Uchambuzi Wa Albam: X-Files
Msanii: Shahidi XCalibur
Tarehe iliyotoka: 24.04.2021
Nyimbo: 11
Muunda Midundo/Producer: Musyoka (Musyoks)
Mchanganya Sauti na Midundo: Musyoka(Musyoks)
Studio: Decimal Records
Shahidi XCalibur alianza kuskika kwangu kama mtu aliyebobea kwa mambo ya freestyles battles nchini Kenya. Kwa mtu yoyote ambaye ni shabiki wa Hip Hop ya handaki ya Kenya nadhani Shahidi hatakuwa mgeni kwani shahidi ameshawaangusha wapinzani kibao aliokua akishindana nao kwenye mashindano haya ikiwepo kushinda tuzo ya mitindo huru ya Nokia Don’t Break The Beat mnamo 2012. Mwaka huu emcee huyu aliamua kuingia booth ili kuweza kutupatia mradi wake X-Files ambao mimi binafsi nilipoona mradi ukinadiwa nilimtafuta ili niweze kujinyakulia mradi huu.
X-Files ambao umeundwa kwa asilimia 100 na mkongwe wa Hip Hop na emcee wa zamani wa kundi la Nanoma Musyoka aka Musykos anayepatikana studio zake za Decimal Records pale Nairobi unaanza na utangulizi Intro ambayo inakupatia kipande cha audio toka kwa moja ya battles zake kama mojawapo ya njia ya kukumbushia chimbuko lake endapo utakuwa humjui au pengine umemsahau.
Mradi huu ambao umeundwa ki boombap mwanzo mwisho umeamua kukuletea vitu classified au vya kipekee. Wimbo wa kwanza unaotufungulia mradi ni Keep Going On Part 1 akiwa na Kipsanif ambao anatia moyo mtu yoyote ambaye anaanza kwenye hii fani ya kughani akisema kua we piga kazi tu hata kama watajitokeza wale ambao hawaamini unachofanya. Pia anakumbushia changamoto zilizojitokeza wakati wakianza na hizi harakati za Hip Hop na mafanikio pamoja na mashabiki waliomtia moyo akisema,
“The other day tuki host shows za Hip Hop Thursdays/
Only 20 fans man si hii rap game ni rat race/
Haters wana sell lies na mziki hawa purchase/
Go getters wana get by despite hiyo nonsense/
Hiyo ni past tense tume upgrade/
Blueprint done and dusted/
No quitting no stopping hadi real Hip Hop iwe anthem/
Mi si king wa anything but thanks for royalty/
Treatment na fans wote wameni show loyalty/…”
Kwenye Keep Going On Part 2 akiwa na Monique kwenye kiitikio japokua mada ni ile ile ya kututia moyo na kutuinua, emcee Shahidi anagusia changamoto za watu wa kawaida zikiwemo za akina dada zetu. Mdundo wa Keep Going On Part 2 unagonga vizuri vinanda, violins vizuri sana ukibarikiwa vizuri sana na sauti nyororo ya dada Monique kwenye kiitikio. Shahidi nae anatendea haki wimbo huu akitema mashairi akinyosha mkono wa umoja kwa akina dada akisema,
“Hii ni special dedication kwa every lady heartbroken/
Eyes swollen, future bleak but a daily lies broken na hussy/
Body weary, future scary life torment/
Marriage vows zime turn to some bad omens/
Move on sister lenga dialect ya dead poets/
Ka ni thorns pekee una feel kwa bed ya dead roses/
Una deserve better than cocktail ya sour grapes/
Better than hate lies na bottled pain/
Live your life love yourself/
Hawa mafala waseti kwa shelf/
We ni queen your highness kwa pedestal wanafaa kukuset/
Hizo zingine hapana skiza uchungu ibada hepa misa/
Wee ni jewel mwana wa Hawa look inside utapata power/”
Kando na wimbo huu nyimbo nyingine nilizozipenda ni kama Addicted ambao ni wimbo wa mahusiano, Where Am From akiwa na Kalimani Tha Mc ambao unahimiza kutosahau tunapotoka hata baada ya kupata mafanikio, Auski akiwa na Toshi Nanoma ambapo wawili hawa wanajigamba kuhusu uwezo wa kuchana, Live Life ambao wimbo wa shukrani kwa zawadi ya uhai na Victory akiwa na Ojiji ambao ni wimbo wa kutia moyo kuwa ushindi upo karibu kama hutokata tamaa, wimbo huu umekua on rotation kwangu sana.
Mradi upo vizuri, mashairi yamepangwa yakapangika ilhali Musyoka ameonesha kwa nini emcee huyu aliamua kumpa chaka Musyoka na kusema kweli emcee huyu ambaye kawa producer kaonesha umahiri wake. Pata nakala yako ya X-Files upate vitu adimu.
Kupata nakala yako wasiliana na Shahidi XCalibur kupitia;
Facebook: Shahidi Matigari XCalibur
Instagram: shahidixcalibur