Flyin Saucer

REKUSA (Rudisha Elimu Kupitia Ujasiriamali Na Sanaa Asilia) leo walitua Dar ili kuweza kukutana na emcee mmoja hatari anayetoka kwenye kundi la Pochaz. Kama vile jina lake linavyoonesha jamaa mistari na michano yake inatoka nje ya dunia hii na amekuja kuvamia himaya ya Rap bongo na Africa Mashariki akitumia mtutu wa peni yake, karatasi na kinasa.

Karibuni mpate elimu toka kwa emcee huyu.

Majina yako kamili katika vyeti

Majina yangu ya serikali ni Constantine Martin Vangwani.

Ulianza lini game yako rasmi, je ni watu gani kuanzia hapa nyumbani mpaka ughaibuni walikuhamasisha kuingia kwenye game?

Mimi rasmi ku rap nilianza 2001 katika ma concert ya shule, shule secondary, lakini rasmi kuingia studio ilikuwa 2004 hivi ndio moto ulipamba.

Watu walionihamasisha sana wengi ni wa Marekani hii ilitilokana na mazingira niliyokulia na kuishi ilikuwa ni sanasana watu wanafuatilia watu wa mbele sana kuliko bongo lakini naweza sema watu kama Pharcyde, De La Soul, A Tribe Called Quest, Organized Confusion, Snoop Dogg, Spice 01, MC Eight, Nas, Fugeez, Mos Def, Keith Murray na wengine kibao lakini bongo ilikuwa Kwanza Unit, Weusi Wagumu Asilia na Diplomats ndio nilianza kuwasikia lakini siku ya kwanza nilipomsikia  2Proud nikawa shabiki yake toka that day. Wengine kina SOS B, GWM walinihamasisha sana.

Na kwa nini ulichagua upande wa Hip Hop Rap na sio upande mwingine?

Nilichagua Rap coz ilinivutia sana, ilikuwa kitu kipya masikioni toka utoto, nimekulia familia ya wapenzi wa muziki so toka mdogo dada na kaka yangu wanaimba na kuwa na ma album ya kina Dona Samma, Ace Of Base na compilation za Break Box, Shaba Ranks, Coco T, Chakademus and Playaz sasa nikawa naigiza sana hizo nyimbo ila bro alikujaga home na tape ya Snoop Doggy " Doggystyle" akawa ana rap ile "Lo di da di" yote ambayo iko kwenye album ya Silk the Jeweler aka Bald Head Silk "The Story Teller" hiyo 94 nadhani ilinichanganya sana na mimi nikawa naimba ile track nikiwa na umri mdogo sana bila hata kuelewa maana yake.

Toka hapo Hip Hop ikawa na mimi pia bro wangu alikuwa anapenda sana na anafuatilia mno hivyo kama albums za ma emcee nyingi nilizisikiliza home nikiwa bwana mdogo sana toka hapo nikakuwa na Hip Hop mpaka leo.

Now unajulikana kama Flyin Sosa, kabla ya hapo umepitia identity nyingi kutokea Cons CADA mpaka hapo ulipo, nini kimechangia kubadilisha identity zako mpaka hapo ulipo, na ni tofauti zipi ulizo nazo mpaka sasa kwa mabadiliko ya identity zako katika game?

Cons Caddah ilikuwa tu kifupi cha Constantine hadi leo mitaani na home wananiita Cons, na Caddah ilikuwa kifupisho cha Caddahuno ilikuwa ni movie moja ya mambo ya madawa kulevya ya zamani. Kuna mhusika mmoja miondoko yake walikuwa wanadai nafanana nae basi wakanibatiza hivyo mimi nikafupisha tu jamaa aliitwa Caddahuno, nikaamua kujiita hivyo miaka mingi wengine wanadhani ni kada kama kiongozi tena.

