Adam Shule Kongwe ni mmoja wa underground emcees wakali kuwahi kutokea bongo. Inapokuja kwenye maswala ya uandishi, uchanaji, uwasilishaji, kukaa ndani ya mada, kunata na midundo, Adam Shule Kongwe amekolea kwa haya yote.
Adam Shule Kongwe ameachia miradi zaidi ya mi nane binafsi mbali na miradi aliyoiachia pamoja na kundi lake DDC. Pia tumepata fursa ya kufanya nae kazi hapa Micshariki Africa kama mhariri mkuu wa makala zetu za Kiswahili pamoja na kuws mwalimu mkuu kwenye darasa lake la Shule Na Shule.
Karibuni ile muweze kusoma historia ya maisha yake pamoja na ndoto zake kwenye hii rap game.
Tuanzie hapa. Tunaomba majina yako unavyoyatumia katika cheti chako cha kuzaliwa.
Oii inakuaje wandugu? Mimi naitwa Adam Hamisi Selemani
Ni lini ulianza career yako ya muziki na ni watu gani waliku-inspire katika career yako tukianzia hapa nyumbani na ughaibuni.
Mimi nakumbuka kuanza kuandika ilikuwa kitambo kidogo. Mwaka 2005 hivi ndio mara yangu ya kwanza kuandika ngoma ya kwanza kabisa ila ilikuwa ni mwanzo tu nikawa najiandikia tu mpaka mwaka 2010 ndio nikaingiza vocal au kurekodi kwa mara ya kwanza kabisa kwenye wimbo wa jamaa mmoja alikuwa anaitwa Gilya Madede au Dede Bwax pale Babati mkoani Manyara hapo ndio nikawa naenda studio mara kibao kupiga verse za kushirikishwa mpaka nilipoona nimeiva kabisa ndio nikarekodi track yangu rasmi mwaka 2012/2013 inaitwa Mbali niliyomshirikisha One Six.
Pia kuhusu inspiration nadhani nilikuwa inspired na Rap na muziki wote kwa ujumla maana kwa kipindi hicho ilikuwa napenda tu muziki wowote uliokuwa unapatikana na ukavutiwa nao ukiskiliza..
Ila nilipochagua kufanya Rap nilipenda Kikosi Cha Mizinga zaidi, na kwa uchache ngoma za Kalamashaka na K South (zile nilizobahatika kukutana nazo).
Vile vile miaka ya mbele mbele baada ya kujua internet ndio nikajikuta nimezama kwenye miziki ya watu wa New York na mingine mingi (West Coast kidogo) ambapo nilijikuta ni shabiki mkubwa wa Duck Down Music, Sean P akawa ndio my favorite…
Baada ya hiyo kazi na One Six vipi kulikuwa na muendelezo wa track nyingine au miradi kama album, mixtape na kadhalika?
Baada ya ile nakumbuka niliendelea kupiga kazi na wana (DDC) hapo tukiandaa miradi ya kundi zaidi na ilikuwa poa sana maana ndio zikazaliwa The Element II (Duke Tachez x DDC) mwaka 2014, Mechanism (2015), Fasihi simulizi (2016) mpaka kufikia Chini Kabisa (CK nikiwa na Javan) 2017 and the rest mpaka sasa.
Track Yako ya kwanza ulirecord mwaka gani?
Mwaka 2013 ndio nilirekodi… Beat ilikuwa ya 9th Wonder. Nakumbuka na production ilifanyika AJ Records Dodoma
Kwanini ulijihusisha na Hip hop Rap na sio genres nyingine za music?
Najihusisha na hip hop music sababu nilipenda sana michano zaidi na pia nilipokuja kujifunza kuhusu Hip Hop kama culture nikaona huku ndiko kwenyewe maana historia yake ni pana na ni mali sana kwa fikra zangu.
Utambulisho wako Ni Singida ilikuwaje mpaka ukaibukia DDC ambayo base yake ni Dodoma?
Naam, mimi Dodoma nilienda mwaka 2010 kwa ajili ya shule ila nikabahatika kukutana na kufahamiana na watu waliokuwa wanapenda na kufanya au kuishi kile nilichokuwa nakiamini mimi (Hip Hop) na hapo ndipo nikawa mwana familia wa DDC. Pia muziki wangu (serious career) ulianzia Dodoma( kuanza kufanya rasmi) na hata baada ya shule kuisha nikajikuta naishi kule kule. Kwa hiyo mimi nawakilisha sehemu mbili; Singida (nilipozaliwa na nilipokulia) na Dodoma (nilipozaliwa na kukulia kimuziki).
