Uchambuzi Wa Album: Mimi Ni Huyu
Emcee: Rama Wise
Tarehe iliyotoka: 01.07.2022
Nyimbo: 16
Watayarishaji, Mixing & Mastering: Abby MP, Kise P, Mock Beatz, Gs, Duppy
Studio: Digg Down Records, Kinasa Records, Non Stop Music, Uprise Music

Nyimbo Nilizozipenda: Mradi Wote

Rama Wise

Mtu anapokuwa mdogo huwa anajikuta ana ndoto nyingi sana ambazo cha ajabu zinaweza kubadilika kila kukicha ikitegemeana na maisha ya yanavyompeleka. Kijana atajikuta leo akisema anataka kuwa daktari, mara kesho mwalimu mara keshokutwa mchezaji mzuri wa mpira, mara hili mara lile.

Kwa Rama Wise safari yake ya kimaisha pia ilikuwa hivyo hivyo ila yeye ilifika mahala akasema anataka kuwa mchanaji na akasimama kidete hadi akafikia lengo lake. Emcee huyu baada ya kuachia singo kadhaa ambazo zilimzolea mashabiki kadhaa alikuja na mradi wake wa kwanza rasmi Mimi Ni Huyu.

Najirudi

Unapoanza kuskia mradi huu moja kwa moja utaona kuwa Rama Wise alifanya maamuzi sahihi kuwa mchanaji. Mradi huu ambao una ngoma kumi na sita unaonesha uwezo wa uandishi, uchanaji na uimbaji wa kijana huyu.

Kazi inaanza kwa mdundishaji Abby MP kumpatia midundo minane na kusema kweli wawili hawa wameshirikiana freshi sana kwenye ngoma zote.  Kwenye singo ya pili iliyoachiwa rasmi Majaribu unaliona hili bayana. Akiwa na Rhino King ambaye anasimama kwenye doria la chorus, Rama Wise anatupatia mawaidha, onyo na wosia akisema,

Majaribu

“Kuchakarika kila kunapokucha/
Pilika pilika kuipigania future/
Naumiza kichwa wakati ni ukuta/
Najichanganya palipo na wengi utanikuta/

Palipo na wengi kuna ya kujifunza/
Naamini palipo na wengi kujitunza/
Palipo na wengi kuna mengi nachuja/
Ya kuzingatia na kuna mengi yanakuja/

Wenye moyo safi pia kuna wakuda/
Wapo wanafiki na wazee wa kukunja/
Wajuaji wakianzisha ujuaji navunga/
Nipo kama sijuagi mi nna yangu sina muda/

Wa kupoteza, napambana kuwekeza/
Changamoto zinaegama nilipo jielekeza/
Nikiziendekeza ntajikuta napoteza/
Uelekeo kama nisipojiongeza/

Imani yangu kuna siku itafunguka milango/
Nimejitoa kwa hili naiamini mipango/
Ndio muda sahihi ningali na nguvu bado/
Kwa uwezo wake Allah itafunguka milango/”

Kemia hii nzuri unaiona tena kwenye Mimi Ni Huyu ambao ni wimbo uliobeba jina la album na maudhui yote ya mradi huu. Pia wimbo huu ndio utakutambulisha rasmi kwa Rama Wise kama ulikuwa umfahamu. Hakuna ngoma za kuruka hapa wanapokutana hawa wawili kama vile enzi hizo marehemu G.U.R.U na DJ Premier au tukiwa hapa nyumbani kama vile Dizasta Vina na Ringle Beats. Baada ya hapa wawili hawa wanaongelea mapenzi vile yana run dunia kwenye All About Love akiwashirikisha Mantik Barz na Steven Viza.

Wawili hawa wanashirikiana vizuri tena kwenye Jipe Muda akiwa na Trayo Version ambao ukiweka bass vizuri kwa woofer yako utamuelewa Abby MP vizuri ilhali treble litakuletea hisia freshi Rama anapokuhimiza ujitafakari kwa kina kwa lolote unalofanya. Pia Rama Wise anaonesha freshi kuwa inapokuja kwenye kuimba yeye pia sio ki polepole akituambia,

“Jipe mda unapotaka kusogea/
Jipe mda unapotaka kuongea/
Jipe mda unapotaka kitu/
Jipe mda ukiamini kwamba iko siku/”

Kwenye Nenda akiwa na Shobi Mzawa na Bosco Tones mapenzi ndio mada tena ila wakati huu watatu hawa wanawaaga wapenzi wao kwani wameshindikana.

Nyimbo mbili za mwisho walizo shirikiana Rama na Abby ni wimbo wa tisa Chombo Mrama akiwa na Amphoterick Tanzania, na singo ya kwanza toka kwa mradi huu akiwa na mwana Morogoro mwenzake Nyenza Emcee na muimbaji Jay Oncer kwenye Nimejirudi ambao unaongelea umuhimu wa kutambua mapungufu yako na kujirekebisha.

Baada ya hapa watayarishaji wengine wanashika doria na wote pia wanacheza na viwango vya TBS/KBS alivyoviweka Abby MP. Mtayarishaji Duppy analianzisha nae pia kwenye kwenye Only Love akiwa na Duppy ambapo Rama Wise anamuimbia mpenzi wake kabla ya mtayarishaji Mock Beats kuendelea kwenye Mawazo Yangu, Zawadi ya Mchoro akiwa na Duga Mawe (Nginja Nginja) na Junior Prosper na tena kwenye Iko Hivyo ambao ndio wimbo unaotufikisha tamati kwenye mradi huu.

Mtayarishaji Gs kutoka Non Stop Studio naye anatamba kwenye Ushauri Sio Amri (USA) ambao unapiga tarumbeta flani mzuka sana. GS pia anaskika kwenye Wana wakati huku akishirikishwa malkia muimbaji/mchanaji Jadah MaKaNTa wakitutahadharisha kuhusu wanafki wanaojiita marafiki zetu.

Mtayarishaji Kise P akiiwakilisha Kinasa Records sawia na Mock Beats anakwenda na Vina ambapo wapo wageni waalikwa mnyama “Tripple Double” Experience na Makunga. Kise P anafunga shift yake ya kazi na wimbo Siongei ambapo Rama anajipima uwezo na Fivara anayeiwakilisha  Mwanza, Mwamba Mgumu aki represent Shy town na Adam Shule Kongwe akibeba jiji la Dodoma na manispaa ya Singida begani mwake.

Rama Wise kawasili. Ni vyema mkae chini, mumpatie mda na maskio yenu ili muweze faidi madini yaliyopo kwenye mradi huu. Mradi umesimama ndani ya maudhui ya elimu mwanzo mwisho na wote walioshirikishwa kwenye kanda hii wamemuwezesha emcee huyu kuacha alama ya kudumu. Mimi Ni Huyu ni Rama Wise na msingi mzuri wa safari yake ya muziki.

Pata nakala yako ya mradi huu kwa shilingi alfu kumi tu (10,000Tshs/500Kes). Mcheki Rama Wise kupitia

Instagram: ramawise
Facebook: Rama Wise(Rahaswa)
WhatsApp: +255 782 395 998