Rapper/Producer SlimSal

SlimSal ni producer ambaye yupo mda mrefu  kwenye game japokua amefahamika na watu wengi hivi majuzi baada ya kufanya kazi na mwanadada wa Hip Hop Fridah Amani. SlimSal sio tu producer bali pia ni rapper mwenye uwezo wa kughani kama vile role model wake Slim Shady.

Rapper/producer huyu amefanikisha kutoa albam yake ya kwanza mwaka huu na tuliona ni vyema tukiwasiliana naye ili kuweza kumfahamu na kuweza kujifunza kutoka kwake. Karibuni mumfahamu SlimSal.

Karibu sana Micshariki kaka. Kwanza uanze kwa kutuambia, SlimSal ni nani,kazaliwa wapi na anatokea/kupatikana wapi?

Shukrani sana Micshariki Africa kwa mwaliko wenu.

Slimsal amezaliwa mkoani Tanga ambapo ni chimbuko la wazazi wangu walipokutania. Baada ya kama miaka miwili marehemu baba akahamishiwa Dodoma na makazi yake  yakawa huko.

Unaitwa nani rasmi?

Jina langu rasmi lipo kwenye track namba 14 toka kwa albam yangu B.L.I.N.D; Salim Mohammed.

Kwanini wajiita au waitwa SlimSal? Jina lilikujaje na lina maanisha nini?

Wanasema jina ambalo unapewa ndilo linakukaa vizuri, linakua halichomoki, hauwezi kulipindua. Kwa mapenzi ya mimi na msanii wa Marekani Eminem ndio iliokuja kuleta hilo jina kwa hiyo Slim Shady waliligeuza na kuanza kuniita SlimSalim na mimi nikaona SlimSalim imekaa ki namna gani vipi,  nikaona liwe SlimSal.

Salim Mohammed - SlimSal

We ni muunda Midundo tu/beat maker au producer au hata pia Emcee?

Mimi ni producer, full kabisa na nilianzia kwa kuwa beat maker na kisha nika evolve nikajua kuwa naweza nikawa producer. Kwanini nasema mimi ni producer? Ni kwa sababu nina vision kwani ninapotengeneza beat huwa najua hii beat inatakiwa ifanyiwe nini.

Kwa hiyo mimi ni rap producer. Mimi nina uwezo wa ku produce mziki mzuri wa rap. Nikitengeneza beat nikasema hii nai filter, ninaifanya hivi nina sababu kuwa akija msanii nataka afanye hivi.

Nikupe mfano mdogo. Marehemu Andre K (R.I.P) alikuja na idea ya wimbo ambao nikautengeneza beat na kisha nikampa chorus. Wimbo wenyewe ulikuwa unaitwa Bora Usingeenda Shule. Mimi nilimwambia kuwa huu wimbo unahitaji nyimbo nyingine tatu, yani inahitajika project, EP, na mimi nitaifanya kazi hii. Nilimwambia nita produce beat, nimtumie kisha ataandika wimbo wa kwanza utakaoitwa Nenda Kasome, kisha wimbo wa pili atauandika unaitwa Karibu Chuo na atashirikisha watu flani. Wimbo watatu nikamwambia atauita haonekani class au Kachetuka ambao atamshirikisha Adam Shule Kongwe.

Hivi ndivyo tulifanikisha ile EP ya Andre K (RIP) Elimu Ya Juu japokua sikuwa na furaha nayo kwani nilihisi quality ilihitajika kuwa kubwa zaidi ya ilivyokua kwani nilikuwa na mipango mikubwa sana na EP ile. Nilikua na wish tungeirudia lakini Andre K akaona tuitoe.

Kwa hiyo, hiyo ndiyo vision ya kwamba unakuwa producer ya kwamba unajua product inatakiwa itokeje. Kwa kujua product inatakiwa itokeje ina maana ume i produce ile product. Kwa hiyo mimi ni producer. Hilo nimemaliza

Swala la mimi kuwa emcee nafkiri hicho kina determine kitu gani ninacholeta kwa watu kwa hiyo hio sio swala la ku question, sijui kama unanielewa?. Una bring nini kwa watu? Ukisikiliza Shauri Yako, Target na nyimbo nyingine utajua kwamba nina play part gani kama emcee. Kwa hiyo hilo ni kwa walio na uelewa wa hivyo vitu wata determine kwamba level ya u emcee ya SlimSal is…

Historia yako ki mziki ipoje?

Historia yangu ki mziki imeanza kwa ku admire watu niliokuwa nawaona na kuwasikiliza wakati  nilipokuwa mdogo nikiandika mistari na ku rap nikiwa shuleni. Nikiwa darasa la tano tu nilikuwa naandika nyimbo za ukimwi na vitu kama hivyo. Baadae unakuta kilikua ni kitu serious kwani kipo ndani yangu na kimekaa.

