Sehemu Ya Kwanza - ‘Kamanda’ Ya Daz Nundaz - KAZI YA KITUME Ilituheshimisha KIZAZI JEURI.
'Kamanda' ya Daz Nundaz ni moja kati ya tenzi chanya sana za kipindi hicho.
Ujumbe wa wimbo wa ‘Kamanda’ ni kutukumbusha kwamba, duniani tunapita tu na ipo siku kila mmoja wetu ataiaga Dunia. Cha muhimu ni kuishi kwa upendo na kutenda mema. Na pindi safari ya mmoja wetu ikifika basi tuombeane dua.
Ni ujumbe wa kitume kabisa huo, hakika Daz Nundaz walifanya kazi ya kitume, na haikuwa rahisi maana kwa wengine ingeweza kuonekana kama kujichuria vile.
Enzi hizo kazi hii inatoka, wazazi wetu waliulizana "Hivi hawa watoto wamepataje akili ya kulinganiana kwa namna hii!?” Namna ile "Kama mtu ndio anaenda kufariki" ilikuwa ni namna ya kipekee sana.
Eti wazazi walifurahia pale waliposikia itakuwa huzuni "Kwa ndugu" lakini ilipokuja "Na masela" wakaguna kuona masela wanavyojaliana!?
Basi na masela tulivyokuwa tunapenda Sifa, kwenye misiba ya wanetu tunabeba jeneza tukiimba "Alazwe pema (peponi) kamandaaa…" ni upendo ulioje huu, ‘Kamanda’ ikachezwa mpaka misibani aisee! Acha kabisa!
Ujumbe mzito haswa, Ilikuwa hata ukikaa mbele ya Mzee, kisha ukipigwa wimbo huu, ndio kwanza unajilaza vizuri kwa kochi, unaweza hata kupandisha miguu kwa meza ya chakula na mdingi akakosa kauli.
Hakika Daz Nundaz walituheshimisha na kufanya tuonekane vijana wa maana kwa wazazi wetu na hata mitaani pia.
Kumbe vijana wanajitambua, wanawaza mbali hivi, pamoja na mambo zao za zile ila kumbe vichwa vipo full chaji!
Utaniambia nini enzi hizo, nimeshika mistari ya wimbo mzima, hata mbele ya baba na mama najiimbia tu.
"Mja rudi kwa mola wako kama ulipotea/
Kumbuka akhera ndipo unapoelekea/
Anza kutenda mema kabla kifo hakijakukuta/
Ukipuuza haya, we utakuja kujuta/”
Cha zaidi hapo baba atasema "Unajua lakini maana yake au unajiimbia tu?" Hahahaaa! Hakika lilikuwa bao la kisigino.
Miaka sasa imeshapita na hatimaye Deiwaka Show inaenda kuwaheshimisha wale waliotuheshimisha.
Kubwa Sana hii.💪🏿💪🏿

Sehemu Ya Pili - Daz Nundaz Family - Kundi Nje Ya Kundi
Daz Nundaz family ndani ya kundi ilikuwa ni full upendo. Namna walivyojipanga kwa nyimbo zao ni ishara tosha kwamba, kwao ilikuwa kundi kwanza.
Tazama, verse ya kwenye ‘Maji ya Shingo’ alichora Kritik kisha akapita nayo Larumba…
Tazama Sajo alianza kuchora verse yake ile ya kwenye ‘Nipe 5’ ila kabla hajaimaliza akahitajika shule, so ikabidi Kritik, Feruz na Daz waimalizie kisha Kritik akapita nayo kwenye Nipe 5, ndio pale Kritik anakwambia "Sikiliza verse ya Chupa..."
Daz hata wakihojiwa kwa media kwamba idea ile au hii ilikuwaje ikawaje na nani aliitoa idea na hivi na vile, watakujibu tu ni Idea ya kundi na ikachakatwa na kufanyiwa kazi na kundi, miaka yote majibu yao ndio hayo. Vipo vingine wanaweza kusahau ila sio jibu hilo, haijalishi tunajua au hatujui wao jibu lao ni hilo hilo. Kundi nje ya kundi.
Feruz alipotoa albamu yake ya ‘Starehe’ pamoja na nyimbo nyingine lakini kuna mgoma moja matata sana wa "Jahazi la Daz" mle ndani featuring ni Daz Nundaz na akina Scout Jentaz nk. Kundi Nje ya Kundi.
Daz Baba alipotoa albamu yake ya "Elimu Dunia" mle ndani kuna magoma makali ile mbaya lakini kuna mgoma matata wa kuitwa "Nipe 5" featuring Daz Nundaz na akina Scout Jentaz nk. Kundi nje ya Kundi.
Hata Makamanda (Sajo, Critik na Larumba) walipofanya track zao kama ‘Kwenye Line’, ‘Karata’ nk bado utasikia Sauti ya Feruz nk. Kundi nje ya kundi.
Kuna mgoma flani matata sana wa Kritik a.k.a N Star mgoma unaitwa "Mnizoee" ule mchorus kaupiga Scout Jentaz ila utasikia pia sauti ya Feruz mle. Kundi nje ya kundi.
