Roy Kisielo - 3M - Mhathiri, Mbunifu, Muunda Michezo

Sanaa pamoja na mziki wa Hip Hop umenipa fursa ya kuwasiliana na kufahamiana na watu wengi. Mmoja wa watu hawa ni Roy Kisielo ambae ni mhadhiri wa chuo kikuu cha ufundi kilichopo nchini Kenya(Technical University of Kenya), mbunifu kwenye idara ya Ubunifu na Vyombo ya Habari(Design and Creative Media Department) na pia ni muunda michezo(Game Developer) - 3M.

Roy ametengeneza michezo kadhaa na pia ameshinda tuzo kadhaa. Yeye ni mtaalam wa mambo ya ubunifu mwenye kampuni yake na pamoja na haya ni mwanafunzi wa mziki wa Hip Hop na amechangia pakubwa kwenye game la Hip Hop nchini Kenya.
Leo tumepata fursa ya kuwa na mahojiano nae kwa njia ya WhatsApp. Karibu upate madini yatakayokujenga!

Historia yako ni ipi? Jina lako rasmi na unajishughulisha na nini kimaisha?

Natambulika rasmi kama Roy Kisielo na Nairobi, Kenya ndio nyumbani. Najihusisha na maswala ya graphics design pamoja na hili pia ni 2D Animator na ni Game Developer pia (mtaalam wa kutengeneza michezo inayotumika kwenye simu, tablets na kadhalika)

Niambie kidogo kuhusu Roy Kisielo umetokea wapi, ulikulia wapi, utoto wako ulikuwaje, umesomea wapi na nini, na umefikia wapi hadi sasa?

Nilizaliwa Mombasa ila nilikulia Nairobi mitaa ya Eastleigh. Utotoni nilikuwa mchangamfu sana kwani nilijihusisha na vitu viliyonivunja mifupa na kunitoa jasho! Shule ya Msingi, nilisoma shule ya kutwa hadi nilipofika darasa la tano ambapo nilipelekwa shule ya bweni.

Nilipata changamoto sana kusoma shule ya bweni nikiwa sekondari hivyo basi nilifukuzwa nikiwa kidato cha pili. Nilimalizia kidato cha nne nikiwa nyumbani. Ilikuwa changamoto sana ila nilifanikiwa kufaulu.

Nilisomea Stashahada yangu ya Graphics Designs na kuhitimu 2008. Kwa sasa nasoma kwa bidii ili niwezekupata Shahada yangu(Bachelor’s Degree).

Unafanya sanaa ya aina gani?

Digital Art au kwa tafsiri Sanaa ya Kidigitali.

Kwenye shughuli hii ya graphics designing ni kipi kimekugusa sana kwenye ujuzi wako wa kubuni?

Kwa ujumla, ninafanya utafiti kabla ya kuingia katika kazi yoyote. Hii huniongoza na kunisaidia ni kipi nitakachokitoa na pia mapokezi ndiyo huongoza na kunipa motisha kwenye kazi yangu inayofuata. Ninapenda kukosolewa na kupata mtazamo wa watu tofauti juu ya mambo ninayoyafanya. Kwa hivyo ningesema kujifunzaji ndio kunaelezea kazi yangu ya sasa na inayofuata.

Kazi yako inatoa maoni gani juu ya maswala ya sasa ya kijamii au kisiasa?

Maoni yangu yamelindwa kweli, ila kama ni lazima niongee juu ya jamii, huwa nashughulikia maswala yanayoendelea, kwa mfano; tungekuwa na marafiki wengi wanaopigwa risasi na familia zinaathiriwa sana na athari hiyo, kwa hivyo wakati mwingine ningependa kukamata ishu hii katika kazi yangu. Wakati huo huo ningependa kuwasilisha jinsi wenzangu wanavyohisi kuhusu vile jamii imeundwa kukula wewe ukiwa hai! Kwa hivyo ningesema ninafanya kazi ya kumfanya mtu atafakari, kufundisha na kuinua haya yote ili yapate kuonekana wakati mimi pia nikipata masomo yangu katika mchakato huu.

