Bio ya PaulinArt_tz pale Instagram imemtambulisha mwanamama huyu kama mchoraji, illustrator na mwandishi wa vitabu vya watoto. Ambacho hakijasemwa pale kwenye bio yake ni kuwa yeye pia ni mke wa mtu na mama wa familia mwenye watoto watatu.

Akiwa na umri wa miaka 33 Paulina ameweza ku balance maisha ya familia yake na sanaa yake licha ya kuanza tena kuchora alipofika miaka 30. Baada ya mazoezi ya muda mrefu dada Paulina ameweza kufua karama ya uchoraji aliyopewa na mwenyezi Mungu hadi hapa ambao kazi zake zimeanza kuonekana, kufahamika na pia kumlipa.

Leo tumejikita na mwana Mwanza huyu ili kuweza kumfahamu yeye na sanaa yake. Karibu ujifunze toka kwake.

Jina lako rasmi na unajishughulisha na nini kimaisha?

Naitwa Paulina Barnabas Lugabulila, najishughulisha na sanaa ya uchoraji.

Niambie kidogo kuhusu Paulina umetokea wapi, ulikulia wapi, utoto wako ulikuaje na umesomea wapi na nini na umefikia wapi hadi sasa?

Nimezaliwa Mwanza, Tanzania na bahati nzuri nikakulia hapo. Shule ya msingi nimesomea Saruji Tanga ilhali shule ya upili nimesomea Athi River, Nairobi, Kenya. Kule Nairobi nimesoma toka kidato cha kwanza hadi cha nne na nilimaliza 2009. Baada ya hapo nilijiunga na Zetech college pale Nairobi na kusomea Graphics Designing na kisha kurudi nyumbani Tanzania na kuanza maisha na kutengeneza familia toka 2011.

Utoto wangu ulikuwa kama wa watoto wengine, ku struggle na kusoma  kwa ajili ya kujenga  future nzuri.

Historia yako na sanaa ni ipi?

Mie nilipenda kuchora tokea utotoni; nilipoingia kanisani nilijikuta nikimchora mtu au pastor, au mpita njia. Nilikuwa nachora sehemu yoyote ile; kwenye ardhi, kwenye karatasi na kadhalika ila kadri umri ulipozidi kwenda passion ya kuchora ikazidi ku disappear japokuwa  nilikuwa na ndoto za kuwa designer.

Baadaye nilianza familia na hapa ndipo nilipopata uamsho mpya wa sanaa ambao ulitokana na mimi kuchorea watoto picha tofauti tofauti kama vile chungwa, embe kwa ajili ya shule mwaka wa 2017.

Baada ya hapa nikaanza kufanya mazoezi ya kuchora sura. baada ya watoto kunipatia picha ya sura ya mtu na kushindwa na wao kunicheka kuwa sijawai kuwa mchoraji baada ya mimi kujisifia vile nilikuwa mkali enzi hizo, hapa ndio nikapata hamasa ya kurudia uchoraji tena baada ya kuzidi kuboresha michoro yangu ya watu. Familia na marafiki wakanipa msukumo zaidi kurudi kwenye fani hii japokuwa nilikuwa naogopa kuwa itanichukulia muda wangu.

2018 nilikata tamaa na sanaa hii hadi kushindwa kuchora hadi 2019 mwishoni ndio nikaanza kuchora rasmi baada ya kujipanga vizuri. Kutoka hapa nilijikuta 2020 nikikaa kwenye kiti na kuendelea kuchora tena hadi leo. Huwa nakaa kwenye kiti toka asubuhi hadi jioni nikichora tu!

Unafanya art ya aina gani? Bio yako ya Instagram inakutambulisha kama, “Illustrator, Writer, Character design, Comic artist, Painter"...tueleze kuhusu hili.       

Kwenye suala la art mimi kwa ufupi napenda sana uchoraji wa kila aina. Napenda illustration cha kwanza. Kwa sababu gani napenda illustration? Ni kwa sababu niliona illustration inaongea na hainifungi, naweza kuchora matukio mbalimbali yakifuatana, kwa hiyo nikasema kwanza wacha nichague illustration. Kisha nikaona kwamba illustration ikawa inaniskuma kuweza kufanya cartoon pia nikajifunza kuweza kuchora cartoon kwa sababu ukifanya illustration kwenye kuchora cartoon haikushindi. Nikajaribu cartoon nikaona ninaweza.

Lakini sikuanza na illustration, nilianza kuchora, paintings, kuchora sura, abstracts na kadhalika. Kwa ufupi mimi kwa art au sanaa unaweza kuniweka sehemu yoyote na nika fit.

Pia napenda kuandika na ninaandika na nina story zangu nyingi nilizoandika na zipo tayari na nimejikita sana kwenye story za watoto kwani napenda watoto sana. Story hizi nilizoziandika nimezitunza nyumbani nikiwa na matumaini kuwa siku moja nitakuja kuzichapisha rasmi ili watu wazisome.