We ni moja ya wachenguaji hodari sana wa kizazi cha karibuni kuwahi kuwasikia, kuanzia uandishi ,uchaguzi wa midundo na pia uwasilishaji mzuri wa mada. Unafungua mada vizuri na kuifunga vizuri pia tofauti na wachanaji wengi wa kizazi chako .
Swali, je ni vitu gani unavyovizingatia unapopata wazo la kuandika mada fulani?
Kwanza kabisa ni kuitafiti mada yenyewe. Kufanya ka research kidogo ambapo hii huhusisha na maswali kama je mada hii imewahi kufanyika na aliyeifanya aliongelea kwa undani upi na aliyofikisha au kuacha ni yapi?
Maana wanasema kila kitu ni marudio kwa hiyo hii hufanya mtu uwe makini zaidi ili kuleta mada katika ubora zaidi, pia mtindo wa uwasilishaji nao ni muhimu sana kuzingatia, uchaguzi wa maneno pia kulingana na mada nao ni msingi pia hufuatia mdundo, mazoezi ya kuu masta kisha kurekodi.
Baada ya kukusikia katika miradi mingi ya DDC mradi nje ya kundi lako ulikuwa Chini Kabisa ukiwa na m’DDC mwenzako Javan (Chuna Ngozi) hili wazo la huu mradi ulianza vipi?
Aisee nakumbuka kipindi namsikia Javan kwa mara ya kwanza nikasema huyu sasa ndio moja ya wale wengi niliokuwa natamani kuwasikia. Umri wake na vitu alivyokuwa akifanya ulinifanya nikubali sana…na ni mmoja ya wana ambao LC alinikutanisha nao mapema zaidi. Nikamwambia mwanangu lazima tuje kupiga project ya pamoja. Simple kama hivyo tu.
Tulikuja kutulia miaka kama minne mbele ndio nikaona ni muda sahihi na tukawa tayari kuufanya. Nakumbuka tulirekodi kwa mara ya kwanza Dodoma pale ila haukuisha kwa sababu tofauti tofauti ndipo tukapata connection ya North Block Arusha na kwenda kuupigia pale. Aisee love tuliyopata kwenye mapokezi ya huu mradi ilikuwa kubwa sana.. Huwa inanipa feeling poa sana nikikumbuka.
Mradi wako wa Chini Kabisa ulifanikiwa sana na jamaa yako katika maudhui, na niwe mkweli huo ndio mradi naoukubali zaidi kutoka kwako, je mauzo ya huo mradi yalikuaje? Ulipata mavuno mazuri yanayoendana na quality ya mradi?
Shukran sana kwa compliment bro. Pia huu ni mradi wetu mimi na Javan (duo project)…Mauzo yalikuwa fresh kwa nilivyoona maana tulishajenga imani kwa watu wengi kwenye miradi ya nyuma ambayo tulifanya na DDC. Watu walitusapoti vizuri nashukuru na pia ulituongezea watu wengine waliokuwa mbali hii pia ni faida sana…
Una mpango wa kufanya duo project mbeleni? Msanii gani unatamani kufanya nae program hapo mbeleni?
Naam naam. Ninatamani sana kaka nadhani nitarudi tena na Javan kufanya naye album rasmi raundi hii... Ila kuna wana kibao pia naona tuna chemistry na tunaweza kutoa kazi nzuri kama emcees na pia duo ya emcee na producer.
Baada ya mradi wa Chini Kabisa ,ukafuatia mradi wako ukiwa kama solo artist uliobeba jina la ANKO iliyobeba vibao kama Kurasa Zilizopotea na Mjomba Kongwe. Kwanini uliamua kuiita ANKO na idea hii ilipatikana vipi? Vipi mafanikio ya huu mradi?
Naam mwanzo kabisa nilikuwa na hiyo ngoma ya Achana Na Kongwe kama track tu. Nilipopata wazo la kufanya album nilimshirikisha Javan na nikamwambia natafuta jina la Album yangu tukaanza mjadala kuna siku akaniambia halafu ile Anko mbona inafaa kuwa album kabisa na hiyo ngoma isimame kama title track.
Sikuwaza mara mbili zaidi ya kuanza kuiangalia hiyo title kwa upana zaidi na kuivunja vunja hadi kupata nyimbo zenye mtiririko unaoendana nayo. Kuhusu mafanikio (mradi) huu ndio uliweka rekodi zaidi kwenye kila upande wa mafanikio aisee...Huwa nashukuru sana watu wangu maana support ni kubwa kila wakati.
