Ukaguzi wa Ep: Kumbukumbu Isiyofutika (K.I.F)
Msanii: Rabi James
Tarehe iliyotoka: 26.06.2020
Nyimbo: 7
Producer/Mpiga midundo: Black Ninja
Mchanganyaji sauti na midundo: Black Ninja
Studio: Boom Bap Clinic (B.B.C)

Mtwara inafahamika sana kama eneo linalozalisha gesi asili nchini Tanzania. Gesi hii imeifanya Mtwara kutambulika na watu wengi tofauti na awali. Gesi hii ilishaanza kusafirishwa kwenda Dar Es Salaam kwa njia ya mabomba hadi kiwanda cha kuipokea, kuiboresha na kisha kuisambaza kwa wateja kwa ajili ya matumizi.

Hivyo hivyo kutoka kule Temeke, Dar Es Salaam mnamo tahere 12 Mei miaka ya tisini baraka tofauti ilipatikana kwa kupitia kuzaliwa kwa mtoto Rabi James ambae ki asili ni mtu wa kusini mwa Tanzania Mkoani Mtwara. Rabi James ujio wake ulikuja kwa mazingira magumu kama vile gesi inayosafirishwa kwenda Dar tokea Mtwara ilivyopatikana kweye mazingira magumu wanayo ishi wakazi wa Mtwara. Kijana huyu alipewa majina James Victor Chilumba.

Baada ya kukua na kugundua kipaji chake cha uandishi na uchenguaji kijana James alijitosa kwenye ulingo wa muziki wa Hip Hop kwanza akitumia jina Monster wa Stanza kabla ya kubadili jina lake kuwa Rabi James kama anavyo tambulika na mashabiki wake wengi kwa sasa.

Kama vile majina yote ya emcee huyu Rabi James yana maana flani EP ya Kumbukumbu Isiyo Futika (K.I.F) ina maana yake pia. Rabi ni jina lenye maana tofauti; Rabi lina maana ya mwalimu kwa Kirumi ilhali kwa Kiarabu lina maana ya Mungu Mlezi. Kupitia msingi huu James alitohoa jina Rabi kumaanisha Rhymes and Bars Immortality.

Pia jina James lina maanisha “yule anayefuata” na kama vile gesi ya Mtwara inavyofuata bomba hadi kufika Dar kipaji cha James kimefuata mkondo wa ukoo kuja kuleta madini ya uchenguaji Dar.

Mradi wa K.I.F ni hatua ya pili kubwa aliyopiga mchenguaji huyu baada ya kuachia kanda mseto yake ya kwanza 2016 iitwayo Hisia Zangu. Kwenye mradi huu wa K.I.F Rabi ameamua kuongelea maisha yake na mambo aliyoyapitia hadi hapa alipofikia. Mradi huu unaonesha vile Rabi ni mbunifu kwenye uandishi wa mashairi yake, vile ana uwezo wa kutuhadithia na pia kutumia sitiari na mafumbo kutuelimisha.

“Mei 12” ambayo ni wimbo wa kwanza kwenye mradi huu ni wimbo wenye huzuni, masikitiko, majuto na matumaini. Rabi anajikuta akitupeleka alivyokuja duniani na changamoto za malezi alizopitia mama yake. Pia Rabi haogopi kutuonesha vile maamuzi ya baba yake yalivyochangia pakubwa maisha ya familia ya Rabi kuwa magumu. Kwenye mdundo mzuri unaogonga taratibu, Rabi anaachia hisia zake akikumbuka ujio wake hapa duniani,

“Kwa zile tabu ulizopata msafiri/
Hukuzifanya sababu ya kusitisha safari/
Hukujali ulipokwenda yaweza kuwa mbali/
Hukuwaza mateso ya jua na mvua kali/
Ulitunza ulichojenga na ukakipenda maradufu/
Ulipenda ulicho beba moyo ni mahabusu/
Hukujali japo ulitingwa na mengi/
Kilicho tumboni ni mali ilowindwa na wezi/
Uliibuka mshindi walipokupangia njama/
Walimwengu wenye chuki wakakufanyia drama/
Ukasimama imara leo najivunia mama/
Tumboni miezi tisa sio kitu rahisi/
Nilikula ulichokula kwa upendo thabiti/
Ni mengi ulipitia ila hukukata tamaa/
Mei kumi na mbili siku iliyofanyika shujaa/”

Wimbo huu unaonesha vile Rabi huyu alipokuwa ndani ya tumbo la mamake aliweza kuona mamake alivyokuwa akipitia magumu; ndugu walivyomtenga mamake, majonzi yaliyomjia mamake hadi alipojifungua. Wimbo wa kinabii kwa nabii.

