Romi Swahili

Romi Swahili amekua kwenye ulingo wa Hip Hop kwa muongo mmoja sasa. Romi Swahili ni mwalimu wa fasihi kitaaluma lakini pia ni emcee wa Hip Hop. Emcee huyu ana miradi kibao, binafsi na ya kushirikiana na tumeona ni vizuri tumcheki ili kuweza kumfahamu.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Romi Swahili. Kwanza tuanze kwa kukufahamu, majina yako rasmi, unatokea wapi na unajishughulisha na nini?

Shukran kwa mwaliko kaka, it's been a long time coming. Wazazi walinipa majina Elijah Njenga, natokea jimbo la Laikipia ila kwa sasa naishi Jimbo la Nakuru ambapo nimekuwa nikirekodi muziki wangu kwa karibia miaka kumi hivi.

Tueleze historia yako ya nyuma, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi na umefikia wapi ki masomo? Pia utoto wako ulikuaje?

Nilizaliwa Laikipia lakini utotoni wazazi walihamia jiji kuu la Nairobi, ambapo nilikaa kwa mda wa sehemu ya utoto wangu Nairobi lakini baadaye nilirudi Laikipia kujiunga na shule, naweza kusema kutoka shule ya msingi hadi sekondari. Baadaye nilijiunga na Chuo Kikuu Cha Moi, Eldoret, masomo yangu yamefikia hapo kwa sasa.

Kukaa kwenye mazingira tofauti nikiwa mtoto kulifanya niwe na maisha ya kufurahisha. Nilikuwa mtoto mkimya sana, kitu ambacho kiliniruhusu kutazama mengi, nilijifunza vitu vyote vya ubunifu kutoka kwa ndugu zangu; kaka mkubwa alifanya ufundi wa electronics, dadangu akawa muigizaji na mchekeshaji, na kaka ninayemfuata alikuwa mwana sarakasi, pia amekolea kwenye ufundi wa vitu vingi.

Tueleze kuhusu jina lako Romi Swahili, jina lilikujaje na linamaanisha nini?

Jina Romi lilikuja wakati mwalimu aliponiomba nihusike katika ngano tuliyokuwa tunaisoma darasani. Mhusika mkuu katika kitabu hicho aliitwa Romi, na yeye aliokoa kijiji kutoka kwa mashetani akisaidiwa na mbwa aliokuwa anawafuga. Mimi pia nilikua nafuga mbwa wengi pia utotoni. Wanafunzi tuliokuwa tunasoma nao walionijua toka nyumbani walianza kuniita Romi na ikawa ni hivyo. Ila kupatana na Level Next na kufanya kazi naye kwa muda ali break down Romi kuwa Realness Owns My Individuality.

Wakati ule Genetic Disorder alijulikana kama Johny Blaque akiwa na kundi halisia la Blaque Swahili pamoja na msanii mwingine, Eddy Swahili aka State of the Art. State alipopumzika kwenye maswala ya muziki Genetic akawa anataka kuendeleza kundi hili hivyo nikawa Romi Swahili. Kundi likawa linashirikisha Johny Blaque na Romi Swahili, Blaque × Swahili.

Tueleze kuhusu historia yako ya muziki, uligunduaje kua una kipaji cha kuchana, na ulianzaje kukikuza hadi kufikia hapa?

Baba yangu alikua anamiliki duka la kuuza muziki ambapo aliuza music systems, santuri na cassettes. Utotoni nilijikuta mda mwingi nikiwa pale dukani kwake kila siku nikimsaidia ambapo iliniwezesha kuskia aina tofauti ya muziki. Aliunda mixtapes za Reggae kwa sana. Mama pia alikuwa na mkusanyiko wa muziki wa gospel na vitabu alivyo nakili nyimbo kwa kusudi la kuongoza nyimbo kanisani. Vitabu vyangu vya mashairi hunikumbushia vile vitabu vyake alivyokua anaviandikia (akicheka).

Pale kwenye music store baba akiunda mixtapes/kanda mseto alinikubali niseme maneno mawili kwenye microphone, niliposikia sauti yangu kwa mixtapes zake nilivutiwa sana na maisha ya sanaa.

