Ringle Beatz

Ringle Beatz ni mmoja wa watayarishaji bora inapokuja kwenye uandaaji wa midundo ya Hip Hop. Japokua amekuwa kwenye game kwa zaidi ya muongo mmoja wengi wetu hatumfahamu yeye ila tunafahamu mchango wake kwenye utamaduni huu kupitia midundo murua ambayo ameweza kutupatia.

Baada ya kuanza kuonekana/kuskika vizuri miaka ya 2012 wakati akiandaa midundo kwa ajili ya kipindi cha Fidstyle Friday, mtayarishaji huyu alijiendeleza na kuweza kufanya kazi na wasanii kibao kama vile One The Incredible, Young Killer, TK Nendeze, Nikki Mbishi, Stereo, Mansu Li, Chid Benz, Zaiid, Songa, Dizasta Vina…Na hivi majuzi combination yake na Dizasta Vina ndio imemfanya mtayarishaji kuzidi kuonesha umahiri wake inapokuja kwa uandaaji pale unapocheki kazi waliounda pamoja The Verteller.

Tumeona freshi tufike kitaa tumcheki mwana ili tuweze kumfahamu the man behind the keyboards…

Karibu sana kaka Ringle Beats hapa Micshariki Africa. Nashkuru sana umetupatia mda wako ili tuweze kumfahamu mtayarishaji Ringle Beats. Kwanza kabisa tuanze kwa kukufahamu Ringle Beats ni nani? Majina yako rasmi ni nani na unajishughulisha na nini?

Ahsante. Majina yangu halisi ni David Ringo. Ni mtayarishaji wa muziki na pia ninajishughulisha na mambo yanayohusiana na teknolojia ya habari na mawasiliano, yaani TEHAMA.

Tuanze nyuma kidogo; Ringle Beats ulizaliwa wapi, unaiwakilisha Hip Hop ukiwa pande zipi za Africa Mashariki yetu hii. Tueleze kuhusu maisha yako ya utotoni, mpo wangapi kwenye familia yenu na umesomea wapi na umefikia kiwango gani kimasomo?

Mimi ni mzaliwa wa Moshi, Kilimanjaro. Nilisoma elimu ya sekondari Moshi Technical school, baadaye nikasoma Stashahada ya uhandisi kompyuta Mbeya University of Science and Technology (MUST) na kisha shahada ya kwanza ya uhandisi Kompyuta Dar es Salaam Institute of Technology (DIT). Nimefanya shughuli zangu za kimziki Moshi, Mbeya na Dar es salaam. Naweza kusema ninaiwakilisha Moshi, sababu ndipo asili yangu ilipo na pia ni mahali paliponikuza kimuziki.

Ringle Beats ulianzaje hizi mbanga za utayarishaji? Wazazi wako na wana familia walichukuliaje haya maamuzi yako ya kujitosa kwenye muziki?

Kabla ya kuwa mtayarishaji wa muziki, nilijifunza kupiga vyombo vya muziki (Guitar na Kinanda). Hii ni wakati nikiwa mdogo sana (darasa la tano). Baadae nilipofika kidato cha kwanza nikajifunza kurecord instruments kwa kutumia kinanda (Yamaha PSR). Na baadae nilianza kujifunza utayarishaji kwa kutumia computer (FL Studio) mwaka 2007 nikiwa bado sekondari. Niliweza kufanya full production mwenyewe mwaka 2009. Nilipata support nzuri kutoka kwa familia na ndugu, sikuwahi kupata kipingamizi chochote kwenye maswala ya kimziki.

Mbona Hip Hop na sio tasnia yoyote ile au wewe unapiga midundo aina yote na sio tu Hip Hop?

Ninatengeneza aina zote za muziki. Kazi zangu zilizofahamika na watu wengi sana ni kazi za Hip Hop lakini haimaanishi ndizo nazofanya pekee. Shout out kwa Fareed Kubanda (Fid Q) kwa sababu ndie aliyenitambulisha kwa wadau wengi wa tasnia hiyo (2012) kwa kuona uwezo wangu wa kutengeneza midundo hiyo. Nilikua nikimtengenezea midundo aliyoitumia kwenye kipindi chake cha Fid Style Friday, ambapo baadhi ya midundo hiyo

aliona ina hadhi ya kutumika kutengeneza nyimbo kamili na sio freestyle tu. Kwa mfano, wimbo wa Ushauri Nasaha wake Fid Q na Stamina. Nyimbo hizi ziliposikilizwa na wengi, watu walipata imani kuwa ndio mziki ambao ninauweza zaidi.

