Sela Ninja

Inapokuja kwa utamaduni wa Hip Hop wa bongo moja wa ma emcee/watayarishaji anae kuja kwa kasi ni Sela Ninja. Sela anaepatikana kule Kingamboni Dar ni moja ya watu wanaojituma sana kwenye kazi zake na inakua hivi kwani kabarikiwa na karama mbili sana kwenye utamaduni huu wa Hip Hop; kughani na utayarishaji.

Japokua kijana bado ni mdogo utendaji kazi wake ni wa ki utu uzima kwani hadi sana ana album tatu na beat tapes kama tano kando na kuhesabu miradi kibao aliopiga na jamaa kutoka sehemu tofauti duniani.

Sela Ninja leo tupo nae ana kwa ana ili tupate madini toka kwake.

Karibuni.

Karibu sana kaka Sela Ninja Micshariki Africa jukwaa la Hip Hop. Hongera kwanza kwa hatua ya kimaisha uliochukua hivi karibuni. Unajiskiaje sasa kua vikao vya wazee vikiitwa mtaani kwenu wewe pia lazima uhudhurie?

Shukrani sana brother. Binafsi nafurahia kuwa karibu na wazee sababu bado kuna vingi vya kujifunza kutoka kwao. Kama kuchota busara na hekima.

Tuanze kwa kukufahamu kaka Sela Ninja. Majina yako rasmi ni nani, unapatikana pande zipi za Africa Mashariki yetu hii?

Jina Kamili ni Christopher Robert Kasela. Napatikana Kigamboni Dar Es Salaam Tanzania mashariki mwa bara la Africa.

Tueleze kuhusu historia yako kidogo; wewe ni mtu wa wapi, ulizaliwa wapi, ulisomea wapi na ulifikia wapi kimasomo? Je nyie mlikua wangapi kwa  familia yenu?

Kabila langu Ni Mngoni, nilizaliwa Chimala Mission Hospital. Elimu ya msingi nilipata shule ya Kibaoni Primary School (mkoani Kilimanjaro), kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu, kisha nikahamia Kigamboni Primary School (Dar es Salaam) kumalizia elimu ya msingi. Baada ya hapo nilijiunga na Navy Secondary School, shule ya jeshi kwa elimu ya O Level. Baada ya hapo nilikwenda Mbeya Igawilo High School.

Familia yetu tulizaliwa watatu na wote ni wanaume; kaka yangu Jospeh na mdogo wangu Kennedy.

Tueleze kuhusu muziki wako, hivi ulianzaje sio kuchana na pia kutayarisha kazi zako na za wana? Jina lako la kazi Sela Ninja lilikujaje na linamaana gani?

Nikiwa darasa la tatu Kibaoni Primary School kuna brother anaitwa Allas Glad (ALLY) ambaye baada ya kuona madaftari yenye nyimbo zangu alinifunza kuhusu vina na huo ndo ulikuwa mwanzo wa mimi kufanya muziki japo haikuwa rahisi hususani upande wa familia.

Nilijikuta nina mapenzi na kuchana toka kipindi naanza na hii lilitokana na mzee wangu alikuwa na package kubwa sana ya muziki kama Reggae, Afropop, Zilizopendwa etc. Kipindi hicho ilikuwa ni tape (cassette), kabla ya CD. Watu kama Professor Jay, HBC Sugu, etc nilikuwa nasikiliza album nzima na sio track moja. Hii ilichochea kuingia kwenye muziki ambapo kipindi hicho ndugu zangu wengine nao pia walionekana kupokelewa vizuri kwenye game (Jhiko Man/Squeezer na Dataz) ilinifanya kupenda zaidi muziki ambao nilianza kufanya kabla ya music production/kua producer.

Kwa upande wa production ilisababishwa na ugumu wa kulipia recording session especially kipindi bado nasoma so ikapelekea niweke nguvu kwenye kujifunza kutengeneza muziki kupitia watayarishaji mbali mbali wakati huo. Momba / Den Texaz / Robi Songea etc ni moja ya watu walionisaidia ku master baadhi ya vitu kwenye suala la utayarishaji wa muziki.

