Uchambuzi Wa Album: Nyuma Ya Kitabu Cha Historia
Emcee: Rabi James
Tarehe iliyotoka: 26/06/2021
Nyimbo: 15
Watayarishaji: Duke Tachez, Pallah Midundo, Black Ninja
Studio: Boom Bap Clinic

Nyimbo Nilizozipenda: Afrika Lazima Tuungane, Wakati Ni Sasa, Ninapoitazama Dunia

Rabi James

Mwaka 2021 ni miongoni mwa miaka pendwa toka kwa Rabi James, kwani ndio mwaka ambao alitupatia zawadi nzuri kwenye utamaduni wa Hip Hop na zawadi yenyewe ni NYUMA YA KITABU CHA HISTORIA.

Ni jina lililobeba album yake kwa mwaka huo yenye jumla ya nyimbo 15. Kwenye album hii Rabi kawashirikisha wasanii sita. Nash Mc, Trump Mc, K Wa Mapacha, Trickson bila kumsahau Frege toka WABETI.

Album ya nyuma ya kitabu cha historia ilibebwa na nyimbo nzito zenye ujumbe wa kutosha zifuatazo.

  1. Ninapoitazama Dunia.
  2. Mama Afrika.
  3. Afrika Lazima Tuungane.
  4. Nakukumbusha.
  5. Mashujaa waliopotea.
  6. Nyuma Ya Kitabu Cha Historia.
  7. Wakati Ni Sasa.
  8. Amka ft Nash Mc.
  9. Wasaa Wa Imani.
  10. Sitaki Kutoka.
  11. Majigambo ft Trump Mc(Mfalanyombo)
  12. Maujanja ft K Wa Mapacha.
  13. Sina ft Frege (Wabeti)
  14. Tulizo La Fikra.
  15. Sitihari 2 ft One Incredible, Trickson, Frege.

Watayarishaji waliotengeneza hii album ni watatu, Duke Tachez katengeneza wimbo namba 3. Palla Midundo katengeneza wimbo namba 8 na Black Ninja katengeneza nyimbo namba 1, 2,4,5,6,7,9,10,11,12,13,14,15.

Kwenye album hii nitazungumzia wimbo namba 3  Afrika Lazima Tuungane ambao umetengenezwa na Duke Tachez. Huu ni mmoja kati ya nyimbo kali sana zinazopatikana katika hii album ya Rabi. Huu wimbo kwa viwango naupa 8/10 sababu mdundo umesimama na mashairi yamesimama pia.

Rabi James anaanza kwa kutuambia.

Kinachotuweka mbali ni itikadi za kidini na ubinafsi/
Vita vya  umaskini na ujinga vipi tufaiti/

Ikiwa atupendani tunauana kila siku ili kupinga unyonyaji/(AFRIKA LAZIMA TUUNGANE)

Ukiyasoma au kusikia mashairi ya wimbo huo kwa alivyoanza lazima utajua na kutambua kwa sasa vita kubwa ya utengano juu yetu waafrika ni hizi dini zilizokuja na wakoloni tukiacha utofauti wetu wa kipato.

Rabi anazidi kuzungumza kiukombozi zaidi kwa kusema

Afrika tajiri bila umoja tunakufa umaskini/
Hakika tafsiri afande muoga hufa kambini/
Stop xenophobia Afrika kusini/
Tuishi kiujamaa tupinge vita dhidi ya umimi/
Vua uzungu vaa uafrika, tuishi kindugu/
Tuna tamaduni zetu ya nini tuishi kizungu/
Chini ya lugha moja hoja nyeupe hazitotumudu/
Kufika mafanikio(afrika lazima Tuungane.

Yaliyotokea bondeni kwa Madiba si mageni masikioni mwetu wengi wetu tunafahamu kilichowapata wenzetu toka kwa waafrika wenzetu Ilikuwa ni hatari juu ya hatari.

Afrika lazima tuungane ni mmoja ya wimbo ambao inapaswa watu wengi tukaupa sikio kwa ukaribu zaidi ili kuyajua mengi zaidi.

Tukiachana na wimbo huo naweza kusema tusimame kwenye  wimbo namba 7 Wakati Ni Sasa.

