Rasta Michael

Unaposikia jina lake Rasta Michael, moja kwa moja kinacho kuja kichwani ni kuwa lazma jamaa ana dreads, ni shabiki wa mziki wa Reggae na kula ganja lazma ni mambo yake.

Ila unapopata fursa ya kuongea naye unapata picha tofauti; Rasta Michael ni emcee wa Hip Hop na kinyume cha matarajio ya wengi hana rasta kabisaa!

Toka nilipoanza kumfuatilia Rasta Michael pale Instagram baada ya kuona mtu aki share picha ya kazi yake Nje Ya Dunia nilichogundua kwa emcee huyu ni kuwa ni mpiga kazi. Ndani ya miaka 6 Rasta Michael amefanikisha kuangusha albam 9 na zote zipo Boomplay bure kwa ajili ya mashabiki zake kuweza kuzipata kirahisi, kuzipakua na kuziskiza. Cha kushangaza ni kuwa mwaka huu 2021 Rasta Michael kaachia albam tatu na moja japokua ishatoka na ipo Boomplay inatakiwa itoke rasmi 27.11.2021

Kusema kweli kwa albam tatu kati ya hizo tisa nilizoweza kuziskiliza  kando na idadi, hata ubora wa miradi yake upo vizuri.

Leo nimepata fursa ya kufanya mahojiano naye kwa njia ya kisasa ya WhatsApp ili tuweze kumfahamu.

Karibuni sana!

Karibu sana Rasta Michael hapa Micshariki Africa. Kwanza kabisa tuanze kwa kufahamu. Unaitwa nani rasmi na unatokea wapi?

Nashukuru sana, na asante kwa muda wako Kefa.

Naitwa Michael Fratern Temu.

Natokea Buza kwa Osama Temeke. Nyumbani kabisa ni Kilimanjaro. Mimi ni Mangi(yaani Mchaga )

Rasta Michael mimi nakufahamu kama mwana Hip Hop. Jina Rasta sana sana linahusishwa na watu wa Reggae. Ilikuaje hadi ukaanza kujiita Rasta Michael?

Nilijiita Rasta Michael kwa sababu Rasta sio kuimba Reggae bali Rasta inamaanisha kuzaliwa upya kiroho. “Rasta ndio jina jipya la kristo" na mimi si Michael mimi ni roho ambayo ni Christ (Rasta). Michael ni jina ambalo nilipewa na wazazi so nikaamua kujiita uhalisia wangu ambao ni Christ (Rasta) Michael.

Tupe historia yako ki mziki? Ulianzaje na upo wapi kwa sasa?

Kuhusu mziki na history yake ki ujumla, baba anapenda sana mziki na mama anapenda sana sanaa ya ushairi na alishawahi kunipatia vitabu viwili vya mashairi ambavyo ni mashairi ya Shabani Robert na mashairi ya Sadani. Hapo nilijikuta napenda sana kuandika mashairi kutokana na mama. Kuhusu mziki baba alikua na kanda nyingi za mziki wa akina Gatho (Beevans),  Pepe Kale, Papa Wemba, Madilu (System) na siku za jumapili akiwa nyumbani alikua  anapiga mziki sana hivyo basi tokea mdogo mziki ulinichukua kutokana na mshua

Ila sikuweza kuonesha kipaji changu kiurahisi kutokana na wazazi wangu wote walikua ni waalimu halafu mimi ni mtoto wao wa kwanza na walitegemea niwe daktari, engineer (mhandisi) au  padri au nirudi kwenye uwalimu. So sikuwa na njia ya kuonesha kipaji changu mpaka nilivyoenda chuo Mwanza (Kusomea Mahusiano na Jamii  na Masoko) nikawa mbali na wazee ndio mwaka wa pili chuoni nikiwa na miaka kama 23 ndio nikaanza rasmi harakati za muziki, kurekodi na kwenda ku perform kwenye majukwaa kama Gogo Vinu, Back To SUA na kilingeni.

Nilipomaliza chuo ndio nikarudi mjini Dar Es Salaam na nikaanza harakati rasmi za muziki na ilikua ngumu sana kwani wazazi walichukia na ndugu wali nipotezea hata na marafiki kwa sababu nilikua kama naanza safari wakati nimeshamaliza chuo na badala nitafute kazi ya ofisini nahangaika na mziki wangu

Sikujali nikaanza kurekodi album yangu ya kwanza inaitwa Mkono Wa Jah huku nakwenda ku perfom kilingeni Msasani Open Mic kwa Fid Q, Kinasa kwa Nash Emcee, kwa Watunza Misingi, Nafasi Art Lyric Lounge pamoja na Chi And Friends Masaki. Niliendelea kutoa album hadi sasa nina albam tisa kwa kwa kipindi cha miaka kama sita na nusu . Kiukweli na mshukuru Mungu maisha yanaendelea . Ordinary person extra ordinary work!

Rasta Michael, nimeona we ni mpiga kazi sana. Nimeona una kama albam 9 kama sijakosea pale Boomplay. Unaweza kutuorodheshea miradi yote na lini ilitoka? Ulifanikiwa vipi kuachia miradi yote hii?