Je ni nani alikuvutia pakubwa kwa mambo ya designing na kukupa hamasa ya kuwa graphics designer? Pia ni nini hukupa hamasa na motisha ya ku design?

Nimekuwa nikichora tangu nikiwa mtoto. Kweli, nilitaka kuwa animator lakini hakukuwa na vyuo vyovyote vinavyotoa mafunzo ya animation kwa hiyo nilienda kusomea uchoraji. Familia yangu ilinisaidia kutambua shule na jambo hilo lilikuja wakati mzuri ambao tayari nilikua nikijifunza uchoraji, picha za watu na fulana pamoja na t-shirt zilizochorwa kwa mikono. Nimezoea kujitia motisha.

Kusema hivyo, ningesema nimesukumwa na kazi nyingi ninazoziona mitandaoni, kuna wabunifu wengi wanapiga kazi na ninajitahidi kujiboresha kila siku ili viwango vyangu pia vizidi kuimarika. Mifano ya wanasanaa wanaonivutia nchini Kenya ni Avandu Vosi, Studio za Sirnare, Chel Wek, Arnold Lakita, Swift Graffiti, Bankslave, wanafunzi wa wanafunzi toka chuo kikuu ninachofanya kazi. Kimataifa; Saint Chase, Koteri Ink, Kim Jung Gi, Unorthodox Fox... kuna watu wengi sana wanafanya mambo mazuri. Ninawapigia salute kwa hili!

Tueleze kidogo kuhusu kazi yako, ni nini unahitajika kuwa nacho ili uweze kufanya hii kazi vizuri?

Kama nilivyosema hapo awali, utafiti unahusika kwa sana. Pia inachukua mazoezi mengi kupata ujasiri wa kuweka kazi yako huko nje. Mwishowe, jaribu kupata kompyuta au graphics tablets ili kupata kazi yako kwa dijiti. Kompyuta pia hufanya iwe rahisi kutafiti na kusambaza kazi zako. Pia kumbuka kujitia motisha kwani wewe ni shabiki wako mkubwa kama na vile vile uwe mkosoaji wako mwenyewe mkubwa…

Umekuzaje kipaji hiki hadi kimekupa ajira? Je umejiajiri au umeajiriwa?

Ninajaribu kuunda mtandao wa masiliano mzuri na watu kadri iwezekanavyo. Pia huwa ninahudhuria warsha ili kuweza kuonesha kipaji changu.

Nimeajiriwa katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya lakini pia ninaendesha studio yangu binafsi na nimeshirikiana na rafiki yangu kuanzisha kampuni iitwayo Square Earth Interactive, itafute!

Je unatafutaje fursa za kazi?

Ninapata kazi kupitia mapendekezo na pia kwa kuweka kazi zangu kwenye mitandao ya kijamii.

Kazi zako hupatikana kwa bei gani?

Bei ya kazi inategemea na maelezo ya kazi ya mteja na pia ukubwa wa kazi. Ila bei elekezi ni Kshs 5,000 na kwenda juu.

Ilikuaje hadi kufikia kufanya kazi na ma emcee wa hip hop? Umeshawafanyia kazi na akina nani nje na ndani ya Kenya?

Ningependa kusema, ninapo hudhuria matamasha ya Hip Hop ndipo watu hupata fursa kuona kazi zangu na pia wakati mwingine huvaa t-shirt zinazo onesha kazi zangu.

Nimefanya kazi na Kambi Halali (Kalimani the MC & Shahidi) wa Poetry Education, UFO (Eli Sketch & Ojiji) kwenye albamu yao ya Makinika, 1183 ya the R.I.F.T, albamu ya Bishop Tokanduki- Tokanduki Zaidi Ya Struggle, Kitu Sewer na Mutant kwenye Campus Diary, Dabliu & Magode kwenye Mahat Mabangi: The Untold Story na Wazalendo Raia ya Fikrah Teule. Sijaunda majalada ya albamu nje ya Kenya.