Baada ya hapo ikafuatia Mixtape ya Moto Umewaka. Baadae Album ya Uwanja Wa Fujo.
Na miradi hii inakupa taswira gani katika career yako siku za usoni kutokana na mapokeo unayoyapata katika uuzaji wa miradi yako?
Taswira ninayoiona ni ile ya kufanikiwa zaidi kufikisha nilichokusudia kwa jamii yangu na watu wengi zaidi duniani. Kwa kuwa ninaamini nilichobeba kina ulazima kushea na watu ni lazima nijitahidi kukifikisha kama kilivyo. Na watu wanavyozidi kusogea karibu ndipo naona asilimia za kufanikiwa zinaongezeka. Mafanikio mengine ni ziada tu na bonus za kuongeza nguvu ya kufikia lengo la kwanza.
- Katika miradi yako huwa unazingatia vigezo gani katika kuchagua guest artists?
- Unaitazama vipi kwa sasa hii game ya Hip Hop hapa nyumbani ilikotoka na inakoelekea?
- Vitu Gani huwa vinakufurahisha katika game yetu ya Hip Hop hapa nyumbani na vipi havikufurahishi?
- Na unawaasa nini wenye Rap zinazoleta taswira za ukakasi kwa Jamii na kuirudisha ile dhana ya Rap ni uhuni?
- Kwenye guest artists /features kwanza mi napenda kuwaweka watu ambao naamini wanaweza kufikisha kile nilichowaza kwenye wimbo husika, maana kuna watu ambao ukiwaskiliza unajua kabisa kama ni majigambo huyu anayapatia sana, kama ni siasa flani anaiweza sana etc hilo huwa la kwanza, pili upatikanaji wa muhusika na utayari wake. Maana kuna mtu unaweza kumcheki ila mkashindwa kumaliza kazi kutokana na ratiba zake.
- Game ya hip hop mi naona iko poa tu na inaenda vyema kama unavyoona hata huku tulipo sisi tumeweza kufikia wengi na kutambulika kiasi chake kama watu wa miziki mingine. Emcees na rappers wengi wanapata mwamko na mzuka kama unavyoona miradi inadondoka kila leo. Hatupo pabaya sana kwa maoni yangu
- Vitu vinavyonifurahisha ni hiyo ya kuona rappers wanajitahidi kutoa na kupush kazi zao, producers kukaza ili kuwa bora kwa upande wao na kuwa na miziki mingi yenye ubora na iliyotengenezwa kwa skills kubwa.
- Vitu vinavyonikata ni baadhi ya rappers na producers kutokuwa na muda wa kujifunza na hata kuishi utamaduni (kwa wana Hip Hop na wanaojiita wana Hip Hop). Pili ni kutoka kwa kazi zenye viwango visivyo vya kuridhisha (baadhi ya kazi), kingine ni baadhi ya rappers kutumiwa na watu bila kujijua wanatumika, pia watu kukosa muda wa kuwekeza kwenye ujuzi na muziki wao kama biashara na kutaka mafanikio makubwa na ya haraka. Haya ni baadhi ya mambo yanayonikata stimu mimi.
Naona link nyingi za audio kati ya Kongwe na Micshariki Africa? Unalipwa ? Na Kama hulipwi kuna kitu gani kilichopo kati yako na hawa jamaa zetu?
Naam naam.. Kuhusu kulipwa kuna kiasi huwa nachangiwa na kikubwa kinaenda kwenye production.. Pia mmiliki wake ni jamaa ambaye tumekutana kwenye huu huu utamaduni naweza sema ni mwana Hip Hop so ndio tukaunga majeshi kufanya "for the culture".
Unadhani Micshariki Africa ni suluhisho la underground movement bongo?
Sidhani sana kwa sababu neno suluhisho ni pana sana ila lengo lake (Micshariki) kama umepata kusikia baadhi ya ngoma utaona kwamba ni kuelimisha kwa asilimia mia moja kwa hiyo kama sehemu ya fasihi kipengele cha elimu kimezingatiwa.. So underground emcees tuna/wana cha kujifunza hapa kama kweli wapo kwa ajili ya mitaa.
Unashauri nini kwa underground emcees wengine kuhusu ku balance umaarufu na mafanikio ?