  1. Mkono Wa Jah -27.04.2017
  2. Nafsi Ya Mtu Ndani Ya Utu - 28 .01.2018
  3. Nguvu The Album akiwa na Dizzo (White Mkatikili)– 10.02.2019
  4. Nani Kama Mungu – 26.05.2019
  5. Fuvu La Mtu Wa Kale - 27.11.2019
  6. Tunu The Album - 16.07.2020
  7. Mzunguko Mzima 360 – 21.05.21
  8. Nje Ya Dunia – 13.08.2021
  9. Yedidia - 27.11.2021

Ilikua rahisi kwa sababu niko kwenye mpango. I mean, I walk to follow my will nikimaanisha Nanuia, natembea kufuata kile nilichonuia.

Mbona uliamua kuweka miradi hii kwa streaming apps, sanasana Boomplay? Je inalipa?

Mwanzo nilianza kutoa CD lakini sikuweza kufikia watu wengi. Kwa mfano Mkono Wa Jah album yangu ya kwanza haikusogea sana lakini wakati huu kwa kutumia teknolojia nimefikia watu wengi sana kwa muda mchache sana na ni moja ya mafanikio.

Kando na mziki Rasta Michael unafanya shughuli zozote tofauti ili kuweza kujikimu kimaisha?

Mbali na kufanya mziki nina studio yangu na ninauza mitumba pia. Pia nina kazi ndogo ndogo za udalali wa viwanja  na pia ni fundi rangi.

We umesajiliwa na record label yoyote au ni emcee wa kujitegemea?

Sijasajiliwa na label yoyote najitegemea mwenyewe. Familia yangu  ndio inani push hapa na pale.

Je wewe unapiga chombo chochote cha mziki?

Kuhusu kupiga kifaa hapa bado sija master kifaa chochote ila najifunza kupiga gitaa na kinanda pia.

Ni ma producer au ma emcee gani wewe una ndoto za kufanya nao kazi?

Natamani kufanya ngoma na Damian Marley, Nas, Adele, Lauryn Hill, Joey Bada$$, Dizzy Wright kwa upande wa wasanii. Kwa ma producer Pharrell William., Dr Dre, Timbaland, Justin Blaze  na Stephen Marley.

Ulishawai kupiga show iwe ni yako binafsi au kwenye matamamsha? Je wana Hip Hop wanafanya matamasha ya kutosha ili mashabiki wawaone au hamna kitu? Changamoto ni nini juu ya haya matamasha?

Kiukweli bado sijaweza kuandaa show zangu mwenyewe ila nina mpango huo soon if Jah Bless. Bado hakuna matamasha ya kutosha ya Hip Hop na kuhusu matamasha ya Hip Hop mengi niliyohudhuria yamejaa ubinafsi na ukanda na kujuana.  Hilo nalo ni changamoto anayopitia underground emcee.

Kwenye nyimbo zako huwa nakuskia unapoongea kwenye wimbo huwa una lafudhi ya ki Nairobi, hii imetoka wapi au kwa nini wapenda kuongea/kuigiza kwa lafudhi hii?

Oioi kaka hii imetokana na mimi kusikiliza sana ngoma za kina Jua Cali, Kinga Kaka (Sungura) , Wyre, Bobbi Mapesa,  Gmwat , Nyashinski na wengine wengi! Kutokana na kuwasikiliza sana nikajikuta napenda kuigiza kuongea kwa hiyo lafudhi.

Ni kipi kinachokupa hamasa ya kuandika mashairi yako na je mashairi yako yamelalia upande upi sana au mada za aina gani ?

Matatizo, furaha kiujumla mlolongo mzima wa maisha ndio unanifanya kuandika mashairi yangu. Mashairi yangu hubeba maudhui ya kujitambua na kuwa na mtazamo chanya.

Unaona ni kipi sisi wadau wote tunaohusika na Hip Hop ya handakini tunatakiwa kufanya ili kuhakikisha kua mziki wa underground Hip Hop unaendelea kuwa relevant?

Kama underground artist tunatakiwa kuishi tunachokihubiri ili kikubalike pande zote maana Hip Hop ni maisha halisi.

Una maoni gani kuhusu Hip Hop ya nchi zinazotuzunguka hapa Africa Mashariki?

Maoni yangu kuhusu Hip Hop ya Afrika Mashariki ni sisi wana Hip Hop wa Afrika Mashariki kujikubali kufanya mziki unaoendana na mazingira yetu na sio kuiga maisha ya magharibi. Pia tuenzi utamaduni wetu na lugha yetu kwenye utamaduni wa Hip Hop.

Kipi cha mwisho ungependa kusema ambacho sijakuuliza kando na kupatia vijana wenzako wanaotaka kuwa ma emcee pia wosia?

Kila emcee anatakiwa ajitambue na kujua kuwa utofauti ndio utampa heshima na pia sio kufuata tu mtiririko. Inabidi tuweze kuanzisha vitu vipya na chanya kwenye utamaduni. Na kingine ni kuuelewa mchezo kabla hujaucheza na kujiwekea malengo ya kutimiza la sivyo tuta tengeneza wana Hip Hop masikini.

Pia tuzingatie sana upendo, amani na umoja, ufahamu na ushawishi juu ya mambo chanya kwa sababu ndio malengo makuu ya Hip Hop.

Nashukuru sana ndugu maswali yako ni mazuri na yenye ujazo ndio maana nimechukua muda mrefu kuyajibu kadri ya uwezo wangu. Pamoja Sana .One Love

Mcheki Rasta Michael kupitia mitandao ya kijamii;

Instagram: rasta_michael
YouTube: Rasta Michael