Ukaguzi Wa Albam: Nje Ya Dunia
Msanii: Rasta Michael
Tarehe iliyotoka:13.08.2021
Nyimbo: 15
Ma Producer na Wapiga Midundo: Odilla Beats, Crazy Newton, Kali, Yowen Beats, Pinna, JB Beats
Wachanganya Sauti na Midundo: Tinnie Cousin, Crazy Newton
Studio: Cosmic Sounds

Rasta Michael

“Tembea uone mengi” ni msemo wa Kiswahili ambao lengo lake kuu ni kukuhimiza kuondoka kwenye himaya yako ulioizoea na kwenda nje ili uweze kuona mazuri yaliojaa duniani. Japo kua neno tembea linamaana ya kuhamisha mwili wako toka eneo moja hadi nyingine kwa kwenda kalesa au route 11 ambayo ni tafsida inayo maanisha kutembea kwa miguu, au kwa kutumia chombo cha usafiri kama vile baiskeli, gari, meli au hata ndege kuna njia zingine za kutembea bila ya kunyanyuka toka kitini mwako.

Aina za kisasa za matembezi ni kama kutumia utanda wazi uliopo, vitabu na pia mziki. Kwa kutumia mbinu hizi pia mtu anaweza kutembea ki akili na kunusa mchanga wa ardhi iliyo mbali, anaweza kuona wanyama pori ambao pengine angeiacha dunia bila hata kujua kama wanyama aina hii wapo duniani na pia anaweza kuskia ngoma za mataifa tofauti bila hata ya kwenda kwenye nchi zinazo piga ngoma hizo.

Nikiwa katika matembezi yangu ile mitaa ya Instagram nilivutiwa na tangazo moja la jamaa flani anae jiita Rasta Michael. Katika hali ya kutaka kufahamia nae ilibidi niongee nae anipe bio yake na ndipo nikafahamu kua jamaa ni mwanamziki wa Hip Hop ambae kama Solomon anamalengo ya kua na Wisdom au Hekima. Kuongea nae zaidi ndipo nikagundua kua kama mimi Rasta ni mtu anaependa kutembea na anamalengo ya kwenda hata Nje Ya Dunia!

Kama vile safari ya kilomita alfu moja huanza na hatua moja mradi huu unaanza na mlio wa gari likiwashwa tayari kuanza safari ya kwenda Nje Ya Dunia akisema Rasta Michael, “Chuma Imewaka” ilikutuambia kwamba chombo kimenoa n’anga. Na ili kulifanikisha hili Rasta Michael ameshirikiana na watu wenye uwezo wakumpeleka na kutupeleka hata sayari za mbali yaani Cosmic Sounds kwenye albam hii.

Wimbo wa kwanza unaotufungulia mradi unaitwa Shairi ambapo unapiga vinanda taratibu ukisindikizwa na sauti nyororo ya dada flani kwenye kiitikio akisema,

“Shairi umenistiri sitakuacha nyuma/
Shairi mwenye asali zawadi toka kwa mama/
Shairi zaidi ya kauli umezifuta lawama/
Shairi umeniajiri nakupenda umenisoma/”

Wimbo huu unaonesha vile shairi ambalo Rasta Michael alipewa na mamake utotoni ulivyo badili maisha yake na vile anavyolithamini shairi lake. Wimbo mwingine ambao unaonyesha umihumu wa shairi kwa emcee huyu ni Juu Ya Piramid akiwa na producer Tinie Cousin akisema Rasta,

“Kawaidi unachoskia ukielewa utapata heri/
Ndani ukiingia utapata bila shari/
Unaimani vumilia upate jibu la swali/
Ushairi umenimendea umenipiga kabari/
Unaimani vumilia upate jibu la swali/
Ushairi umenimendea naona umenipiga kabari/”

Kama kawa kiitikio kinapiga freshi sana roundi hii akiwepo Tinie Cousin. Viitikio vya kuburudisha na kuelimisha vinapatikana kwenye nyimbo kibao kwenye mradi huu.

