kwenye wimbo uitwao Inatosha Sasa akiwa na Nikki Mbishi ambao wanakutanishwa na Pallah baada ya beef lao. Kwenye Inatosha Sasa Pallah anatumia sampuli toka kwa magwiji wawili wa rap Proffessor Jay na Sugu ambao pia wao kitambo walikuwa na wimbo uendao kwa jina hilo hilo. Nikki pia alipata fursa ya kuwa na wimbo wake wa pili akiwa peke yake unaoitwa Sun Zu Wa Bantu.

Hivyo hivyo ma emcee wengine ambao walishiriki nyimbo zaidi ya moja ni kama vile Nash Mc aliyeangusha ngoma tatu; Chatu, Maruhani na Mama Watoto. Mama Watoto ni wimbo wakusikitisha wenye mdundo unaonasa na kutoa hisia hizo pia. Kwenye wimbo wa Chatu Pallah anatukumbusha zilizopendwa akitumia sampuli ya wimbo uitwao Chatu Mkali toka kwa Orchestra Safari Sound.

Zaiid naye pia ameshirikishwa kwenye nyimbo tatu; Habari, Njema na Mshindi. Kwenye nyimbo mbili Pallah aliwakaribisha magwiji wa Taarab Isha Mashauzi kwenye Njema ilhali Rukia Ramadhan amefanya kazi nzuri kwenye Habari. Kwenye wimbo wa Habari, Zaiid anaonesha uwezo wake wa uandishi na uchanaji akielezea changamoto za Africa, jamii yake na mziki wake aupendao wa Hip Hop wakati Rukia Ramadhan akimfariji kwa sauti yake nyororo kwenye mdundo unaopiga taratibu.

Shua Mkuu naye alichangia nyimbo mbili kwenye mradi huu zikiwa ni Hatufanani na Jipange sawia na Ghetto Ambassador akichangia I told you na Balozi wa Ghetto.

Mwingine aliyechangia nyimbo zaidi ya moja ni Jay Moe akishirikishwa kwenye nyimbo za Tafsida na Tafsida Remix. Nyimbo zote mbili zinaonesha vile Kiswahili cha mtaani kimekua hadi na Jay Moe anajaribu kutupa kamusi ndogo ili tuweze kuelewa maana ya maneno kadhaa yanayotumika mtaani. Anasema Jay kwenye Tafsida Remix inayosikika kwenye mdundo mzuka,

“Yo tafsida kila neno sione faidi kwa asiyekuemo/
Tafsida juu ya michano mbwiga usisome hili somo/
Shada mi naita Kappa Laga naita botinyo/
Kwenda wengi si kusepa mi kwangu kwenda andiamo/
Anayejibana ni manzi anayefanya ili apate mshiko/
Bitozi fashion designer machizi wana maana choko/
Ndio lugha yetu sisi baba akiwa mkali tunamuita mnoko/
Na hanisi hatumuiti hanisi afadhali aitwe mbwa koko/
Ntokapo mi Air Jordan jina lake babu kipara/
Ntokapo kupeana uroda tafsida yake ni kipara/
Aliyependeza amenoga aliyemboso amelala/
Sio nyoka ni mtu miyeyusho kutoka hapo anaitwa swila/
Popo asiependa kulala kunguru kuwa mtu mwoga/
Wambea vigagula bila tunguli wanaroga/
Na tafsida mchepuko kitambo tulitumiaga/
Kabla hata kibonde kwanza kibonde kwetu anayefungwa/”

Kwenye albamu hii pia ameshirkishwa D Ukingo ambaye ni emcee toka Tanzania aliyejikita Ujerumani kwenye singo nzuri iitwayo Kamusi yenye vesi moja tu.

Pallah pia aliwakaribisha ma emcee wa kike akiwemo Tifa na wimbo Nipe Pesa Remix unaotumia sampuli ya Bwana Nipe Pesa wa Super Mazembe na Mwajiha akiwa kwenye wimbo uitwao Unavyoniona ambao Pallah anapiga gita linalo jirudia rudia vizuri sana. Mwajiha anasisisitiza kwenye wimbo huo kua yeye ni wakipekee na haipaswi kumfananisha na mtu yoyote. Pia dada Mau Kolimba ametupia sauti yake kwenye wimbo alioshirikiana na mshairi Salu T uitwao Binti Remix pamoja na Singo yake iitwayo Challenge.

Challenge wa Mau Kolimba ndio wimbo pekee ambao ni wa kuimba ambapo unamkuta Mau Kolimba akiongea ana kwa ana na Challenge au kwa lugha ya Kiswahili changamoto na kumwambia usoni kwake kuwa yeye hamchukii, hamuogopi bali anakabiliana nae ana kwa ana hadi pale atakapomdhibiti na kumfanya Mau Kolimba kua mtu bora zaidi. Wimbo mzuri sana wa kumuinua yoyote anayepitia changamoto zozote zile.

Wasanii kama Young Killah, Chindoman, Mansu Li na Stereo Singasinga pia wana nyimbo kwenye album hii iliyojaa midundo mizuri sawia na mashairi mazuri. Hiyvo hivyo nyimbo za ma rapper waliopo handakini Tanzania ambazo nilizifurahia kwenye mradi huu ni kama Watupa Mbao wa msanii Kurasa, Dark Master akichana kwenye Life Style pamoja na Ghost The Living akishika kinasa kwenye wimbo Main Camp ulioundwa ki ustadi ilhali Ghost akimwaga moyo wake kwenye kinasa. Pia XP na wimbo wake Nawakumbushia una madini muhimu yanayotukumbushia kuhusu ile siku yetu ya mwisho, kiitikio kikipita taratibu juu ya mdundo ambao juu yake kunapiga  violin kuwa;

“Kumbuka taa yako iliwashwa siku moja/
Kumbuka taa yako itazimwa siku moja/
Kumbuka ulipotoka kumbuka unapokwenda/
Kumbuka matendo yako ya sasa unayoyatenda/”

Album hii ni ya kipekee kwani Pallah alitupatia mradi wenye nyimbo 34 ambayo ni rekodi ya kipekee kwenye mziki na Hip Hop ya Tanzania na amehakikisha kuwa vigezo na masharti vimezingatiwa ili kuwezesha mradi huu kudumu. Maudhui, burudani, mashairi mazuri pamoja na midundo ilioundwa ki ustadi na Pallah vimechanganywa vizuri kutupatia album nzuri na muhimu kwenye tasnia ya hip hop na mziki ki ujumla na kufanya Africa The Album ikamilike.

Kupata LP hii ya  Africa The Album wasiliana na Pallah Midundo kwenye namba ya simu +255 713 659 043
Au kwakupitia mitandao ya kijamii:
Instagram: @palla_midundo | Twitter: @PallahMidundo |Facebook: Palla Midundo |