Albam: Hazina
Msanii: Salu Tee
Tarehe iliyotoka: 01.03.2020
Nyimbo: 18
Producer/Wapiga midundo:
Ndulla B,Chzn Brain
Studio:
Faraja Records, B Records, 95 Records

Salu Tee ni mshairi aliyezaliwa Muhimbili Dar Es Salaam miaka ya sabini. Jina lake rasmi ni Salutaba Ally Mwakimwangile au ukipenda kwa ufupi Salu T/Tee kama walivyo mbatiza mashabiki zake.

Salu T amekuwa kwenye game kwa muda mrefu na kama vile mto huanzia kama matone ya mvua milimani na kufuata mkondo hadi baharini, yeye pia mkondo wake wa ushairi ulianza toka utotoni, ujanani hadi sasa ni mtu mzima. Enzi hizo akiwa mtoto Salutaba alianza kuonesha upendo wake kwa mziki kwa kuunda bendi na marafiki zake kwa kutumia vifaa vya kuungaunga kule mtaani. Pia ubunifu huu na uhuru huu wa kujitegema ulimkuta yeye akianza kurekodi demo zake miaka ya tisini kwa kuchukua midundo ya wasanii waliopo mamtoni kisha kwenda kujirekodi studio halafu kuzisambaza ngoma zake bure mtaani.

Baada ya kuangusha albam yake ya kwanza Miaka Tele mwaka wa 2015 na ukimya wa mda mrefu Salu Tee alirudi tena kwenye game na kuangusha albam yake ya pili rasmi mwaka wa 2020 Hazina.

Hazina ni tunu, ni akiba ya milele ya elimu halisi ya maisha tunayoishi, ni halisi na sio vitu vya kutunga tu au kujisifia kwa maana tunu ikifukiwa ikafichwa miaka nenda rudi na ukabahatika kuifukua bado thamani yake itakua vile vile au pia itaongezeka maradufu.

Unaposikia mradi huu wa Hazina toka kwa Salu Tee moja kwa moja utaona kuwa ni album iliyokomaa na kushiba maudhui ya hekima, busara, ubinadamu, upendo baina au kati yetu na mradi huu unaenzi hivi kuliko mali au vitu vinavyoonekana kwa macho.

Mradi huu unaanza na utangulizi mzuri ambapo Salu Tee amemshirikisha mhadhiri wa chuo kikuu kilichopo America Daktari Msia Kibona Clark ambae ni Mtanzania aliyekulia kule. Daktari Msia anasoma shairi dogo kwa lafudhi ya kimamtoni ambalo linaweka msingi mzuri wa mradi huu,

“Nalala wima utu uzima/
Ushakua mwingi hekima lazima/
Hazina hua haipingwi/”

Muundo wa mashairi ya Salu T ni wa kipekee pamoja na midundo anayoitumia kwa ajili ya mradi huu. Nyimbo mbili za kwanza zina mashairi mazuri yanayo chanwa juu ya midundo mizuri iliyoundwa kiubunifu sana. Pia Jasiri part 2 ni wimbo ulioandikwa ki ustadi wenye kiitikio mzuka sana uliojaa ujasiri wa maneno. ukemia kati ya Salu T na producer Ndulla B unaonekana vizuri sana hapa wakati Salut T akiachia madini mwanzo mwisho akisema,

“Madogo wakituelewa itasaidia sana/
Wakikosolewa vigogo njia itapatikana/
Tulia mbogo ghasia hazitoungana/
Siasa imejaa mazogo mikasa ya kutoelewana/
Anasa ya hongo wachache kufaidishana/
Darasa ubongo tusikache kuelezana/
Uheshimiwa ukweli wote tutaelewana/
Zipigwe vita kejeli sote tutaheshimiana/
Tujenge nguvu kazi tuondoe lawama/
Acheni unazi utukutu hauna maana/
Usitukane kazi utu ubebe dhamana/
Dunia ya utandawazi thubutu iwe ya maana/”

Upendo ni mada ambayo Salu anaipenda sana, upendo kwa muumba, upendo kwa watu wa dunia na pia upendo kati ya wana Hip Hop. Kwenye Hasara kwa Jamii anaonesha upendo wake dhahiri anapoamua kufanya kazi na ma emcee toka Kenya anapomshirikisha Rudi(wu) Makeke toka Makeke Family pamoja na producer gwiji toka Mombasa Chzn Brain ambaye kwa sasa anafanya kazi zake Tanzania. Utajua Rudi(wu) ni mtu wa Mombasa pale anapoangusha mstari flani unaopendwa na wana Mombasa, “Kama nalia, Kama nacheka!” Hasara ni kwa jamii kama bado hawasikii jumbe za mradi huu.
Pia interludes au mapumziko kidogo kwenye albam hii yameundwa ki ubunifu sana. Mara nyingi kwenye interludes ma emcee wengi huweka kama igizo dogo au kwa kingereza skits ila Salu T anatumia mda huu kutupatia Somo-Ukweli pamoja na Somo–Wazazi. Yote mawili ni mashairi mazuri sana.