Kando na wana Hip Hop umepata fursa na kufanya kazi na watu gani wengine ?

Nimefanya kazi na Mercy Corps, Afrika Esports Series pamoja na Doc Moyo kama naweza kuwataja wachache.

Ulianzaje kupata kazi za hawa wasanii wa Hip Hop?

Nilianza kwa kujitolea, niliunda jalada la kandamseto ya Eveready, nimesahau jina… samahani. Halafu, nilitafutwa na Kambi Halali (Kalimani The MC na Shahidi) ili kubuni jalada la EP yao kisha nikaanza kupata simu toka kwa watu wengine wakiomba tufanye nao kazi.

Tofauti yako na designers wengine nini? Ni nini mtu akiona kazi yako atajua moja kwa moja hapa Roy Kisielo kahusika?

Naam, ninachora majalada mengi ya albam kisha napenyeza picha za kompyuta hapo. Mimi huwa na ubaguzi kuelekea kutumia rangi nyeusi na nyeupe, pengine silhouettes(vivuli) pia …lakini sikai na mtindo mmoja kwa muda mrefu sana. Napenda kuendeleza kazi zangu.

Design/mchoro ya kazi zako unapopata kazi huwa unaanzaje kuiunda? Unapataje wazo kutoka mwanzo hadi jalada kukamilika?

Kawaida napenda kumuuliza mteja maswali mengi hata tukiwa tunaongea nae kwa njia ya simu na kuanza kuchora taratibu huku nikimsikiliza. Hatua inayofuata ninaingia kwenye Google kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu mada husika alafu naendelea kuchora. Nimekuwa na mazoea ya kuuliza maswali kila wakati kati kwa njia ya WhatsApp / barua pepe na wakati mchoro unaanza kuja vizuri huwa naanza kufanya kazi hiyo kwenye kompyuta.

Nimeona pia unajishughulisha na Game development, je sector hii umekua kwa kiasi gani nchini Kenya? Je inalipa?

Nilianza game designing mnamo mwaka 2015. Na ndio, inalipa! Nimebahatika kushirikiana na marafiki na watu nisiowafahamu na kushinda tuzo kwa michezo tuliyoiunda ndani ya masaa 48. Kazi yangu imekuwa kuunda mtu au chochote nitakachokipa tabia flani na hadithi. Pia nimeingia kwenye shughuli za game animation(uhuishaji wa michezo). Bado ninazidi kujifunza kuhusu biashara hiyo.

Je Africa Mashariki tuna uwezo wa kuunda games au animations za hali ya juu kama vile nchi za ughaibuni?

Inawezekana sana; kinachohitajika ni kupenda kujua. Muhimu zaidi jifunze michakato ya kuunda michezo ya kidigitali na maendeleo. Pia usisahau kusambaza kazi yako ikiwa unataka kukuza ujuzi wako.

Shughuli ya kubuni kazi ya mteja huchukua muda gani kukamilisha?

Hili hutegemea na mahitaji ya mteja. Kazi inaweza kunichukua siku moja kwa kazi ndogo au hata mwezi mmoja.

Muziki na uchoraji je vinaendana? We unapenda kusikiliza mziki gani? Una miradi gani ya wasaniii iliyotoka 2021 ambayo unapenda kuiskia mara kwa mara?

Ninaweza kucheza sinema kwa nyuma wakati nikifanya kazi, haswa ile niliyoiangalia hapo awali kwa mfano The Mask, How High, Friday, The Godfather (cinema zinazokubalika hadi sasa), documentaries au hata NatGeo.