Jina lako lako la kazi Ringle Beatz lilikujaje, linamaanisha nini?

'Ringle' ni neno la kiingereza linalomaanisha sauti ya Kengele (bell). Ni jina ambalo mimi binafsi nilikua nikilitumia kutambulisha aina fulani ya midundo yangu ambayo nilikua nikiitengeneza, na sio kujitambulisha mimi. Midundo hiyo ilikuwa na Groove (Swing) tofauti na midundo mingine yote ambayo nilikua nikiisikia, kiasi niliamini ni ubunifu wangu mwenyewe. Pia ilikua na sauti nyingi zilizofanana na vyengele (ringing). Kwahiyo 'Ringle' niliitumia kama adjective inayotambulisha aina ya mdundo (Ringle Beat). Lakini pia nilifanya hivi kwa sababu inaendana na jina langu (Ringo). Baadae watu waliokua wakinizunguka na kunisikiliza walizoea kuniita Ringle Beatz. Kabla ya hapo wengi walinifahamu kama DVD, ambayo ndio a.k.a yangu ya utotoni. :).

Twitter bio yako inasoma kama Curriculum Vitae; Music Producer, Programmer, Software and Electronics Expert, Pianist, Music, Investor (Creativity and Technology). Ukienda Bio ya Instagram ni kama ukurasa wa pili wa CV; Rapper and Song Writer. Naomba uzungumzie kimoja kimoja hapo kaka maana hivi vipaji kuvimiliki sio mchezo. Pia tueleze umewezaje kua multi-talented hivi na umekuzaje vipaji hivi?

Programming, Software Engineering na Electronics (Robotics) ni vitu ambavyo nimevifanya kwa muda mrefu sana na pia nimevisomea. Nilikua na passion navyo tangu nikiwa mdogo. Nilijifunza kuunda circuits na devices mbalimbali ikiwemo amplifiers, transmitters, mixers tangu nikiwa sekondari. Nilijiendeleza zaidi na kuingia kwenye advanced circuits na baadae nikapenda zaidi Programming ya circuits. Baada ya kumaliza kidato cha nne nilijiunga na chuo kusomea Computer Engineering ambapo nilijiendeleza sana kwenye Computer programming na Robotics.

Kuhusu Pianist, kama nilivyosema awali, nilianza kupiga kinanda nikiwa mdogo (kama darasa la tano) na kwa kuwa nilikua nikifanya mazoezi mara kwa mara niliendelea kubobea nakujifunza mbinu mpya siku baada ya siku. Kuhusu

Songwriter/Rapper, kama unavyojua watu wengi wanaojihusisha na upigaji ama utayarishaji wa muziki mara nyingi hupenda kufanya mziki pia (kuandika, ku-rap ama kuimba). Mimi pia si tofauti. Nilianza kuandika nyimbo kipindi bado nasoma sekondari, na nilijiendeleza kwa kujifunza mbinu mpya zaidi, multi-rhyming, metaphors, word-plays, cadences na vingine kadiri nilivyozidi kufanya. Kipindi hicho nilikua pia nikirekodi nyimbo zangu binafsi.  Japo mwaka 2015 niliamua kupunguza nguvu kwenye ku-rap na ku-focus zaidi kwenye utayarishaji. Nimekua pia nikiwaandikia watu nyimbo, ama kuwasaidia kiuandishi pale inapohitajika.

Ringle Beats unamiliki studio yako mwenyewe na je gharama zako za kazi zipoje?

Niliwahi kumiliki studio kwa kipindi fulani, ila kwa sasa nimesitisha kwa muda kuendana na mikakati binafsi niliyojiwekea. Kama wanavyosema, hakuna utajiri mzuri kama kuwa na watu. Hivyo kwa sasa ninapohitaji kufanya kazi muda wowote nina studio kadhaa ninazotumia.

Gharama zangu zinategemeana sana na kazi au mradi ninaoufanya na aina ya makubaliano baina yangu na ninaofanya nao kazi. Siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja kwenye hilo. Studio ninazotumia zaidi kwa sasa ni pamoja na MV09, Jay'Cob Studio na Mevid Records.