Wakati ni sasa Rabi anaanza kwa kukwambia
Rafiki wa mvivu ni usingizi/
Umaskini na ujinga humfanya mzawa kuwa mkimbizi/
Tupa shuka mpiganaji halali zama hizi/
Ndoto ukifanya kuwa ndoto kitandani hautimizi/

Kwa mashairi madogo tu hayo inapaswa wale ndugu zetu wa Madiba kama tuwape wasikie wataweza kujua nini cha kufanya kwa maisha yao maana kumtoa uhai mgeni au kumchukia sio njia ya wewe kufanikiwa kimaisha njia ya wewe kufanikiwa ni kujaribu kujifunza kutoka kwa wageni yale mazuri yao.

Umaskini ni kuchagua kuwa tegemezi/
Hatua za kushindwa ni kumaanisha kuwa huwezi/

Na umalaya sio duka la mapenzi.

Apo pia kawagusa dada zetu na wakata tamaa wote. Utamu na ubora wa huu wimbo ni bora ukadaka kopi yako ukasikiliza mwenyewe neno baada ya neno mstari baada ya mstari.

Majigambo ni wimbo namba kumi na moja ambao yupo Rabi na Trump Mc, huu wimbo beti ya kwanza kaanza mtu mzima Trump. Trump kapita kwa kujitamba kama unavyomjua Trump ukimpa nafasi anakutambia na kukuchana pia .

Trump anafungua beti kwa mtindo huu

Mimi ni emcee wa karne, nisiyehasibika/
Nawachana wachache wasioelimika/
Nafundisha wafalme waliojivika/
Napunguza wanaume wasio na kipa/
Sogea ukatwe na panga la shika/
Jichanganye ubebwe na gari la taka/
Jivimbishe uchanwe na biti la kita/

Kwa mistari hiyo ushapata picha Trump ni mchanaji wa aina gani kwenye mitindo ya kujigamba. Tuachane na Trump tuje mpaka ubeti wa pili kwa kijana wetu Rabi mwenye album yake.

Nishachafuka tenzi kama fundi rangi kwenye ukuta/
Zaidi ya kidonda Rabi ni risasi kwenye mfupa/
Sikopeshi mimi ni mangi kwenye duka/
Dhambi ni kuhusisha Hip Hop na hizo bangi mnazovuta/
Pumbavu sifanyi kapuka ni bombamp/
Sina swaga za kihindi kati mkwiji juu kanzu/
Zaidi ya mjeshi ni jemedari/
Juu ya mdundo nachokifanya ni mauaji ya kimbari/
Rapa nuksi ukijihisi mkali njoo uzame booth/

Tusimalize utamu wa wimbo wa majigambo kikubwa ni kupata nakala na wewe ujigambe ulipo kama walivyojigamba Rabi na Trump kwa mbwembwe kama msemaji wa chama cha mziki.

Mama Afrika ni wimbo wa pekee sana huu naupa 9/10 humu Rabi kaonesha kile ambacho mama wengi wa kiafrika wanadata navyo wakiamini ni jambo sahihi kwao kumbe ni upotevu wa fikra na kizazi chao kinachokuja.

Nani asimame kutetea upuuzi wako/
Utandawazi ndio umefanya umepoteza asili yako/
Umepoteza uhalisia kwa kudhani kuwa mweusi haupendezi/
Ukanunua rangi ya dukani ukauchubua mwili
Hili ufanane na mzungu/
Umegeuka mtumwa wa fikra unaendeshwa kinguvu/
Mama Afrika umevua lemba unavaa wigi/
Umechonga sigi usoni umejaza makeup nyingi/
Nyinyi kwa nyinyi hampendani mnajikweza/
Mnahisi maendeleo ni ushindani wa kujilemba/
Ipo wapi ngazi mliyopandishwa/
Medani ya maarifa umeshaitupa/
Hauna hadhi hauna jipya /

Vizuri ukapata nakala yako kuweza kujua wimbo mama Afrika kaambiwa nini juu ya uafrika wake na afrika yake kiujumla.

Nakukumbusha ni wimbo namba nne toka kwenye hii album yetu bora kabisa. Humu tunakumbushwa mengi na emcee wetu yale ambayo tunataka kuyazoea kumbe sio mazuri kwetu.