Pia utandawazi ulisaidia kwani niliweza kumuona Eminem, Dr. Dre na kuanza kujifunza na kwenda deep. Mimi na wenzangu pia tukaunda makundi  ya kuchana kama vile N. 07, Centrozone akina Moni, na kutengeneza kitu ambacho watu wangeweza kukiskia. Baadae nikakua na kubahatika kufanya kazi na wasanii waliopo mainstream kwa pande zote za production na pia kama msanii.

Hii ndio historia yangu kwa kifupi na nadhani inaeleweka freshi hivyo.

Ulianzaje shughuli ya u producer na ni kipi kilicho kupatia motisha kubaki hapo?

Mimi nilikuwa nawa admire akina Eminem na Dr. Dre, DJ Premier na baadae nilifanikiwa kukutana na Qwitch ambaye alinionesha program ya kutengeneza midundo. Hapo ndipo nikaanza kujifunza hiyo program na kisha baadae nikanunua computer mimi mwenyewe.

Wimbo wa kwanza kuutengeneza ulikua wimbo wa marehemu Andre K, Medication wa pili ukawa Block Of Ice wa Moni Centrozone. Hapo ndipo ambapo nilipoanzia.

Katika watu walionifanya ni baki kwenye production ni Fridah Amani kwa sababu kupitia kwake nimeona mafanikio kiukweli ya production ndani na nje ya nchi. Nimeona mafanikio kupitia yeye kwa hiyo she is one of the artist wanaoniskuma niendelee na maswala ya production.

Tueleze kidogo kuhusu album yako B.L.I.N.D…

Albam yangu ya B.L.IN.D ni albam iliyokua inspired na maisha baada ya muda mfupi baada ya kifo cha mzee(wangu). Kwa hiyo mimi kama artist nikawa nime stop kufanya mziki kwani niliingiwa na vitu vingi moyoni mwangu na ndio hapo inspiration ya project hii ikaja na ikawa ni kama self-therapy ili kukaa sawa kwa sababu siwezi  nikampigia simu mtu nikamtukana, I’m not that kind of person kwa hiyo nikatumia hiyo nafasi kutoa vilivyo kwenye moyo wangu kisha nikaanza kui build kuanzia hapo.

B.L.I.N.D ina maana tatu au concept tatu; ya kwanza ni kijana ambaye haelewi nini kinacho endelea, yaani kuna mkanganyiko na mzigo mkubwa sana mbele yake baada ya mzee wake kufariki.

Maana ya pili ya B.L.I.N.D ni rapper ambae watu wanafkiri ameisha ila anataka kuonesha kuwa bado yupo na hajapotea na kuwa naweza kuendelea kuchana na nikiwa kwenye conversation na ndio maana inakuja kwenye ule wimbo wa kwanza kwenye albam yangu Game Of Death inasema “Billy Law is not dead” kama vile movie ya Bruce Lee inayo itwa jina la wimbo huu watu walifkiri amekufa kumbe bado yupo hai.

Maana ya tatu ni B.L.I.N.D kwa msikilizaji ambae anaweza kusikiliza albam na akashindwa kuelewa maana ambazo zimejificha kwenye albam.

Je unatengeneza aina gani ya mziki ?

Mimi mziki ninaoutengeneza kwa asilimia 99.99% ni rap music na ndio maana unaona wasanii wengi ninaofanya nao ni rap music. Nimefanya kazi na wasanii wa Rn’B na Soul Naomisia na pia msanii wa Reggae Hard Mad lakini asilimia kubwa nafanya ni rap music, simply rap music.

Ulishawahi kuwa na shaka kuwa utafanikiwa kwenye hili?

Wakati nilipokuwa naanza sikujua kuna biashara kwenye mziki, nilichokuwa najua ni kuwa mimi ni noma ila nilipojua kwamba kuna biashara na kuna vitu vingi ndani yake ndipo ambapo nilipo step back na kutambua kuwa kuna maisha mengine ya ki biashara.

Ninajua kwamba kwenye mziki kuna vitu vingi sana ambavyo vinaendelea na sihitaji kuwa star au kuwa na jina na ndio maana nina shughuli zangu za pembeni ambazo zinaniendeshea maisha.

Ni kipi kilichokusukuma uwache fani hii?

Kilicho nisukuma nifanye hivi ni kwamba niliona mziki ninaoufanya unapigwa mawe sana alafu nauweza kuufanya kwa hiyo kwa nini ni ung’ang’anie ilhali naweza kufanya kingine maishani.