Tueleze kuhusu partnership yako na emcee Dizasta Vina. Tupeleke wayback, mlianzaje kufanya kazi pamoja na mkafanikiwa kutengeneza timu nzuri kama DJ Premier na GURU (R.I.P)?

Nilifahamiana na Dizasta Vina mwaka 2012 nikiwa mbeya. Nilitambulishwa kwake na Dubo (Jesus' Son) ambaye tulikua tukisoma nae kwa kipindi hicho na nilikua nikimtengenezea kazi kadhaa ikiwemo 'Dingi Sela'. Dubo alikua 'excited' sana alipokutana na Dizasta kutokana na namna yake ya flow, uandishi na kufikiri. Mimi pia nilipomsikiliza nilipata the same impression.

Dubo na Dizasta walikubaliana kuanzisha 'duo' (kundi) na wakaliita 'Panorama'. Mimi pia niliona ni wazo zuri. Hatua ya kwanza kabisa ya utekelezaji wa wazo hili ilikua ni kutengeneza wimbo wa kwanza kwa kundi ulioitwa 'Pano-rhymes' ambao mimi ndio nilikua mtayarishaji. Niliandaa mdundo na tukaenda kwenye studio ya Stimella (Lucky Music) kurekodi sauti. Japo kwa bahati mbaya huu wimbo haukufanikiwa kuachiwa rasmi kutokana na sababu kadhaa zilizojitokeza. Hapo ndipo ikawa mwanzo wa kufanya kazi na Dizasta.

Baada ya hapa tuliendelea kukutanishwa na matukio ya kimziki, na wakati mwingine alichukua midundo kwangu na kurekodia kwenye studio nyingine. Kipindi hiki nilifanya kazi nyingine kadhaa na Dubo, ikiwemo 'Underground' ft. Big Philly na 'Mayweather'.

Baada ya miaka kama mitatu tulikutana tena na Panorama na kufanya nyimbo kadhaa ikiwemo 'Wengi wao' ambao ulikua ni wimbo wa pamoja, ‘Kanisa’ ya Dizasta, ‘Sauti Ya Mtaa. ya Dubo, pamoja na ‘Siku Mbaya’ ya Dizasta.

Dizasta aliendelea kufanya miradi mingine yeye binafsi pamoja na kushirikisha watayarishaji wengine. Siku moja nilimuuliza Dizasta kuhusu mkakati wa mziki wake na akaniambia ana mpango wa kuandaa album. Na akaniambia angependa tushirikiane kwenye hili. Tulikubaliana kushirikiana kuandaa album yenye nyimbo ishirini ambazo zitakua na consistency na kubeba wazo moja.

Dizasta aliandaa nyimbo na tukaanza kurekodi wimbo mmoja baada ya mwingine. Ilichukua muda kiasi kuweza kumaliza huu mchakato, hatimaye tulimaliza na kuachia mnamo 27 December 2020. Kipindi hicho pia tulifanya nae nyimbo nyingine kadhaa ambazo hazikua ndani ya album. Na huu mwendelezo ndio umejenga hiyo partnership inayoonekana kati yetu.

Unaona ni nini kinachowafanya muendane pamoja kama msanii na mtayarishaji vizuri kati yako na Dizasta Vina?

Nafikiri mimi ni 'Critical Thinker'. So, obviously napenda sana vitu vinavyonifanya nivikiri ili kujifunza zaidi au kupambanua ujuzi zaidi juu ya jambo fulani, pamoja na kujiuliza maswali kuhusu vitu vinavyonizunguka. Dizasta pia yupo hivyo hivyo. Ni mtu anapenda ku-question vitu na kufikiri nje ya boksi bila kua na bias, pia ana uwezo mkubwa sana wa ku-research kitu na kukiwakilisha kwenye maandishi. Lakini pia ni kati ya wasanii wachache ambao wanafanya kazi zao zote kwenye 'Sober Mind'. Hii inafanya iwe rahisi kuelewana na kufikia kwenye makubaliano sahihi kwa kila kazi tunayoifanya. Lakini zaidi ya hapo, ni kati ya wasanii ambao wana uwezo mzuri sana kiuandishi yaani lyrical skills, kitu ambacho mimi pia napenda sana.

