Panishit "Nipo Njiani"

Msanii: Panishee Mdudu (Panishit) ft. Wise Man
Wimbo: Nipo Njiani
Album: Single

Wazo

Wazo la wimbo huu lilipatikana katika studio za "Slums Musik" Kinondoni Dar Es Salam.

Panishit anasema wazo la wimbo huu lilikuja tu kama mawazo ya nyimbo nyingine lakini kikubwa kilichochangia kukua kwa chemchem ya wazo hilo ni sababu kesho yake Panishit alikuwa na Safari ya kuelekea nyumbani kwao Arusha.

Ujumbe

Nipo Njiani ni wimbo unaoelezea changamoto ambazo jamii inakutana nazo katika maisha ya kila siku. Falsafa ya safari imetumika kufikisha ujumbe huo.

Katika safari ya maisha yetu tunakutana na mengi sana, mengine yanafurahisha na yapo ya kukatisha tamaa lakini mwisho wa siku safari lazima iendelee.

Panishit amevaa uhusika wa fukara anayeishi bila kujua mustakabali wa maisha yake. Fukara huyo ambaye si hayati si mamati anaishi maisha ya kubahatisha tu na hana hakika ya kesho yenye majaliwa. Uhakika pekee alionao ni kuwa kesho maisha yake yatakuwa magumu zaidi ya leo.

Wimbo umegusia pia usaliti, urafiki wa kweli, mikasa, utawala mbovu na changamoto nyingine kadha wa kadha na vipi kama jamii tunaweza kukabiliana na changamoto hizo na kujipatia ustawi wa maisha na kuwa na jamii iliyo bora.

Uandishi

Baada ya kupata wazo akiwa studio pande za Dar, kesho yake mapema tu akaelekea stendi tayari kwa safari, akiwa kwenye basi pale Ubungo akaanza kuandika mdogo mdogo, kadri basi lilivyoshika kasi na yeye ndio mzuka na kasi ya uandishi ulivyozidi. Toka Ubungo mpaka anafika A-Town alikuwa amekamilisha verse zote mbili za Nipo Njiani, hivyo ndivyo ilivyokuwa. Nipo Njiani iliandikwa njiani ikielezea njia mwanadamu anayopitia katika maisha yake ya utafutaji.

Ushirikiano na kurekodi

Wimbo ulichukua muda mrefu sana studio, zaidi ya mwaka na hii ilichangiwa pia kwa kuchelewa kwake kurekodiwa chorus. Ras Magere kutoka "Warriors From The East" ndiye aliyeandaliwa kusimama katika chorus ya wimbo huo, wakati maandalizi yakiendelea ghafla alipata safari na kuelekea pande zao za Kenya, akasubiriwa lakini alikaa muda mrefu bila kurejea bongo na mawasiliano hayakuwa mazuri baina ya pande hizo. Changamoto kubwa ikawa ni mtu wa kusimama kwenye chorus. Kutokana na ukubwa wa idea na wimbo wenyewe alitafutwa mtu wa chorus si chini ya miezi nane lakini hakuna aliyeweza kufit fresh.

Baadae ndiyo likaja wazo la kumsaka Wise Man. Kwa Arusha, Wiseman ni mpigaji mzuri wa chorus za Hip Hop, kama ujuavyo Arusha waimbaji ni wachache sana. Wakati Wiseman anaingiza kiitikio Panishit hakuwepo alikuwa masomoni, hivyo Kz akamcall na kumwambia Wise Man kashapita kwenye chorus kisha akamtupia demo, Panishit akasema Yeees! Changamoto kwisha. Kila mmoja ni shahidi kwa kile Wiseman alichokifanya mule. Alimaliza kinoma noma.

Mapokeo

Kwa Panishit huu ni wimbo ambao ulipokelewa vizuri zaidi. Changamoto kubwa ni namna gani Pani ataweza kufikia kiwango kile au hata na zaidi.

Kiwango kilichofikiwa kwa wimbo "Nipo Njiani" ni kikubwa mno. huu ndio wimbo wake kuwahi kuwafikia watu wengi zaidi na karibia wote waliridhishwa na kazi hiyo.

Nyota njema kwa wimbo huu ilianza kuonekana tangia studio, wimbo ulikubaliwa hata kabla haujamalizwa kurekodiwa, kipindi tu Panishit alipomaliza kuingiza verse zake basi wadau waliousikia pale studio waliona kusubiri chorus kunapoteza muda kama vipi ngoma iachiwe tu vilevile, lakini Panishit akaona hapana, sababu kuna mtu alishampanga kumfanyia chorus na aliamini kabisa hiyo ingeleta kitu bora zaidi na zaidi kama ambavyo asingeweka chorus.

Producer Kz kutoka studio ya Kazawaza ndiye aliyesimamia mpango mzima wa utayarishaji wa wimbo huo, ndiye producer ambaye kwa kipindi hicho Pani alifanya nae kazi zaidi na kiukweli haina ubishi walikuwa wana Chemistry nzuri na ushirikiano wao ulikua 100%.

Nipo Njiani ilirekodiwa mwaka 2013 na ikaja achiwa rasmi mwaka 2014, ina maana wimbo ulikaa stoo kwa mwaka mzima kabla ya kuachiwa.

----

Mpaka hapo safu hii ya NYP haina la ziada…tusomane next time.

Mcheki Zee Maya kupitia;

Facebook: Panishee Mdudu (Panishit)
Instagram: panisheemdudu
Twitter: panisheemdudu

Pia mcheki Iddy Mwanaharamu mwandishi wa makala haya kupitia;

Facebook: Iddy Mwanaharamu