Ukaguzi wa albam: B.L.I.N.D
Msanii: Slimsal
Tarehe iliyotoka: 26.02.2021
Nyimbo: 15
Muunda Midundo: Slimsal
Mixing & Mastering: Tunchy Master, Zack, J Murder
Mtayarishaji Mtendaji: J Murder
Studio: Tongwe Records

SlimSal

Mwaka 1999 nikiwa Mombasa ulikuwa muhimu sana kwangu kwani ndio mwaka nilioweza kufanya mtihani wa kidato cha nne kitaifa nchini Kenya, Kenya Certificate of Secondary Education (KCSE). Ila mwaka huu pia ulikuwa muhimu kwangu kama shabiki mkubwa wa mziki wa Hip Hop kwani nilianza kuskia ngoma za emcee flani toka America pale Metro FM, ambayo ilikuwa ndio FM radio ya kwanza na kipekee Kenya nzima. Moja ya  Ngoma zake zilizo pata  kupigwa kwenye kituo hicho cha radio ni My Name Is na emcee mhusika alikuwa ni Eminem toka Marekani.

Takriban kilomita 700 toka Mombasa kule jijini Dodoma Eminem alikuwa ameanza kuskika kwa yanki flani ambaye licha ya kuzaliwa Tanga aliuchukulia mji wa Dodoma kama nyumbani. Kijana huyu ambaye hapo awali alikua ameshaanza kuvutiwa na mziki wa Hip Hop na kuanza kuandika mashairi yake na kuyachana mwenyewe, alikaa na kumskia kwa umakini emcee huyu mpya aliekuwa akiskika kila kona ya Tanzania. Eminem alikuwa amewasili Dom pia na kijana huyu kwa jina Salim Mohammed alimkubali kichizi hadi washkaji zake wakambariki na jina lake la sanaa SlimSal ambalo limetokana na Slim Shady ambalo ni jina lingine na Eminen ilhali Sal limtoka kwa jina Salim ambalo ndio jina rasmi la SlimSal

SlimSal kama vile mwenzake Slim Shady ni mbunifu ambaye anapenda ukamilifu kwenye shughuli zake za mziki, toka uandishi wa mashairi yake, uundaji midundo hadi hata nani anaye fanya kazi nae. Baada ya kufanikisha kuachia miradi kadhaa ya ma emcee pamoja na rappers tofauti wakiwemo akina Moni Centrozone, Nikki Mbishi, Adam Shule Kongwe na Andre K aliamua kuingia booth kutuandalia mradi wake mwenyewe.

Baada ya kimya cha mda mrefu kilichosababishwa na Salim kumpoteza mzazi wake, mwaka  huu  SlimSal alitangaza ujio wa debut albam yake B.L.I.N.D. Japo kua waswahili wanasema “Kimya kingi kina mshindo” wana Hip Hop tunasema “Kimya kingi kina ushindi” kwani kimya kilimuwezesha Salim kujitibu, kujihoji, kubuni ili kuweza kutupatia albam yake ya kwanza.

Ujio wake unatangazwa rasmi kwenye wimbo wa kwanza wa mradi huu Game Of Death ambapo SimSal anaonesha kuwa bado yupo hai ki mziki kama producer na emcee. Kama vile kwenye cinema iendayo kwa jina la singo hii watu walidhania kuwa starring Bill Lo (Bruce Lee) kafariki kumbe yupo hai sawia na vile watu walidhania SlimSal kafariki ki fani lakini ndio kaibuka toka chini ya maji. Wimbo huu moja kwa moja unakuonesha ni nini utarajie toka kwa ujio huu mpya wa kaka Salim; mistari iliyo andikwa ki ujanja, mashairi yenye ucheshi na vilevile huzuni pamoja na production tight toka kwake.

