Stan Rhymes

Stan Ryhmes au ukipenda muite Njombe Town Finest ni mmoja wa ma emcee wa kizazi kipya wakali anaepatikana kule Dar es Salaam, Tanzania ambaye ana uwezo sio tu wa kuandika mistari mizuri ila pia anachana freshi tu pamoja na ku freestyle.

Kipaji chake kipo bayana pale unapopata fursa ya kumskiliza na kama akiendelea kwa moyo huu bila ya kutia tembo maji basi kama vile mixtape yake ya hivi karibuni atakuja kuwacha History nzuri sana.

Kwanza kabisa kaka karibu Micshariki Africa jukwaa la Hip Hop. Tuanze kwa kukufahamu braza unaitwaje rasmi, unatokea wapi na unajishughulisha na nini?

Asanteni sana Micshariki Africa.

Kwa majina naitwa Stanley Halidi Wissa ilhali kisanaa nafahamika kama Stan Rhymes. Ni emcee na mfanyabiashara.

Tueleze historia ya maisha yako; ulizaliwa wapi, mpo wangapi kwenye familia, ulisomea wapi na umefika hadi wapi kielimu. Ulikujaje kuanza hii shughuli ya muziki?

Nilizaliwa Njombe na kukulia Njombe na katika familia yetu tumezaliwa wawili mimi ni wa kwanza na wa pili ni dada yangu Witness H Wissa. Nimesoma shule ya msingi Mpechi iliyoko Njombe nikahamia Iringa ambako nilisoma shule ya sekondari Tagamenda. Sikuendelea na masomo baada ya kumaliza kidato cha nne na baada ya kuwa kuwa mtaani kwa muda mrefu ndipo nilianza rasmi shughuli za muziki.

Jina lako la muziki Stan Rhymes lilikujaje na linamaanisha nini? Mbona unajiita Njombe Town Finest?

Jina la Stan rhymes nilipewa na watu walionizunguka kwa kipindi hicho nilikuwa napenda sana ku rap na mara nyingi nilikuwa nikipiga stori na watu maneno nayapanga kwa vina (Rhymes) basi wakawa wananiita Stan Vina ndipo baadaye nikatoa vina na kuweka neno Rhymes.

Najiita Njombe Town Finest kwa sababu niko proud na mitaa ninayotoka na ni desturi yetu ma emcee kuwakilisha maisha halisi ya jamii tulizo kulia. Mimi ni Njombe Town Finest kwa sababu Njombe wananitambua kama emcee bora na mwenye uwezo wa kuiheshimisha Njombe popote duniani.

Mpaka sasa una miradi mingapi na ilitoka lini?

Mpaka sasa nina mixtapes tatu; ya kwanza ni Heshima iliyotoka mwaka 2016 ya pili ni Miaka 800 mwaka 2018 ya tatu ni History mwaka 2022.

Ni nini kinachomtofautisha Stan Rhymes na emcee yoyote yule?

Tofauti yangu na ma emcee wengine ni sound yangu na pia mimi nagusa angle nyingi katika nguzo ya emcee yaani naweza ku freestyle kutokana na mazingira yaliyonizunguka na pia nafanya freestyle battle. Pia ukija kwenye uandishi nazingatia content na mitindo, hutojua kama ndo yule Stan wa freestyles.

Mixtape yako ya hivi majuzi History The Mixtape ilipokelewa freshi na mashabiki. Tueleze kuhusu kazi hii; mbona mradi ukaupa jina hilo?

Mixtape yangu ya History niliipa jina hilo kutokana na ukubwa wake so ni mradi ambao umekuja kujenga historia mpya kwenye kiwanda cha muziki so ni History The Mixtape.

Ni watayarishaji gani ulikuwa unawaangalia na kukubali midundo yao?

Kwa upande wa watayarishaji nilikuwa nikiwaangalia P Funk (Majani), Miika Mwamba, Duke Tachez n.k

Ma emcee gani ulikuwa ukiwaangalia wakati ukianza uchanaji?

Ma emcee niliokuwa nawacheki ni Fid Q, Prof Jay, Hashim Dogo, Nikki Mbishi, One The Incredible, Salu T, n.k

Hii miradi yako yote umeamua kuiuza mwenyewe. Mbona hujaiweka kwenye digital streaming apps ili ipatikane kwa urahisi? Tatizo nini?

Miradi yangu huwa naiuza mwenyewe kwa sababu ndio njia inayonipa faida maradufu. Mfano nikitoa mixtape na nikauza elfu kumi kwa nakala mia moja nitapata milioni moja lakini kwenye streaming platforms watu kumi wakisikiliza mixtape yangu hata elfu hamsini hakuna pia kuna wadau wangu ambao wanathamini ninachokifanya na wanaweza kuja na offer wakalipa hata laki kwa nakala moja.

Inapokuja kwenye muziki na malipo je uchanaji wako unakulipa? Na kando na muziki huwa unajishughulisha na mbanga zipi nyingine ili kuweza kuongeza wigo wa kipato chako?

Uchanaji wangu unanilipa kila uchwao naona mafanikio zaidi mbeleni. Nje ya muziki nafanya biashara nyingine kitaa na deal na mavazi na vyakula kutanua wigo wa kipato.

Kwa maoni yako ni nini kifanyike ili ma emcee wa underground waweze kuonekana mainstream na kupata fursa zilizopo kule bila ya kuongeza maji uhalisia wao?

Inawezekana kwa ma emcee wa undergound kuingia mainstream bila kuchakachua uhalisia kikubwa ni kusimamia na kuheshimu unachokifanya. Uhalisia una nguvu sana popote pale. Kila mtu ni shabiki wa uhalisia kwa sababu hata wanaofeki pia wana maisha yao halisi nje ya u feki wao. Na pia tukiwa kama wana Hip Hop tunapoanzisha vilinge tutoe elimu zaidi pia kuhusu soko.

Nini tutarajie kutoka kwako Stan, unaandalia nini mashabiki zako?

Kwa sasa niko katika maandalizi ya album lakini kabla sijaitoa hapa katikati wategemee mawe kadhaa.

Una ushauri gani kwa ma emcee chipukizi, wachoraji au yoyote yule anayejihusisha na sanaa?

Ushauri wangu kwa ma emcee chipukizi au yeyote anayejihusisha na sanaa ni wajitahidi kuwa wabunifu zaidi na wakipe thamani chochote wanachofanya.

Neno la mwisho kwa yoyote yule?

Neno la mwisho ni kwamba tusikatishwe tamaa hata tunapopata changamoto kubwa kiasi gani.

Tumalizie kwa kutueleza unapatikana wapi kwenye mitandao ya kijamii?

Mimi na napatikana kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo

Instagram: stan_rhymes
Facebook: Stan Rhymes
Twitter: Rhymeccah
Youtube: stan rhymes