Nakukumbusha kumbuka kuwa kuna maisha baada ya kifo/
Mungu mmoja kuna mwanzo pia na mwisho/
Tofauti za kidini tuziheshimu kama miiko/
Mwafrika uwe muislamu ama mkristo/
Nakukumbusha kijana pambana na hizi zama/
za sasa na utandawazi
Epuka kuishi kwa drama/
pinga ushoga na mabinti wanaosagana/

Kwa kifupi umeona kile ambacho anatukumbusha ndugu yetu basi na mimi nakukumbusha ununue hii album ya Rabi James upate elimu zaidi na zaidi.

Amka ni wimbo namba nane nao unapatikana kwenye album, humu yupo na Nash Mc hakuna mtu asiyejua na kutambua uwezo wa Nash katika kuandika mpaka kuwasilisha kile alichokiandika kwa jamii yake. Huu ni wimbo mzuri kwani ma emcee wote wawili wamefanya makubwa kwenye kuandika mpaka kuwasilisha kile walichonacho.

Maujanja ni wimbo namba 12. kwenye huu wimbo yupo maujanja mwenyewe K wa Mapacha hakuna asiyejua Maujanja na ubora wa tungo wa K wa Mapacha akiwa kwenye kinasa. Humu K Wa Mapacha kakupa maujanja anayopiga na matumizi anayofanya kibabe sana.

Sina ni wimbo namba kumi na tatu, humu kasimama na Frege toka WABETI. Frege ni miongoni mwa ma emcee wabaya sana kwenye kuandika mpaka kuchana. Frege mpe mada na mdundo kisha ngoja mauaji yatakayotokea kwenye huo mdundo ndio utajua Rabi hakukosea kumpa nafasi kwenye santuri hii.

Nyuma ya kitabu cha historia ni wimbo ambao umebeba album nzima ya Rabi ni wimbo ambao umesimama sana ni wimbo ambao unaturudisha tena darasani kujua na kufahamu historia yetu waafrika kwa uzuri na undani zaidi.

Nyuma ya kitabu cha historia kuna ukungu/
Iweje historia ya muafrika iandikwe na mzungu/
Waliotuaminisha kuwa hatukuwa na mungu/
Asili yetu ni manyani hatukuwahi kujimudu/
Mwafrika narudishwa mtumwa vitabuni/
Kwa kuonesha ushaidi wa picha za kubuni/

Beti ilianza kwa mtindo huo ambao kama tukichunguza zaidi kinachoimbwa tunaona ukweli upo na umesimama vizuri juu ya historia yetu.

Harakati za uhuru mababu twawapongeza/
Kina mama mashujaa kitabuni wamepotezwa/
Kitabu kinaficha uhalisia wa historia ya mwafrika/
Tafakari usomacho kilichoandikwa/
Nyuma ya kitabu vingi vinafunikwa/

Chunguza yaliyomo kitabu kinapindisha.

Leo tunafunga na wimbo uliobeba album Nyuma Ya Kitabu Cha Historia tusapoti kwa kununua kazi ya kijana wetu. Naamini utakipata kile kilicho bora na chenye ubora wa hali ya juu sana. Tuishi na Rabi James tuishi tukisikiliza nyuma ya kitabu cha historia toka kwa Rabi.

Kisha naweza sema ukidaka kopi yako jaribu kusikiliza wimbo namba moja Ninapoitazama Dunia  ni wimbo ambao unazungumzia mengi juu ya dunia yetu kiujumla.

Napoitazama dunia ni udhia umekithiri/
Vya asili vinaangamia ushetani umeshamiri/
Binadamu tunauana hizi zama za ukatili/
Ndani na nje ya mipaka nyuklia imeshamiri/
Hatupendani tunajengeana matabaka/
Ubaguzi wa rangi na tofauti za kisiasa/
Kisa dini tunauana/
Lini tutaungana/
Tunasahau dunia sio yetu tunahama/
Makundi ya ugaidi yanazidi/
Al Shabab Boko Haramu IS kwenye miji/
Zinazalishwa sumu tunauna sisi kwa sisi/
Dunia hadaa ulimwengu umejaa na ibilisi/

Tudake kopi  ya kijana wetu Rabi James.

Anakwambia wanapinga mitara wana promote ushoga.

Album inapatikana kwa njia ya zote cheki na Rabi James kwa namba hizi +255673099139.

Mfuate Rabi James kwenye mitandao ya kijamii:

Facebook: Rabi James
Instagram: Rabi James