Moja ya baraka kubwa tuliyopata wapenzi wa Hip Hop mwaka huu 2021 ni kuwepo kwa matamasha mengi ya Hip Hop tofauti na miaka ya nyuma. Matamasha haya yamefanyika maeneo tofauti tofauti Africa Mashariki.

Moja ya matamasha haya lilifanyika nchini Kenya na tofauti yake na matamasha mengine ni kuwa tamasha hili lilihusisha wasanii toka nchi mbili tofauti; Kenya na Tanzania. Tamasha hili lilifanyika kule Nairobi, Kenya mwezi wa July, 2021.

Tamasha hili ambalo lilikwenda rasmi kwa jina SEKeTa lilikuwa na wawakilishi 6 toka kwa nchi hizi mbili. Tanzania iliwakilishwa na Jadah MaKaNTa(Mbeya,Tz), Blackwin(Bagamoyo, Tz), Dambwe La Hip Hop (Dar Es Salaam, Tz), Vitali Maembe(Bagamoyo, Tz) pamoja na Nash Mc(Dar Es Salaam, Tz).

Kutoka kwa upande wa Kenya waliohudhuria ni Ach13ng’(Nairobi, Ke), Githuku(Nairobi, Ke), Monaja(Meru, Ke), Nile Dawta(Nairobi, Ke) pamoja na Dorphan(Meru, Ke).

Leo hii tumepata fursa ya kukutana na kufanya mahojiano na Monaja ambaye kando na kuwa mmoja wa wasanii waalikwa alihusika pakubwa kuhakikisha tamasha hili linafanikishwa. Karibu ujifunze ili uweze kuelewa SEKeTa ni nini na wana malengo gani.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Monaja.

Shukran sana kaka na pongezi kwa kazi yako Micshariki Africa manake Hip Hop ni kama sauti ya vijana ambayo sio rasmi. Hip Hop ya underground ni sauti ya vijana inayoongelea shida zetu tunazokabiliana nazo kila siku maishani. Hip Hop ndio the unofficial yet most genuine sound of the youth.

Kwa mda huu ungekuwa unafanya kazi kutafuta hela ila umeamua kuangazia maswala ya underground Hip Hop kwa hiyo hapo naona kinachokuskuma ni ari wala sio maswala ya hela japokua hela ni muhimu. Wasanii wa Hip Hop na underground wana wigo mpana wa mada tofauti kando na zile zinazopata nafasi kubwa mainstream kama vile mapenzi. Kwa hiyo underground Hip Hop ndio sauti ya vijana, kwa hiyo pongezi kwa kazi yako, kongole!

Tuanze kwa kukufahamu kaka. Majina yako rasmi ni nani na unahusika vipi na SeKeTa?

Mimi ni Monaja, ni msanii na muimbaji na nilianza kuimba 2003 na nilikuwa na freestyle sana na kisha kuanza kuandika mziki wangu. Majina yangu rasmi ni Mwongela Kamenchu.

Pia mimi ni mwana historia na kuna mda ambao nilikuwa ni mhadhiri chuo kikuu cha Machakos, Kenya ila niliwacha kazi hii Na kurudia  kuwa mwana mziki. Kando na mziki, mimi pia hujishughulisha na harakati za kuboresha maisha ya watu, ukombozi japokua pia mimi nahitaji ukombozi huo huo, nisingependa kujifanya kuwa mimi ni masihi, mimi si masihi.

Mimi ndio mwanzilishi wa SEKeTa.

Tueleze kidogo kuhusu historia ya SEKeTa.

Origin ya SeKeTa ni hii; Kenya na Tanzania tumekua na uhusiano mkubwa ki mziki, ki historia, ki harakati na kadhalika. Wakimbizi wa kisiasa toka nchi zote mbili wamepata hifadhi kwenye nchi hizi na pia kuna ushirikiano mkubwa kati ya nchi hizi mbili.

Kwa nafsi yangu nimekuwa nikifuatilia mziki wa Tanzania toka mwaka wa 2000 wakati kulikua na Professor J, East Coast team, Afande Sele, Jay Moe nk. na nimependa mziki wenu(sio wenu, wewe ni mkenya! Akicheka). Japo kua huku tunazungumza Kiswahili cha sheng (Nairobi), Tanzania Kiswahili ni sanifu kiasi ukilinganisha na Kiswahili chetu(Nairobi). Pia nimekua nikijishughulisha na harakati ambazo zimeniwezesha kufanya kazi na kikundi toka Dar, Tanzania, JuLaWaTa(Jukaa La Wajamaa Tanzania) na ni marafiki zangu na walinialika show Sinza, Tanzania ambapo nilikutana na Nash Mc kwa mara ya kwanza ana kwa ana na kununua albam yake.

Pia nimeweza kushirikiana na kundi la Hip Hop Tanzania, Dambwe La Hip Hop na tuliweza kurekodi wimbo pamoja.Kutoka 2009 tulinyamaza ila mawasiliano yaliendelea mitandaoni.

