Testa Tungo Tata

Mwaka umepita sasa tangu nijinyakulie nakala yangu ya Jandoni Mixtape toka kwa Testa. Kusema kweli mradi huu ulinifurahisha kwa sababu kijana huyu kwenye kandamseto hii aliongelea mada muhimu sana kwenye jamii yetu. Pia mradi wenyewe ulikuwa na ubunifu kibao ki mashairi, uchanaji na uwasilishaji mzuri pamoja na uchaguzi mzuri wa midundo.

Hiyvo basi nikaamua nimtafute emcee huyu ili niweze kumleta Micshariki Africa ili mashabiki wa Hip Hop waweze kumfahamu emcee huyu mwenye tungo tata.

Karibuni.

Karibu sana Micshariki Africa kaka Testa Tungo Tata. Kwanza kabisa tuanze kwa kufahamu jina lako rasmi.

Jina langu rasmi naitwa Rajabu Khassim Abdi.

Testa unapatikana wapi na unawakilisha mitaa gani ?

Napatikana Arusha. Nimezaliwa katika Hospitali ya Mount Meru Arusha,wakati ambapo baba na mama walikuwa wakiishi mitaa ya Ngarenaro kabla ya kuhamia maeneo ya Uswahilini ,ambapo ndipo nilipokulia. Ila asili yangu ni Dodoma.

Japo siishi mtaa wa Uswahilini kwa sasa ila nawakilisha Uswahilini, ndiyo mtaa nilioishi kwa miaka mingi ya utoto wangu.

Testa unajihusisha na shughuli gani ?

Najihusisha na ufugaji pamoja na biashara.

Tupe historia yako ya nyuma ki mziki.

Muziki nilianza kuvutiwa nao muda mrefu sana tangu shule ya msingi, kaka yangu alikuwa akichana ila pia nilikuwa nikiishi jirani na familia yenye kupenda Hip hop, mapacha wawili Peter na Paul pamoja na mdogo wao Richard ambao hawa walikuwa na ukaribu na mchanaji Stopper Rhymes.

Nilikuwa nikivutiwa walivyokuwa wakichana nyimbo za stopper Rhymes na baadhi ya nyimbo za wasanii wengine kama Donnie, Chindo na wengineo. Hii ilinifanya nizidi kuvutiwa na muziki huo, mwaka 2008 niliingia kidato cha kwanza shule ya sekondari Kimaseki inayopatikana Katika eneo la Kimandolu eneo lililo jirani na eneo la Kijenge ilipokuwa inapatikana studio ya Watengwa na baadhi ya member wa kundi hilo.

Asilimia kubwa ya marafiki zangu niliopata shuleni walikuwa wanatokea eneo la Kijenge na walikuwa nao wanavutiwa na uchanaji, mara nyingi walikuwa wanaandika mashairi tukiwa darasani au kufanya freestyles, nilizidi kuvutiwa na uchanaji na rasmi nikaingia kwenye uchanaji mwaka huo 2008 kwa kupata hamasa kutoka kwa marafiki Emmanuel Uronu (Rap Boy), Babcore, Melkizedek William (Underground Tembo) na wengineo.

Mwaka 2010 nilianza kurekodi kwenye studio baadhi zilizokuwa kijenge, kwa msaada wa marafiki, kwa producers kama vile Ebeny (sijui yupo wapi kwa sasa) na Khassim (Dj Kas, producer wa Grand Master Records kwa sasa) wakati huo nikiwa na umri wa miaka 15 .

Baadaye niliendelea na studio nyingine kama vile Majembe Records iliyokuwa chini ya Fido Vato na producer Goncher (producer wa Wanene kwa sasa),BM Records na baadae nikapata label katika studio ya TVC (True Vision's Colour) ambayo nilidumu kwa mwaka mmoja (nina historia ndefu ila kwa ufupi tuishie hapo,tukipata muda siku moja tutazungumza yote hayo.)

Testa Tungo Tata hili jina lako lina maana gani na lilikujaje?

Hapa itawachanganya sana maana hili jina lina historia yake kubwa na ndefu,ila kwa kifupi Testa ina maana nyingi ikiwemo KICHWA (kwa kiitalia)Testa ni Kichwa siku zote.

Testa,una miradi mingapi hadi sasa na mixtape hii ni mradi wa ngapi wako?

Ninao mradi mmoja tu Jandoni .

Tueleze kidogo kuhusu huu mradi wako. Ulitoka lini na kwa nini unaitwa Jandoni? Pia uliundwa na ma producer gani, mixing and mastering kafanya nani na studio zipi zilihusika kufanikisha huu mradi?

Mradi wa Jandoni ulitoka rasmi tarehe 24 mwezi wa 8 mwaka 2020, producer aliyeusimamia mradi huu anaitwa Mandellah, studio ni J.M Music.

Ni kipi kilichokuskuma kutengeneza mradi huu wa Jandoni ?

Wazo la kufanya Jandoni Mixtape lilikuja baada ya kupata wazo la kutoa mixtape itakayobeba elimu na burudani itakayolenga zaidi watoto wa kiume hasa vijana na hapo ndipo nikapata wazo la kufanya mixtape nitakayoiita Jandoni.

Ni nini kilicho inspire cover la mixtape yako? Tueleze kidogo kuhusu jalada la albam, ulinuia kufikisha ujumbe gani kwa kupitia jalada hili?

