Uchambuzi Wa EP: Mask Off EP
Msanii: Demetrius Eugen - Ponera (Hon)
Tarehe iliyo toka: 01.06.2020
Nyimbo: 6
Utayarishaji wa beat: 10th Wonder | Bigdilla | Salii tecnik | Flyboyjr

Kwa lugha ya Kiswahili Mask ina maana mbili, barakoa na kinyago cha usoni, na vyote ni muhimi sana maishani mwetu. Madaktari, wauguzi na watu flani kama wachomeleaji (welders/boilemakers) utumia barakoa ilhali waigizaji na hata kwenye tamaduni tofauti dunianu utumiaji wa vinyago umeshamiri.

Kwa sasa kifaa kinachotumiwa na watu wengi duniani cha kujikinga dhidi ya maradhi ya Covid 19 ni masks au barakoa lakini kama vile walivyo piga ugonjwa wa Corona buti na uvaaji wa barakoa hapa Tanzania msanii Ponera (Hon) nae pia ameamua kutushawishi tutoe vinyago vyetu ili tuishi maisha halisia. Ponera anatuomba kutoa vinyago vyetu ili tuweke vitu wazi, ili tuishi maisha ya kweli, na tutofautishe kati ya nyeusi na nyeupe na sio kusema vitu kwa kujificha au kutoa vitu gizani na kuviweka palipo wazi, kwenye mwanga.

Ishu za vinyago kwenye sanaa ni kawaida; angalia cinema ya The Mask, au nyimbo ya Mask Off ya The Future au M.A.S.K ya The Fugees toka album yao ya The Score.

Kama wasanii wengi wa bongo wanavyo anzia sanaa, Demetrius Ponera anavyo julikana rasmi alianza mziki akiwa bado shuleni Songea, Tanzania. Aliingia rasmi studio mara ya kwanza 2007 akiwa kidato cha tatu (Form 3) na kuachia nyimbo yake ya kwanza rasmi iitwayo Nyuzi 90 kule Songea nyumbani kwenye studio iitwayo Seyfee Records. Toka hapo hakuwai kurecodi tena hadi 2011 alipokua chuo IFM na akabahatika kurekodi ngoma tena na wataalam toka Mlab Duke Tachez na Mujwahuki na track iliitwa Matrix ambayo ilimtambulisha rasmi kwenye game.

Mheshimiwa (Honerable) Ponera amepata heshima kubwa toka kwa mashabiki wake kwani yupo makini na uandishi wake wa mistari na kupitia EP hii nadhani heshima yake itazidi kuongezeka. Mask Off inamtambulisha rasmi Ponera ambae ni msomi mwenye Shahada ya Bima na Udhibiti wa Majanga (Bachelor of Insurance and Risk Management) na Post Graduate Diploma ya Education (PGDE). Amekuja kutuelimisha kuhusu umuhimu waku ondoa vinyango vyetu na anatupa Bima ya uhakika kua majanga yoyote yanayo weza kutukumba yatadhibitiwa.

1. MaskOFF

Nyimbo inaanza kwa Rais wa Tanzania Dr. John Joseph Pombe Magufuli akiwahimiza watu wasiogope ugonjwa wa Corona na wasijisumbue kuvaa mask (barakoa) kwani ugonjwa utapita bali wachukue tahadhari. Mask Off. Ponera anaanza intro akisema,

“Mask Off/
Eyo, Covid 19/
Dunia nzima kwenye vita/
Hakika, uchumi umetinghisika/
Raia ina angamiza/
Muhuni navua mask alafu ghetto najifukiza!/
Malimau, matangaziwi na maji/
Nakunywa, pembeni nina chupa ndogo ya ‘nyag/,
Sijajifungia ndani, ila naishi kwa tahadhari/
Naepuka pia mitandao inayo potosha habari/
Msome Mange, Instagram, au Twitter Kigogo/
Utahisi dunia imekwisha kwa stori za uongo/

Pia anaonyesha vile viongozi walikua na maamuzi magumu yakufanya kuhusu kuweka watu lockdown au kuwaacha wawe huru kama zamani ila wakichukua tahadhari,

“Endeleeni kuchapa kazi, “Ooh viongozi vichaa”,
Basi kaeni ndani, “Ooh mta tuua na njaa!”

Ni dhahiri toka kwa wimbo huu kua Ponera anakubaliana na Rais kua watu waishi kwa uhuru bila ya woga unao letwa na Covid 19.

2. Chumvi ya mawe ft Ghost The Living na Gamba Junior

Kwenye mdundo huu ulio undwa na 10th Wonder, Ponera ana ungana na wenzake toka kwa kundi la Sau State Huru kutupa maajabu ya mistari kama vile maajabu ya Bibilia yalio tokea ambapo mke wa Lutu alibadilika na kuwa chumvi ya mawe pamoja alipo geuka nyuma kuangalia Sodoma na Gomorah ilipokua ikiangamizwa kinyume na maagizo waliyo kua wame pewa,

Anasema hivi Ponera,

“Chumvi nyingi kwenye game/
Dingi gwiji la mistari/
Ghost ana niita shem navo rhyme ki ukali/
Vile mi hu rhyme wana conflict sana/
Complete kama, Sau State wana/"

Nae Ghost anaachiwa mistari ifuatayo…

“Weka kando stress na miziki ya mihemuko/
Kichwa kiko race, na mititi uhamie huko/
Kama ishu ukombozi mziki wangu niambe upo/
Nachokupa madini yateme u force salo/
Nachotema usiripoti kama upo sharo!/”

Gamba Junior nae anakuja kwa hasira akitukumbushia hivi,

“Na wa acha mbonge/
Nikiibuka ni kama Chuna ka kutana na Kongwe/
Booth inageuka ring, shusha makonde/”

Mlio zoea vitamu leo utatu huu wana walisha chumvi ya mawe.