Sasa naweza kusema chimbuko la SeKeTa lilianza rasmi toka kwenye group moja la WhatsApp ambalo Nash Mc yumo. Nash alitoa wazo la kufufua ushirikiano ambao ulikua miaka ya nyuma kama ilivyo kua kati ya Kalamashaka na Watengwa (kwenye wimbo wa Mangirima).

Hili wazo nililichukua na kuanza kulifanyia kazi na ndipo nikapata wazo SEKeTa-Sanaa Endelevu Kenya Tanzania kwani ukiona mziki ninaofanya, mziki anaofanya Nash Mc au hata Dambwe La Hip Hop, ni mziki ambao mada huwa nzito. Hapa namaanisha ni mziki unaoongelea maswala  ya jamii, siasa,dhulma na hivyo basi nikaona ni muhimu sana kwa sisi kushirikiana kwani siasa hata kwenye siasi zetu tunahitaji sauti za vijana ambazo sio rasmi hata kama sisi si wabunge.

Je SEKeTa mna wafadhili au mnaendeshaje shughuli zenu?

Ndio wafadhili tunao – Rosa Luxenburg Stifung walitusaidia na kuchangia kufanikisha usafiri wa wenzetu toka Tanzania ila tunanuia kujitegemea kwani ukijitegemea unakuwa na agenda zako ila sio kusema hatuna agenda zetu kwa sasa ila tunanuia kujitegemea.

Pia Kenya tunashirikiana na Ukombozi Library na nakukaribisha Kenya, nikuoneshe vitabu vya historia ya Kenya tofauti tofauti. Ukiwa Nairobi nichapie(nipigie). Maktaba ya Ukombozi ilitusaidia pakubwa kufanikisha hafla ya kwanza ya SEKeTa.

Malengo ya SEKeTa ni yapi na mnanuia kupata nini toka kwa shughuli za SEKeta?

Matarajio ya SEKeTa ni kulitumia jukwaa hili kuboresha maisha ya watu kwa kutumia vipaji vyetu na kuleta waafrika pamoja haswa Kenya na Tanzania kwa sasa. Tuna malengo matano ambayo tunaazimia kuyatekeleza mojawapo ni kupingana vita dhidi ya dhulma kwa kutumia mziki.

Pia sote tumeaminia Umajumui (Pan Africanism).

Je tamasha la SEKeTa ndio lilikua la kwanza?

Sisi ni vuguvugu changa na tumeanza rasmi mwaka huu. Kwa hiyo kongamano hili ndio lilikua la kwanza la SEkeTa na tulipata fursa ya kuzungumza na kubadilishana mawazo

Wahusika wakuu wa SEKeTa walipatikana vipi hadi wakahudhuria tamasha hili? Walichaguliwa kwa vigezo vipi?

Tuliweza kuchagua wasanii watakaohudhuria kongamano hili kwa kupitia network zetu; kuna wasanii wa Kenya ambao walishafanya kazi na wenzetu wa Tanzania hivyo ilikua ni rahisi kuwapata.

Pia tuliangalia aina ya mziki waliokuwa wanaufanya. Kwa mfano msanii kama Nash Mc (Tz) anafanya mziki wa watu, msanii kama Vitali(Maembe) (Tz), msanii huku Kenya kama Dorphan, msanii kama Githuku(Kenya) pamoja na Dambwe La Hip Hop(Tz), kwa hiyo content ya mziki wao ni muhimu sana.

Pia watu wangu wa Kenya walitoa mapendekezo yao kuhusu nani aalikwe. Dambwe La Hip Hop kwa mfano Hamboni, Tanga(TZ) pia walialikwa kutokana na wao kujituma kwenye harakati zao kwa kutumia mziki kuangazia dhulma katika jamii na nchi yao.

Asante sana kaka Monaja kwa na karibu tena Micshariki Africa

Shukran sana Micshariki Africa.

Je SEKeTa pia ina nia ya kualika wasanii toka nchi zingine zinazo unda jumuiya ya Africa Mashariki kando na Kenya na Tanzania kama wana mawazo sawia na nyie?

Swala hili pia tulilijadili katika kongamano hili ila tuliona tuanze na nyumbani kwanza yani Kenya na Tanzania kisha tunaweza ku expand polepole.

Kisha kwenye SEKeTa ya mwaka huu naona mlikua na tamasha pale Kenya National Theatre, lengo la tamasha hili lilikua nini, walengwa walikua akina nani na ujumbe ulikua upi?

Kile kilichofanyika Nairobi ni hiki, siku mbili tulikaa na kufanya maongezi kuhusu maswala flani kama vile changamoto wanazopitia wasanii marufuku hupitia pamoja na kuongelea swala la tofauti kati ya mziki wa kikombozi na kiharakati.

Siku ya tatu ya kongamano hili tuliweza kufanya performance ilhali siku ya nne tulifanikiwa ku record nyimbo ambazo tutaziachia.

Kwa nini kulikuwa na performance? Wajua wasanii kama hawa wakiungana wenye jumbe nzito toka Kenya na Tanzania pia huongeza thamani kwenye mziki wao.