Kwa upande wa kuchana brother Jhikoman pamoja na Squeezer wame play part kubwa sana kunifikisha hapa nilipo ikiwa pamoja na ku perform kwa live band pamoja na mambo mengine mengi yanayohusu muziki.

Jina La Sela limetokana na jina la babu yangu Kasela kwa hiyo nikaibadilisha kwani yule Kasela kadogo sasa amekua kwa hiyo ni Sela kuwakilisha Kasela. Waswahili au wajuzi wa lugha huwa wanaita kutohoa.

Mpaka sasa una miradi mingapi kama mchanaji, inaitwaje na imetoka jini?

Hadi sasa kuna miradi mi tatu upande wa uchanaji;

1) Maisha Ya Kibongo EP, imetayarishwa na June Kid kutoka Russia (5 Tracks) 2017
2) Street King EP, imetayarishwa na Veeja Muziki kutoka Belgium (5 Tracks) 2021
3) Maelekezo The Mixtape (25 Tracks) 2022

Pia nina beat tapes 5 kwa upande wa utayarishaji;

 1. Street Blessings The Beat Tape – 2016
 2. Black Is Beautiful The Beat Tape - 2021
 3. Tutu Bee The Beat Tape - 2021
 4. Chiulu The Beat Tape - 2021
 5. Kigambonian The Beat Tape – 2022

Je kama mtayarishaji umeshapiga kazi na wasanii gani na kwenye miradi gani?

Kama Mtayarishaji nimefanya kazi na wasanii tofauti kama Jos Mtambo 🇹🇿 / Black Wa Uswazi 🇹🇿 / Jawnraw 🇨🇦 / Prestigious 🇺🇸 / Defi Ant 🇺🇸 / Jaykah Mtengwa 🇰🇪 / Jombaa Unculy 🇰🇪/ Nem R 🇰🇪/ Soulsaga 🇸🇪/ Proficient 🇺🇸/ Subtex 🇺🇸/ Katanga Jr 🇦🇺/ Pupi Jing 🇨🇳 / Hiwazu 🇮🇹/ na kadhalika

Hivi unapolingalisha ubunifu na mchakato mzima wa emcee kuandika na kuchana mistari yake na mtayarishaji anavyochukua mawazo ya msanii na kuyafanyia kazi hadi ikawa wimbo nani ana shughuli nzito?

Zote ni shughuli nzito kuandaa wazo, kutengeneza santuri pia urahisi wake ni pale unapofanya kazi na wasanii wataalam inafanya hata production kuwa rahisi same as idea creation pia kama msanii kukutana na producer mkali inaleta urahisi wa kazi.

Je kuna advantage yoyote unayo ipata inpokuja kwa utayarishaji wako unaoletwa na wewe kua emcee pia? Na je wewe inapokuja kwa talanta hizi mbili ni ipi unaipenda sana na ni ipi unaona upo vizuri zaidi?

Ndio kuna advantage na ni nyingi zaidi ya disadvantages lakini kubwa zaidi ni kuepuka usumbufu wa foleni za studio au kazi kucheleweshwa imepungua kwa kiasi ki kubwa.

Kwenye suala la kupenda talanta ipi naweza kusema kuchana ndo ilifanya nianze music production so kwangu kuchana is everything then midundo inafata.

Mchakato wako wakufanya kazi na wasanii ni upi toka mteja aje kwako na wazo hadi kufanikisha wimbo?

Mchakato wa kufanya kazi na Sela Ninja mara nyingi unategemea mahitaji ya mteja mara baada ya makubaliano ya kazi husika. Whether kutumiwa beat ama kuja physically kutengeneza tukiwa wote kutoka mwanzo.

Sela Ninja unamiliki studio yako mwenyewe na studio unayopiga kazi zako inapatikana wapi?

Sela Ninja kwa sasa bado hana studio binafsi kitu kinachopelekea ku book session kwenye studio za watu wengine kwa ajili ya kufanya kazi.

Nimeona umepiga kazi na ma emcee pamoja na watayarishaji kadhaa kutoka nchi tofauti tofauti duniani. Hili umelifanikisha vipi?

