Shazzy B

Damaris Yilva (amezaliwa Oktoba 1998) umri wa miaka 24, anayejulikana zaidi kwa jina lake la kisanii Shazzy B. Ni mwanamuziki, mwimbaji, mtunzi wa nyimbo na rapa. Jina lake Shazzy B lilikuwa ni jina la utani alilopewa hapo nyuma na rafiki yake. Alianza kwa kuitwa Shaz na baadaye Shazzy B.

Alianza kazi yake ya muziki mwaka wa 2018 akiwa na kikundi kinachoitwa Ngonglywood Production ambacho kiko Ngong, na waliachia wimbo wao wa kwanza unaoitwa '111 My Home Town' na kisha baadaye alitoa wimbo wake wa kwanza akiwa peke yake uitwao 'Usichoke' mwaka 2019. Tangu wakati huo ameshiriki zaidi katika miradi ya 'The Mic Gym', 'Icon Radio Vault Cypher', 'Door Knockers Cyphers' na 'The All African Cypher'.

Kwa miaka mingi amefanya kazi kwenye nyimbo kama vile 'Follow The Leader' na 'Love The Way You Wine'. Kwa sasa anafanyia kazi yake ya kwanza, EP ambayo ina wimbo uliotoka hivi majuzi, 'Swagger’, wimbo wake mpya uliotoka ambao amemshirikisha Nevo. Pia amewashirikisha  wachanaji wengine kama Trabolee, Brimarainman, Msito kwenye Ep yake inayokuja hivi karibuni pamoja na kuachia single kadhaa, kabla ya EP yake kukamilika. Ana miradi zaidi njiani.

Karibu Micshariki Africa dada. Jina lako la kisanii, Shazzy B lilikujaje na lina maana gani?

Doh, huwa naulizwa hili swali sana. Lilikuwa jina la utani ambalo nililipata siku za nyuma. Nadhani nilikuwa shule ya upili wakati watu walikuwa na majina ya kuchekesha kwenye mtandao ya kijamii Facebook. Niliamua kulitumia kama lilivyo.

Safari yako ya muziki imekuwaje, nini kilikufanya uingie kwenye muziki wa kuchana?

Muziki umenisaidia kujifunza mengi na kitu kizuri zaidi ninachojivunia ni ukuaji wangu kama msanii. Si rahisi kuwa katika tasnia ya muziki, haswa kujaribu kupenya (na kuonekana). Nimekumbana na changamoto za kutolipwa shoo, mara nyingine nimefanya jitihada za kuonyesha kipaji changu lakini nilijihisi siko vizuri.

Naamini nisingekuwa na mapenzi na muziki wangu ningeacha zamani. Njia yangu ya kukabiliana na changamoto ni kwa kuchukua hatua kwa wakati. Safari yangu ya muziki ilianza bila kutarajia na ninashkuru kwa hapa nilipofika. Kimsingi sikujua kuwa naweza kurap mpaka siku moja nilipofika studio nikiwa na baadhi ya marafiki zangu nikapewa nafasi ya kuingiza sauti kwenye track na ikawa hivyo...nikawa rapper.

Muziki umekuwa sehemu ya maisha yako kwa muda gani?

Mnamo mwaka wa 2018, nilianza kujihusisha na muziki, lakini baadaye nikaipa shule kipaumbele na ikabidi nipumzike. Baadaye niliendelea kufanya muziki mnamo 2021. Nimekuwa nikishiriki tangu wakati huo na sasa muziki ndio unaofanya maisha yangu kuwa na maana.

Ulitambuaje kwamba muziki ulikuwa njia ya kusonga mbele kwako?

Sote tunapenda kitu ambacho hatuwezi kukosa au kuwa na siku bila kukifanya, kwangu muziki umekuwa jambo kuu! Kwa hivyo siku hizi najikuta naandika tu…Silazimishi chochote, mistari inakuja tu. Nimeikubali hii shughuli kabisa na ninatarajia nizidi kujijenga zaidi ki muziki.

Je, unalenga kuleta mabadiliko kwa njia gani?

Muziki ni chombo chenye nguvu kwa sababu kila mtu anausikiliza. Ninataka kuutumia kama njia ya kujieleza, kuzungumza juu ya mambo yanayohusiana na mambo yanayoathiri maisha yetu. Kadiri ninavyoweza kuwafikia watu na muziki wangu ndivyo nitakavyoweza kuungana nao na kuleta mabadiliko katika maisha yao.

Unalenga nini na huu muziki wako, maono yako ni yepi?