Salu T pia anatuonesha upande mwingine wa uwezo wake utunzi na ubunifu wa kuandika hadithi. Wimbo kama Bado nakumbuka ni wimbo unaoelezea matatizo yanayomkumba Salu T wakati anapojaribu kutenda mema kwa kumsaidia binti aliyemkuta njiani kabakwa. Uzuri wake unamponza pale kesi inamgeukia yeye kuwa ndiye kahusika kumbaka binti huyo. Wimbo huu umejaa matumaini kuwa utu upo, taharuki kuwa mtenda mema kafikwa na mabaya, majonzi ya uonevu na matumaini tena kuwa wema hulipwa kwa wema tu kama kiitikio kinavyosema.

Hewani au Mtaani ni wimbo mzuri sana na wenye mafunzo kwa mtu yoyote anayetaka kujitosa kwenye sanaa hii kwani unanuia kuonesha changamoto ya mtu anayetaka kujitegemea na pia changamoto atakazozipata yule anayetaka kusikika kwenye vyombo vya habari kama vile radio na televisheni. Wimbo ni madini tupu ambao juu yake inapigwa violin nzuri sana.

Mambo ya imani pia yamegusiwa kwenye wimbo Kila Jema. Salu ana uwezo wa kuchukua mada ngumu na kuiandikia mashairi mafupi na mazuri na yanayolenga mada mwanzo mwisho. Hivyo hivyo Yote Heri ni wimbo makini sana unao kutia moyo kutotilia maanani maneno ya wanaokusema, wanaokukejeli, kukusimanga, kukutukana na kukukatisha tamaa maishani mwako.

Nyimbo za Shukran (final cut) na Baraka anaomshirikisha Jadah MaKaNta ni nyimbo ambazo walengwa ni familia yake na zinatupa mwanga kidogo kuhusu maisha ya emcee huyu kama vile wimbo wa Hazina. Wimbo Hazina akiwa na Damian Soul ni wimbo uliobeba jina la albam na ni wimbo mzuka sana ambao unatupa historia ya maisha ya Salu Tee. Kwenye wimbo Shukran unatumia sampuli ya mziki uitwao Nawashukuru wazazi wangu toka kwa kundi la DDC Mlimani Park Salu Tee anaongea na wazazi wake akisema,

“Wangu wazazi mliyoyafanya ni kubwa kazi/
Udogoni mwema ukubwani kichwa nazi/
Huu ni ujinga mlipinga roho ya kibazazi/
Niliwatinga lakini hamkunipa radhi/
Mlinivumilia ingawa niliwashusha hadhi/
Kwa hilo najuta nahisi kujipiga kitanzi/
Bila ya nyie wapi ningepata hifadhi/
Mimi na kaka zangu mlitupa ya uhakika makazi/
Elimu makini bila kusahau mavazi/
Sikuthamini nimeamini utoto ni uduanzi/
Sasa nimekua njia zote ni bazazi/
Malezi yenu nyinyi si ya mjomba wala shangazi/
Najua mnazeeka uzee una maradhi/
Hakuna kucheka kiuchumi mmeshuka ngazi/
Mnateseka nikipata ntaokoa jahazi/
Ntaondoa kila uzia sitokua jambazi/
Toeni uwoga msiwe na wasiwasi/
Siwaongopei sikosei mi si Awadhi/
Shukran nyingi sana kwenu naweka wazi/

Nyimbo zilizosimama pia ni kama Yote Heri remix pamoja na Baraka na Upendo ambazo ameshirikishwa muimbaji mzuri wa kwenye nyimbo za Hip Hop toka Tanzania dada Jadah MaKaNTa.

Album hii ni nzuri toka mwanzo hadi tamati. Hakuna wimbo wa kuruka. Hazina haiozi, ndivyo walivyosema wahenga. Kwa kuzingatia wosia wa wazee wetu emcee Salu Tee toka Kyela Mbeya ametupa albam ambayo ni Hazina ya milele kwenye rap game ya Tanzania na Africa Mashariki ki ujumla. Kongole kaka Salu Tee kama ulivyosema, “Utu uzima ushakua mwingi/ Hekima lazima, hazina hua haipingwi!”

Mfuate Salu Tee kupitia mitandao ya kijamii:

Facebook: Salu Tee
Instagram: salutaba_