Msanii: Dizasta Vina
Wimbo: ‘Kanisa’
Album: Jesusta

Mwanzo

Kuna nyimbo za dini halafu kuna wimbo wa Kanisa kutoka kwa Dizasta Vina, Kanisa ni zaidi ya wimbo, huu ni ufunuo wa kifikra katika mambo ya kiimani.

Upekee wa kimaudhui wa wimbo huu ndio ulifanya segment hii ya Nyuma ya Pazia(NyP) kucheki na Dizasta ili kupata mawili matatu kuhusiana na wimbo huo.

Dizasta hebu tueleze namna ulivyopata wazo la kanisa?

Dizasta: Wazo la kanisa nilipata mwaka 2015 nikiwa chuo mwaka wa pili. Na wazo lilikuja baada ya kushawishiwa kushiriki misa ya kanisa fulani na ndugu zangu katika dhehebu tofauti na langu, dhehebu ambalo sikuwa muumini. Ndugu zangu walikuwa wakiniambia kuna ukombozi wa kweli kwenye kanisa lao. Na nilipata picha kubwa juu ya mitazamo ya kiimani tuliyonayo baada ya kushiriki ile misa. Na jambo mojawapo lililonishawishi sana kuanza kufikiria upya kuhusu imani zetu ni baada ya ile misa kushindwa kujibu mafumbo ya maisha yangu. Hii ilinishawishi kuanza kufanya research. Kushiriki misa tofauti, za makanisa tofauti.

Kwenye uandishi wa wimbo ulitumia muda gani? Na uliandika moja kwa moja tu au kwa kadri mawazo yalivyokujia?

Dizasta: Nilitumia muda mfupi kuandika kanisa, kwa kuwa nilitumia muda mrefu kufanya research. Nilikuwa na taarifa zilizoniridhisha kufanya maamuzi ya kuandika wimbo wa “Kanisa”. Sikuandika kwa kadri ya mawazo, bali kwa kadri ya kumbukumbu nilizojiwekea baada ya kukusanya taarifa za research niliyofanya. Sehemu ya wimbo niliandika nikiwa nyumbani na sehemu nikiwa studio.

Imani ni suala nyeti sana. “Kanisa” ni wimbo ambao unagusa imani za watu unalionaje hili?

Dizasta: Kanisa ni simulizi ya kweli. Siwezi kuzuia watu kuwa skeptical kuhusu taarifa za wimbo. Lakini ni ukweli. Kama kuna yeyote ambaye ana shaka na taarifa za mule ni vyema akaanza kufanya uchunguzi binafsi kabla ya kukubaliana na zile hoja. Na kama anaona baadhi ya taratibu za imani yake zinamzuia basi ni ruhusa kuuchukulia wimbo huu kama burudani tu. Naamini sanaa yangu ni ya uhuru wala sio sheria.

Hebu tuambie ushirika na nafasi ya producer wako katika wimbo huu na muda mliotumia kuandaa kazi hii?

Dizasta: Producer wa wimbo ni Ringle Beatz. Sikuwa na shaka na yeye kwa sababu tulikuwa tumeshafanya nyimbo kadhaa na zilikuwa na mafanikio makubwa production-wise. Alikuwa na ideas nyingi za kuongeza kwenye biti ambayo nilipiga hivyo akaamua aondoke na vocals akaweke biti upya ili mood ya wimbo na mood ya biti zilingane kwa asilimia mia. Tulitumia almost 2 hours Kurekodi. Hakukuwa na shida sana kwenye kurekodi kwa kuwa nilikuwa na taarifa nyingi sana. Na tayari nilikuwa nime design aina ya uwasilishaji. Nilichagua kufanya kanisa kama mtu. Yaani naongea naye kama mtu mwenye uhai. Mfano namwambia "Kuwa mkweli, ni wapi uliposhindwa nielewe, hiyo siri yako hauwezi ukaificha milele milele, kama nitachomwa moto wa kukushika ni wewe, nishakusafisha kuliko kujisafisha mwenyewe"

Kwanini haukuona umuhimu wa collabo?

Dizasta: Sikufanya kolabo kwenye huu wimbo kwa sababu naamini imani ni suala binafsi sana na suala nyeti. Si vyema kumshawishi mtu awe na hisia sawa kuhusu suala hili kwa ajili ya wimbo tu. Na isitoshe research nilifanya peke yangu. Hivyo nimeiweka hewani hiyo hoja. Nategemea critics kama wakitokea.  Ndio ushirikiano ninaosubiri.

Kwa kifupi tu, nini hasa ujumbe wa wimbo wa kanisa? 