Ilikuchukua mda gani hadi  uanze kusikika kama producer?

Kama nilivyosema Fridah(Amani) ndiye ambaye amewaamsha watu wengi sana na wakafahamu kuwa mimi ni producer ila kuna watu ambao toka kitambo walioniamini kwamba mimi ni producer ni kama vile Adam Shule Kongwe, Gftd Son, Moni ambao walikua na imani na mimi kabla hata Fridah hajatokea na kuonesha watu kuwa mimi ni producer mzuri.

Ni changamoto gani zinazo endana na shughuli yako ya production? Na unapata vipi wateja wako?

Kiukweli kabisa ni kuwa sihitaji wateja kwenye mziki bali nahitaji talent zaidi kwa sababu inanikera mtu akiingia juu ya beat yangu halafu awe hajui kuchana. Inanikera sana!

Ungetoa ushauri gani kwa yoyote anayependa kufuata nyayo zako?

Kwa mtu ambaye anataka kufuata nyayo zangu…itabidi aangalie tu mbele (heheeh, I’m kidding) ila kwa mtu ambaye anapenda ninachofanya anatakiwa ani study, anisome na itamsaidia yeye kuweza kujua atafanya nini kwa sababu najua kuna admiration ambayo inaweza kutokea. Pia a study na watu wengine pia.

Mziki huu wa Hip Hop unalipa?

Mziki wetu huu wa Hip Hop ki ukweli alichosema Madee kina ukweli ila kina chumvi nyingi sana ndani yake. Ki ufupi mziki una kundi la watu wachache sana ambao wanafaidika, sio watu wengi, ni mziki ki ujumla sio tu Hip Hop ilhali wengine wanaokota okota tu.

Hivyo mtu akitoboa basi ana uwezo wa kutengeneza hela zaidi. Ndio mana sahizi sio lazima mtu aimbe au awe na ngoma kali ili aweze kutengeneza hela. Unakuta tu ana kitu flani ambacho sio cha kimziki ambacho kimepokelewa sana na watu, kimepewa sana attention ndio ambacho kinaenda. Kuna vitu viwili ambavyo vinauza duniani, cha kwanza ni time, cha pili ni attention. Ukipata hivyo vitu viwili you are rich.

Umeshafanya kazi na ma emcee gani na kwa miradi gani?

Watu ambao nimewai kufanya nao kazi kwa karibu kwenye project ni Andre K ambayo ilikua project niliyoisimamia mwanzo mwisho. Wengine kama akina Moni Centrozone, hapa na pale, ilhali Adam Shule Kongwe huwa namtumia sana beats. Kwa hiyo sina circle ya watu wengi sana.

Pia kuna Gifted Son, akina Amani na kadhalika.

We uko chini ya umiliki wa studio ya mtu au una miliki studio yako mwenyewe?

Mimi sipo chini ya umiliki wa studio yoyote lakini ni part ya Tongwe Records.

Umeshafanya kazi na wasaniii wa ulaya na marekani au nchi jirani?

Nimeshawahi kufanya kazi na wasanii wa nje kama vile wasanii toka Canada. Kuna wimbo wao mmoja ambao unaitwa Get To Step In ila nimemsahau mwimbaji mwenyewe kwa sababu nilikua na deal na Sierra na si yeye moja kwa moja.

Je unaelezeaje mtindo wako wa kufanya kazi na msanii?

Mtindo wangu wa kufanya kazi na msanii cha kwanza ni lazma nione mbele, lazma nione kama kuna wimbo. Sio tu msanii anajua ku rap lakini kama tunataka kutoa wimbo lazima uwe wimbo ambao ni tofauti ambao mimi mwenyewe nitaridhika na sitaumia nitakapo usikiliza baadae.

Ukiskiliza nyimbo nyingi ambazo zimetoka kwangu we angalia tu Madam President, Kabla Hujaja, Godoro Jiko na Subwoofer yaani hata hiyo B.L.I.N.D album utaona kuna kitu ambacho nakihitaji ki ukweli.

Kwa hiyo ninachoangalia kwanza hii kazi ikoje, naangalia lyrics zako kama zimekaa sawa na vitu kama hivyo.

Albam ya Uwanja Wa Fujo ulitubariki na Midundo murua sana, ilikuaje kufanya kazi na Adam?

Nikizungumzia albam ya Adam Shule Kongwe, Uwanja Wa Fujo  ni kwamba Adam mtu ambaye sisiti kumtumia beats kwa sababu najua anachohitaji na ningependa kufanya kazi na Adam ki ukaribu kabisa yaani mimi niko hapa na Adam yupo hapa tunafanya kazi. Ingekua noma zaidi sema tu ni swala tu la mda.