Baada ya kutengeneza vibao kadhaa, natarajia kutengenezea vizazi vyangu urithi, ndicho ninachokilenga. Sio kuhusu hela kwa ajili yangu, ninaibua taswira ya kazi ambapo ninaweza kuunda muziki kwa sababu tofauti na miradi inayoathiri maisha na mitazamo katika jamii yetu.

Je, ni mradi gani unaoupenda kufikia sasa?

Ep yangu inachukua ushindi kwa hili. Nimekuwa nikifanya kazi kwenye cyphers, lakini mwishowe kufanya kazi kwenye mradi wangu mwenyewe ndio kitu bora kuwahi kutokea kwangu.

Ni akina nani walio na ushawishi mkubwa zaidi wa muziki wako haswa hapa Kenya?

Tukianzia kileleni lazima niwataje Kendrick na J Cole lakini hapa Kenya ninavutiwa sana na Nyashinski na Khaligraph Jones, sio kwa sababu wana vibao la,...mimi ni mbunifu na kazi zao zinanigusa sana.

Nini kinakufanya uwe tofauti na wasanii wengine wa rap kwenye tasnia hiyo?

Mimi ni msanii wa kike ambaye ana rap kuhusu mambo ya kweli. Sijaribu kujificha nyuma ya sauti ya kuvutia. Nina mistari mizuri na ninaamini mtindo wangu wa rap ni wa mauaji  japokua nimetulia (akicheka) na ninaifanya ionekane rahisi, kana kwamba sihitaji kuhangaika, ninatiririka tu.

Nani ni shujaa wako mkuu na kwa nini?

Mungu ni shujaa wangu mkuu. Ninaamini mambo mengi ambayo yametokea katika maisha yangu na jinsi nilivyoyapitia nikiwa hai, yasingewezekana kabisa kama ningekuwa nategemea uwezo wa kibinadamu.

Ninaelewa kuwa una EP, inaitwaje, ina ngoma ngapi, ulipataje msukumo wa mradi na umewashirikisha akina nani?

EP inaitwa THE BOSS LADY. Haijakamilika lakini kwa sasa ina nyimbo 9 ambazo moja kati yake nimetoa kama wimbo mmoja unaoitwa Swaga kwenye chaneli yangu ya YouTube. EP imechochewa na mapambano ya maisha, mahusiano, matarajio ya mtindo wa maisha na mengine mengi. Wasanii walioshirikishwa kwenye EP ni pamoja na Nevo, Msito, Brima Maovete na Trabolee.

Mradi unatoka lini?

Ep nzima itakamilika hivi karibuni na tunatumai kuifanya ipatikane kwenye majukwaa yote ya muziki tarehe 30 Desemba.

Je ulijiskiaje uliposhiriki wenye Door Knockers Cyphers 2 na pia All African Cypher 2?

Inashangaza! Nimejifunza mengi na imeniunganisha na wasanii wengi wa wazuri, wa nchini na  pia kimataifa. Ninathamini sana kazi kama ya Muziki Jared wanafanya na ningewahimiza watu kama hao kuendelea kufanya kile wanachofanya, wasanii wengi wazuri wako handakini  lakini na fursa kama vile DKC au All African Cypher inatuwezesha kugundua vipaji vipya.

Je, unapanga kufanikiwa vipi katika soko la Kenya?

Kufanya kazi kwa udhibiti na uzuri kila kukicha (kucheka). Najua kwa hakika nikifanya kazi itanilipa. Ninahitaji tu kuhakikisha kile ninachotoa kina thamani ya juu.

Tutarajie nini kutoka kwa Shazzy B?

Muziki zaidi na zaidi, sababu iliyonifanya niamue kuachia EP yenye nyimbo 9 ni ili nipate msukumo wa kuunda kikundi kingine cha kazi katika mfumo wa albamu. Ninatumai kufanya muziki kwa busara zaidi.

Your Official music/social media platforms?

YouTube:@ShazzyB
Twitter: @ShazzyB
Instagram:bossladyshazzyB
TikTok: bossladyshazzyb
Facebook: Ladyboss Shazzyb

Je, ungependa kuwagotea akina nani?

Marafiki zangu, kaka yangu mdogo, watu wangu wote wa Ngonglywood, mama yangu na mwisho kila mtu huko nje anayeskiliza muziki wangu.

Neno lako la mwisho?

Ninawasihi kila mtu huko nje asiogope kufuata ndoto zake. Yote yatatimia...lazima uwe na msimamo na usiruhusu chochote kiingie kati yako na ndoto zako. Mwisho wanawake, mzidi kujitokeza ili muonekane huku nje.