Smallz Lethal ni mwimbaji wa Hip Hop kutoka Kenya ambaye amesajiliwa chini ya lebo ya rekodi ya KRK. Smallz Lethal ni emcee ambaye haogopi kutema kile kilicho akilini na moyoni mwake. Anazungumza kwa niaba ya watu wengi na anachukua talanta na shauku yake ya kuandika mistari na kuchana kama dhamira yake kuu duniani.
Tuliungana na rapper huyu aliye bobea kutokana na wimbo wake I’m Offended ili tuweze kujua zaidi kuhusu yeye na dhamira yake na kujua alianzaje, ni nini malengo yake na miradi ya baadaye inakuja.
Karibuni.
Kwa wale ambao hawakujui, Smallz Lethal ni nani?
Smallz Lethal ni emcee, rapa, mjasiriamali, mwanaharakati aka raptivist.
Unapata wapi msukumo wako wa kisanii?
Ninatiwa moyo na shughuli za kila siku, masuala ya sasa yanayotokea duniani kote na pia maisha yangu.
Imepita dakika na haujatupa kitu kipya, ni nini kinaendelea kaka?
Imekuwa dakika, lakini tayari nimedondosha video mbili, na bado niko jikoni ninapika. Nipo studio naanda mradi wangu mpya Leaders Of Today ambayo ilipaswa kushuka mnamo Septemba lakini nimeisukuma mbele.
Katika nyakati hizi zisizo na uhakika umefanya nini ili kuendelea kuwa mbunifu?
Katika nyakati hizi za Covid, mambo bado yanaendelea kama kawaida. Kwa sasa ninafanya kazi na Dandora Hip-Hop City (DHC), chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wetu, mwanzilishi, mshauri na mlezi Juliani (Julious Owino) na tuna miradi kadhaa ambayo tunafanya. Kuanzia kurekodi muziki, madarasa ya uongozi, jamii, afya, huduma za kujitolea na mengine mengi.
Tupe maelezo mafupi jinsi Washamba Wenza walivyoanza (Smallz, Kev Mamba & Flamez) je nyie bado mnafanya kazi pamoja kama kitengo?
Nilikutana na Flamez miaka kumi iliyopita huko Dandora na tukaanzisha Washamba Wenza, Kev Mamba alijiunga nasi miaka 3-4 baadaye. Bado tunafanya kazi pamoja, Washamba Wenza ni harakati kubwa na haitafifia, ukweli ni kwamba kwa kuwa kila mtu anafanya kazi kwenye miradi yake binafsi haimaanishi kuwa tuliachana, bado tuko pamoja.
Hadi sasa una albamu mbili (Common Mwananchi & Mogaka Music) una mpango wowote wa kutoa mradi mwingine?
Ndiyo, albamu ya Leaders Of Today inakuja hivi karibuni. Pia nina kanda mseto iitwayo Bud For Business iliyotolewa mapema mwaka huu, ambayo nilishirikiana na Alto KFlow chini ya KRK.
Je, kama msanii wa hip-hop ni yapi baadhi ya mafanikio yako?
Kwanza kabisa, kujumuika na watu kwa kutumia maudhui niliyoyaweka kwenye muziki, ili waweze kuelewa ulimwengu unaelekea wapi. Kama msanii ninafanya muziki kwa ajili ya watu wengi, kuhamasisha, kutoa motisha na kuelimisha. Kuzungumza kwa ajili yao juu ya yale wanayoyapitia. Mimi ni sauti kwa wasio na sauti, hiyo ndiyo njia yangu.
Pili, albamu zangu mbili. Kufanya albamu si jambo rahisi kama msanii. Big up kwa Snipper G-Ganji, aliniamini tokea siku ya kwanza. Shout out pia kwa Agano, Labalaa Makau na Ukoo Flani Mau Mau. Ni mafanikio makubwa kufanya kazi nao kwani ni miongoni mwa waanzilishi wa hip-hop Kenya. Walichukua jukumu muhimu katika kuunda miradi yangu na katika safari yangu ya muziki.