Hapa sasa ndio huwa pagumu sana kwa watu wengi. Kwa kuwa mimi sijawa maarufu naomba niongee mtazamo tu kwenye hili swali hapa. Kuna saa binadamu akiwa na uhitaji wa kitu huwa ni mtu mmoja na baada ya kukipata kuna namna anaweza kujikuta mtu mwingine. Ndio life. Sababu hata tabia binafsi hazifanani kabla ya umaarufu na vitu vingine. Ila umaarufu upo tu unaweza kuupata, kuukosa, kubaki nao au kuupoteza. Kikubwa ni kuwa humble tu maana umaarufu ukikuzidi kimo huja na athari zake. Kwa hiyo underground emcee kwanza asidate na attention na pia hiyo fame yenyewe... Watu wazoee kila hali haitokuja kuwatesa ikiwa kinyume.
Na vile vile kwenye mafanikio... Kila kitu huenda kwa hatua hakuna njia ambayo rahisi. Waache kudanganywa kuwa kuna sehemu ukienda au ukifanya kitu fulani utakutana na majani mabichi zaidi ya ulipo. Hiyo huwa ni dhana ya wengi sana na hupoteza au kudhoofisha wengi walioaminika mwanzo kule kule walipokuwepo. Umaarufu na mafanikio yanayokuja polepole huwa ni bora zaidi na huenda vikadumu.
Sasa hivi Sokoni una mradi unaoitwa CHI hebu tufafanulie maana yake na pia wazo la hii mixtape ilivyopatikana na mapokezi yake yakoje?
Na pia kabla sijaondoka katika miradi yako niliwahi kusikia kuna Album ulifanya na Duke Tachez pamoja na Lindu ,je kuna ukweli wowote,kama ukweli upo itaachiwa lini?
Hii ni kandamseto (mixtape) yangu niliyotoa karibuni. Ni tape poa sana na kuhusu nyimbo za kutambulisha niliachia moja audio na video inaitwa Mafuriko Ya China 1931..hivi karibuni nitaachia pia nyimbo mbili au tatu kutoka humo. Ikiwa poa zaidi zitakuja na videos pia…
Chi ni nishati au energy kwa lugha rahisi ile energy ya ndani inayotumika kwa mambo mbali kama kuponya, kujilinda na kadhalika. Neno hilo lina asili ya Asia..nitakuja na maelezo yake kirefu zaidi.
Yeah kaka ni kweli. mwaka wa 2018 mwanzoni nilirekodi album na brother Duke na Big Lindu ila ilikuja kusimama na haikuisha mpaka sasa ila nitawacheki pia niwaulize kama itaendelea au vipi. Ilikuwa kali sana kama unavyojua hao wakubwa ni watu hatari kwenye upande wa production.
Shule Kongwe ni mradi wako upi ambao umefanya vizuri zaidi kwenye mauzo kuliko mingine?! Na unadhani ni kwa nini?
Hii siwezi kusema ni mradi flani au ni flani sababu swala la mauzo huenda na muda pia. Kingine ni miradi inaendelea kuuzwa kila siku hii mipya na ya zamani vile vile. Siwezi kutoa jibu la moja kwa moja kuwa ni huu maana ni bidhaa ambazo ziko sokoni muda wote.
Kaka Adam, pia kuna chata lako la Adam Shule Kongwe 100% Hip Hop. Hebu tueleze historia yako na chata hili, linamaana gani na linapatikana wapi na kwa shilingi ngapi?
Shule Kongwe imesimama mara mbili kwenye chata kwa maana ya kwamba uwakilishi wa Old School Music na Golden Era Music (Hip Hop) na pili ni uwakilishi wa nickname yangu... Kwa hiyo ukivaa unakuwa either umewakilisha hiyo Old School au ufuasi wa Adam Shule Kongwe au vyote viwili. Kule mwisho kuna alama ya kofia ya ku graduate inaonesha kufuzu (ukomavu) kwenye Hip Hop music Shule na Kongwe na 100% ni raw strictly Hip Hop. As we all know kwamba ile Hip Hop ya vizazi vya mwanzo ilikuwa ni ile halisi kabisa.. Mimi ni hiyo lineage ya emcees wa vizazi vya mwanzo kwenye hip hop music.
Kama unahitaji hili chata nicheki na nitakutumia popote pale ulipo. Bei ni Tshs 20,000 kwa T-shirt moja.
Tumalizie kwa kutuachia anwani zako za mitandao ya kijamii na namba zako za simu kwa yoyote yule angependa kukucheki na kukusupoti kwa njia yoyote ile.
WhatsApp/Simu: +255629192107
Facebook: Adam Shule Kongwe Hamisi
Instagram: adamshulekongwe_
Twitter: AdamShuleKongwe
Shule Kongwe shukran sana kwa muda wako ,ushirikiano wako umekuwa mkubwa sana ,karibu tena.
Amani sana, Baraka tele.
Copyright ©️ Rekusa ©Shule Kongwe