Uchambuzi wa Mixtape: Dunia Yangu
Wasanii: Sau State Huru
Tarehe iliyotoka: 15 June 2018
Nyimbo: 14
Wapiga midundo na ma producer: Black Junior, Rex Beats, Mopolo, 10th Wonder, Dr. More
Studio: 99 Records

Kitu nilichogundua miaka kadhaa iliyopita ni kuwa kwenye Hip Hop kuna ma emcee kibao independent wanaotoa miradi mingi chini ya maji ambayo aidha wengi huilalia maskio au hawapati fursa ya kujua imetoka na hawajui wataipata vipi.

Moja ya miradi ambayo mimi binafsi nilinunua toka kwa emcee Ponera ni Kanda Mseto ya Dunia Yangu kutoka kwa kundi lake liitwalo Sau State Huru. Japokua biashara yetu ilihusu Mask Off Ep niliamua ku support na kuchukua mradi wa SSH pia na sikujutia.

Sau State Huru ni wanafamilia (hawataki kuitwa kikundi) ambao chimbuko lao ni Songea, Ruvuma na hapo awali walijulikana kama Ngoni Rap Zone. Ma emcee wanaounda familia hii ni Ponera(Hon), Eddy Mc pamoja na Christom Staff. Japokua kila mmoja ni emcee anayejitegemea, toka 2015 walikuwa wakikutana pamoja ili kuweza kuunda mradi wao kwa kwanza wa pamoja ambao unajulikana kama 'Dunia Yangu'.

'Dunia Yangu' ni mradi simple sana ukiuskia kwa haraka ila kwenye simplicity hii ndio unakutana na mawazo complex kwenye mashairi ya wachanaji hawa. Kama vile mchoro wa jalada unavyoonesha SSH wanakufungulia dunia yao kwa kupitia mziki ambao enzi hizo ungekuwa unapigwa toka kwenye radio cassette tofauti na siku hizi ambapo aidha tunatumia CD, simu au pengine tuna stream toka kwa apps.

Wimbo wa Dunia Yangu ulioundwa na 10th Wonder ndio umebeba jina la mixtape. SSH wakimshirikisha WD Waddy wanatupatia positive vibes kuhusu wanapotokea wakisema kuwa japokua unaweza ona hawana vitu vingi maishani mwao, upendo walionao ndio kinachofanya wafurahie maisha. Bass ya WD Waddy inatukumbushia kuwa love ndiyo inawaweka pamoja akiimba,

“Usione dunia yangu nai enjoy sana/
Sababu tuna love yakutosha aah/”

Ponera anachora picha ya simplicity ya dunia yake akisema,

“Aliishi Malcom X, Nyerere na Mandela/
Aliishi Saraphina, Brenda Fassie, Vuli Ndela/
Nami nipo naishi zangu ki fikra/
Kwenu mnauziwa maji huku kwetu yanamwagika/
Madini kibao ardhini mafao/
Weka sofa si tunatamba hata kwa viti vya mbao/”

Mada hii ya 'Dunia Yangu' imebebwa pia kwenye nyimbo kama Nataka na Toka Ndani ambazo zote zimesimama kimashairi na ki midundo. Nyimbo zote zinatoa mitazamo chanya juu ya maisha yetu ya kila siku na kutufanya tuzidi kuthamini vya kwetu.

Kwenye dunia ya ma emcee hawa pia mapenzi yapo. Mada hii wameigusia kwenye nyimbo mbili; Usisahau pamoja na Miss Njinji ambao unatumia sampuli flani nzuri sana toka mamtoni.

Safari Njema ni wimbo mzuri sana ambao wazazi wanamtakia mtoto wao baraka tele anapoamua kutoka kijijini na kwenda mjini kusaka unga. 10th Wonder alisimama vizuri kwenye beat hili linalokupa “nostalgia” ukikumbuka vile wazee wanajielezea kuwa waliuza hata pombe ili kuhakikisha mtoto anapata malezi mazuri. Wimbo umejaa wosia kibao ambao unaweza kumsaidia kijana na yoyote yule ambae anaanza au kuendeleza maisha ugenini. Christom Staff ndio anatema madini kibao hapa.

Kando na hadithi nzuri ya Safari Njema kuna hadithi utazikuta kwenye wimbo kama Mfungwa na Radio Zao.  Story zote hizi ni fire! Mfungwa inamkuta Eddy MC akiongelea hadithi ya binti flani aliyepumbazwa na kutekwa na utandawazi na kuufanya ndio mfumo rasmi wa maisha yake, akaona bora jela (utandawazi na athari zake) kwani kila kitu ni bora na anafanya kila awezavyo  aendelee kuishi huko. 10th Wonder kama kawa kafanya mauaji kwenye mdundo.

Radio Zao inamkuta Ponera akituchekesha na story flani inayosikitisha kuhusu changamoto wanazopata ma emcee wanapotaka ngoma zao zipigwe kwenye radio zao. Mdundo mzuri sana unapiga mdogo mdogo Ponera akitupatia story murua sana akidai yeye ni “mc mkali”. Ponera anabadili sauti yake ki Eminem ili kuweza kucheza role tofauti. Wimbo huu ni ucheshi mwanzo mwisho haswa pale presenter anapolia anapoambiwa akaoshe vyombo kwa kukosa hela ya kulipia msosi aliokula hotelini.

Majigambo kwenye albam za ma emcee ni kitu cha kawaida hivyo basi SSH wanajisifia uwezo wao kwenye nyimbo kama Mkemia,Mikono 100 na Chuma Kikoli Moto.

Sau State Huru wanatoa shoutout kwa wote wanao wa support kwa namna moja au nyingine kupitia wimbo Watu Wangu pamoja na support kwa ma sister zao kwenye wimbo uitwao Guantanamera unaotumia vizuri sampuli ya wimbo wa jina hilo toka kwa Cuarteto Caney na uliotumiwa tena na Wyclef Jean wa the Fugees. Yeye mwenyewe akipata fursa ya kuskia version ya Sau State Huru ataukubali kama nilivyoukubali.

Anasema hivi Ponera kwa sister anayeongea nae,

“Unaamini Yesu unapiga goti/
Yeye anaamini kuna Yesu na bado anasaka noti/”

Bonus track ya Narudi Nyumbani iliyoundwa na Black Junior ndio inafunga mradi huu kwenye wimbo ambao unazidi kuweka wazi zaidi maudhui ya 'Dunia Yangu'. Mdundo ni mzuri sana na watoto wanaotumiwa kwenye kiitikio pia wananogesha wimbo.

Sau State Huru wamefanikisha lengo lao la kutuonesha dunia yao na pia wametuonesha kuwa wao ni Wakolonjinji kwa lugha ya ki Ngoni au wazawa kwa lugha ya Kiswahili wanaopenda wanapotokea na wanapenda kuenzi vya nyumbani. Kama wanavyosema kwenye kiitikio cha Narudi Nyumbani.

“Tambua mtumwa mzuri ni yule anayekataa nyumbani/
Acha wakate kivuli si tunachumia juani/”

Mimi kama Mkolonjinji nathamini vya nyumbani, nyie je? Karibu kwenye Dunia Yangu.

Wasiliana na wana Sau State Huru kupitia mitandao ya kijamii:

Ponera: ponera_283
Eddy Mc: eddy_mc_sau_state_huru
Christom Staff: staffchristom