Napenda ku design ma character kwa sababu nimekuwa nikifunzwa kubuni characters. Ni kitu kigumu ila kwa sasa nimeweza na namshukuru mwenyezi Mungu kuwa naweza kufanya comics na painting.

Kwa sasa nimejikita sana kwenye illustration ambayo kusema kweli inanilipa japokuwa mwanzoni haikuwa rahisi kufanya illustration inayolipa na imeni~ cost muda wangu sana hadi kuanza kunilipa!

PaulinArt, ni nini story ya nyuma kuhusu hili jina? Lilitoka wapi na lina maana gani?

Wakati nikianza sanaa yangu nilipenda kujiita jina langu rasmi ambalo nalipenda, Paulina Barnabas Lugabulila ila watu wengi mtaani walipenda kuniita “Yule mchoraji wa kike!” na mie sikupenda walivyokuwa wananiita hivyo(akicheka), nikasema hapana mie sipendi kuitwa mchoraji wa kike. No! Ningependa kujulikana kama mchoraji tu!

Hapo nilipata wazo la kuanza kutumia jina la PaulinArt baada ya walio karibu kunishauri nijiite Paulina artist. So jina sasa linaonesha dhahiri kuwa mimi Paulina napenda sanaa!

Kazi zako nyingi naona zimejikita kwenye characters za vibonzo na cartoons, kwa nini au unachora vitu tofauti tofauti?

Wakati nilipokuwa nachora sura ya mtu kwa mfano ya mdada mrembo au mwanaume mwenye sura ya kuvutia, nilikuwa naona kama kuna kitu kina miss kwenye picha nilizokuwa nazichora hapo awali. Nilijiuliza muda mrefu nikitafuta kiungo kilichokuwa kina miss kwenye michoro yangu.

Watu wakanishauri nijaribu kufanya michoro ya comics na illustration. Sikujiamini ki hivyo kama naweza kufanya illustrations kwani hata hapa Tanzania wanawake wengi wamejikita kwenye kuchora sura na paintings ila baada ya kushauriwa kwa muda mrefu niliamua kuanza kujifunza illustration.

Nilianza kwa kujifunza figure drawings, kuchora mistari na kwa kukaa na kutulia kwenye kiti kwa miaka mitatu hadi nikawa mtaalam na kujikita kwa vibonzo na cartoons au illustrations.

We huchora hizi kazi kwa mkono wako mwenyewe au hutumia tarakilishi?

Mimi kwenye illustration nachora kwa mkono kwanza kwa sababu sijawa fiti sana, kila kitu kinakuwa kwangu ni kujifunza. Kisha mchoro huo huwa naupiga picha au ku scan kisha nauingiza kwenye PC na kuurudia kwenye Drawing Tablet nikitumia software ya Adobe Photoshop.

Hapo huwa nauchora upya mchoro huo kwa kutumia sketch yangu ya mkono na kuweka rangi kwenye mchoro huo hadi mchoro kukamilika.

Kwa hiyo natumia vitu vyote; penseli kwa sababu bado sijawa mtaalam sana, kisha tarakilishi kumalizia kazi yangu.

Je ni nani alikuvutia pakubwa kwa mambo ya uchoraji na kukupa hamasa ya kuwa mchoraji? Pia ni nini hukupa hamasa na motisha ya ku chora?

Toka nikiwa mtoto nilikuwa nakuta kuta zimechorwa mitaani jijini Mwanza na nilikuwa navutiwa sana na michoro hii hadi ilikuwa inanivutia kuisogelea  ili kuona majina ya wachoraji wale kama vile Marco Tibasima. Kwa hiyo Marco Tibasima alikuwa mtu wa kwanza alienivutia kwenye sanaa ya uchoraji.

Kisha nilipoanza kusoma nikavutiwa na wachoraji kama Goodluck Mashala ambae nilipenda kazi zake nikawa nafuatilia kazi zake kwenye magazeti. Pia kwenye magazeti ya bongo nilikua nafuatilia wachoraji kama Fortunatus Ndilla ila wapo wengi.

Kila mchoraji ana kitu tofauti, kionjo chake flani ambacho nilivutiwa na kujifunza toka kwake.

Ukubwani nilikutana na kazi za akina Dohu, paintings za akina Haji Chilonga, akina Kambi na wachoraji kibao wa kike ila wapo kibao!

Pia mtu alienipa motisha kwa karibu ambae namchukulia kama mwanafamilia ni Angelo Kakorozya. Kusema ukweli Angelo alinishaka mkono na kunipa mawaidha kibao kando na kuamini kipaji changu hata wakati mimi mwenyewe nilikua sijiamini sana. Pia alinisaidia nikapata mchongo wangu wa kwanza kupitia sanaa yangu.