Najua nikikaa nae hapa na hapa ninauhakika kuna step ambayo itaonekana, atapiga step moja mbele. Kuna sehemu ambapo najua atafika.

Ni wimbo gani au mradi gani unaoupenda sana ambao uliufanyia kazi?

Katika kazi nzuri ambazo nimewahi kuzifanya ni B.L.I.N.D ambayo ni package na ndio maana haikuwa na singo. Albam yote ile ipo complete, kila kitu kinabebana. Vile vile ni mradi ambao nili dedicate mda wangu kwani nimefanya production mimi mwenyewe na pia ku rap mimi mwenyewe. Huu ndio mradi ninao upenda mpaka sasa.

Gharama zako kwa kazi hii ni kiasi gani?

Gharama za kazi kwa kweli mimi sina gharama ambazo naweza sema eti ni gharama za kufanya kazi, hapana. Naangalia talent pia naangalia ni mtu gani ni msanii mkubwa au mdogo ndio nimchaji.

Unajua wasanii wengi hawana hizo pesa za kulipia studio na vitu kama hivyo. Kwa hiyo ninacho angalia talent halafu nitajua tunafanyaje.

Je ni jambo gani moja kila wimbo lazima uwe nalo ili uwe thabiti?

Kwanza wimbo lazima uwe na thought ili kuwa wimbo, uwe na wazo kuu yani mstari wa kwanza mpaka wa mwisho lazima uwe una lenga wazo kuu. Kama ukiwa na chorus, hakikisha chorus ni summary ya kile unachokiongea kwenye vesi zako na line ya kwanza na ya pili viwe vina connection, kuwe kuna muendelezo na kila kitu ni story kuwe kuna story ipo. Hicho ni kitu ambacho ni kipana siwezi kukielezea. Kila kitu ni story, kile unachoelezea ni story.

Ni nani mtayarishaji bora wa muziki anayefanya kazi katika tasnia hii leo unayemkubali?

Nawakubali wengi kama vile Goncher wa Wanene Entertainment, nampenda CJaMoker. Hawa ni wawili ambao beat zao huwa zinanigusa. Pia kuna jamaa mmoja anaitwa Black beats anafanyaga kazi sana na Mex Cortez, moja kati ya rappers wakali sana nchini Tanzania. Yule producer pia ni mkali sana yule jamaa.

Ni watayarishaji gani,waimbaji au wasaniii waliokupa motisha yako ya msingi?

Kwa watayarishaji kuna mtu anaitwa Dr. Dre, Dj Battle Cat,kuna Swizz Beatz kuna Jake One. Hawa ni watu ambao ninapenda sana style zao za production pamoja na Kanye West.

Kwenye wasanii Eminem, Papoose, Tech9, Royce da 5’ 9, kundi la Slaughter House, Hopsin ni watu wengi kusema kweli kwani kila siku rappers wengi wanaibuka. Pia kuna Ransom sasa hivi namskiliza sana ila wapo kibao sana.

Unazungumziaje game ya Hip Hop underground/handakini toka Tanzania na Africa Mashariki?

Naweza nikasema kuwa tunahitaji kuelewa kwamba kuna underground lakini pia kuna hiyo biashara ya juu so ukishajua don’t hate. Kaa ambapo ulipo, fanya ambacho unaamini.

Napenda sana anachofanya Dizasta (Vina) ni mmoja kati ya underground emcee ambao napenda wanachokifanya na Dizasta kama ameona hivyo.

Nje ya muziki SlimSal hujishughulisha na nini?

Nje na mziki mimi nashughulika uandishi wa matangazo ya biashara ya makampuni makubwa kwa hiyo mimi ninatengeneza matangazo yale katika njia ya kibunifu ili kuyasaidia yale makampuni kufikisha ujumbe kwa wahusika au wateja.

Ni nini cha mwisho unachoweza kutuambia ki ujumla ambacho sijakuuliza? Tutegemee nini toka kwa hivi karibuni na baadae?

Sasa hivi nipo katika space ambayo ninatumia sana hisia zangu na jinsi ambavyo ninavyoona nini natakiwa nifanye vile vile kulingana na watu walivyo respond. Kwa hiyo ninachanganya hivyo vitu nakuona gap gani ambalo sijaliziba, labda ninajaribu kuliziba ki mziki kwa hiyo ndicho ambacho watu wategemee. Nikiona kama sina sababu ya kufanya kitu flani ina maana nitakaaa kimya.

Tupe majina unayotumia kwenye mitandao ya kijamii

Mimi kwenye mitandao napatikana kama

Instagram: slimsal_daresalim
Twitter: slimsalmusic

Shukran sana!