Nyimbo nilizozipenda: Tabia mbaya, Mr. Policeman, Nairoberry, Warui, Pata Pata, Skit, Mi Na We, Who Izet, The Plague

K-South lilikuwa kundi la wana Hip-Hop wa Kenya lilioundwa na "Bamboo" (Tim Kimani) na "Doobeez'" (Jerry Manzekele), ambaye sasa anajulikana kama "Abbas Kubaff" au pia “Abbas”. Ilianzishwa mwaka wa 1995, K-South ni miongoni mwa waanzilishi mashuhuri wa muziki wa Hip Hop nchini Kenya. Jina la kundi hili ni kifupi cha Kariobangi Kusini(South), kitongoji cha Nairobi walikokuwa na makazi. Kundi hili lilitumia rap za Kiingereza na Kiswahili katika muziki wao. (Wikipedia)

Wakati wakianza, kikundi hicho kilijumuisha washiriki watatu, Bamboo (Tim Kimani) KC (ndugu mdogo wa Abbas) na msanii aliyejulikana kama Doobeez, ambaye sasa ni Abbas. Kikundi kilitumia Kiingereza, Kiswahili (na Sheng) katika muziki wao kama lugha. (The Standard)

Albamu yao ya kwanza Nairoberry ilitolewa mwaka wa 2002, Mei tarehe 1 na Samawati Studios na ilikuwa na baadhi ya vibao vyao vya awali kama vile Tabia Mbaya, Tunapenda Zote na War Song.

Mara yangu ya kwanza kuskia album hii Nairoberry ilikua 2002 nikiwa chuo kikuu Moi University Chepkoilel Campus (Sasa ni University Of Eldoret), Eldoret, Kenya. Mdogo wangu naye alikuwa chuo hicho hicho ila Main Campus. Chepkoilel Campus hadi Main Campus kuna umbali wa kilomita 45.

Mwaka huo 2002 nilisafiri hadi Main Campus kuweza kushuhudia Tamasha La Wiki Ya Utamaduni (Cultural Week Festival). Tukiwa kule jioni moja mdogo wangu akanipeleka kuwasalimia masela wake ambao kwa zali tulikuwa tumetokea wote mtaa mmoja Mombasa (umbali hadi Eldoret ni kilomita 800, takriban masaa 13) na wakawa wanafanya kozi moja na braza. Cha kushangaza hawa masela tulikuwa tumesoma shule ya msingi pamoja na baada ya kila mtu kwenda shule tofauti za upili tutakutana tena chuo kikuu, Eldoret.

Tulipofika nikakuta kwanza masela wenyewe walikuwa waarabu flani ambao kitaani mzee wao alifahamika kwa kumiliki duka kubwa liliouza vitu vya jumla, Mzee Karama. Umaarufu wa duka lake lilifanya eneo walilotokea kuitwa “Kwa Karama” (mitaa yetu, Kongowea, Mombasa).

K-South - Abbas (Kushoto) na Bamboo (Kulia)

Tulipoingia pale kwao ilikuwa ni mida ya saa tatu usiku na kilichonasa maskio yangu kwanza ni aina ya ngoma zilizokua zinapiga kwenye spika, ngoma mpya toka kwa kundi la K-South. Cha kushangaza jamaa hawa waarabu walikuwa wamenunua na kumiliki cassete original ya Nairoberry ambayo tuliiskiliza hadi usiku wa manane. Hapa ndipo niliona uwezo wa mziki wa Hip Hop ulivyoweza kuvunja mipaka kwani pale sote tulikuwa mashabiki kindakindaki wa Hip Hop bila kujali umri, itikadi za dini, rangi wala matabaka.

Japokua kundi hili halipo pamoja tena leo nimeona nikumbushie kuhusu mradi huu ambao ulikua wa kibunifu sana na uliongelea changamoto wanazopitia wa Kenya kwa njia ya ucheshi. Jina la mradi huu Nairoberry lilinuia kuonesha kiwango cha juu cha uhalifu enzi hizo kule Nairobi.

Ngoma zilizoonesha changamoto hii moja kwa moja ni kama Mr. Policeman iliyoangaza changamoto walizokua wanapitia raia kwenye mikono ya polisi. Wimbo ulitumia mdundo toka kwa magwiji wa Hip Hop toka America Missy “Misdemeanor” Elliott, Magoo na Timbaland na waimbaji 702 uitwao Beep Me 911. Wimbo Nairoberry uliobeba jina la album uliangazia zaidi changamoto za mji wa Nairobi.

Tracklist ya Nairoberry;

  1. Who Izet
  2. Tabia Mbaya
  3. Mr. Policeman
  4. Nairoberry
  5. Warui
  6. Illekrik Posse
  7. Pata Pata
  8. Plague
  9. Skit
  10. Mi Na We

Shukran ziende kwa Abbas na Bamboo kwa kutuachia mradi huu mzuka sana.