Uchambuzi Wa Album: Panga Mbili
Msanii: Pizzo Madawa
Tarehe iliyotoka: 01 November 2020
Nyimbo: 17
Utayarishaji wa Beat na Mixing na Mastering: Wise Genius,
Studio: AMG Records

Mji wa Mbeya una ma emcee kibao kwenye historia ya hip hop hapa nchini Tanzania. Unapotaja ma emcee wa Mbeya lazma miongoni mwao watakuwepo wafuatao; Lugombo MakaNTa, Nala Mzalendo, Teddy Boombap na wakongwe kati ya wote aliyewahi kutokea Mbeya City, mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Mr. II aka Sugu) Mbunge wa awali wa Mbeya Urban.

Kwenye mwaka uliopotea kama wanavyodai watu wengine, 2020 ulikua mwaka wa baraka kuu kwa wana hip hop wa Mbeya kwani ma emcee kadhaa toka mkoa huo waliachia album na EP zao kama vile Nala Mzalendo ila baraka kubwa iliyotokea ni emcee Pizzo Madawa kuachia album yake ya kwanza rasmi.

Pizzo ambaye amekuwa msanii toka mwaka 2015 aliachia album yake iitwayo Panga Mbili. Album hii ambayo imewapita mashabiki wengi wa hip hop ni album iliyolaliwa maskio na mashabiki wengi wa hip hop mwaka huu wa 2020.

Pizzo Madawa anaejulikana rasmi kama Ipyana Ngoloka ni mzaliwa wa Mbeya. Jina “Pizzo” ni urefu wa kiwakilishi cha pili (P) toka kwa jina lake rasmi Ipyana ilhali “Madawa” ni jina la utani alilopewa bibi yake mzaa baba ambaye alikuwa maarufu kwa kutibu na kutabiri kitu kuhusu mtu na kitu kile kikaweza kutokea maishani mwa mtu yule.

Kwenye album hii Pizzo anaonesha kuwa mbegu haianguki mbali na mti wake maana album hii inajaribu kubaini na kutibu yanayoisibu jamii kwa mfano kwenye nyimbo kama Mgonjwa wa Jamii au kutabiri kama kwenye Njiwa.

Album hii ambayo imeundwa studio za AMG kule Mbeya chini ya usimamizi wa Wise Genius imejaa sitiari, historia, mafumbo na hekima. Kwa mfano nyimbo kama Safari akimshirikisha Jay P na Msitu ni nyimbo zimeandikwa kwa mtindo wa mafumbo na zinakufanya utafakari kwa umakini anacho chana Pizzo.

Panga Mbili ni lugha ya picha yenye tafsiri mbili tofauti ambazo ni Lugha na Mashairi. Kwenye wimbo Baba Wawili picha hii inaonekana vizuri pale Fasihi anapoongea na wanawe Andishi na Simulizi,

Anasema hivi kwa Andishi,

"Mwanangu Andishi, wee nguzo nakuegemea/
Tatizo kubwa hupindishi, pindi ujumbe ukipokea/
Unanipa simanzi wee ni pato la wachache/
Vipi unakosa ujenzi hip hop udongo wenye tope/"

Pia anamwambia Simulizi hivi,

"Wewe ni kaka mkubwa kwa jina la Simulizi/
Unapofoka kama jibu usiku unakosa usingizi/
Hakika wee ni kongwe toka zama za enzi/
Kirwa kivirinje Korogwe misafara ya kinyamwezi/"

Hii album imeundwa na kuandikwa kwa ustadi, hakuna nyimbo ya kuruka hata utangulizi wa album ambayo ina anza na kinanda kizuri na mwongozo unao tolewa na Pizzo kuhusu utakachokipata toka kwa album hii ni mzuka sana

Nyimbo zilizosimama ambazo sijazitaja hapo juu ni kama Vita Ya Kale ambayo inaonesha kuwa kijana anathamini mchango wa askari wetu wa jadi waliopoteza maisha yao ili tuweze pata uhuru wetu. Pia anatoa tahadhari kuhusu uvutaji wa Sigara na kutuelezea umuhimu wa Laki Tatu Na Nusu na vitu ambavyo yeye anaweza kufanya akiwa na pesa kiasi hiki.

Kwangu binafsi, album hii ni moja ya album bora ya mwaka wa 2020 na naweza sema kwa uhakika Pizzo Madawa amejipatia shabiki mpya.

Kupata mradi huu wasiliana na Pizzo Madawa kupitiia;

Facebook: Pizzo Madawa
Instagram: pizzo_madawa
WhatsApp: +255768243864