3. Naua Polisi (Remake)

Nyimbo hii mtunzi wake halisia ni Adam Shule Kongwe ila yeye ali uita NP badala ya Naua Polisi. Ponera anaendeleza zoezi la kuweka vitu wazi na anauita wimbo kwa jina lake kamili kama ilivyo takikana…Hana ubaya na polisi bali polisi mweye ubaya . Anatanguliza samahani kwa IGP(Inspector General of Police) kwanza, kisha anatupa historia ya beef yake na polisi huyo anae mlenga akisema,

“Umetoka bush kuja kuanza kazi hapa Dom/
Huna paku fikia/
Jogoo la shamba hali wiki town/
Waka kupokea wana, ndani ya chumba kimoja/
Cha ajabu umepata vumba umeenza kuleta vioja/”

Ana endelea hivi kwenye vesi ya pili

“Kitaani si hatukai kwa raha/
Unavyo timba na hizo gwanda/
Unatutisha balaa/
Unapelekesha wana,wakupe beer/
Unakunywa Heineken wahuni wanakulipia/
Dakika mbili, Defender inafunga breki/
Una mchota teacher Tall, unamchota Fule na Eddy/
Hadi Celli, afu kutoka hadi madusco/
Mna tu search na pukutisha mifuko/
Umeniweka ndani, umeni bandikia ngada/
Uraini naskia una mtamani mama Jada/
Kitoka kitanuka kama Kongwe/
Nikushike, nikubake, nikunyonge/”

4. Naendeshwa

Ushawai skia mwana mme anae endeshwa kama gari na mke au mpenzi wake na bado anafurahia? Basi mapenzi ya Ponera kwa mpenziwe yapo hivi na hajali,

“Tunavyo ishi tunajua sisi/
Oya kausheni/
Ndivyo ninavyo jibu wana wanapo uliza wana, “What happened?”/
Saa kumi mbili nisharudi home/
Barazani nimechill natafuna pop corn/
Ninekunja nne kwenye sofa nime enea/
Simu yangu anayo wife, ukipiga ata pokea/
Tunachezea vidoli, ninamsuka nywele/
Mara anipe mastori yaku msuta Sele!/"

Na tabia zake je?

“Kuchelewa kurudi maskani wife ana nuna/
Chakula siki kuti, hata unyumba hakuna/
Nikimgusa tu makofi na viwiko/
Ata kupiga hata na mwiko/
Mkorofi hadi mwisho!/
Nyumbani kwao nimejenga/
Na kisha wanaosema naendeshwa/
Wa ambie ni gari jipya!/”

Asalaa la!

Sio siri Ponera ana endeshwa kinyama ila anasema kua moyo wake hauna tatizo.

5. Viboko ft Eddy Banega

Kwenye biti mdogo mdogo ambalo juu yake imepigwa guitar nzuri Ponera anashirikiana na Eddy Banega wa Sau State Wana kuwachapa ma MC viboko.
Eddy Banega kwenya vesi la pili anasema hivi,

“Ma rapper wao ndio wana tuchekesha mtaani/
Eti, “Mii nafanya hip hop yakuchezeka flani”,/
Punch heavy weight kwa tembo sio sisimizi/
Presha ya ma rapper kwenye kila anoa ni dizi!/
Wakolonjinji!/ ”

Eddy Banenga anasisitiza kua wao ndio Wakolonjinji yaani kwa lugha ya Kingoni ni Wazawa halisi wa hapa nyumbani na kwenye hili game la hip hop Tanzania.

6. Maisha na Kifo

Nyimbo hii ina sheherekea uhai na kifo, inakubali kua kifo ni kitu cha kawaida na lazma tu kubaliane nacho kam vile kuishi ni kawaida. Kama vile tunavyo furahi binadamu anapo zaliwa, basi kifo nacho ni sherehe kwa namna yake pia. Kiitikio kinatuonyesha kua kama vile mtu anavyo kuja duniani ni siri basi kuondoka lini ni siri pia,

“Kuna sababu ya kuishi/
Pia na sababu ya kifo/
Kama chuma kinaisha/
Uhai unaisha hivyo/
Hamna utayari unapo taka kuzaliwa/
Ndio maana hatubishi unapo taka chukuliwa/”

Ponera anatukumbishia kua, “Kifo ni sawa na nyumba ndogo ambayo imezuiwa na gorofa!”

Japo kua album haikuwekewa nembo ya tahadhari kwa msikilizaji( Parental Advisory Explicit Lyrics) ilipaswa kua nayo kumpa shabiki tahadhari kua yaliyopo ndani ya EP si ya kitoto kwani, (Mask Off), kinyago kishavuliwa.

Kupata nakala yako cheki na Ponera kupitia;

Facebook: Demetrius Ponera
Twitter: DemetriusPonera