Kingine ni kwamba, Dizasta ni mtu anayependa ku-craft mziki mzima kulingana na mada atakayoiwakilisha, na sio kukuta mdundo na kuandikia mashairi. Hivyo atataka mdundo utengenezwe kuendana kabisa na maudhui yake. Hii ni aina ya utayarishaji ambayo mimi hua ninaifanya zaidi. Kuandaa mdundo from scratch kulingana na maudhui na hisia. Ukichanganya vyote hivi unapata mazingira ambayo wote tunakua comfortable kufanya kazi.

Midundo yako ina ubunifu flani wazimu sana, hivi hua unachukua mda kiasi gani kuandaa midundo yako na gharama zako za utayarishaji zipoje?

Ahsante. Nadhani mimi ni kati ya watayarishaji wanaoweza kutumia muda mfupi sana kutengeneza midundo kutokana na upigaji wa vyombo na uzoefu. Lakini hua napenda kujilazimisha kutumia muda mwingi zaidi ili kupata kitu bora zaidi. Kuja na version ya kwanza kabisa la mdundo inaweza kuchukua dakika tatu tu. Lakini itanichukua hadi masaa kadhaa kuweza kuufanya mdundo usikike vyema na kuvutia zaidi.

Kuhusu gharama,kama nilivyosema awali, zinategemeana sana na mkakati, aina ya kazi na makubaliano ya kikazi kati yangu na mtu ninayefanya naye kazi.

Kando na Dizasta Vina umeshapiga kazi na wasanii gani wengine na kwenye miradi gani?

Nimeshafanya kazi na wasanii wengi sana hususan kwenye tasnia ya Hip Hop. Baadhi ni maarufu ila wapo wengi sana ambao si maarufu sana. Sio rahisi kutaja miradi yote niliyoifanya. Baadhi ya wasanii niliofanya nao kazi ni pamoja na GodZilla (RIP), Kamusi, Tommy Thommas, Fid Q, One The Incredible, Young Killer, TK Nendeze, Nikki Mbishi, Stereo, Mansu Li, Chid Benz, Zaiid, Songa, Dizasta, Dubo, Boshoo, Bokonya, Wakiafrika, Odong (Jaco Geez), Mapacha, P Mawenge, Jygga Lo, legendary Zahir Zoro, One Six, Baraka Da Prince, Mabeste, Wakazi, Buddah, G Nako na wengine wengi sana, siwezi kuwataja wote.

Tuzungumzie "The Verteller", mchakato wakuanda huu mradi classic ulikuaje na experience ki ujumla ilikuaje?

Mchakato wa kuandaa 'The Verteller' haukua rahisi sana. Tulitumia takriban miaka miwili kukamilisha mradi huu wa 'The Verteller'. The Verteller ni moja kati ya miradi mikubwa niliyowahi kufanya so far.  Imekua ni experience kubwa kwangu hasa pale ninapokumbuka changamoto tulizokabiliana nazo na kuzilinganisha na matokeo ya baada ya kuachia mradi huo.

Dizasta aliandaa nyimbo takriban mia moja kwa ajili tu ya kupata nyimbo kadhaa ambazo zitaingia kwenye album hii. Ilibidi kuchambua, kuunganisha na kuondoa baadhi ya materials kwa ajili ya kupata nyimbo bora zaidi. Sessions za recording pia hazikua rahisi maana nyimbo nyingi zilikua ni ndefu na baadhi zilihitaji drama na background effects. Nyimbo nyingi tulizirudia kurekodi mara kadhaa pale tulipoona hazikufikia kiwango au impression iliyotegemewa.

Karibu nusu ya midundo aliiandaa Dizasta mwenyewe lakini mingi ilihitaji uboreshaji na kurekebishwa ili kufikia kiwango ambacho tulikiona kua bora kwa mradi kama huu. Midundo mingine pia niliirudia (re-make) ili kuendana na hisia na maudhui tuliyoipata baada ya kurekodi visa husika. Kwa ujumla experience ilikua nzuri na pia I'm proud kwa sababu imekua ni moja kati ya album bora za Hip Hop Tanzania. Naamini itabaki kwenye kumbukumbu kama alama muhimu kwenye utamaduni huu.

Mafanikio yako yanayotokana na hizi mbanga za utayarishaji ni zipi?