Utafutaji kwa ajili ya kujikimu ni mada ambayo imeguswa kwenye nyimbo kama vile Kazi Iendelee akiwa na Micky Greyz pamoja na Fanikisha. Nyimbo zote mbili zimeundwa ki ustadi sana na mashairi yanatiririka freshi kabisa. Kitu ambacho amefanikisha kuweka kwenye nyimbo hizi mbili na nyingine zilizopo kwenye mradi huu ni uwezo wake wakutumia lafudhi ya sheng kama madoido au nakshi zakuongeza ladha albam yake.

Katika matembezi yake Nje Ye Dunia Rasta Michael pia akaona vile mapenzi yapo kila alipo kwenda na kwenye Show Me Some Love akiwa na Teddy na Gwanta wanashirikiana kutupatia wimbo mzuka sana ambao Teddy anaua kwenye kiitio ilhali wimbo wenyewe unakuchangamsha na kukuingiza dance floor na mdundo mzuka ambao juu yake inapiga tarumbeta nzuri sana. Wimbo mwingine japokua si wa mapenzi ambao unanondo kibao na unauwezo wakukuingiza dance floor ni Cheza Unapo Chezaga ambao una flow nzuri na midundo wazimu sana; echo sounds, key board sounds safi, xylophone sounds, kicks na snares kwa sana na msisitizo toka kwa Rasta Michael akikwambia “Cheza, Cheza Unapo Chezaga”. Bata na sherehe ni hali ya maisha nyumbani na popote pale duniani utakapo kwenda.

Nyimbo zingine ambazo nimezipenda kwenye mradi huu ni kama Chagua na Unaweza akiwa na MickyGreyz tena na pia Nadhubutu ambazo zote zinaonesha vile vitu flani maishani mwako ni maamuzi yako tu. Kwenye Nadhubutu kuna mluzi au mbinja inapiga vizuri sana kwenye mdundo flani unaotumia kinanda. Nyimbo hizi zote ni chanya sana na zinakufanya utafakari kuhusu uwezo uliowekwa ndani yako.

Changamoto za kimaisha na  za kidunia kiujumla hua hazikosekani na kwa kulitambua hili Rasta Michael anatupa nyimbo mbili zinazo gusa mada hii ambazo ni Nakumbuka Mbali na Nipe Dakika na zote kama kawa zimeundwa ki ustadi sana. Tinie Cousin na Rasta Michael wana blend vizuri sana. Nipe Dakika ni wimbo mzuka sana yenye mashairi ki Shaaban Robert.

Nyimbo nyingine zilizosimama toka kwenye mradi huu ni kama Kiumbe Kipya ambapo Rasta anakiri kuzaliwa upya na kupenda chimbuko lake la Africa kwenye beat kinanda tu na kiitikio kinachotumia autotune flani mzuka sana wa Tinie Cousin. Tinie noma sana na kambariki Rasta Michael na midundo safi sana kwenye albam hii wakati Rasta anatema mashairi yake…

“Silence is more than an answer/(naam)
Ukimya ndio kitu natafuta/
Fanya kujituma mbio ukifunguka/
Maarifa kutafuta utafika wasipo fika ukibadili tabia/
Relax, fanya kujiachia kwa fas/
Mengi utaelewa unahitaji kua happy kufika ulipo dhania/
Usimeze makapi kiini ukaachia/
Wanauliza ni saa ngapi ukungu umewazidia/
Naipotezea limelight legend anapata fear…/”

Pia Wapange Wasikupange ni wimbo mzuka sana ambao mashairi, midundo na kiitikio vyote vimepikwa vikapikika. Bass ya wimbo huu pia unapiga tofauti sana. Daah.

Single ya kwanza iliyo beba mradi huu ni Huu Sio Muda akiwa na Dully Fashion. Mdundo, mashairi, backup vocals, na lead gita flani wazimu sana zinapiga taratibu.

Mimi binafsi nilifuharia matembeze yangu Nje Ya Dunia na nimekuja kuleta ripoti chanya juu ya kile nilicho kiona na kukisikia kama Joshua na Caleb walivyo leta ripoti chanya kuhusu Caanan. Tembeza skio lako handakini na utatambua kua emcee unadhania anajajua kua anae jua zaidi Hawakukosea wahenga walipo nena kua kama unadhania mama yako pekee ndio anajua kupika chakula basi wewee unapaswa kutembea Nje Ya Dunia ndio utajua hujui!