Dizasta: Ujumbe wa Kanisa ni kwamba, kwanza ni kuchochea social awareness (muamko wa kijamii) kwamba si kila tunachofundishwa kina lengo la kutukomboa, baadhi vina lengo la kutufanya tuwe tegemezi kwa imani zetu na kupitia utegemezi huu, taasisi za kidini zinatimiza matakwa binafsi. Na pia kurudi kwenye mlengo mkuu wa haja ya kanisa. Na sio viongozi wa dini zetu ambao wanatakiwa kujibu mafumbo ya maisha yetu wanatumia njia hii kutimiza haja zao binafsi au za taasisi zao tofauti na lengo kuu.

Baada ya kuiachia kazi hii, vipi yalikuwa mapokeo yake? 

Dizasta: Mapokeo yalikuwa kama nilivyotegemea kifani na kimaudhui. Kwenye upande wa fani, watu wote regardless imani zao wamependa muundo na mtindo wa uwasilishaji, matumizi ya lugha na ushairi wenyewe. Mazingira ya theme ya wimbo na hisia ya wimbo wenyewe. Ni watu wachache sana walikuwa na shaka na wimbo kwenye upande wa fani. 

Ila upande wa maudhui nilipata shida kidogo. Mfano siku ya kwanza narekodi producer alikuwa ananiuliza if I'm very sure kuhusu kufanya wimbo ule. Alisema ni hoja sensitive sana zinaweza kunisababishia matatizo. Pia kuna msanii mwenzangu yeye alikuwa na wazo tofauti. Yeye alisema wimbo wangu sio mzuri kibiashara. Watu wanapenda mada zinazohusu starehe na mapambano ya maisha zaidi kuliko mada za aina hii. 

Nakumbuka siku ya kwanza kutangaza cover ya wimbo nilipata critics kuhusu jina la wimbo kuwa linatenga waumini wa dini nyingine. Kwa jamii iliyonizunguka wengi walionekana kupata mwanga wa kinachoendelea na baadhi yao wakifikia conclusion kuwa hawatashiriki misa tena (jambo ambalo napinga. Sidhani kama ni vyema kuamua haraka bila kujiridhisha mwenyewe).

Napenda kufahamu pia, malengo yako ya kufanya wimbo huu na malengo hayo yamefikiwa kwa kiasi gani?

Dizasta: Kwa kiasi lengo nimelifikia. Lengo lilikuwa ni kutoa mwamko. Kwani wengi wetu tulikuwa tunaamini taasisi za dini ni safi na hazina shaka. Lakini wimbo wa kanisa umetoa mwanga kwamba kila mtu anatakiwa asiamini moja kwa moja. Ni vyema kuheshimu lakini ni vyema kutilia shaka pia.

Je, kuna changamoto zozote ulikutana nazo katika mzunguko mzima wa wimbo huu?

Dizasta: Changamoto zipo, producer alipata shaka siku narekodi (nadhani kwa sababu kilikuwa ni kitu kipya), kuna baadhi ya watu walikataa kusambaza kwa kuwa ni waumini wa dini tofauti, kuna baadhi walikuwa wananiona kama mtu aliyebadilika kitabia.

Kazi ishatoka na kuifikia jamii, tuna chochote cha kujivunia angalau kwa muda huu?

Dizasta: Cha kujivunia kipo. Unapofanya wimbo na ukazua maswali unapata jibu kuwa jamii imesikia wimbo. Baadhi ya watu wameahidi kuwa skeptical kwenye imani zao na kuchunguza na baadhi wameburudika na sanaa ya wimbo. And of course Nimepata pesa kidogo.

Kama una lolote la ziada la kumalizia katika muktadha huu...

Dizasta: Jambo la ziada ni kwamba, kitu chochote kinachohusu imani kinahitaji ushawishi kwani huwa hazionekani wala hakishikiki. Hivyo ushawishi hutumia nguvu na sometimes manipulation. 

Hakuna ambaye anaamini kitu kwa matakwa binafsi. Wengi tunaamini kwa sababu ya manipulation. Kukosa majibu ya maswali magumu kama kifo, maisha baada ya kifo, kipimo cha ubaya na wema vinafanya kufata dini bila ku-question. Swali ni je…”Unauliza kuhusu chakula unachokula, ubora na rangi ya nguo unazovaa Umeshawahi kuuliza chochote kuhusu ukweli wa unachokiamini?”

Mfuate Dizasta Vina kwenye mitandao ya kijamii;

Instagram: dizastavina
Facebook: Dizasta Vina
Twitter: dizastavina

Pia unaweza kumfuate mwandishi wa makala haya Iddy Mwanaharamu;

Facebook: Iddy Mwanaharamu