Wimbo Empty akiwa na Fetty Sley kama vile Subiri Mkeka akiwa na Andre K (R.I.P) ni nyimbo mbili ambazo kando na kua na ucheshi zipo serious kwa upande wa kukuhamasisha kutafuta hela. Empty inapiga freshi juu ya bass gita flani mzuka na zito sana sana ilihali sauti murua ya Fetty inailainisha. Mistari ya kiujanja ya SlimSal inaonekana kwenye vesi ya kwanza akisema,

“Unanijua unaniskia umeniskia wapi/
Uliza kiatu changu Frank knows nothing/
Hata kama nina pay I don’t roll like that/
Siogopi Vunja Bei ‘Fred for what/
Hata kama nina figures kwenye bank account/
Sipigi nazo picha coz I ain’t for clout/
Ndio maana Instagram huwezi niona na Account/
I mean Instagram huwezi niona na count/…”

Pia kwa kupitia wimbo huu anaanza kuweka wazi mambo yalivyobadilika alipoondoka mzazi wake akisema,

“Because ndugu zangu wote they be counting on me/
Tangu baba aondoke R.I.P/
‘All Eyes On Me’ Tupac Shakur/
I’m not that rich and I’m not that poor”

Nyimbo nyingine ambazo ni personal sana kwa Salim ni kama vile Melodies & Memories akiwa na Lulu, Leila, Salma & Neema pamoja Salim Mohamed, jina rasmi la emcee huyu. Memories & Melodies unapiga mdogo mdogo freshi sana na unamkuta SlimSal akitukumbushia maisha yake ya utotoni kwenye vesi moja ndani ya wimbo uliomilikiwa pakubwa na sauti nzuri ya Lulu kwenye kiitikio. Wimbo mzuka sana.

Leila, Salma & Neema pamoja na Salim Mohamed ni nyimbo mbili mzuka ila ni wimbo mmoja! Ni kama ume hit ume hit play kuskia Leila, Salma & Neema ukajikuta unaskia Salim Mohamed au vice versa. Wimbo huu toka beat, mistari hadi sauti za mizuka ndani yake hadi mashairi umejaa majonzi na unamkuta kaka Salim akitema nyongo kuhusa kifo cha mzee wake, changamoto wakati wa msiba na baada ya msiba. Mstari wa mwisho ndio unaweka mukhtasari mzuri wa wimbo mzima akisema SlimSal,

”This is not based on true story/
This is not even a true story/
Hii hata sio story/
But this is the truth! /
Ukweli! /”

Mada ya mapenzi imegusiwa kwenye nyimbo kadhaa pia kama vile Aikambe na Online akiwa na Fredrick Mulla. Aikambe ni wimbo wa vichekesho sana ambapo SlimSal kaanza kwa kumtongoza mrembo Aikambe na kisha kaenda kuwacheki wazazi wa mpenzi wake wa kichaga na huko anakutana na vituko tu. Hapo ndio unaona vile kaka Slim karithi ubunifu, storytelling na ucheshi wa role model wake Eminem. Pia hapa unaona uwezo wa SlimSal kuimba pia.

“Mama Aika shikamoo mimi naitwa SlimSal/
Samahani if I’m wrong kwa kuongea na Aika/
Na usijali mimi na mwenzangu jinsi tulivyovaa/
Ila mi ni kijana safi na binti yako ninamfaa/
Kwanza sivuti gambe wala sinywagi bange/
I mean sivuti bange wala sinywagi gambe/
Ila nitaanza kunywa mbege kwa sababu ya Aikambe/
Shule sijakimbia umande naenda church hadi Monday/
Ilibaki nusu tu yani ningeshakua Padre/”
Wimbo ni ucheshi mwanzo mwisho!

SlimSal anaonesha kuwa pia anaweza kurusha Cold Rock Party kama Mc Lyte kwenye wimbo wa Mwaga. Kwa wala bata huu wimbo hauwezi kosa kwenye playlist yenu.

IDGAF ndio wimbo wa mwisho kwenye mradi huu nilioupenda kwani umeundwa ki West Coast sana. Wimbo wenyewe unanikumbusha vitu kadhaa; beat za old school, marehemu DMX (R.I.P) ilhali kwenye uimbaji nimemkumbuka Nate Dogg (R.I.P).

Japokua mtu anaweza kuwa kipofu ki afya anaweza akawa anaona ki maono, ki upeo, ki mawazo na kifikra. Hata kama kumpoteza mpendwa wake wa karibu kulimpofusha SlimSal hisia zake kwa mda, upofu huu umewuwezesha kutafuta njia mbadala ya kupata mwanga wa kuona na mwanga huo kwake ulikua ni mziki. Kupitia uwezo wake kwenye kinasa na midundo yake makini rapper SlimSal ameweza kuondoa upofu wake na kuweza kuwa huru kupitia mradi wake B.L.I.N.D. Kuondoa B.L.I.N.Dness ndio hatua ya kwanza ambayo imekua nzuri na nina matumaini huko mbeleni miradi itakuwa bora zaidi.