Daz Nundaz ni full Package, ukitaka kusikitika basi watakuliza kabisa kwa ngoma kama ‘Kamanda’, Maji Ya Shingo’, ‘Barua’, ‘Nitafanya Nini’, ‘Starehe’, ‘Elimu Dunia’, ‘Bosi’ nk.
Na kama utataka kuruka basi watakurusha mpaka juu kwenye mawingu kwa ngoma kama ‘Kwenye Line’, ‘Nipe 5’, ‘Shuka Rhymes’, ‘Jahazi’, ‘Jirushe’, ‘Wife’, ‘Namba 8’ nk.
Sehemu Ya 3 - Daz Nundaz - Na Simulizi Ya 'Mtanzania Wa Mfano, Si Hayati Si Mamati!
Naileta kwenu simulizi ya kijana wa Kitanzania ambaye maisha yake si hayati si mamati kama ilivyo kwa wengi wetu.
Katika wimbo wa ‘Maji Ya Shingo’ inasemwa kwamba misukosuko ilianza tu pale mwamba alipofiwa, wazazi walimuacha na kubaki mwana mkiwa. Ndugu na jamaa wakasepa na mali, mwamba sio tena kuishi bali alianza kuishia, jua lake mvua yake. Mwamba alipigika mpaka akawa katika hali ya kukata tamaa, ndio pale hajali wala hana habari kwani kama vikesi mbuzi vingi tu kashasingiziwa, kama jela kwake ni kitu gani? Kama kwenda, atakwenda ataachiwa.
Amini kwamba, wengi tunatoka kwa familia hohehahe so hata kama mwamba aliachiwa mali lakini ukweli si mali kitu.
Daz wanakazia hapo, katika wimbo wa ‘Matatizo’ inasemwa;
"Nikikumbuka maisha yangu tangu nipo utotoni/
Mama mizigo kichwani, mimi nipo mgongoni/
Alitafuta maisha huku anapigwa na jua/
Na ndio maisha yangu mpaka sasa nimekua/"
Ndio, tangu enzi za utotoni ilikuwa ni ‘Matatizo’ mfululizo japo baada ya uyatima ndio ikawa sasa mbombo ngafu, maji ya shingo.
Mwamba hajakaa kizembe, kama rhymes anashuka balaa! Hiyo inasemwa kwa wimbo wa ‘Shuka Rhymes’ lakini pamoja na kushuka rhymes kote baado hakuingia ‘Kwenye Line’. Umri unasogea na majukumu hayasubiri. Shida zinapendana shida zinaitana, shida moja huita nyingine ili isiwe pweke, na hii ndio sababu mwamba kuendelea kuishi maisha ya tabu na mashaka mpaka haelewi afanye nini kama inavyosemwa katika wimbo wa ‘Nitafanya Nini’.
Usiku kucha, mchana kutwa, matatizo hayaishi kumghasi mwamba. Mwamba mpaka anawaza kupiga ngeta na kutumia shortcut maana mianya yote imekuwa blocked.
Masikini hapendezi, masikini hapendeki, ndicho kilichomkuta mwamba baada ya kuingia kwenye mahusiano. Mwamba si alizama penzini, akapigwa na kitu kizito, almanusura apate wazimu. Sikiliza wimbo wa ‘Barua’. Demu si alimchana mwamba live, kwamba ufukara na umasikini ndio kuwatenga vimechangia.
Kwamba gashi alichoka na zile ungaunga mwana.
Hamza Kalala anakwambia binadamu ana hatua kuu 3; kwanza kuzaliwa, pili mapenzi na 3 ni Kufa.
Hatua ya 3 hii ndio pale inaposemwa ‘Alazwe pema peponi kamanda, alazwe pema peponi kamanda.’ Ndio hatua hii inaonekana kwa uzuri katika wimbo wa ‘Kamanda’.
Na baada ya hapo kinafuatia nini, Daz wanaielezea hatua ifuatayo katika wimbo wa ‘Kiama’.
Kwa simulizi hii ya kijana wa Kitanzania tunakubaliana kwamba, Daz Nundaz ni kioo nasi kama jamii twaweza kujitazama...Nao Daz Nundaz wanasisitiza hilo katika wimbo wao huo wa ‘Kioo’.
Sehemu Ya Nne - Daz Baba - Nduli Na Nunda Wa Bongofleva
4 brothers.
Mh. Temba enzi hizo akifahamika kama Ice Temba, Das P, Tsuki Lee na Davi Killer. 4 brothers wakaunda kundi la kwenda kwa jina la Sky Image. Kisha ukaachiwa wimbo wa kwenda kwa jina la ‘Kupeta Kwa Zamu’.
Tuokoe muda, Sky Image baadaye walikuja kubadili jina na kujiita Manduli Mob...
So, Sky Image ndio mwanzo wa Manduli, na hapo mwanzo kwa Sky unamkuta Daz Baba, hivyo kiasili Daz Baba ni Nduli.
