Stan Rhymes

Uchambuzi Wa Mixtape: History The Mixtape
Emcee: Stan Rhymes
Tarehe iliyotoka: 26.01.2022
Nyimbo: 15
Watayarishaji: T3pro, Crush Selecta, Bagasco (Kunene)
Mixing & Mastering: T3pro
Studio: Tornado Vibez, 24 Records, Expensive Sound

Nyimbo Nilizozipenda: Stan, One day, Nakwambia, Mwisho Wa Reli, Kwangu, Watu, Soda, Goma, NFT, Thinking About You, Haki Elimu, Pengo

Unapokuta mtu anajiita kwa mfano Njombe Town Finest basi ujue moja kwa moja emcee huyu kaamua kujitwika jukumu la kubeba mtaa au mji aliotokea mgongoni mwake. Je ana uwezo huo? Emcee huyu ambaye alianza kwa kushiriki kwenye mashindano ya mitindo huru (freestyles) anatokea nyanda za kusini (Njombe) na ndio chimbuko la kujiita Njombe’s finest. Ili kuweza kumpima uwezo ilibidi tupate muda tupige mbizi ndani ya kazi yake mpya iliyotoka mapema mwaka huu, History The Mixtape.

Cha kwanza nilichokipenda kuhusu mradi huu ni hali ya juu ya utayarishaji pamoja na mada zilizogusiwa kwenye mradi huu. Kazi inaanza rasmi na wimbo unaoitwa Stan ambao unamkuta emcee Stan Rhymes akiongea na yeye mwenyewe akijionya na kujipatia mawaidha kuhusu maisha na umuhimu wa kuishi vizuri na kuacha mambo ya kihuni. Huu ni ujumbe kwa yoyote yule japokua anayeimbiwa ni Stan. Anasema hivi Stan Rhymes kwa Stan,

“Stan umekata ringi mbaya uko na sifa nyingi alafu nyingi mbaya/
Everytime kikopo alafu umesizi kaya/
Wee Stan utaitwa mwizi shauri yako haya/
Tathmini kesho utakua babu wa aina gani/
Huna mahusiano mema umekua kavu ki aina flani/
Umekua rafu haina kifani/
Jenga future yako haya maisha hayapigwi ngumi hata uwe mbavu wa aina gani/
Hii track nai dedicate kwako wala usizuge ni kama vile hai endi straight kwako/
Unazidisha tungi ukiwaga na stess zako/
Niko Tornado Vibes na send message kwako/
Haya mawaidhi sio ku kandia Rhymes nakuchapia/
Siogopi lawama kazi yangu kukanya vijana na wana wabandia/
Stan ni mshenzi wa tabia Ndugu wamechoka kukwambia/
Piga misele tafuta mikwanja wazazi wanataka kusaidiwa/”

Baada ya mawaidha emcee huyu anatutia moyo kwenye Oneday. Wimbo huu ambao umetumia mdundo wa Tallen and DJ Proof One Day toka kwa mradi wao Boom Bap Behaviour Vol. 2 ni wimbo chanya sana unaokupa matumaini maishani hata kama unapitia changamoto gani.

Nakwambia ndio wimbo wa tatu kwenye mradi huu na ndio single ya kwanza kuachiwa kutoka kwenye mradi huu.

Baada ya hapa emcee Stan anazama kwenye hoja ya mahaba akichana alivyofika Mwisho Wa Reli wakati akitusimulia kisa chake kilichomfanya mrembo amuache baada ya Stan kubadilika

“Nikaanza kumchukulia poa na kumuona fala/
Mida ya kurudi home ikawa ni msala/
5 O’clock in the morning hajui nilipolala/
Nikiwa kwenye game kimoja tu nalala/”

Wimbo ambao umeandaliwa na T3pro umetumia sampuli ya wimbo No Te Merezco wa Zendor.

Kisha baada ya hapa tunazama kwenye wimbo unaoongelea changamoto anazazopitia Stan Rhymes akimshirikisha mwimbaji Chipipi anayeimba vizuri kwenye ngoma iitwayo Kwangu.

Uwezo wa emcee huyu kuchana hadithi unaonekana freshi kwenye Soda wimbo flani wenye ucheshi ambao unamkuta Stan amekwenda club na akaamua japo kua yupo club ila akaamua yeye leo ni Soda kwa kwenda mbele na si kwa uhaba wa hela. Akiwa pale anaona vituko kama vile,

“Kuzama toi’ nikaanza kuona vitimbi/
Mshkaji katapika hadi kalala kwenye sinki/
Nikapata jibu mwanangu kaupiga mwingi/
Pombe kama hizi unaweza ukapigwa miti/”

Tukiwa pale batani emcee huyu anakuja kitofauti kwenye Goma ambalo ni kwa ajili ya kuonesha ujuzi wako kwenye dance hall kwenye mdundo ulioandaliwa na mtayarishaji Bagasco Kunene na uliotumia mdundo/sampuli toka kwa wimbo wa Cheezy Bxss, Je t’aime.

Toka kwenye ngoma inayotumia mdundo wa Joey Bada$$, Paper Trails Stan anaamua kudandia beat na kuchana kinoma hadi mimi binafsi naamini hata Joey mwenye atafurahi alivyowakilisha vyema emcee huyu Right Here.

NTF au kwa urefu Njombe Town Finest ni wimbo unaomkuta emcee akijigamba kwa nini anajiona yeye ndio the best kutokea Njombe. Moja ya madini niliyoyapenda humo ni,

“If you don’t come from rich family/
You must know that rich family must come from you/”

Kuonesha uwezo wake wa kuchana kwa mdundo wowote emcee huyu pia anachana kwa dundo flani la London Beat ambao uliitwa I’ve Been Thinking About You ilhali Stan kaita wimbo wake Thinking About You. Aisee jamaa ananata na mdundo mbaya sana.

Baada ya ngoma inayohimiza kila mtu ajipangie maisha yake Utajua Mwenyewe emcee huyu anaongelea watoto na elimu akitumia sampuli tofauti tofauti nzuri sana kwenye Haki Elimu, ni wimbo mfupi ila niliupiga sana.

Kanda Mseto hii inafunga na ngoma mzuka sana Pengo ambao unatumia sampuli nzuri toka kwa wimbo Baby wa Franky Style ambao unamkuta emcee akikumbuka watu aliowapoteza kama vile mama yake pamoja na watu waliotangulia mbele za haki lakini walichangia pakubwa kwenye tasnia ya sanaa nchini Tanzania. Anatuchekesha kwa nini ana mmiss Kanumba akisema,

“Na bongo movie siku hizi sijui nini kimewakumba/
Wachache wana vipaji ila wengi wanaigiza pumba/
Juzi nimeona jambazi ana vua viatu kwenye nyumba/
Ikabidi niwashe kitu maana nili mmiss Kanumba/”

Wimbo mzuka sana.

Stan Rhymes kaacha alama kupitia mradi wake History The Mixtape, ulivyo mzuri tunasubiria album yake sasa kwa hamu na gamu!

Kupata nakala yako ya Mixtape hii History The Mixtape kwa Tshs 5,000.00 (Kes 250.00) pekee wasiliana na Stan Ryhmes kupitia;

WhatsApp: +255687488529
Facebook: Stan Rhymes
Instagram: stan_rhymes