Mwana FA

Mwaka 2001 ndio mwaka ambao Mwanafalsafa (kwa sasa Mwana FA) ndio alizama rasmi kwenye game ya mziki wa kizazi kipya na wimbo wake wa “Ingekuwa Vipi” akiwa na Jay Mo. Safari ya Mwanafalsafa kimziki sio nyepesi kama wengi wanavyoweza kuwaza. Kwenye mishe mishe za kuhangaika kutaka kutoka kimziki safari yake ilikuwa na vikwazo vingi sana upande wa studio.

FA anakwambia siku moja alikutana na Prof Jay akamsikia kisha akamwambia nenda Bongo Records kuna wimbo pale unaitwa ‘Na Bado’ kaingize mistari utakuwa wewe na washkaji wengine wawili. Baada ya kuambiwa hivyo mzee hakutaka kuvunga wala nini, fasta mpaka kwa Majani kufika kampa story yote aliyoambiwa na Prof Jay.

Majani alimsikiliza na mwisho wa siku akamwambia wimbo ushakamilika, watu wawili washaingiza mistari yao. “Hatuwezi kuingiza mistari ya mtu wa nne wimbo utakuwa mrefu sana!” Baada ya kusikia hivyo mtu mzima FA akasepa tu, hakuwa na sababu ya kuendelea kukaa tena pale, atangoja nini ikiwa kila kitu kimemalizika. Kwa mujibu wa FA mwenyewe anasema ubeti wake kwenye ‘Hii Leo’ ndio alipanga kuutumia kwenye wimbo wa ‘Na Bado’ na kama Majani angempa nafasi ya kumsikiliza basi angekuwa msanii wa Bongo Recordz.

Mawingu studio kwa mtu mzima Bony Luv ndio studio ya kwanza kwa FA kurekodi akiwa na mchizi wake Jay Mo ambaye yeye tayari alishakuwa katoka kimtindo kwenye mziki wa kizazi kipya. Wakati anataka kutoka kimziki aliwaza atokeje ili kila mtu apate hamu ya kumsikiliza ndipo akatoka na ‘Ingekuwa Vipi’ wimbo ambao ulibeba mashairi ya kupokezana (majibizano) kati yake na Jay Moe.

Wimbo ambao uligusa watu waliomtangulia kutoka kimziki kabla yake. Wengine walikaushia kumjibu, wengine waliamua kumjibu tu wenyewe waliona kukaa kimya kwao sio jibu la mjinga, jibu la mjinga kwao waliona ni kumjibu ajue ujinga wake ulivyo. Miongoni mwa wasanii waliomjibu alikuwa Sister P. Kwenye wimbo wa FA aliuliza

"Angeimba nini Sister P asingekuwepo Zay B? /"

Wakati Sister P anatoka kimziki alikuta mwanadada Zay B kashatoka kimziki na wimbo wake wa ‘Gado’ akiwa na Inspector Haroun (Babu). Sister P alitoka kwa njia ya kumdiss Zay B, sasa ile diss ya Sister P kwa Zay B, Mwana FA aliona kama ni njia ambayo ilimtoa Sister P kimziki.

"Nini visado watu tumejaza rumbesa/
Na bado katika fani tunazidi kutikisa/"

Huu ni mstari ambao FA aliona kama Sister P kampiga dongo Zay B ilikuwa baada ya Zay B kufanya remix ya wimbo wake wa Gado akiwa na Juma Nature.

"Zay B sasa yupo gado/
Mashairi yamejaa visado"

Baada ya hiyo ndio FA akapata cha kuandika. Sister baada ya kusikia wimbo wa FA akiwa na Jay Mo hakuona tabu kutoa ya moyoni akazama studio akajibu

"Mpumbavu anauliza ungeimba nini Sister P asingekuwepo Zay B? /
Swali linarudi kwako sasa ungeimba nini Mwanafalsafa kama tusingekuwepo wasanii/
Au nikuite Fredro Starr kwa wimbo uliotafsiri? / "

Baada ya Sister P kujibu kama balaa likazidi kusogea kwenye njia ya kutokea ya FA. Si unajua wimbo wa ‘Ingekuwa Vipi’ uligusa wengi sana. Mtu mzima Dully Sykes nae akaona hapana sio bure kupondwa mtindo wangu ngoja nizame studio nijibu mapigo. Dully aliguswa na mstari huu

"Ingekuwa vipi Dully Sykes angeimba hardcore/
Mashairi kama Jay Mo/
Neno mwanasesere nina imani lisingekuwepo/
Mauzo ya rap ya bongo yangefika platinum tano/”

Baada ya mtu mzima FA kufanya yake ndipo Dully akaja na wimbo wake wa ‘Mr Misifa’. Kwenye wimbo huo kuna mstari ulikuwa jibu la FA na ‘Ingekuwa Vipi’ yake. Dully alijitamba sana kwenye huo wimbo ubeti wa kwanza wote anajitamba kwa misifa ya kijinga. Katika ubeti wa pili ndio akaja na jibu matata sana;

"Ma dj asanteni mnanipigia nyimbo zangu ilo nashukuru kwa Mungu/
Kila napopita wajanja wananiona mzungu,
Washamba nao wananiona mchungu/
Na kila siku sichuji sina tena gundu/”

Alianza tu kwa kumwambia maneno hayo mbeleni pia akaendelea kumwambia

"Mwanasesere ndio style yangu ndio iliyonipa ujiko,
Hata mseme vipi hardcore siimbi ng'o/
Nafanya nitakavyo sifanyi utakavyo wewe vipi? /
Kumbe ndivyo ulivyo una kijicho wewe vipi? /
Izo vipi chuki za kishamba we vipi? /
Unajihangaisha kumchukia star basi umedunda/
Galasa umelamba nami nazidi kutamba/
Kwenye top ten za Bongo na mimi pia natamba/
Oya we oya we vipi umechunda/
Oya we vipi oya we vipi umechunda/
Akili zangu fyatu zipo kushoto nimepinda/
Mitambo ya hatari na walinzi nalindwa/
Mimi ni mshindani nisiyekubali kushindwa/
Bwege unashindana nami wakati wewe kinda/
Najulikana kote Dully bingwa wa mabingwa/"

Hii ndio ilikuwa mistari ya mtoto wa Kariakoo kwa kujibu kilichomgusa. Katika majibu hawakuwa Dully na Sister P tu kwani masela toka Temeke Wandago nao walijibu wimbo kwa kile walichoguswa japo wimbo wao ulikuwa wa majibizano kama ulivyokuwa wimbo wa FA Ingekuwa Vipi’. Wasanii wengine walijibu kwenye interview za redio tu, hawakutaka kuingia studio kwani wengi wao walisema ni ngumu kujibu wimbo uliotafsiriwa kama angekuwa na uwezo angetoka bila kutafsiri wimbo wa kizungu kuja kiswahili. Safari ya Mwanafalsafa na ‘Ingekuwa Vipi’ yake ndio ilikumbana na mitihani hiyo. Wimbo wote ulifanyika chini ya Bony Luv.