Kipaji hiki cha kuandika mashairi tamthilia yanaendelea kwa wimbo kama vile “Macho Yangu” inayoongelea matatizo yanayowakumba baadhi ya familia tofauti zinazomzunguka Rabi James mitaa aliyokulia. Kwenye wimbo huu kalamu ya James inakuwa kama brashi la wachoraji lenye uwezo wa kutuchorea picha kwa maneno. Uwezo huu wa kuchora picha kwa kutumia maneno unaonekana pia kwenye nyimbo kama Simulizi Ya Rafiki na Mitaa Nayotoka. Pia stori za emcee huyu zina ucheshi kinoma kama kwenye wimbo wa Mitaa Nayotoka anaposema,

“Napotoka ni balaa kila baada ya nyumba gesti/
Sistaduu mmoja bar anakunywa bia kreti/
Ugomvi wa kina dada silaha ni viwembe/
Mabwana wanagombaniwa wanaibiwa ukiishi kizembe/”

Pia anaendelea kusema,

"Napotoka mimi wengi huogopa lakini/
Nyumba zetu ni vibanda mabati yapo chini chini/
Buchani ni kitimoto mezani miguu ya kuku/
Supu za mapupu kipande ni mia hamsini/
Kila siku ni vilio misiba watu wanakufa/
Wengi wanaishi kibishi baadhi yao wanajuta/
Vigodoro vinakesha singeli na viduku/
Mavazi ni chupi dera hereni na vikuku/”

“Kumbukumbu Isiyo Futika” ni wimbo uliobeba jina la album na hapa Rabi anafunguka zaidi kuhusu maisha yake ya utotoni aliyoyapitia. Mashairi ya huzuni yanamwagika kwenye mdundo wa ki boom bap wenye huzuni pia. James anashika kinasa na kukumbuka,

“Ugumu wa maisha ndio ulimfanya baba nyumbani akimbie/
Elimu yangu duni mi ni mtoto wa “Mama Ntilie”/
Wadogo zangu wawili nyumbani kaka ndio mie/
Ikabidi niishi kitumwa kwa amani nanga itulie/
Ndani ya nyumba ya kupanga kodi ni majanga/
Maisha magumu tunachomiliki ni kitanda/
Mawazo kichwani vipi pesa ntazichanga/
Mwanzo wa kuzurura kuokota chuma zisizo na shaba/”

Anaendela kufunguka zaidi kwenye vesi ya pili kuhusu kilichomfanya baba yake kuwatelekeza,

“Dunia ina vingi vya kutosha japo msingi ni ku focus/
Thamani ya ndoto hutegemea jinsi ulivyoota/
Umbali wa safari huanzia mbali ulipotoka/
Kuna watu walishashabikia nilivyosota/
Nilishapita visa vingi dhiki na mabalaa/
Sio simulizi kwetu kawaida kulala njaa/
Pongezi kwa mama James mama shujaa/
Tetesi za mdingi maisha yametiki analala baa/
Ndugu walipotutenga, majirani wakatupenda/
Tukajijenga japo maskini wa mali na fedha/
Kuna vitu nikikumbuka huwa nabaki na maumivu/
Nilipoziona mbichi nikaamini kuna mbivu”

Kwenye nyimbo mbili za mwisho Rabi anabadili mtindo kutuonesha uwezo wake wa kutema na pia kufanya kazi na ma emcee wengine aliowaalika.

Ep hii iliyoundwa kwa nia ya kumtambulisha kiundani Rabi James kwa mashabiki wa hip hop imefanikisha lengo alilonuia emcee huyu. Zoezi amelifanikisha vizuri akishirikiana na Black Ninja ili kutupatia mradi ambao utakuwa ni Kumbukumbu Isiyo Futika milele kwa atakayepata nakala yake.

Kupata EP hii ya K.I.F wasiliana na Rabi James kwenye namba ya simu +255 787 876 653 na mitandao ya kijamii:

| Facebook: Rabi JamesInstagram: @rabijames_raps |