Wazo la cover lilitoka kwa Obby Mjuzi Mtu Makini, sikuchangia wazo lolote lile,mawazo na ubunifu wote ulitoka kwake. Naam nilimuamini kwa asilimia zote na ama kwa hakika alifanya vile ambavyo nilitarajia. (Amehusika pia katika Intro na Outro ya Jandoni.)

Album ya Jandoni naona ni kama haujamshirikisha msanii/emcee yoyote, kwa nini?

Nilihisi kumshirikisha mtu huenda asingeenda sawa na maudhui ya mradi japo kuna wakati niliwafikiria watu kadhaa wa kuwashirikisha kama vile Dizasta Vina, Adam Shule Kongwe na wengineo. Mungu akipenda watahusika katika mradi ujao, Jandoni Mixtape Volume 2.

Mradi wako hukuachia hata single moja ya kutambulisha mradi, kwa nini? Kwa nini hukuweka mradi huu kwenye streaming apps kama vile Mdundo na Boomplay?

Sikuona ulazima wa kutoa single ya kutambulisha mixtape kwa wakati ule, ila pia sikuiweka mixtape kwenye streaming apps kama vile Boomplay na Mdundo maana asilimia kubwa apps hizo hazina faida kwa upande wa album na mixtape.

Changamoto unazokabiliana nazo kwenye shughuli zako za mziki ni zipi?

Changamoto kubwa ni uchache wa studio zenye ubora, asilimia kubwa studio ninazoweza kufanya nazo kazi kwa haraka(zilizo karibu) huwa zina mapungufu katika upande wa utayarishaji.

Mashairi yako ulijifunzaje kuyaandika ? Je mtu anaweza kufunzwa kuandikiwa mashairi na akawa vizuri kwa hili?

Mashairi yangu nilijifunza kuyaandika kwa kuwasikiliza baadhi ya watu waliokuwa wakinivutia kwa wakati huo, kama vile Bonta, Jay moe, Solo Thang, Fid Q na wengineo na pia mtu kama Malle Hanzi.

Ndiyo mtu anaweza kuwa muandishi mzuri wa mashairi kama akifundishwa.

Je mdundo una umuhimu wowote kwa kusaidia kuwasilisha ujumbe wa emcee yoyote yule?

Naam!!!mdundo una umuhimu katika kusaidia uwasilishaji wa ujumbe kwa emcee. Mdundo huleta burudani na pia muda mwingine huleta maana ya kile kinachochanwa kwa wakati ule kwa mfano kusikiliza midundo yenye sample zinazoendana na kile kinachochanwa kwa wakati ule. Midundo huongeza ladha.

Tutarajie nini toka kwako huko mbeleni kwani umekuwa kimya sana kaka Testa ?

Watu watarajie kazi nzuri na zenye ubora mkubwa. Watarajie ujio mkubwa na wenye kishindo kikubwa wa kazi zangu mpya. Sipo kimya, ninazo kazi nilizoachia zaidi ya 5 na zinapatikana kwenye account yangu ya Mdundo

Ni kwa nini mziki Hip Hop haupewi kipaumbele kama miziki mingine hapa bongo? Ni kipi kifanyike ili kuweza kubadili hii hali ?

Hip hop haipewi kipaumbele kwa kuwa bado watu hawapewi elimu ya kutosha kuhusu Hip Hop. Tunaweza kufanikiwa hili kwa kuongeza elimu kwa watu,na kuongeza matamasha ya wazi ya Hip Hop.

Huwa wanasema Hip Hop ni uhuni? Hip Hop hailipi? Hivi hizi kauli unazionaje, ni za kweli?

Hip hop siyo uhuni bali matendo ya kihuni ya wana Hip Hop wachache yanafanya watu kuitafsiri vibaya Hip Hop(ulevi, ubabe, matusi na lugha mbaya)naweza kuutoa mfano mmoja rahisi.

Testa hajawahi kutumia kilevi chochote tangu azaliwe na hatatumia, wapo wakina Testa wengi katika Hip Hop ambao watu wengi hawawajui. Hip Hop ina watu wengi wema na ina upendo mkubwa ambao wasioijua Hip Hop hawawezi kuelewa kilichomo kwa watu wa Hip Hop.

Hip Hop inalipa na mimi ni shuhuda katika hilo. Wengi wanatarajia kuona magari na majumba ili kupima thamani ya kile tunachofanya ila kiukweli kuna faida inapatikana katika Hip Hop japo siyo kubwa sana, kikubwa ni kuwa kama, “Haiingizi hasara basi ina faida.”

Kipi ambacho ungependa kutuambia ambacho sijakuuliza?

Cha mwisho ni kuwa wana Hip hop inabidi tupendane, upendo hujenga ushirikiano na ushirikiano hujenga nguvu na nguvu yetu ndiyo itafanya elimu iwafikie watu kwa urahisi na mwisho kuleta mapinduzi katika jamii zetu.

Tuachane na vita ndogo za wenyewe kwa wenyewe ili tuungane kupambana na vita kubwa ya kuondoa ujinga na dhana potofu juu ya Hip Hop katika jamii zetu. Jamii ya watu wa Hip hop ndiyo jamii pekee iliyobaki katika kuifunza jamii, vizazi vinaangamia, dunia inabadilika kila uchwao. Tuungane na tuelimishane ili tuweze kuzielimisha jamii zetu.

Ahsanteni

Mcheki Testa Tungo Tata kupitia mitandao ya kijamii;

Facebook: Testa Tungo Tata
Instagram: testatungotata