EP: TuTaLeTa EP Vol 1
Msanii: Plate MdaiJasho
Nyimbo: 5
Tarehe Iliyotoka: 20.02.2021
Wapiga Midundo na Ma Producer: Stim Master, Black Ninja, BornStar & Moz, Mwamba Mgumu(Sima On The Map), Ghost Kifaa, 10th Wonder
Mix & Mastering: Stim Master na Ghost Kifaa
Studio: Nexus Studio, Action Records, Boom Bap Clinic (B.B.C)
Plate MdaiJasho amekuwa kwenye game la Hip Hop toka 2005, ila ukitaja jina lake nina uhakika baadhi ya mashabiki wa hip hop hata wanaofuatilia ma emcee waliopo handakini watauliza huyu emcee ni nani.
 
Plate MdaiJasho ni emcee aliyezaliwa Kigoma 12 mwezi wa 4, Msukuma-Mnyantuzu anaye wakilisha mitaa ya Ushirombo, mkoa wa Geita. Baada ya kuanzisha mradi wake wa t-shirt 2015 wenye chata liitwalo “Dai Jasho Lako”, alianza kufahamika kama MdaiJasho ilhali Plate likiwa ni tafsiri kwa kimombo la jina Sahani ambalo ni la ukoo wa msanii huyu.
 
Plate ni emcee mzalendo ambae baada ya kuwaza nini anaweze kufanya ili kujenga taifa lake la Tanzania alipata wazo la kuwahamasisha vijana wenzake kwa kutumia kauli mbiu ya Tujenge Taifa Letu La Tanzania au ki ufupi TuTaLeTa ambalo baada ya kuwashirikisha wadau kwenye mitandao ya kijamii mmoja akashauri atoe mradi ambao ni EP iendayo kwa jina TuTaLeTa EP Vol 1. Plate ananuia kuachia miradi ya TuTaLeTa baada ya huu wa kwanza nia ikiwa ni kuona jinsi gani atachangia ujenzi wa taifa lake la Tanzania ili kuliokoa toka kwa majanga ya njaa, magonjwa na ujinga ambao ndio maadui wakuu watu wa nchi nyingi duniani kote.
 
Kwa emcee anayetoka ukanda wa madini, Tanzania, je EP hii yake ya kwanza itakolea madini?
 
Mradi huu ki ujumla ni madini mwanzo mwisho. Sahani ya TuTaLeTa ina milo mitano mizuri inayoweza kukunawirisha ki mawazo. EP imejaa somo la kihistoria kwa mfano kwenye wimbo wa kwanza uitwao “Kalamu Inakumbuka”. Kwenye wimbo huu Plate anaichimba kwa kina historia ya nchi yake iliyofichwa na kutuletea historia ambayo haifunzwi hata mashuleni kwetu. Kalamu ya Mdaijasho inaanza hivi,
 
"Kalamu yangu inamkumbuka, historia imemtupa/
Mwasisi wa Tanu aliyeshiriki kutupa/
Uhuru tulionao kwa kuvumilia shuruba/
Za mkoloni, kwangu ni shujaa mkubwa/
Sikufunzwa darasani/
Kadi ya Nyerere namba 1 ilisainiwa na nani/
Wala sikuskia mtaani/
Sikuskia jina la shujaa Ally Sykes bingwa wa shabaha vitani/”
 
Sahani hii pia inatupatia chakula cha kiroho kwenye wimbo uitwao “Mungu Hakupanga” ambapo Plate anatoa onyo kwa wale wanaopenda kumsingizia Mungu kwa kifo chochote kinachotokea dunia. Utaskia wengine wakisema, “mipango ya Mungu” hata kama aliyekufa alikua jambazi aliyemiminiwa risasi na polisi. Plate anasema wazi kuwa vifo vingine ni sisi wenyewe tunavisababisha kulingana na vitu tunavyofanya na maisha tunayoishi. Anasema hivi Plate kwenye vesi ya pili ili umuelewe vizuri,
 
“Magonjwa yanatengenezwa, yanaenezwa, dawa inauzwa/
Dawa iki expire, mwaka mwezi hugeuzwa/
Ilikua 2020, inaandikwa 2030/
Hawajali madhara yake wanachosema wao ni Thanksi! /
Dawa Ya kutibu kichwa inazalisha mwilini cancer/
Pesa wanaingiza, wanajiliza unapodanja/
Wanaigizi kifo chako na kusema, “Mungu kapanga!”/
Ila ukweli wanaujua dawa zao zina kisanga/
Ni binadamu anauza sukari feki/
Mafuta, chumvi, vinywaji vingi vina mu affecti/
Mbegu za GMO madhara yake hayaelezeki/
Na wanayaita maendeleo kwa maskini hayakwepeki/”
 
Plate ni emcee anayejua kinachoendelea duniani na iwe ni mbegu za GMO au chanjo tunazoletewa toka nje, yeye anahoji kama zinatumwa kwetu ili kutuangamiza.
 
“Mpwa” iliyoundwa ki ustadi na emcee Mwamba Mgumu (anayejiita producer Sima On The Map pia) Ni singo ambayo Plate anaongea na sisi wapwa zake kuhusu nini tukifanye ili tufanikiwe maishani. Singo imejaa madini mwanzo - mwisho na kwenye vesi ya pili Sahani anatukumbusha,
 
“Bora ugali bila masimango/
Kuliko wali kuku, huku unapigwa mabango/
Weka mpango endelevu/
Usiombe hela, omba hekima na werevu/”
 
Single Mama iko ndio ya nne kwenye Sahani hii na inaongelea haki za binadamu hususan kwa wanawake sanasana ambao kwasababu moja au nyingine ni baba na mama kwa watoto wao.
 
MdaiJasho anatuachia ya kutafakari anaposema,
“Majina mabaya yote umepewa/
Unaitwa malaya, mzazi mwenzako anaheshimiwa/
Anajisifu, kwenye jamii anasifiwa/
Pongezi anapewa, hahudumii, anazingua/”
 
Stim Master ndio anatupakulia msosi wetu wa mwisho uitwao “Fanya Yako” inayotuhimiza tu jishughulishe na maisha yetu kuliko ya watu wengine kwani hii ni ndio njia ya uhakika na kipekee ya kujijenga mwenyewe na pia ya kujenga taifa lako.
 
TuTaLeTa EP Vol. 1 ni mradi uliokamilika kiujumla; sauti, midundo, viitikio, mashairi, wageni walioshirikishwa kwenye mradi hadi hata jaladio la mradi limekamilika kwani vyote hivi vimemuwezesha emcee huyu kufanikisha nia yake ya kuleta kauli mbiu itakayowasukuma vijana wa Tanzania ili Tujenge Taifa Letu Tanzania.
Plate ameshatupa madini, fanya jukumu lako tulijenge, tujijenge, tuyajenge.