Kinachonipa motisha ya kuchora ni jinsi dunia inavyovutia; kwa mfano uzuri wa beach, mti, theme ya environment, matukio yote yanayonizunguka, mawingu na kadhalika hunipa hamasa pamoja na matukio tofauti.

Je ni changamoto gani unazozipata unapotaka kuchora picha zako?

Changamoto kubwa ni vifaa ninavyovitumia kwani havina ubora. Kwa sasa hivi PC yangu iliharibika kwa hiyo inanibidi kuazima ya mtu mwingine ambayo ni kero kwani muda wa kufanya kazi ninao ila vifaa ndio changamoto kwani hunilazimu mara kibao kukataa kazi ambazo nina uwezo wa kuzifanya ila vifaa nilivyonavyo ni duni.


Tueleze kidogo kuhusu kazi yako, ni nini unahitajika kuwa nacho ili uweze kufanya hii kazi vizuri?

Vifaa ndio kipaumbele kwenye kazi hii na ningekuwa navyo ningekuwa mbali sana, sana kwani nina malengo mazuri na makubwa na sanaa hii sio tu kwa Tanzania tu bali hata East Africa. Vifaa ndivyo vinavyonirudisha nyuma kusema ukweli.

Ni changamoto gani unazo zipitia kwenye shughuli zako za uchoraji sana sana kama mwanadada?

Hehehe, changamoto zipo kibao sana Aisee! Heheheh, changamoto ni nyingi ila inabidi uwe na moyo mgumu na unajua mie husemaga hivi, kama una talent una talent kwa hiyo unaweza ukakutana na changamoto tofauti tofauti.

Kuna kipindi nilitaka kujifunza kufanya painting za acryic, oil kwenye canvas toka kwa kaka mmoja, aisee nilisumbuliwa!  Aisee, toka siku hiyo sijawahi kumfuata mtu kunifundisha pengine nione huyo mtu anajiheshimu kwanza kwani huyo jamaa alitaka kunitumia ili aweze kunielekeza jinsi ya kuchora(akicheka!)Hivyo basi niko radhi nijifunze kwa njia ya tutorials Ili kuepukana na yule anayetaka kunifunza mimi kwa kutumia mwili wangu, hivyo siwezi kukubali.

Kitu kingine ni kwa mfano kama mimi nimeolewa, ni mke wa mtu, nina watoto na ukute kuna kazi au hata mafunzo natakiwa kwenda. Sasa changamoto ni jinsi ya ku balance familia na shughuli hizi kwani mwisho wa siku lazima kazi za nyumbani zifanyike, watoto waende shule, wauguzwe kama wanaumwa na kadhalika.

Kwa kweli changamoto ni nyingi nyingi sana kama mwanamke(wanawake) lakini tutaweza!.

Umekuzaje kipaji hiki hadi kimekupa ajira?

Mazoezi ya kuchora. Mimi nimekaa chini miaka 3 nikipiga zoezi ili kuboresha michoro yangu. Siri ni kujifunza usiku na mchana kwa kupanga masaa ya kulala na masaa ya mazoezi. Uwe mtu wa kujifunza kila wakati, download tutorials, kaa utulie ili ukuze kipaji chako. Mazoezi, mazoezi, mazoezi!

Soma na uzidi kujifunza hadi ukolee kwenye mchoro na pia sikiliza wengine.

Je unatafutaje fursa za kazi?

Kusema ukweli bado sijafanya kazi nyingi, sitaki kudanganya. Nishafanya kazi moja na sasa hivi nipo naendelea kazi ya Pili. Kusema kweli kupata kazi za illustration kama mwanamke inakuwa ni changamoto kwani mtu kukuamini inakuwa ngumu sana kwani hii sana sana hufanywa na wanaume.

Pia mimi  ni mpya kwenye sanaa hii ya illustration halafu watu wanafahamu sana kazi za oil on canvas kuliko za illustration na huwa wananishangaa sana na hii sanaa yangu nikienda kwa mfano mashindano ya sanaa.

Kwa sasa kuna shirika flani limeniamini na kunipa hizi kazi ninazofanya baada ya wao kunipa mafunzo mimi pamoja na dada mwingine wa Arusha.

Nina imani watanzania na makampuni ya kitanzania yataniona na kunipa kazi, nitashkuru sana japokuwa mwanzo ni mgumu kwani watu hawanifahamu au kuniamini.

Kazi zako hupatikana kwa bei gani na je inakulipa?

Bei ya kazi yangu ni Tshs 60,000.00 tu kwenye kazi ya illustration ila nawaza kuiongeza juu zaidi.

Je mapokezi toka kwa wanafamilia na mashabiki kuhusu sanaa yako yakoje?