Jinale halisi ni David Selestine Nyika na alipoingia kwa game akatambulika kama Davi Killer enzi hizi anarap michano ya kufa mtu, sio tu kwa beat hata akapela (Acapella) akifanya anaua.
Davi Killer alikuwa close sana na Das P wakiroll pamoja kwa kitaa na vile yeye alikuwa chalii tu ndio ikapelekea raia kumuita Das Mdogo (mkubwa Das P).
Ndio, siku zikasogea na Das Mdogo akajiona amekua na akatoka kwa udogo na kwenda kwa ukubwa-ubaba! na jina likaenda kama Das Baba.
Muda flani Das Baba nae akajiunga na washkaji na kuasisi kundi la Daz Nundaz na jina likabadilika tena kutoka Das Baba na kuwa Daz Baba.
Haukupita muda Tsuki Lee nae akaenda kujiunga na washkaji zake wa kiwalani wa Gang Gost Killer.
Das P na Mh. Temba wakabakia mtu bee na kuja na ‘Masikini Jeuri’.
Daz Baba na familia yake ya Daz Nundaz wakaja na ‘Maji Ya Shingo’ na nyinginezo na Jina la Daz Baba likawa kubwa Tanzania nzima.

Daz Baba
Muhimu
å Daz baba ana albamu 3
1. Elimu Dunia
2. Dunia Ya Leo
3. Karibu Tanzania
√• Daz baba na familia yake ya Daz Nundaz wana albamu 1 inayokwenda kwa jina la ‘Kamanda’.
√• Daz baba na familia yake ya Tanzaniano wana albamu moja inayokwenda kwa jina la ‘Fanya Kweli’.
---
So, kiasili Daz ni Nduli na tena ni Nunda la Manunda. Kwa upande wa Daz Baba, I hope hapo inatosha kwa leo...
Tchao.

Sehemu Ya Tano - Daz Nundaz - Historia Inaenda Kuandikwa
Siku walipoachia single yao ya kwanza ‘Maji ya Shingo’ wengi tuliulizana, hii imekaaje hii? ilikuwa ni kitu kipya eh! Enzi hizo Rap ilikuwa rap kweli, ile Gangsta Rap, watu wanachana ile mbaya. Kwenye kuimba huku Jaydee, Unique Sister na wengineo walikuwa wanafanya ile RnB yenyewe.
Mapokeo ya muziki yalikuja kwa namna hiyo, namna hii ya Daz Nundaz ilikuwa ngeni. Angalau Sajo, Larumba na Criktik ila Daz Baba na Feruz hawa mbona kama wanarap ila tena kama wanaimba? Ndio, wanaimba ila mbona uimbaji wa haraka haraka hivi kama wanarap?
Huo ulikuwa mwanzo tu, mwisho wa siku miziki ya aina hii ikatamalaki anga lote na ndio sasa Bongofleva ikawa kwenye ubora wake.
Kipindi kile wengi tulidhani kutokana na style yao ya huzuni- kulialia basi watakuwa wamejifunga humo, miaka na miaka.
Nyimbo kama ‘Jirushe’, ‘Nipe 5’ zilitu prove wrong, kumbe washkaji kwa style zao zile zile wanaweza kuimba ngoma za ku party na zikawa tamu ile mbaya.
Baada ya hapo yakaanza mashambulizi kila pande, ni washinde au wasuluhu, Daz Nundaz hawakuwahi kuchanaa mkeka
K-sal alimpa kolabo Feruz kwenye wimbo wa ‘Mkiwa’, alichofanya Feruz humo ni full ile laana! ilikuwa pigo takatifu, wimbo ukawa mkubwa kwa ukubwa wake nawaza labda ulikuja kumsumbua K-sal, maana kila aliporejea raia wanasema bado, bado hujafika kwa level za ‘Mkiwa’....
Chorus ya ‘Nikusaidiaje’ unaikumbuka? ni chorus na nusu.
UVC walimtaka Feruz kwenye Chorus ya ‘T-shirt Na Jeans’, Feruz akawa bize, ila akaja kufanya chorus ya wimbo wao wa ‘Vumilia’. Ile chorus ikalipa na deni lao la mwanzo na nahisi kama Feruz anawadai mle!
Daz Baba alishirikishwa kwa ngoma ya huyu jamaa wa Boni Crew...Ukweli wengi wenu mnakumbuka ule mchorus wa "Wanamuita kaka poa huyu jamaa…" wengi hata jina la kundi hawakulijuaga!
Daz Baba alikuwa na msauti flani hivi....Niko bizeeeeeee! Mwamba huyo hapo.
Hawa jamaa hawanaga cha mechi ya ugenini aisee....Ni mwendo wa kutupia tu.
Tarehe 19/7 Ndani ya Warehouse Masaki. Tanzania itasimama kwa Muda. Kisha saa zitarudi nyuma mpaka enzi zile za ‘Maji Ya Shingo’, ‘Barua’ na ‘Kamanda’. Hapa Daz Baba, pale Feruz, kisha Larumba namba tata na Sajo a.k.a Chupa....
Kuna nini tena!???
√--------
0754 220011
IddyMwanaharamu2024