Ninasikiliza muziki mwingi au ninasikiliza tu ala, bila shaka. Wakati mwingine mimi hupenda mazingira yangu yawe na ukimya.

Albamu ninazopenda sana mwaka huu 2021 ni Afrika ya Pallah Midundo, Kiswahealing ya Kitu Sewer & Maovete, Victims of Madness ya Wakadinali, Azania Na Wanawe ya Fikrah Teule. Kimataifa napenda kuskiliza miradi ya Port King Hus ya Hus Kingpin, RI.B.S ya Eff Yoo na Spit Gems lakini huwa napenda kuskiliza Reggae na Dancehall pia… inategemea na siku. Maadamu ni chakula kizuri kitakuwepo kwenye sahani yangu!

Siku yako huanzaje?

Ninaamka na kupiga sala ndogo nikimshukuru Mwenyezi Mungu kwa pale aliponifikisha hadi sasa. Kisha naanza kuangalia taarifa za habari wakati nikiandaa kifungua kinywa. Baada ya haya yote napata kifungua kinywa wakati nikiangalia ratiba yangu ya siku na pia kucheki kazi za jana na kisha naanza shughuli.

Wewe unapenda nini sana kuhusu kuwa designer na je ni kitu uliwachowahi kuwaza kuwa utakuja kufanya?

Ninapenda mwanzo mpya katika kazi ninayofanya kila mara. Kila wakati ninapoingia katika kazi fulani najifunza kitu kipya juu ya mbinu ambayo nimetumia ndani yake. Kuhusu kuwa mbunifu, ningesema nimekuwa mbunifu kwa hivyo nimekuwa nikipenda kuunda vitu. Kwa hivyo, ndio, ninaamini ningekuwa graphics designer, sijawahi kuhisi tofauti juu ya uamuzi wangu.

Je kuna design au kazi uliyoifanya ambayo unajivunia zaidi?

Mimi napenda kazi zangu zote! Nimejifunza kukubali kazi zote nzuri na mbaya…nayachukulia haya kama maumivu ya ukuaji na ushindi!

Kando na shughuli hii ya ku design una vipaji au talanta gani nyingine? Pia unafanya kazi gani nyingine tofauti na digital art?

Ninaweza mchezo wa kuteleza(juu ya theluji) na kuogelea vizuri sana, ingawa ni muda mrefu tangu nifanye hivyo.
Tueleze kidogo kuhusu Studio Doido?

Studio Doido ni kampuni niliyo ianzisha wakati wa janga la corona. Imejikita sana kwa "Maisha katika Uzoefu wa Ubunifu"; ikimaanisha kuwa kazi ninayounda hapo inanuia kugusa watu wote. Ninakusudia kuwasilisha ubunifu wa kipekee kwa njia ya utoaji. Ninaijenga kutoka chini kabisa.

'Doido' kwa urefu ni madoido neno ambalo linamaanisha urembo, mapambo, nakshi au hata ubunifu kama wanavyolitumia wana sheng huku Nairobi. Ninazingatia Uhuishaji wa 2D(2D animation), Ukuzaji wa Mchezo (Game Development), Ubunifu wa Picha na Mapambo ya Vitambaa(Graphic Design & Fabric Decoration).

Una ushauri gani kwa mbunifu yoyote anayeanza kwenye fani hii?

Ni muhimu kuanza! Jielimishe wakati ukiwa kwenye mchakato huu, kutofaulu ndio hujenga tabia yako! Inapima jinsi unavyobadilika. Usiogope kuwashirikisha wengine waone maendeleo yako.

Kipi kingine ambacho ungependa kusema ambacho sikukuuliza?

Soma na Jielimishe, ukishasoma na Kuelewa, chukua kile kinachokuhusu.

Cheki na Roy kupitia mtandao wake pamoja kwenye mitandao ya kijamii:

Tovuti: www.kisieloroy.com
Twitter: Roy Kisielo
Instagram: k1s13I0