Baadaye nikiwa shule ya msingi nilipendezwa na kuanza kuandika maandishi. Insha zangu ziliweza kuwapendeza walimu kwa sana. Vile vile nilianza kuandika mashairi; mashairi haya yakaanza kugeuka kuwa beti za kughani kadri mda ulipokua unaenda. Nilipojiunga na shule ya upili niliweza kuingia studio kwa mara ya kwanza na nilipofika kidato cha tatu nilikuwa na album yangu ya kwanza. Sijaangalia nyuma kutoka mda huo

Mara yako ya kwanza kuingia studio ilikuaje na ni ngoma gani uliunda na je ulipoiachia mashabiki zako walipokeaje wimbo huo?

Mara ya kwanza kuingia studio nilirekodi freestyle ambayo ipo YouTube. Kipindi kile nilipatana na marafiki ambao waliupenda muziki wa Hip Hop, standard zangu zilikuwa juu sana manake niliwaskiza wasanii kama vile Nas, Masta Ace, Immortal Technique na Killah Priest. Wali challenge pen game yangu kwa sana. Hakuna Open mic ambazo sikuwakilisha, hadi makanisani, haha

Mziki ulipokelewa vyema sana, album yangu ya kwanza niliuza nakala 70 shuleni pekee kwa bei ya shilingi hamsini kwa CD Moja. Nilijiamini sana na nikawa na imani nitakuwa one of if not the best to ever do it!

Romi una miradi kadhaa ambayo umeshaachia. Tueleze kuhusu kazi hizi, zinaitwaje na ziliachiwa lini?

Nina kanda tatu;

Knowledge Mashairi (2015)

Fungu La Kumi (2018)

Antidote nikiwa kwenye kundi la Blaque Swahili pamoja na Genetic Disorder (2020)

Tupe historia kidogo kuhusu kundi lenu Blaque Swahili mlikujaje kupiga kazi pamoja na mradi wenu wa pamoja Antidote ulikujaje na unamaanisha nini?

Nilikutana na Genetic Disorder enzi zile nikiwa shule ya upili. Niliweza kusafiri kwenda Nakuru kuwakilisha kwenye talent show moja. Baada ya kuwakilisha na kutokea wa pili kwenye shindano lile kukatokea marapa waliobishia ushindi huo. Walitualika katika freestyle battle, backstage na hivi ndivyo nilikutana ma emcee wa kundi la 1183, Genetic akiwa mmoja wao. Nili battle Genetic Disorder na baadaye tukawa na uhusiano wa karibu. Tulikuwa tunafanya mitindo huru sana kupitia maandishi na simu. Baada ya miaka minane ndio tuliweza kupatana studio kwa support ya Edd The Beat Smith na Level Next na hapo tukaifanya album iitwayo Antidote.

Nimefanikiwa kuskia mradi wako classic Knowledge Na Mashairi mara kadhaa. Tueleze kuhusu mradi huu pia. Je umeona kuna athari gani kwa jamii na kwako binafsi pia ambazo zimeletwa na mradi huu?

Knowledge na Mashairi ni album niliyoachia 2015. Baada ya miaka kadhaa nikifanya collabo nyingi niliweza kuji challenge na nikaifanya solo project ile.

Album hii ilipokelewa vyema na feedback ninayo zidi kupata mpaka sasa ni chanya. Ilibadili Maisha ya wengi na yangu pia.

Baada ya kazi yako ya mwisho kubwa Antidote hujaachia tena mradi mkubwa kando na singles kadhaa hapa na pale. Hii inakuaje na je  mashabiki zako tutarajie nini kutoka Romi Swahili?

Ni Kweli sijaachia album nyingine baada ya Antidote ila nina kazi jikoni kwenye zinaandaliwa. Kuna bonge la project naachia hivi karibuni.

Pia umefanya kazi kadhaa na magwiji wa uchanaji nchini Kenya kama vile Kamaa wa Kalamashaka pamoja na jamaa za mamtoni Mowa Olodumare na Solare Star. Umuhimu wa hizi collabo kwa sanaa na muziki wako ni upi?

Collabo hizi ni kielelezo kwamba kimo changu kimekolea kwenye game. Nimeweza kujifunza mengi katika mchakato wa kutayarisha muziki na magwiji hawa. Kuna kanda kadhaa ambazo zimerekodiwa tayari na pia tutaziachia mwakani.

Pia hivi majuzi niliona unauza chata lako "Romi Swahili - Est. 2021". Tueleze kuhusu hili chata lako na linapatikana wapi na kwa bei gani?

