Uchambuzi Wa Mixtape: 1522
Emcee: Rota Freestyle Doctor
Tarehe iliyotoka: 10.10.2022
Nyimbo: 10
Watayarishaji: Ambrose Dunga, GQ, Vennt Skillz, Zachaa, S2Kizzy, Marco Chali
Mixing & Mastering: Marco Chali, Ambrose Dunga, GS
Studios: MJ Records, Mandugu Digital, Kwanza Records,

Nyimbo Nilizozipenda: Tochi Ya Mlinzi, Robert Chukwu, Morogoro, Hisia,

Rota Freestyle Doctor

Roterline Flavian Komba au ukipenda kumuita kwa jina la kisanii Rota Freestyle Doctor ni msanii ambaye alijijengea jina kule handakini miaka ya nyuma kama bingwa wa mitindo huru. Alibobea kwa kuonesha ujuzi wake wa kuunda mashairi yake akiwa kwenye majukwaa hivyo akatunukiwa udaktari wa mitindo huru yaani Freestyle Doctor.

1522 ni Mixtape ya Rota ambayo aliita kwa ajili ya kuwataarifu mashabiki zake kuwa yeye karudi tena kwenye game baada ya ukimya ambao aliunza mwaka 2015 na kuumaliza 2022. Hapa ndio unapata maana halisi ya jina la album yake 1522. Mradi huu pia unakuwa kama utangulizi mzuri kwa yoyoye yule ambaye alikuwa hamfahamu Rota.

Kazi hii ambayo imejumuisha ngoma tofauti tofauti ambazo aliwahi kuziunda hapo awali binafsi nimeukubali sana kwani uliniburudisha na kunielimisha sana. Emcee huyu kwenye mradi huu kahakikisha kuwa waskilizaji wake wanaelimika na kuburudika ipasavyo.

Kazi yenyewe imesimamiwa na watayarishaji wazuri na pia imeshirikisha ma emcee na waimbaji kadhaa kama vile Country Boy (kwenye remix ya ngoma yake Aah Wapi Remix, ngoma flani ya ucheshi hivi. Kwenye mradi huu utamkuta mtaalam wa masauti Belle 9 kwenye Hisia kwenye mdundo mkali wa Marco Chali.

Wayajue ni wimbo alioundiwa Rota baada ya kushinda shindano flani enzi hizo na hapa pia anashirikishwa mzee wa Nilipe Nisepe Belle 9, ambaye sauti yake ikishirikiana na vizuri na tarumbeta za Dunga zinahakikisha kuwa ujumbe tunaupata ipasavyo. Am Going Remix ni mdundo wa Dunga na Rota pia anahakikisha kuwa mkitoka dance floor mko hoi chakari na mmeloa jasho kinoma kwenye ngoma hili la kujimwaya.

Baadhi ya ngoma pendwa kwangu ni ile iliyoandaliwa na GQ toka Morogoro Tochi Ya Mlinzi. Hili dude kila ninapoliskia hupiga tofauti sana. Pamoja na ngoma hii kuna Morogoro ambapo wazawa hawa wawili wanawakilisha freshi mji wao, wimbo wa ki utu uzima; mdundo, udonyoaji, chorus na quality ya ngoma.

Story telling ya emcee huyu pia inaonekana bayana kwenye ngoma kadhaa; Robert Chukwu 1 ambao ni noma sana, tunasubiria sehemu ya pili, pamoja na Majuto.

Kutoka 2015 hadi 2022 ni miaka 7 kamili. 7 kama vinavyosema vitabu vya dini huonesha ukamilifu flani hivyo kupitia 1522 ni dhahiri kwamba Rota karudi kwa muda sahihi na sisi mashabiki wake lazima tutapata matibabu na burudani ya kweli toka kwa Daktari bingwa maswala ya Mtindo Huru (Freestyle). Karibu uwanjani Dr. Rota.

Kupata nakala yako ya mradi huu wasiliana na Rota Freestyle Doctor kupitia

Facebook: Rota Komba (The Freestyle Dr)
Instagram: rota_freestyledoctor