Ikaja Flyin Saucer hii ni kutokana kwanza na aina ya uandishi wangu sio wa kawaida sana kama watu walivyozoea jamaa mmoja alisema mimi ni extraterrestrial(alien), na pia kutokana na upenzi wangu wa muda mrefu kusoma mambo ya anga(astronomy), kwa watu wanaofuatilia na wanaojua mambo ya anga wanajua chanzo cha flying saucer(u.f.o), hivyo mimi nikajiona nimekuwa mpya tena kwenye ku elevate my mind nimekuwa kitu kipya duniani kama flying saucer ilivyoonekana mara ya kwanza, nikaamua kujiita Flying Saucer, na SOSA ilikuwa ni acronym ya Soldier Once Set A.W.O.L(Absent Without Official Leave)hii ipo jeshini kwa wanajeshi wanaotorokaga kambini, kuna muda Hip hop ilinitoka sana nikawa sitaki nilivyo.

Na game inabadilika na akili zetu zina evolve hivyo nikaona sasa mimi ni Flyin Saucer kwa namna ambayo nimebadilika kwenye ufanisi wa muziki na harakati zangu kwa ujumla na Flyin Saucer naona ndio jina husika linalonifaa zaidi kwa aina ya emcee nilivyo.

Najua uko katika kundi la Pochaz kwa sasa ila kabla ya hapo ulikuwa kwenye kundi la Roho Saba au Seven Soul Immortal, naomba historia kidogo ya Roho Saba mlivyokutana mpaka mkaungana kuwa kundi, albums au mixtapes mlizofanya, je mlikuwa wangapi na kwa nini hilo kundi halipo tena, na kama lipo mna mpango gani wa baadae?

Kweli mwanzo tulikuwa Roho Saba (Seven Souls Immortal) wahusika watatu kati ya wanne wote tulisoma shule moja secondary ya Azania, shuleni hatukuwa kundi lakini wote tulikuwa ni wapenzi wa Hip Hop na mara kwa mara tulikuwa tunachana madude ya mtoni sana. Baada ya kumaliza kidato cha nne 2002, mwanangu Edwini Mwakalasi (O.N.E (Organize Niggaz Everywhere) akaenda St Anthony, mimi nikaenda Makongo na HONDA (Hope On Nigga with Dead Ambition) akawa Midland High School tukawa tunatembeleana na bado tuna ndoto za kufanya muziki bongo.

Nikiwa Makongo High School 2004-05 nikakutana na classmate wangu Jabir (Wu Bill or The Kill Bill) alikuwa anapenda sana Hip Hop basi tukawa pamoja nikamkutanisha na wanangu kadhaa na yeye akanikutanisha na wanae kadhaa wote tunapenda Hip Hop tukaamua kuwa kundi moja kuleta nguvu, hapo ikaja Roho Saba. Jina hili lilitokana na verse moja kwenye kwenye Ufunuo wa Yohana Mbatizaji, nadhani Ufunuo 1: beti 4 kwenye Biblia hivyo tukajiita Seven Souls Immortal.

Tulifanya track ya kwanza kwa Bonny Luv lakini haikupata nafasi sana tukawa na D Man wa Downtown Records alitaka kutupa label lakini akasafiri kwenda USA na sisi tukaachana nae. Plan yetu ikawa ni kuwa na studio yetu. Taratibu tukaanza kununua vifaa tukarekodi mixtape ya kwanza nyimbo 22 lakin haikuwa katika ubora sana kwa sababu vyombo bado vilikuwa sio bora. Tukarekodi mixtape ya 2 nyimbo 28 pia haikuwa na ubora wakati huo tunakutana na Ludigo akatukubali sana akasema anatupa label. Kabla hatujarekodi akazinguana na mwenye studio anaitwa Chima, mpango ukafa.

Tulipo maliza shule Edwin akaenda kusoma Tumaini University lakini hakumaliza akaachia njiani akaenda India kusoma sound engineering sisi tukabaki na harakati mtaani. Edwin akiwa India akaanza kununua vifaa; akanunua mic, keyboard na mixer, akawa anafanya production ambayo tuliita Jumba Bovu Record. Bahati mbaya Edwin alikuwa na kisukari akafariki India, basi kwa kuwa yeye ndio alikuwa kama nguzo yetu kwa sababu alikuwa anapata msaada toka kwao wa kifedha toka kwa kaka zake ambao wako mamtoni sisi tukapoteza dira. Roho Saba ikapotea, vifaa vilirudi lakini bro wake akavishikilia, rafiki yake alikuwa Langa wote wakawa watu wa kula madude harakati zikaisha.