Mamangu mzazi, mume wangu na watoto wangu wapo proud kabisa na kile ninachokifanya japokuwa kuna family members ambao walikuwa hawanielewi kabisa wakiniambia, “Umekaa miaka mitatu kwenye kiti, kwa nini usifanye biashara au kujaribu kitu kingine, choma hata maandazi uuze…” (akicheka). Ila kwa sasa vile nimeanza kupata kazi walionipinga  wameanza kunielewa na kuwatia wao moyo kwani hapo awali waliniona kama mzembe flani ambaye kakaa tu bila kujishughulisha na chochote!

Pia watanzania wengi na wachoraji wengi wananitia moyo kwenye page zangu za mitandaoni na kuniambia nizidi kukaza buti kwani ninaweza!.

Shughuli hii ya uchoraji hukuchukua muda  gani kukamilisha?

Mimi niko fasta kwenye uchoraji wa mkono ila kwenye computer huwa inanichukuaga muda kwa kweli. Kwa siku naweza maliza illustration moja japokuwa kwa mkono naweza chora picha hata 6 ninapo sketch.

Siku yako huanzaje?

Siku yangu huanza na karatasi na penseli…hua naamka kwenye kitanda niki regret kwa nini nililala(akicheka)!.

Wewe unapenda nini sana kuhusu  uchoraji na je ni kitu ambacho uliwahi kuwaza utakuja fanya?.

Napenda mno kuwa mchoraji kwa sababu naweza kufikisha hisia, ujumbe kwenye jamii ambao mara nyingine kuvizungumza au kutovizungumza haviwezekani ndio hunipa furaha sana pamoja na kuchukua tukio na kuliweka kwenye karatasi.

Kuhusu kuchora mimi niliwaza kua ni kitu nitakuja kufanya baadae japokuwa wakati nakua sikulitilia maanani sana swala hili. Japokua mwanzoni nililichukulia kama hobby lakini ndani yangu kulikuwa na kisauti kilichokuwa kinaniita na kunivuta kwenye uchoraji na nashkuru Mungu baada ya kuanza kufunza watoto wangu kwa njia ya uchoraji kipaji nilikirudisha.

Kando na shughuli hii ya uchoraji una vipaji au talanta gani nyingine? Pia unajihusisha na shughuli gani tofauti na sanaa hii ?

Mimi ni mama wa nyumbani na sina shughuli nyingine tofauti na kulea familia basi ila nishawahi kujishughulisha na ujasiriamali wa kutengeneza sabuni, hereni,shanga, batiki na kadhalika. Pia huwa naandika story.

Janga la Uviko 19 limeathiri vipi shughuli zako za uchoraji ? Na umefanyaje ili uweze kupeleka mkono kinywani?

“Uviko 19 haijanithiri ki vile kwani kazi za illustration huwa nazifanyia nyumbani na sina ulazima wa kukufuata kule ulipo kwani kila kitu tunafanyia online. Hii kazi ninayojifunza saa hii nafanya kupitia Zoom kwa hiyo hamna haja ya kukutana.

Je unafunza watu kuwa wachoraji kama wewe? Gharama zikoje?

Natamani sana kufunza  watoto na watoto wa majirani na nafanya hivyo bure. Nimepewa karama bure, natoa mafunzo bure.

Una ushauri gani kwa artist yoyote anayeanza kwenye fani hii?

Kwa yoyote anayeanza kwenye fani hii anatakiwa kuwa na bidii. Bidii ndio kila kitu! Bidii ya kujifunza, ya kusikiliza wengine,kuskia watu tofauti na kuheshimu watu wote. Pia usikate tamaa kwa sababu kazi ya kuchora utajikuta unapiga zoezi mda mwingi kuliko kuingiza kipato.

Kipi kingine ambacho ungependa kusema ambacho sikukuuliza?

Swali ambalo hujaniuliza ni, “Unajiona wapi miaka kadhaa ijayo?

Najiona mbali kwa kweli, nahisi nitafika mbali kwa kweli. Nataka kuweka jitihada zangu kwenye kujifunza na kufunza wengine. Pia nataka miaka mitano ijayo  niwe na ofisi yangu, niwe nimetanua jina langu East Africa na kuweza kufanya kazi na watu toka Africa Mashariki.

Pia ningependa kujijenga Tanzania nifahamike kama illustrator, comic na artist kiujumla.

Kingine, nina mpango wakujifunza animation zaidi ili niweze kutengeza matangazo na story za watoto na kufanya kazi na mashirika ya wanawake na yanayotetea haki za watoto.

Pia natamani kuendelea kufunza watoto kuchora. Haya ndio malengo yangu ndani ya miaka mitano.

Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii na tovuti ?

Facebook: Paulina Barnabas Lugabulila
Instagram: paulinArt_tz
Safi sana kwa muda wako dada.

Sawa Asante pia kwa muda wako na kutujali wasanii.