Hip-hop Hookup: Kutoa jukwaa kwa wasanii ili kuonesha ufundi wao na kukutana na wasanii wenzao na mashabiki. Ilifanyika kwa miaka 6 na nina furaha kuwa sehemu ya harakati. Imetengeneza wasanii wengi wanaong'ara kwa sasa. Ninajivunia kuwa sehemu ya safari yao.
Umekuwa mwanaharakati wa aina fulani, ukiwaita viongozi ambao unahisi wamekuwa wakikosa watu wao. Je, una mpango wowote wa kujiingiza kwenye siasa?
Sidhani kama kuna kitu kama kuingia kwenye siasa kwa sababu sisi kama raia tayari ni sehemu ya siasa. Tunachopaswa kufanya ni kusukuma mfumo uwajibike. Tayari mimi ni sehemu ya siasa za Kenya, lakini ikiwa unamaanisha kuwania kiti cha kisiasa, nihesabu nje. Nina raha kuwa msanii na nimejitolea kuendelea kuwa hivyo. Mimi ni sauti ya watu.
Je, unahisije athari za mtandao katika tasnia ya hip-hop?
Mtandao umechukua nafasi kubwa sana katika ukuaji wa hip-hop ya Kenya. Mitandao ya kijamii kwa mfano imefanya wachanaji kutambuliwa hata nje ya mipaka. Pia imetuwezesha kuungana na mashabiki, imetusaidia sana katika ufundi wetu.
Tuambie kuhusu KRK (Kisii Rap Kings), na miradi ambayo kampuni inatekeleza kwa sasa katika kuwezesha jamii?
KRK ni lebo, kikundi cha muziki na kikundi cha rap. Ni kama shirika la burudani ambalo nilianzisha miaka michache iliyopita. Tuna baadhi ya programu ambazo tunafanya kama klabu ya soka ya KRK na kikundi cha rap cha KRK.
Kupitia kampuni hiyo tunaweza kuungana na jamii kupitia michezo na burudani pamoja na kuwawezesha kufikia viwango bora zaidi. Kimsingi tunajikita katika kuwekeza kwa jamii kando na kueleza shida zao. Tunapanga kutengeneza albamu ya KRK katika siku zijazo, tunafanya kazi na zaidi yanakuja.
Wewe ni msanii mkubwa katika mji wa nyumbani kwako, Kisii. Nakumbuka kuna wimbo ulitoa wakati mwingine mwaka jana, Kunguni, je ulielekeza wimbo huu kwa wachanaji wenzako ambao hawakuwa na heshima kwako wewe kama gwiji wa rap ya Kisii?
Kunguni haikuelekezwa kwa watu maalum. Lakini nilikuwa najaribu tu kuongea na kizazi kipya cha wachanaji ambao hawana heshima. Ilinibidi kuwaweka mahali wanapostahili, njia ya hip-hop!
Je, una maoni gani kuhusu KE Hip-hop kwa sasa?
254's hip-hop iko katika hali nzuri kwa sasa. Watu zaidi wanakuja kwenye game na wanakumbatia kile ambacho tumekuwa tukifanya miaka hiyo yote. Hip-hop ni muziki usiopitwa na wakati, sio muziki wa vilabu. Unaweza kuona vilabu na migahawa vimefungwa kwa miaka miwili na muziki wao kufifia. Hali ya Hip Hop bado ni nzuri na itazidi kuwepo milele.
Maudhui daima huishi kwa muda mrefu na nitaendelea kutetea maudhui ila naheshimu aina nyingine za mziki kama Gengetone. Ni muziki wa wiki moja au mbili. Ninawashukuru kama wasanii wenzangu kwenye tasnia kwa kufanya mambo yao lakini hip-hop inasimama. Iko katika hali ya afya kama siku zote na milele.
Je, una maoni gani kuhusu tovuti za blogu za hip-hop kama vile Micshariki Africa ukiweka akilini kuwa ni vigumu kwa hip-hop kupenya mkondo mkuu hapa Kenya?