Kwa nini Pochaz? Ilikuaje kuaje mpaka kuanzishwa kwa Pochaz? Na kwa nini awe Ado Tembo na si mwingine katika kuunda Pochaz? Je baada ya album ya Hofu tutegemee kazi nyingine kutoka Pochaz?

Pochaz ilikuwa sio kitu rasmi kama kundi ilikuwa ni mjadala tu. Mara nyingi tulikuwa tukikutana maskani flani Tabata baada ya kuhamia kule toka Ilala, ilikuwa ni ofisi na maskani lakini ilikuwa ofisi ya ki Hip Hop sana, watu wengi walikuwa wanakuja pale.

Sasa huwaga inatokea mijadala mbalimbali kwenye maongezi. Kuna kisa kilitokea tukawa tunajadili maswala ya wawindaji haramu (majangili). Mjadala ukaenda mbali sana mpaka ikafikia hatua tukajikuta hata sisi ni majangili kwa namna moja au nyingine, kwa sababu utakuta hawa wawindaji wengine walikuwa wanaishi kabla ya mapori na misitu kufanywa hifadhi za taifa na walikuwa wanawinda pale miaka yote lakini serikali ilivyokuja ikaweka utaratibu na ukiuvunja utaitwa jangili.

Ingawa wapo watu ambao wanatoka mbali pia kuja kufanya ujangili kwa hiyo hata kwenye maisha halisi tukajikuta kuna vigezo vinatufanya tunakosa uhalali kwenye mambo mbalimbali kwenye jamii hivyo tunaishi kama majangili tu.

Na ilikuwa Ado Tembo kwa sababu ndiye mtu aliyekuwa active katika maskani yetu, hivyo tulikuwa wawili tu ambao tunachana sana mistari. Hivyo ikawa kama utani tunaitana Pocha Pocha basi ikawa mimi na Ado tulikuwa rhyme partners wa muda mrefu tukaamua kufanya jambo pamoja tukajiita hivyo hivyo Pochaz at the same time ni lyrical Pochaz pia.

Baada ya Hofu album tulikuwa tayari tumeshaanza kurekodi album mpya 2020 chini ya Paradise Apple Records. Tulikuwa na tracks kama 5 au 6 hivi lakini studio kidogo ikafungwa kwa kipindi flani ila imerudi tena juzi na mpango uko palepale, nadhani tutaendelea tulipoishia.

Je baada ya Pochaz kwa maana ya album kuna kazi kutoka kwako ukiwa kama solo artist, kama upo unaitwaje na ulitoka lini?

Mimi binafsi nina kazi nyingi pale Paradise Apple. Project ya kwanza ilikuwa ni album yangu iliyokuwa inaitwa "Yakuti Samawi" lakini ilibidi nisiitoe, nadhani sio kipindi chake. Nikaamua kurekodi album nyingine ambayo ndio "Mzimu wa Ngende" itakayotoka hivi karibuni kwani umekamilika kwa asilimia 90%.

Baada ya "Mzimu wa Ngende" itakuja "Yakuti Samawi". Nilitoa track ya utangulizi inaitwa Kwanta 2020 nadhani ndio track ya kwanza kwenye album ingawa haikusikika sana sikuifanyia promotion sana kwa sababu nilibadili mpango nikaiacha tu iwe kwenye album.

Yakuti Samawi unamaanisha nini?

Yakuti Samawi ni rangi ya zambarau imekaa kifalsafa zaidi. Maisha ni Yakuti Samawi kama rangi ya madini ya rubi.

Kwa hapa kwetu game ya Hip Hop unaitazama vipi?

Game ya Hip Hop iko vizuri sana ilipofikia kwa sababu kipindi ambacho sisi tunarap mazingira yalikuwa magumu sana tunategemea radio tu, lakini sasa tunajulikana kupitia mitandao ya kijamii. Ilikuwa ngumu kipindi hicho watu wengi na rushwa imekithiri wote tunataka kupigwa redioni, ila sasa iko mzuka.

Ni vitu gani haukubaliani navyo katika game yetu ya Hip Hop?

Watu wa handaki huku kidogo naona kuna ubinafsi na kuvimbiana bila msingi wowote, kuna matabaka ya watu kusapotiana, haipo love kwa wote kama walivyo wa bongo fleva, huku kila mtu mjuaji saaana.

