Album: Boombap Queen
Msanii: Teddy Boombap
Nyimbo: 16
Tarehe Iliyotoka: 2019
Ma Producer na Wapiga Midundo: Paul Loops
Studio: Home Studio
Akiwa ni emcee ambaye alianza kusikika 2019 kwenye Kipindi cha “Planet Bongo” segment ya “Dakika 10 Za Maangamizi” pale East Africa Radio, Tanzania, Teddy Boombap amepiga hatua sana. Teddy ambaye anajulikana rasmi kama Teresia Sauli Mwakyanjala alizaliwa mwisho wa miaka ya themanini.
Teddy alivutiwa na midundo ya Boom Bap ambayo ni mtindo wa utengenezaji wa muziki uliokuwa maarufu katika Pwani ya Mashariki ya America (East Coast) wakati wa enzi ya dhahabu ya hip hop (Golden Era) kutoka mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kwasababu ya kupenda kuchana juu ya midundo ya Boom Bap, Teddy alianza kuitwa Teddy Boombap rasmi na mashabiki wake.Teddy anapata motisha kutoka kwa ma emcee kama Busta Rhymes, Nas, Tupac Shakur, Mc Lyte, Queen Latifah, Eve, Bahamadia na wengineo.
Boombap Queen ni mradi wa malkia Teddy wa kwanza ambapo amekuja kusimamia milki yake ya Boom Bap Hip Hop iliyomlea na kumkuza akisema kwenye utangulizi wa album “Taji nililovishwa sio taji la mpito/Niko nalo mimi leo mpaka kifo” kuonesha yupo tayari kulinda utamaduni huu kwa nguvu zake zote.
Malkia Teddy kwenye album hii ameonesha uwezo mkubwa wa kujitegemea kwa kuweza kuchana kwenye midundo tofauti tofauti na kuweza kupanua wigo wa mada anazozizungumzia kwenye album yake ya kwanza. Pia kwenye mradi huu ambapo wageni waalikwa asilimia tisini na tano ni ma emcee waliopo kwenye game Muda mrefu, Teddy ameweza kusimama kimashairi na kwenda nao sambamba. Kwa mfano kwenye “Hauniwezi” akimshirikisha Kiraka Tosh wa Viraka, Teddy anarusha ngumi za ki mistari zinazoendana na uwezo wa Tosh. Biti na mistari inavyopiga unajua tu goma si la kitoto.
Anasema Teddy,
“Biti nzito yenye wito sikosei/
Kipawa nilichonacho ni changu sigongei/
Biti imara binti kinara mpenda amani/
Nafasi yangu ni dhahabu yenye thamani/”
Malkia yoyote lazma awe na mfalme wake na kwenye nyimbo kadhaa Teddy ameongelea issue za mapenzi na changamoto zake kama vile wimbo unaoonesha kipaji cha Teddy cha kuandika maishairi-riwaya ya Bonge la ishu anapotumia mdundo toka kwa emcee Nathone kwenye wimbo wa “Free Spirit” ambao ni wimbo wa majonzi, kuvunjwa moyo na mwishowe matumaini na mapenzi ya kweli. Pia mada hii ya mapenzi anaiongelea kwenye nyimbo kama “Love story” na “My Love” ambazo Loops anampatia malkia wetu midundo iliyo na hadhi ya ki malkia. Love Story inatumia biti la wimbo uendao kwa jina “A’int no change” wa Dr. X ilhali My Love unatumia mdundo wa “Gave You My Love” wa Blunted Beatz.
Teddy anaonesha kasha cha mawazo yake ni kirefu kwenye wimbo wa Malezi unao dhihirisha ukubwa wake kiuandishi anapo ongelea changamoto za malezi wanazopitia wazazi. Anasema Teddy,
“Jamii ya sasa hivi ina mengi matatizo/
Inabidi wazazi mpate angalizo/
Kulea watoto kuna changamoto nyingi hizo/
Wanapata majanga wanawindwa mawindo/”
Malkia anawaomba wazazi wasimame kwenye majukumu yao hata kama watoto wao ni pasua kichwa.
“Hip Hop Soja (Soldier)” inamkuta malkia Teddy akiongelea changamoto za kuwa emcee. Teddy anaongelea vile watu hawamuelewi ila yeye hawajali. Pia kwenye wimbo huu Teddy anaonesha uhodari wa kuchana kwa ung’enge’.
Mistari toka moyoni mwake inasikika akisema,
“Nachana kwa hisia sio kupata commission/
Mimi kupenda rap naamini ni right decision/
Hip Hop ndio nguzo ni muhimu tradition/
Kuning’oa ni ngumu situation/”
Pia anasema,
Wananisema kwa kitaa nafanya mziki wa kihuni/
Siwezi wakataa wako wenye fikra duni/
Ni mziki wa dunia unafanywa hata Uarabuni/
Mabaya yanasemwa mema yanawekwa kapuni/
Siishi kama wao naishi kwa misingi/
Najua kuna vikwazo wataweka na vigingi/
Askari wa Hip Hop nasimama na nyota nyingi/
I will never give up siku zote kwangu ni ushindi/”
Wageni walioshiriki kwenye mradi huu kama tulivyokwisha ongelea pale juu wamesimama kwenye nafasi zao kiuandishi kama vile kwenye singo ya Ukituona iliyoundwa na 10th Wonder kwenye mdundo wenye tarumbeta murua. Maujanja Saplayaz pia wameshirikishwa kwenye mradi huu kila mmoja kwenye nyimbo tofauti. “Flowz” inamkuta D Wa Mapacha pamoja na mwanae Young General ilhali K Wa Mapacha naye kashika doria kwenye mdundo wa “Mikwala”.
Teddy anajua pia baada ya kazi dawa na kwenye wimbo wa “Thubuke” anaonyesha vile yeye anaweza kuamsha umati ili waweze kukatika kwani tunajua kufanya kazi tu bila kucheza kulimfanya dogo Jack kua zezeta. “Isiwe Kesi” ndio singo ya kwanza ya album hii na inatumia sampuli nzuri toka kwa wimbo wa J J Barnes uitwao “You are a living doll” na Teddy anajitahidi kuchana vilivyo.
Album hii kiujumla ni nzuri na ma producer wametumia sampuli za nyimbo tofauti ilhali Teddy ameonesha uwezo wa kudandia biti lolote na kusimama vilivyo. Boombap Queen imemtambulisha Teddy kama mchanaji mwenye ujasiri, uwezo wa kuandika mashairi na kumiliki kinasa. Isiwe Kesi Teddy kutunukiwa kuwa Boombap Queen, album hii imemaliza mjadala kuhusu uwezo wake.