Hii linachagizwa na mimi kupenda ku chimba hasa kuhusu misingi kwa kufatilia muziki especially wa Hip Hop/ Rap lakini kwa asilimia kubwa collaboration zilitokana na response baada ya wasanii husika kuona au kusikia nyimbo zangu so story zinaanziaga hapo hususani kwa wale walioonyesha kuwa interested na kazi zangu.

Ni nani anaku inspire kama emcee na pia kama producer duniani?

Inapokuja kwa uchanaji

 1. Biggie Smalls (B.I.G)
 2. Guru Gangstarr
 3. Masta Ace
 4. Sean Price
 5. Eddo G

Kwa upande wa utayarishaji

 1. DJ Premier (Preemo)
 2. Pete Rock
 3. Nottz
 4. Alchemist
 5. Dr Dre

Swali gumu sana hili brother sababu list ni ndefu mno naomba nikupe watano watano.

Hivi wewe na Jos Mtambo ni mtu na mkubwa wake maana kwanza mmefanana alafu pia mmepiga kazi nzuri pamoja?

Mimi na Jos Mtambo ni washkaji tu sio ndugu wa biological. Ni brother kutokea hood moja Kigamboni lakini ukaribu wetu unachagizwa na kila mmoja kumkubali sana mwenzake kimuziki. Namshkuru Mungu kwa kumleta kaka huyu kwenye jamii ya Hip Hop kwani jamaa amebarikiwa na kipaji kabisa mwenye talanta, upnedo na ushirikiano wa kutosha.

Hii sanaa inakulipa hasahasa vile umevaa kofia mbili?

Kusema kweli sanaa bado haijaleta vingi lakini thanks God sikosi chochote kitu waswahili wanasema hamna hamna anajua mwenye shamba.

Ni nini kinakutofautisha wewe Sela Ninja na mtayarishaji pamoja na emcee yoyote yule?

Tofauti ya Sela Ninja na wasanii pamoja na ma producer wengine ni uniqueness. Kila msanii ana kitu cha peke yake ukiachana na wale wanaoigana. Kwahiyo Sela Ninja ana touch zake upande wa midundo lakini pia ana style yake upande wa kurap tofauti kabisa ma wasanii wengine hususani kwenye tasnia ya michano (rap).

Ongea kuhusu ile jingle yako ya kukutambulisha ambayo kuna kisauti cha kitoto kinataja jina lako "Sela Ninja", hii ilikujaje?

Zipo mbili tofauti; moja ni sauti ya mtoto wa kiume Joshua Joseph Kasela ambaye ni mtoto wa bro kisha nyingine ni ya mtoto wa kike Olivia Christopher Kasela ambaye ni mtoto wangu ila zote zinatamkwa sawa (unatakiwa kuwa na skio la mtayarishaji).

Wewe ni mmoja wa watumiaji wazuri wa hizi Digital Streaming Platforms kando na kuuza miradi yako kwa mtu mmoja mmoja. Ni manufaa gani umepata tangu uanze kuweka kazi zako kule maana wasanii wengine hulalamika kua hawavuni wanacho kipanda kule?

Kama nilivyosema hapo awali tunafeli sababu mtu anataka akiweka nyimbo kule ashindane mauzo na Jay Z ambapo ni ngumu. Kwangu mimi bado sijapata pesa nyingi huko lakini sikosi chochote kitu.

Hapa unaweza kusema mchawi promotion hata digital platform needs promotion.

Tutarajie nini kutoka kwako hivi karibuni?

Chakutarajia ni mfululizo wa albums ambazo zipo tayari kwa release, kinacho subiriwa ni wakati sahihi. Lakini pia tutarudisha tena biashara ya Kulture pamoja na T-shirt brand ya Sela Ninja hivi karibuni.

Nini cha mwisho ungependa kutuambia ambacho sijakuuuliza?

Mwisho kabisa mradi wangu mpya (Maelekezo The Mixtape) wenye jumla ya nyimbo 25 unapatikana kwa mchango wa Tsh 10,000/= tu.

Unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii?

Twitter: @ogselaninja
Facebook: Babu la Mababu (Sela Ninja)
Instagram: selaninjaofficial