Blogu za Hip-hop zinafanya kazi nzuri sana. Piga kelele kwa Micshariki Africa, Musiq Jared, Biggest Kaka, Chain Rap Blog Africa na wadau wote wanaofanya kazi katika kukuza utamaduni wetu wa hip-hop. Watu walikuwa wanategemea TV na Redio lakini siku hizi wanapata taarifa za moja kwa moja kutoka kwa watu ambao wanathamini hip-hop. Endeleeni kufanya kazi nzuri jamani.
Miradi yoyote ijayo ambayo ungependa mashabiki wako wapate kijisehemu?
Wimbo wangu mpya Safari niliomshirikisha AY (Ambwene Allen Yessayah), unakaribia kudondoka. Tayari nimedondosha video mpya Leaders Of Today, ambao nilifanya kazi na Katapilla unapatikana kwenye YouTube.
Albamu yangu ya 3 inakaribia kutoka. Nimewashirikisha wasanii kama Katapilla, Raj, Fikrah Teule, Maburguda, Abu Dabi Tembe Kali. Nawaahidi albam Leaders Of Today itakuwa kubwa.
Pia nina mradi na Kitu Sewer, Maburguda na Abu Dabi Tembe Kali, unaoitwa Ni Wakati. Inazungumzia masuala yanayowahusu wasanii kama vile hati miliki, mgawanyo wa mrabaha na dhuluma zote ambazo wasanii wamekuwa wakipitia.
Bila kusahau, pia ninafanya kazi na Abbas Kubaff & Kitu Sewer. Kwa waamini, kaeni macho…Ninaanda kitu kwa ajili yenu.
Neno la ushauri kwa ma emcee chipukizi, wanaojitahidi sana ila wanahisi kukata tamaa?
Piga kazi!. Ikiwa unajua una talanta, pigania. Jiweke kwenye nafasi hizo ambazo zitakusaidia kukua. Ungana na watu sahihi pia uwe na timu ambayo itakusaidia kusonga mbele sio kukaa tu na watu ambao hawakupi motisha inayoweza kukuskuma kuwa bora kwa wakati.
Big up kwa Elisha Elai na Katapilla, ni mfano mzuri.
Neno kwa vyombo vya habari nchini Kenya?
Kwa maoni chanya, ninahisi watayarishaji wanapaswa kutafiti kwa muziki mpya ambao hawaufahamu vizuri.
Tuna watu wanaofanya Reggae, Rock, Dancehall, Benga, na muziki wa kitamaduni hapa Kenya. Tuna aina za mziki zilizowakilishwa vyema katika viwango vya nchi na kitaifa, kwa hivyo tafadhali na bila tafadhali wacheze ngoma zetu. Sheria inasema cheza 60% ya muziki wa Kenya. Kwa hivyo cheza tu muziki wetu na hiyo ndiyo njia pekee ya msanii wa Kenya kupata pesa.
Kuna mtu yeyote unataka kumpa shout out?
Shout out kwa wale wote wanaosukuma hip-hop ya Kenya huko nje. Heshima kwa Snipper SP, & R.I.P kaka, Dandora Hip-hop city (DHC), Ondu Street Lawyer, Khaligraph Jones, Scar Mkadinali, Vioxii Dede, RedTape Nation na kila mtu mashinani anayechangia kitu katika utamaduni huu.
La mwisho toka kwako?
Hip-hop ni hip-hop, ni maneno, mtiririko, tabia, kiunganishi, mtindo huru na vipimo hivyo vyote. Sio tu kuongea na kushindana. Ni harakati ya upendo na kusaidiana. Hatuko hapa kushindana, kila mtu katika tamaduni huu ana kitu kimoja ambacho unakosa. Basi tuwe na umoja.
Mitandao yako ya kijamii / majukwaa rasmi ya muziki ya watu ambao hawajakutana nawe?
Facebook: Smallz Lethal
Twitter: The Raptivist
Instagram: smallzlethal
Pia unaweza kupata mziki wangu Spotify, Deezer, YouTube, Tidal natumia jina Smallz Lethal.
Utapata albamu zangu mbili (Common Mwananchi & Mogaka Music) pamoja na nyimbo kadhaa kwenye majukwaa hayo yanayosambaza muziki kimataifa na kuungana nami. KISII RAP KING!
Big Up kwa Micshariki Africa!