Uchambuzi Wa Album: Reflections
Emcee: Robah Mwenyeji
Tarehe iliyotoka: 18.07.2024
Nyimbo: 16 + 3 Skits
Watayarishaji, Mixing & Mastering: Aress66, Kunta Official Beats, Kdawg, Chzn Brain
Studio: Truce Label, Big Beats Afriq
Nyimbo Nilizozipenda: Hip Hop Is Alive, Isaiah Twenty Eight, Reflections, Cheers, Pen African, Mother Earth, Go Champion, Una Kumbuka, Guthukia, Uzalendo, Mother’s Love, Asante Mama, No Drugs,
Wakati Robah Mwenyeji akitangaza ujio wa album yake akiwa peke yake mwaka huu tulifurahi kwani tulijua wazi kuwa kinachokuja kutoka kitakuwa ni kitu kizuri sana yani hardcore rap. Emcee huyu ambaye ni nusu ya kundi la Wenyeji pamoja na Zakah Mwenyeji kabla ya mradi huu mpya 'Reflections alikuwa ashatubariki na "singo" kadhaa pamoja na EP mzuka sana inayokwenda kwa jina la 'Wenyejibiz'
Robah Mwenyeji x Nem R - 'Reflection' Single Artwork
Album hii ambayo imewashirikisha ma Emcee pamoja na watayarishaji wa kitambo pamoja na wa kizazi kipya ilitambulishwa kwa umma rasmi kupitia singo ya kwanza ambayo imebeba jina la album 'Reflection' ambapo ameshirikishwa dada mchanaji/muimbaji Nem R kwenye kiitikio. Kwenye mdundo wa Kunta Official Beats kaka Robah bado anaonesha wazi tunachokikosa kwenye game letu la Hip Hop kwa sasa ni rap ya ki utu uzima.
Albam ya Reflections inafunguliwa na ngoma inayoitwa Real Life ambapo ameshirikishwa Kitu Sewer ambao .wote enzi hizo walikiwasha sana kwenye kundi lao la pamoja, Ukoo Flani Mau Mau, Kitu Sewer kama vile Robah naye pia enzi hizo akitokea kwenye kundi lake la Mashifta na mwendazake G-Wiji.
'Reflection' Album: Feature Aritsts & Producers Artwork
Project hii ambayo ilikuwa na skits tatu ambazo zote amesimama emcee/mchanganya sauti Chzn Brain (pia kuna mdundo kachangia humo) imegusa mada tofauti tofauti zikiwemo changamoto za madawa ya kulevya akiwa na emcee Frost kutoka Tanzania kwenye ngoma iendayo kwa jina 'No Drugz' wakitukumbushia kuwa,
“Una get high on drugs (Pale pale)/
Usikimbie stress ukiwa… (Pale pale)/
Ganzi ikiisha maumivu ni yale yale/
Uki reharb we mwenyewe utapona ukiamua/”.
Mradi pia unagusia maswala ya imani kwenye ghetto gospel flani mzuka sana ambapo amesimama mtayarishaji Kdawg kwenye Isaiah Twenty Eight ambapo Robah anakubali kuwa kama sio upendo wa mwenyezi Mungu pengine tusingekuwa nae sasa akisema, “At 23 pengine ninge go, ama 33 kama Yesu…”
Mradi pia unasifia wanawake kwa ngoma tatu tofauti na kwenye njia tofauti tofauti; kwenye African Empress mgoma flani wa kudunda dunda Robah anasifia akina dada zetu warembo akiwapatia mdundo wa kunengua kiuno (wahuni pia wanajua mapenzi). Kwenye Mother Earth akiwa na Kamah Kshaka wakisaidiwa na sampuli ya sauti ya kiongozi wa kisiasa Julius Malema wanaongelea shida zinazoikumba dunia hii kama mama yetu. Kisha anamalizia kwa kumsifia mama yake mzazi kwenye ngoma mbili Mother’s Love akiwa na Menelik na pia Asante Mama.
'Hip Hop Is Alive' inaonesha vile Hip Hop ilivyo na umuhimu sana maishani mwetu na vile bado ipo hai hata kama watu wanazidi kuiongezea maji kuilainisha na kusema imekufa. Pen African inawakutanisha Robah na Zanzolo kutoka Africa Kusini wakitumia kalamu na kinasa kuongelea changamoto la bara letu.
'Go Champion' akiwa na Dyana Cods pamoja na 'Cheers' akiwa na Johnny Vigeti ni ngoma za kukutia moyo na kukufanya chanya. Aisee si dada Dyana Cods kaua sana kwenye chorus ya 'Go Champion' ilhali Vigeti kama kawa vigezo na masharti ya mistari si unajua lazima vizingatiwe.
'Una Kumbuka' akiwa na Romi Swahili ni ngoma nostalgic sana kwani inatukumbusha enzi zetu za utotoni na historia ya muziki juu ya mdundo freshi sana wa Kunta Official Beats ilhali kwenye ni 'Guthukia' nayo hata kama hutoelewa kisapere (lugha ya Kikuyu) utaguswa na roho ya mdundo mzuka kutoka kwa Kdawg na lugha yetu ya nyumbani inavyoskika freshi sana akichana Robah na kaka Kobole. Zakah, Smallz Lethal na Aress66 wanashirikiana freshi sana kutuonesha 'Uzalendo' wao.
Japokua Robah kwa sasa yupo ughaibuni kule Ufaransa, ameona hii sio sababu ya kumzuia yeye kufanya kitu anachopenda kufanya na kutubariki na mradi mzuri sisi wafuasi wa Hip Hop. Inapendeza sana kuona jamaa anaendelea kule alipoanzia, kuandika, kuchana na kutupatia mradi mzuri wa Hip Hop. 2024 ni mwaka wa kutafakari, mwaka wa Reflection.
Mfuate Robah Mwenyeji kwenye mitandao ya kijamii na tiririsha muzikiwa wake kupitia dsps;
Facebook: Robah Mwenyeji
Twitter: @WenyejiRobah
Instagram: robahmwenyeji_official