Uchambuzi Wa Album: #EASY
Emcee: Scar Mkadinali
Tarehe iliyotoka: 07.01.2022
Nyimbo: 10
Watayarishaji: Ares66, Dre, Afvka, 25HRS
Mtayarishaji Mtendaji: Churchill Mandela(Scar)
Studio: Big Beats Afriq
Nyimbo Nilizozipenda: Tz, Hera, Mountain Mover, Opps, Millions Dollars, Hallo
Kundi la Wakadinali nimeanza kuliskia kama miaka mitatu hivi iliyopita. Wakadinalli ni kundi linaloundwa na ma emcee watatu; Scar, Domani(Munga) na Sewersydaa. Kitu ambacho nilicho penda toka kundi hili ni uamuzi wao wa kuja kama walivyo na kumuachia mskilizaji aamue kama atawakubali au la.
Na kutokana na halaiki ya watu wanavyowafuata basi ni ishara tosha kua Wakadinali ni watu wa watu. Ma emcee hawa kwa pamoja waliachia miradi kadhaa kama kundi kando na miradi yao binafsi kama vile Ndani Ya Cockpit (1 na 2), Victims Of Madness, Exposed (Munga’s Revenge), Jeshi Ya Katutulu pamoja na Wada (Healing Of A Nation). Cha kushangaza ni kuwa kwenye hii miradi yote isipokua Domani na Sewersydaa ambao walikua wametubariki na miradi yao binafsi emcee Scar alitusubirisha kwa mda.
Mapema mwaka huu mitandao ya kijamii ilianza kunongo’na kua Scar anaweza kuangusha mradi wake wa kwanza Januari na matamanio yetu yalikua makubwa. Na kufumba na kufumbua emcee alietupatia #KovuChallenge aliachia album yake ya kwanza #EASY.
Mradi unaanza na Should Be ambao Scar ametumia sampuli wa wimbo Champion toka gwiji wa mziki wa Reggae Dancehall Buju Banton. Mradi huu ambao una nondo zenye uwezo wa kujenga ghorofa kitaa unamkuta emcee huyu kwenye nyimbo mbili akiimba kuhusu mahusiano na bata zikiwemo TZ akiwa na Dyana Cods pamoja na Hera akiwa na Apesa (singo ya pili ya mradi) ambapo ni nyimbo pekee alipofanya kazi na wasanii wengine tofauti na Haloo akiwa na genge lake la Wakadinali.
OPPs ambao umeandaliwa na Afvka ndio singo ya kwanza toka kwa mradi huu na ni wimbo wa majigambo mwanzo mwisho unaomkuta emcee huyu akichana ili tuone ubaya wake kwenye kinasa na mistari kama,
“None of these rappers know rap/
All the rappers with the sing along bars/
When I’m talking better shut your damn mouth/
Mother**er you’re so lucky you even chill around us/”
Millions Dollars ni wimbo chanya unaokupa hamasa kuhusu maisha ya utafutaji hata kama hauna senti moja mfukoni. Kwenye mdundo flani unaopiga zeze taratibu Scar anakuuzia matumaini kwenye ngoma ya beti moja tu ila changamoto niliyoiona ni uhamaji wa mada. Wimbo mwingine unaobeba mada hii ya kukutia moyo ni Mountain Mover unaokuaminisha kuwa imani yako ina uwezo wa kuhamisha mlima.
Wimbo wa mwisho kwenye mradi huu Hallo unawakutanisha ma emcee wote wa kundi la Wakadinali. Juu ya mdundo mzuka sana wa boombap kila mmoja anaonesha unyama wake akitaka kung’ara juu ya ngoma hii.
#EASY ni mradi mzuri ila binafsi naona kama kuna kitu kimepelea kwani mara kadhaa emcee huyu alitoka nje ya mada na kuna maneno ameyarudia kwenye mashairi yake. Ila ni uhakika Scar karusha jiwe lake la kwanza akiwa peke yake na lazima likikupata litakuacha na kovu.
Mfuate Scar Mkanidali kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii;
Facebook: Scar Mkadinali
Instagram: scar_mkadinali
Twitter: scar_mkadinali