Katika vitu ambavyo haukubaliani navyo, nini ushauri wako?

Tukiweza kuwa kitu kimoja tutapiga hatua nzuri zaidi.

Unaweza kuzungumzia kidogo ile tofauti yako na Nikki Mbishi, ilitokana na nini? Kuna vyanzo vinasema ni kukataliwa kufanya kazi nae.

Hapana sikukataliwa na Nikki Mbishi sio kweli  kua tumekosana na Nikki  kwani yule ni mwana mpaka milele. Ilikuwa tayari tumesha organize mpango wa kurekodi na Nikki tukakutana Msasani Club tukawa vibe tunakula mua kwenye story story mimi nikatoa opinion zangu kwamba japo Duke ni mkali ila mimi beats zake siziafiki sana.

Nikki alikuwa yuko mua kama mimi akadai siwezi kusema hivyo kwa kuwa yeye Duke ndio aliyemtoa kwenye game. Hivyo hii ni kama disrespect kwake, ila mimi sikuona tatizo ni mtazamo wangu ikatokea misunderstanding ya kilevi tu, haikuwa kitu serious ki hivyo. Nikki aka panic kama vipi hata collabo hatufanyi mimi nikaona fresh tu kama amedhamiria poa, siwezi kubeg mtu kwa collabo.

Nikaachana nae ila Kay Wa Mapacha alituita kwenye kushiriki movie ya Bongo Hoods, Kichwa Cha Genge mimi na Ado Tembo. Siku ya uzinduzi tulikutana na Nikki na tukapiga story fresh tu na sina tofauti nae yeye kuvumishwa. Kuna watu walikuwepo wanajua vizuri, nyingine ni story tu za kuvumishwa. Naweza sema mimi na Nikki inawezekana ni watu ambao kiasi tuna kasoro zinazofanana hivyo kutokea vile inaweza kuwa ni asili ya sisi tulivyo ila sina tofauti yeyote nae.

Kuna moja ya lines zako umemzungumzia Fid Q alikupa shavu mpaka uka-freestyle kwa Ncha Kali. Hiki kipengele kikoje mpaka ukafika hapo?

Ni kweli Fid Q alinipa shavu kipindi kile cha tamasha la WAPI pale British Council. Nilikuwa na connection na Fid Q na tulikuwa na mpango wetu lakini kama unavyojua tabia ya Fid Q na wengi wanamjua alivyo basi ikabaki story tu.  Ni mtu ambaye alikuwa ananikubali sana kipindi kile cha WAPI ndipo aliponipigia simu tukutane pale British Council tufanye freestyle, nikafika pale kulikuwa na watu wengi wana rap kina Zavara na wengine wengi.

Sasa mimi nilichelewa kufika sikuwekwa kwenye ratiba ya watu wa ku-rap. Fid Q mshikaji wake alikuwa Ncha Kali ndipo Fid Q akamwambia Ncha Kali kuhusu ukali wangu ndipo Ncha Kali akamwambia nataka nihakikishe ukali wake. Ndipo Fid Q akaniambia ni freestyle mbele ya Ncha Kali huku akiniambia huyu ni Ncha Kali au Ruben Ndege.

Basi baada ya hapo nika rap sana mpaka Ncha Kali akasema huyu jamaa muda wowote mfanye dude, “Fid Q fanya dude na jamaa mlee Studio tuli play, huyu mwanao ni hatari”. Lakini hatukuweza kufanya chochote na Fid Q nikiona siku zinaenda huku nikiona miyeyusho ananiyeyusha basi mimi nikabwaga lakini Ncha Kali alikuwa yupo real na nilikuwa nawasiliana nae na Fid Q ndio aliniambia ni freestyle kwa mchizi na Ncha Kali akaelewa.

SOSA pamoja sana kaka naona muda ulikuwa umeenda lakini tumepata mengi kutoka kwako karibu tena.

Shukrani sana, pia kwa nafasi nyingine ya kuniwezesha kuchangia historia yangu japo kwa uchache tangu niko katika utamaduni huu wa Hip Hop.

Wacheki wana Pochaz kupitia mitandao ya kijamii

Facebook: Flyin Saucer
Facebook: Ado Tembo

Instagram: flyin_saucer_
Instagram: ado_swastik_tembo

© REKUSA 2022.