
Uchambuzi wa EP: Tujenge Taifa Letu Tanzania (TuTaLeTa) EP VOL 2 #Magufulification
Msanii: Plate Mdaijasho
Tarehe iliyotoka: 18.04.2021
Nyimbo: 4
Waunda Midundo/Wtayarishaji/Wahanganya Sauti Na Midundo: Mwamba Mgumu(Sima On The Map Yoh), Black Ninja, Moz B, Stim Masta
Studio: Boombap Clinic (B.B.C), (Best Studio)
Plate Mdaijasho kama emcee na mwanaharakati amekuwa akituhimiza tulijenge taifa letu Tanzania kila kukicha. Mwaka jana wakati yeye binafsi aliweza kugeuza maneno kuwa vitendo na kuanzisha harakati mpya kwa jina Tujenge Taifa Letu Tanzania(TuTaLeta) ambalo alilifanyia kazi zaidi kwa kutumia kipaji chake cha uandikaji mashairi na kughani kwa kutupatia EP yake ya kwanza kwa jina TuTaLeTa EP Vol 1 ambayo kwa bahati nzuri tuliuchambua hapa hapa Micshariki Africa.
Wakati aliyekuwa rais wa Tanzania hayati John Pombe Magufuli alipokuwa akihimiza watu wapige kazi watu wengi waliitikia wito hili la kujenga taifa lao kwa kujihusisha na shughuli tofauti kama vile kilimo, ufugaji, biashara na hata umachinga. Na taarifa zilipotoka kuwa mzee katuacha, Plate kama muasisi wa TuTaLeTa akaona hakuna njia bora ya kumuenzi shujaa wake tofauti na anavyojua na anavyoweza kufanya yeye. Aliingia studio na kutupatia Tulijenge Taifa Letu Tanzania (TuTaLeTa) EP VOL 2 #Magufulification.
Mradi huu ambao upo chini ya usimamizi wa Simple Versity Entertainment unaanza na wimbo wa Alisema aliomshirikisha Ormie29 kwenye mdundo wa Sima On The Map ambao unapiga vizuri sana, tarumbeta, vinanda wakati Ormie 29 akitueleza uzandelo ni nini. Kwenye ubeti wa pili emcee huyu anatupakulia madini kwenye Plate akisema,
“Ifike hatua tuzalishe nguo zetu/
Zikichakaa wazungu wavae mitumba yetu/
Tuthamini vitu vyetu Tanzania ni ya kwetu/
Tutakufa tutaiacha ni urithi wa kizazi chetu/
Msidhani wazungu wanatupenda sana/
Hizi chanjo zinazokuja zingine hazina mana/
Tujiridhishe kinachokuja tukielewe kwa mapana/
Kuna nchi walipigwa chanjo hawakupata mimba wasichana/
Sheria zote ziandikwe Kiswahili/
Ifundishwe somo la historia ya taifa hili/
Wanyonge wapewe haki zao wanazozistahili/
Maskini asionewe na wanojiita matajiri/
Mlizoea kuishi kama malaika/
Mtaishi kama shetani mpaka mtakapobadilika/
Mkilipa kodi itatumika/
Kuleta maendeleo kwa watanzania wenye shida/”
Nakwenda ni wimbo wa pili kwenye EP hii ambao umepigwa kwenye mdundo mzuka sana ambao Sahani anautumia vizuri kutema mashairi yake . Nukuu za sauti za mzee zinaskika mwanzoni mwa wimbo huu juu ya vinanda freshi sana. Kwenye kiitikio emcee anamuaga mzee kwa kutukumbushia pia kuwa baba yake mzee Sahani yuko kule ahera pia akisema,
“Nakwenda nakwenda Mungu kanipenda/
Nakwenda alipo Donii alipo mzee Sahani/
Naaga duniani tutakutana mbinguni/
Furahini kwa sababu nilipo ndo kuna amani/”
Magufulification ambao ndio wimbo uliobeba jina na EP hii ndio wimbo wa tatu toka kwa EP hii. Wimbo unapiga vizuri sana, taratibu ambapo unaskia gita zuri sana kwenye mdundo murua sana wakati hotuba tofauti tofauti za JPM zikiskika kwenye wimbo kama kiitikio. Kwenye wimbo huu Plate anasifia sera za JPM japokua anakubali kama mtu yoyote vile kuna vitu flani pia alivifanya ambavyo hakukubaliana navyo akisema,
“Sikusubiri afe ni msifu/
Sikukosea niliposema muadilifu, mwaminifu na mtiifu/
Nilikosoa kwenye udhaifu siku kashifu /
Nilimponda ki binadamu kwa nidhamu kwenye ukweli yakinifu/”
Na sera ya Magufulification ni nini?
“Misingi ya formula hii kwanza uhuru wa mawazo/
Uhuru wa maamuzi bila kuhofia vikwazo/
Kuamini unaweza kuongoza bila wahisani/
Itakujenga na kusimamia sera zako za ndani/
Urafiki hauhitajiki kwenye uwajibikaji/
Apply utumbuaji kwa wala rushwa na mafisadi
Usisitize uchapakazi kile sector kila ngazi/
Kata minyororo ya unyonyaji na upigaji/
Simamia rasilimali bila woga/
Fuatilia kila miradi wacha soga/
Angalia mikataba inayopora/
Uchumi wa taifa uibadili iwe bora/
Usihofiwe kuwa kera/
Usiingiliwe zako sera/
Kisa wao wana mitaji wakupangie usije mbwela/
Wawekezaji wakwepa kodi waondoke/
Wabaki walipa kodi japo wachache usiogope/”
Wimbo Kundi Lake unatufikisha tamati kwenye somo letu la Magufulification ambapo emcee Plate anatuambia kuwa JPM alikuwa mtu wa kimapinduzi kawa wendazake akina Patrice Lumumba, Che Guevara, Samora Michelle pamoja na Kwame Nkurumah. Kwenye mdundo mzuka Plate anaonesha vile mjomba kama anavyomuita JPM hakupendwa na mafisadi ila watu wa hali ya chini, mama ntilie na machinga walivyompenda sana.
Mradi huu ulikuwa wa kumuenzi shujaa wake JPM na amemuenzi vizuri kwani ukiskia vile hotuba zake zilivyokua na ucheshi zimetumika kwenye mradi huu utahuzunika lakini kufarijika na kuburudika. Kazi kwetu kuhakikisha Tunajenga Taifa Letu Tanzania (TuTaLeTa) EP VOL 2 #Magufulification tunaendelea kuzi apply ili kumuenzi hayati John Joseph Pombe Magufuli (Alale Pema Peponi).