Nimeandaa chata la Romi Swahili kwa minajili ya project ambayo najitayarisha kuiachia. Story ya chata hii na kazi ambayo naiachia hivi karibuni zinaandamana. Mashabiki pia wamekuwa wakiuliza chata la Romi Swahili kando na chata za albums ambazo nimezitoa.

Changamoto zako kama mwandishi na mchanaji ni zipi na unakabiliana nazo kwa njia ipi?

Changamoto zangu kwa muda mrefu zilikuwa ni kufanikisha huo mchakato wa kuandaa kazi na kuzitoa. Nashukuru kwa sana vile nina timu inayoniunga mkono kwa sasa.

Impact ya mitandao ya kijamii pamoja na streaming apps ni ipi kwa sanaa na muziki wako na wana Hip Hop ki ujumla. Je inaleta matunda au bora tungeuza kanda zetu moja kwa moja kwa mashabiki zetu?

Mimi ni old school, kuna kitu kuhusu shabiki kuwa na nakala ngumu ya mradi nyumbani kwao. Mimi pia ni mnunuzi wa kazi za wasanii na collection yangu ni spesheli. Naamini wasanii wataweza kujimudu vyema zaidi kupitia mauzo ya moja kwa moja. Streaming sites ni nzuri kwa ajili ya uwezo wa kuwafikia wengi ila mapato yake madogo, sana sana kwa wasanii wanaochipukia na wanao jifadhili. Kuuza kazi zetu ana kwa ana ndiyo njia mwafaka.

Ule mradi wenu wa pamoja na kimapinduzi Last Warriors mkiwa na ma emcee wenzako kutoka Kenya na Tanzania ulikujaje na unazungumziaje kazi kama hizi zinazonuia kujenga ujirani mwema kupitia sanaa na muziki? Unaongeleaje hali ya utamaduni hapa Africa Mashariki hivi sasa, je tupo pahala pazuri?

Kuwepo kwangu kwa Last Warriors ni kwa juhudi zake Kaa La Moto, aliweza kukutanisha wasanii wote ambao wako kwenye mradi huu, shout out to KLM.

Napendezwa sana na hali ya game, haijawahi fikia nikawa na tashwishwi kuhusu game ilipo ama inapoelekea. Kuna wasanii wengi ambao wanafanikisha ipasavyo kwa kipindi chochote kile.

Kazi hizi zimeniwezesha kuunda urafiki na wasanii wa nchi jirani. Neno kwa Plate mdai Jasho, Nash Mc, Azma, Vitali Maembe na wengineo.

Kando na muziki, ualimu ni taaluma yako. Jamii inakuchukuliaje wewe unapoweka chaki chini na kuchukua kinasa ukiangalia mtazamo wa watu wengine kuwa utamaduni na muziki wa Hip Hop ni wa kihuni?

Hamna tofauti. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Hip Hop na Fasihi ambayo ni somo ninalofundisha. Huenda kuna watu wana maoni tofauti kuhusu kauli yangu lakini kukutanisha hizi taaluma mbili imenikuza kimawazo. Inakuwa rahisi kwa wanafunzi kuelewa Fasihi maanake rasilimali ninazotumia kufundishia zinawawezesha hawa wanafunzi kunielewa.

Ninapojadili beti ya ngoma flani ya Hip Hop katika darasa la Hip Hop huwa inawasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi fasihil. Hip Hop ina uhalisia ambao hauhitaji kutetewa, ni ukweli ambao unasimama mwisho wa siku hata baada ya watu kuwa na kauli eti ni muziki wa kihuni. Ni upanga wa ncha mbili, kuna rap inasifu uhuni ambayo imepewa kipaumbele lakini haimaanishi ni sanaa yote kwa ujumla, ni muhimu watu waelewe kuna utamaduni wa Hip Hop. Hip Hop inaokoa maisha.

Tukimalizia tupe anwani zako za mitandao ya kijamii na streaming apps. Pia tupe neno lako la mwisho na shukran zako kwa mashabiki zako na watu wako pia.

Anwani ni Romi Swahili kwa kila jukwaa, I'm a simple man.

Twitter: @RomiSwahili
Facebook: Romi Swahili (Griot Wa Nyagathanga)
Instagram: Romi Swahili

Shukran sana kwa muda wako kaka

Nashukuru sana pia kwa muda wako. Zidi na kazi nzuri unayoifanya. Dua Njema.