Pia tangazo lilipotoka kuhusu tamasha hili ambalo lilionesha kua show hii itakuwa na wasanii toka Kenya na Tanzania watu kibao walijitokeza hadi kujaza ukumbi.

Nia ya show hii pale KNT ilikuwa kuhimiza, kuwezesha na kuwasha cheche flani katika akili za watu na kuwaambia kwamba ni muhimu watu kuendelea ku support sanaa endelevu kando na kushabikia kwa mfano nyimbo za mapenzi tu.

Waliokuwa wamehudhuria tamasha hili walikua akina nani? SEKeTa mmepania kuipanua vipi toka hapa?

Katika SEKeTa ya mwaka huu kulikuwa na wasanii 12 jumla; 6 kutoka Kenya na 6 kutoka Tanzania. Kando na hawa kulikua na delegates ambao walikua wadogo wetu waliokua wanafuata nyayo zetu na kwani hawakua na uzoefu sana kutuliko na walipata fursa ya kujifunza toka kwetu na kuwatia moyo kuwa nao pia waanzishe harakati chanya kama hizi makwao na kujiunga na harakati kama hizi.

Jinsi ya kupanua SEKeTa ni kuwaalika wadogo zetu ambao wapo chini ya miaka ishirini pamoja na wakongwe ambao wana ujuzi tofauti.

Pia tuliamua ku balance usawa wa jinsia kuhakikisha ma dada zetu wasisahaulike.

Je mwakani mna mpango wa kuwa na tamasha hili la SEKeTa na litafanyika wapi? Je SEKeTa ina mpango wa kukutana kila mwaka, mna malengo yepi yatakayo wasaidia kukuza harakati hii?

Ndio kutakuwa na SEKeTa mwaka kesho tena na tumepania kulifanyia Tanzania na wenzetu pia kule nao watawaalika wadogo wao kuhudhuria tamasha hili pia. Pia tumeona ni vyema kuwa kando na kusubiria tamasha hili wasanii hawa wanapaswa wakutane mara kwa mara kabla ya kongamano kwani SEKeTa ni maishi, sio tamasha tu.

Wasanii marufuku uliowataja hapo juu ni akina nani?

Hawa ni wale wasanii ambao media hazichezi nyimbo zao hivyo basi hutafuta njia mbadala ili waweze kuskika na ku survive kwani media zinamilikiwa na watu ambao hawapendi kuangazia na kuongelea mambo mengine.

Ndugu zangu toka Tanzania husema kuwa kuna wasanii maarufu (mainstream) na marufuku (prohibited). Hii haimaanishi kuwa wasanii maarufu ni watu wa baya la ila ni kusema hawa wasanii marufuku huongelea mada nzito nzito tofauti na mapenzi kama vile dhulma ambazo media za kawaida(mainstream) hawapendi kuzicheza kwenye radio au tv.

Jee kuna steering committee ya SEKeTa?

Hatuna kamati na mimi sio mwenyeketi lakini wasanii wote wana sauti toka SEKeTa. Mimi nilichofanya ni kuandaa ratiba ambayo niliyoipendekeza kwao ila kiukweli ni kwamba kwa asilimia kubwa mimi ndiye nilifanikisha maswala ya malazi kando na kuongoza shughuli yote.

Ila mimi sio kiongozi wa SEKeTa na sitaki kujilimbikizia sifa ilhali sote tulilifanikisha hili.

Ni changamoto gani mlizozipata kwenye kongamano hili la SEKeTa?

Changamoto zilikuwepo kibao. Kwa sasa tupo ndani ya janga la Uviko 19 hivyo basi ilikua ni muhimu kuvaa barakoa pamoja na kuhakikisha social distancing imezingatiwa wakati wa kongamano hili.

Pia nilichoka sana kwani nilikuwa coordinator na kwa vile ulikua ni mradi wetu wa kwanza kuna vitu sikuwa nimekadiria kama expenses ambazo sikudhani nitalipa kama vile gharama za upimaji wa Uviko kwenye mipaka yetu ilahli kwa kawaida kama gonjwa hili lisingekuwepo wageni wetu wangepita bila ya kupimwa.

Pia uchovu wa kuandaa na kuhakikisha tamasha hili linafanikiwa.

 Watu wakitaka kujiunga na SEKeTa wafanyeje? Mnapatikana wapi? Je mpo kwenye kwenye mitandao ya kijamii? Watu wanajiungaje? Je kuna membership fee?

Kwa sasa tunapatikana Instagram account kama SEKeTa East Africa japokua tuna mpango wa kuwa na channel YouTube itakayoweka video za matamasha yetu.

Kuhusu kujiunga na SEKeTa vigezo ni simple tu; lazima mziki wako uwe unazungumzia maswala ya kijamii na usiwe mziki wa kudhalilisha wanawake au utani sana. Lazma uwe na jumbe nzuri na kuongelea changamoto hai za kijamii.

Kupata taarifa zaidi kuhusu SEKeTa fuata tovuti hizi;

Instagram: seketaeastafrica

Pia mpate Monaja hapa:
Facebook: Monaja
Instagram: Monajamwenyewe