Mafanikio ni 'Subjective'. Inategemea ni malengo gani uliweka na ni mangapi yametimia. Na kama unavyofahamu, tasnia yetu kibongo bongo bado ni changa sana hususan kwa Hip Hop. Mafanikio ya kimaslahi sio makubwa sana japo yapo. Mimi binafsi ninaona mafanikio kwenye aspects tofauti na maslahi pekee. Ninaweza kusema nimefanikiwa na ninahitaji kufanikiwa zaidi.

Je kwa mtu yoyote anayetaka kujifunza toka kwako je inawezekana?

Any time. Mimi hua napenda sana kushea ujuzi wowote ninaoupata au kujifunza, kwa sababu siku zote nimekua nikiamini kwamba kushea kile ninachokijua ndio hua inaniongezea kujua vingine vingi zaidi. I'm always available and ready to share everything I know, and I enjoy it.

Kama mtayarishaji unaona kama unapata heshima unayostahili?

Heshima ni kitu cha hiari. Nina-appreciate sana watu wote wanaotambua na kuheshimu kazi zangu na uwepo wangu kwenye tasnia, maana najua wapo wengi. Wale ambao bado hawajatambua au kuheshimu ni jukumu langu kufanya bora zaidi ili niweze kuwashawishi kutambua na kuheshimu ninachokifanya

Kama mtaalam wa teknologia unazungumziaje hizi njia mpya za kusambaza muziki, je zinalipa?

Teknolojia inakua kwa kasi sana. Ni muhimu kila mtu kuji-update kuweza kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ikiwemo kutumia hizi njia mpya za kusambaza kazi za muziki. Japo nina tahadhari moja kwa wasanii hasa wale ambao ni wachanga au wapo underground. Streaming ni mchezo wa NUMBERS, kama hauna mashabiki wengi sana huwezi kunufaika na streaming services kirahisi. Bado unapaswa kua na njia mbadala za kupata kipato kutoka kwa wale mashabiki zako wachache.

Nash MC, kwa mfano, anaweza kuingiza zaidi ya 20 Million kwa kuuza album moja. Lakini hesabu yake hapo ni kwamba ana mashabiki 2000 tu wa kuaminika (loyal fans) ambao wapo tayari kununua kazi yake kwa 10,000. Ingekua ni streaming asingepata pesa ya maana kwa watu 2000. Hivyo tunapaswa kutumia njia hizi mpya za usambazaji, lakini isiondoe ubunifu wa kujaribu njia tofauti kulingana na mazingira yetu halisi.

Nini tutarajie kutoka kwa kwako hivi karibuni?

Bado ninaendelea kufanya miradi mbalimbali na watu mbalimbali. Na ninaamini mingine itakuja huko mbeleni. Hivyo, as far as ninaweka nguvu na akili kubwa kwenye kufanya kile ninachokifanya, tutarajie vitu vizuri zaidi kama tutajaaliwa uzima.

Neno kwa vijana, wachanaji na watayarishaji je sanaa na muziki ni ajira?

Kadiri siku zinavyokwenda tunazidi ku-prove kwamba sanaa ya muziki ni ajira. Kuna watu wamefanikiwa sana kupitia muziki na sanaa kwa ujumla. Na pia kadiri teknolojia inavyozidi kukua na tasnia invyozidi kurasimishwa, uwezekano na uhakika wa kupata manufaa kwenye muziki unaongezeka kwa kasi. Kwahiyo, ushauri wangu kwa vijana wenzangu ni kwamba tuweke nguvu, bidii na ubunifu zaidi kwenye kazi tunazozifanya, lakini pia tusisahau kurasimisha kazi zetu (kuwa professional) ili tuweze kunufaika zaidi sasa na baadae.

Kipi cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza?

Zaidi, niishukuru Micshariki, lakini pia nishukuru wadau wote ambao wananifatilia na kufurahia kazi zangu, pia kwa wale ambao wanasapoti kazi zangu kwa kuzifikisha mbali zaidi.

Malizia kwa kuwapa shout out watu wako na kutuachia anwani unazozitumia kwenye mitandao ya kijamii. Shukran sana kaka Ringle Beatz.

Shout out kwa wote wanaosapoti tunachokifanya. Shout out kwa wale tunaoshirikiana kufanya kazi hizi pia. Shout out to all the fans.

Twitter:@ringunger
Instagram: @ringlebeats

Kwenye music distribution platforms zote napatikana kama Ringle Beatz.